Kuutazama Ulimwengu
Michezo ya Kompyuta Yenye Madhara
Wizara ya Sheria ya Brazili “imepiga marufuku mauzo ya mchezo wa kompyuta wenye kuleta ubishi ambapo wachezaji hupata maksi kwa kuiba magari na kuwaua polisi,” yasema ripoti ya shirika la habari la Reuters. Mchezo huo unaonwa kuwa “hatari kwa sababu unaonyesha wivi na uuaji kuwa mambo madogo sana na ungeweza kuchochea wachezaji wenye umri mdogo zaidi wajihusishe na jeuri.” Katika mwaka wa 1997 wizara hiyo ilipiga marufuku mchezo wa kompyuta ambao “uliwathawabisha wachezaji kwa kuwaua watu wanaotembea kwa miguu, ambao walitia ndani wanawake wazee-wazee na wanawake wajawazito.” Msemaji wa shirika la Procon la haki za wanunuzi, alisema: “Michezo ya aina hii ni hatari na yenye madhara kwa sababu hutokeza jeuri. Watoto huanza kuona utendaji wa aina hii kuwa wa kawaida.”
Bahari Zilizochafuliwa
“Uvuvi wa kikatili, kemikali zenye sumu, na takataka zenye mnururisho katika bahari zinahatarisha msingi wa uhai katika dunia nzima,” laripoti gazeti la habari Nassauische Neue Presse. Kulingana na gazeti la habari Kieler Nachrichten, sehemu iliyoathiriwa zaidi ni Bahari Nyeusi. Inaonwa kuwa mojawapo ya mifumikolojia iliyo hatarini zaidi ulimwenguni, asilimia 90 yake haina uhai. Maji machafu ya choo yamebadili mawimbi yanayotua kwenye kingo za Ukrainia kuwa uchafu wa rangi ya hudhurungi yenye kijani, na fuo za Odessa zilifunguliwa kwa muda wa juma moja tu kiangazi kilichopita. “Bahari Nyeusi imeharibiwa kabisa,” akasema rais wa Rumania Emil Constantinescu. “Tukiruhusu Bahari Nyeusi ife, tutapatwa na mabaya sana tusiyoweza kuwazia.” Umoja wa Mataifa umeutangaza mwaka wa 1998 kuwa “Mwaka wa Kimataifa wa Bahari.”
Dawa Bandia
“Karibu asilimia 8 ya dawa zinazouzwa duniani ni bandia,” lasema gazeti Le Figaro Magazine. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, asilimia ya dawa bandia katika Brazili inakadiriwa kuwa 30, na katika Nigeria inafikiriwa kuwa asilimia 60 ya kushangaza. Inaripotiwa kwamba biashara ya dawa bandia inazoa dola bilioni 300, huku uhalifu uliopangwa ukiongoza. Licha ya jitihada za makampuni ya dawa za kukomesha biashara hii, polisi na mashirika ya kimataifa hayajapata suluhisho kwa tatizo hili. Chini ya hali zinazofaa, dawa bandia yaweza kutuliza; chini ya hali mbaya kabisa, yaweza kuua. “Dawa bandia huhatarisha afya ya mgonjwa,” lasema Le Figaro Magazine.
Kupenda Bunduki Marekani
“Kuna tofauti kubwa sana kati ya Marekani na nchi nyingine,” lasema The Economist. “Katika mwaka wa 1996 bastola zilitumiwa kuua watu wawili katika New Zealand, 15 katika Japani, 30 katika Uingereza, 106 katika Kanada, 211 katika Ujerumani na 9,390 katika Marekani.” Katika Marekani kila mwaka, bunduki huhusika katika visa vya uhalifu karibu nusu milioni na vifo vipatavyo 35,000, kutia ndani kujiua na aksidenti. Na bado, Wamarekani walio na silaha “wanataka kubaki na bunduki zao bila kujali idadi kubwa ya vifo,” lataarifu gazeti hilo. “Badala ya kuchagua hatua imara za kuzidhibiti, kama zilivyofanya nchi nyingi, watu wengi wanatamani kujipatia bastola.” Sasa majimbo 31 hutoa idhini ya kuwaruhusu watu wabebe bastola zilizofichwa.
Daraja la Kuning’inia Refu Zaidi Ulimwenguni
Daraja la Akashi Kaikyo katika Japani, linalounganisha Kisiwa cha Awaji na jiji la Kobe, lilifunguliwa mnamo Aprili na mara moja likaingia katika rekodi ya kuwa daraja la kuning’inia refu zaidi ulimwenguni. “Katika hatua za kulijenga zilizochukua muda wa mwongo mmoja, mradi huu uliogharimu dola bilioni 7.7 unajivunia upana wenye meta 1,991—uliopimwa kuwa umbali kati ya hiyo minara miwili,” lasema gazeti Time. “Kila mmoja wa minara hiyo yenye urefu unaopita jengo lenye orofa 90, una vifaa 20 vya kudhibiti mtetemo; pepo zikiifanya iyumbeyumbe, timazi huvuta minara hiyo na kuirudisha mahali pake.” Pia daraja hilo limejengwa listahimili matetemeko ya dunia yanayofikia kiwango cha 8.0 kwenye kipimo cha Ritcher. Daraja hilo likisambazwa, nyaya zake za feleji zingeweza kuzunguka dunia mara saba.
