Je, Wewe Huokoa Nishati au Huitumia Vibaya?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
NISHATI yenye thamani ya takriban dola za Marekani bilioni moja, inayotosha kutoa nguvu katika jiji lenye ukubwa wa Chicago, inatumiwa vibaya kila mwaka huko Marekani. Jinsi gani? Vifaa kama vile kompyuta, mashine za faksi, mashine za vidio, televisheni, mashine za CD, na hata mashine za kupika kahawa huachwa bila kuzimwa kabisa. Huachwa hivyo ili saa zake zifanye kazi, zidumishe kumbukumbu lake, na kuonyesha mielekeo—au huachwa bila kuzimwa kabisa kwa ajili ya matumizi ya mara moja.
Huko Uingereza inakadiriwa kwamba nishati inayotumiwa kila mwaka na vifaa visivyozimwa kabisa hutokeza tani nusu milioni za gesi zinazoongeza kiwango cha joto duniani, kupitia kwa uzalishaji wa umeme. Gesi hizo husambaa kwenye angahewa na huenda zikawa zinazidisha madhara ya ongezeko la joto tufeni pote. “Mbali na kwamba dhana ya kuhifadhi mazingira inapendwa na watumiaji wapya wa nishati, wengi wao hawajui uhusiano uliopo kati ya uzalishaji wa umeme na kuongezeka kwa joto la sayari,” lasema gazeti The Times la London.
Kwa kawaida wengi hawang’amui kwamba vifaa vingi vya kielektroni hutumia karibu kiasi kilekile cha nishati vinapokosa kuzimwa kabisa na wakati vinapotumiwa kikamili. Kwa mfano, huenda mfumo wa televisheni ya setilaiti ukatumia wati 15 za nishati unapotumiwa na kasoro wati 1 tu unapokosa kuzimwa kabisa. Muundo wenye kasoro pia huchangia tatizo hilo. Mashine moja ya CD ilipokosa kuzimwa kabisa ilitumia wati 28, lakini mashine ya muundo tofauti yenye vifaa sawa ilitumia wati 2 tu. Lakini sasa kisilikoni kipya cha kompyuta kimebuniwa na inadaiwa kwamba, kinaweza kupunguza sana nishati inayotumiwa na vifaa vinapokosa kuzimwa kabisa kutoka kwa wati 10 hadi wati 1 au hata kwa wati 0.1 peke yake. Inatumainiwa kwamba hatimaye watengeneza-bidhaa kotekote ulimwenguni watatumia kwa kawaida kisilikoni hiki kinachogharimu dola za Marekani 2.50, katika pambano linaloendelea dhidi ya uchafuzi. Waweza kufanya nini sasa?
Waziri wa Mazingira wa Uingereza asema: “Kiasi cha umeme kinachotumiwa na kila kifaa huenda kikaonekana kuwa kidogo sana. Lakini hujumlika kuwa kiasi kikubwa sana kwani kuna watu milioni 60 katika visiwa hivi [Uingereza].” Vifaa vya nyumbani kama vile friji kwa wazi haviwezi kuzimwa. Lakini ni jambo bora kuwa na zoea la kuzima taa zisizohitajiwa na kuzima vifaa vingine vya umeme badala ya kuviacha tu bila kuzimwa kabisa. Mbali na kwamba zoea hili litaokoa fedha zako lakini pia litaokoa sayari yetu kutokana na uchafuzi usiofaa.