Mimea Iliyohatarishwa
Baada ya miaka 20 ya kazi, wanabotania na wahifadhi mazingira ulimwenguni pote wamefikia mkataa kwamba asilimia 12.5 ya aina 270,000 za mimea ijulikanayo ulimwenguni—1 kati ya 8—imo hatarini mwa kutoweka. “Katika orodha hiyo mimea 9 kati ya 10 hupatikana katika nchi tu, ikiifanya hasa iwe rahisi kuharibiwa na hali za kiuchumi au za kijamii zinazokumba taifa au maeneo yenye mimea hiyo,” lasema The New York Times. Wanasayansi wanatoa sababu mbili kuu ambazo huhatarisha mimea: (1) kuharibiwa kwingi kwa sehemu za mashambani kwa ajili ya maendeleo, ukataji miti, na kilimo na (2) kukua kwa wingi kwa mimea ambayo si asili ya maeneo hayo ambayo husonga mimea ya asili. Makala hiyo yasema kwamba mimea “huathiriwa zaidi na hali za asili” kuliko mamalia na ndege. Yaendelea kusema hivi kuhusu mimea: “Hutegemeza uhai mwingi, kutia ndani uhai wa kibinadamu, kwa kugeuza nuru ya jua kuwa chakula. Inaandaa mali-ghafi kwa dawa nyingi na akiba ya kijeni ambayo katika hiyo aina mbalimbali za mimea husitawishwa. Na inajumlika kuwa msingi hasa wa mandhari ya kiasili ambayo katika hiyo kila kitu hutukia.”
Maambukizo ya Hospitali
“Maambukizo yanayopatikana hospitalini baada ya kutibiwa au kufanyiwa upasuaji hutokeza tatizo kubwa sana la afya ya umma,” latangaza gazeti la habari la Kifaransa Le Figaro. Katika Ufaransa pekee, watu 800,000 wanaambukizwa kila mwaka, na idadi ya vifo inakadiriwa kuwa 10,000. Hatua mbalimbali zaweza kupunguza ambukizo: kusafisha vyumba kabla mgonjwa mwingine hajaingia, kuchunguza njia zinazotumiwa kuua vidudu, na kunawa mikono kikamili kabla ya kumtibu mgonjwa. Inaonekana kwamba, mara nyingi, nyingi za hatua hizi hupuuzwa. Uchunguzi uliofanywa katika hospitali moja ya Paris ulifunua kwamba ni asilimia 72 pekee ya wafanyakazi wasaidizi wa hospitali waliosema kwamba walinawa mikono baada ya kumgusa kila mgonjwa. Kati ya hawa, asilimia 60 walinawa mikono yao kwa muda mfupi sana kuliko inavyohitajiwa. Gazeti hilo la habari lamalizia kwamba kukiwa na takwimu za kuhofisha kama hizi, “maendeleo makubwa sana yahitaji kufanywa.”
Mikanda ya Usalama Huokoa Maisha Unaposafiri kwa Ndege
Kama ajuavyo kila msafiri wa ndege mwenye uzoefu, ndege zaweza kukumbana kwa ghafula na pepo zenye nguvu ambazo zinaweza kujeruhi au hata kuwaua abiria. Wataalamu wanasema kwamba tahadhari zuri pekee ni kufunga mkanda wako wa usalama wakati wote unapoketi ndani ya ndege. “Upepo mkali usioonekana huwa vigumu sana kubashiri, kugundua, na kuepuka,” lasema U.S.News & World Report. Huku wanasayansi wakitafuta kubuni vifaa vya kugundua pepo kali, sasa ndege nyingi zategemea ripoti kutoka kwa ndege ambazo ziko mbele katika njia ileile. Karibu watu wote waliojeruhiwa wakati wa pepo hizo kali hawakuwa wamejifunga mikanda ya usalama. “Lakini,” makala hiyo yakubali kwamba “mashirika ya ndege hayajabuni njia ya kuwalazimisha abiria kufunga mikanda ya usalama.”
Okoa Umeme
“Asilimia 11 ya umeme unaotumiwa katika nyumba na ofisi za Ujerumani hutumiwa na vifaa vya akiba,” charipoti kijarida Apotheken Umschau. Kulingana na makadirio katika Ujerumani, televisheni, vinanda, kompyuta, na vifaa vingine vya kielektroni vya akiba hutumia karibu kilowatt bilioni 20.5 za saa za umeme kila mwaka. Kiwango hiki chapita kiasi cha umeme kinachotumiwa kwa mwaka mmoja katika Berlin, jiji kuu zaidi la nchi hiyo. Yawezekana kuokoa umeme na pesa zako kwa kuzima kabisa vifaa fulani vya umeme badala ya kuviacha vikitumia umeme.
Bahari Iliyokufa
Bahari Iliyokufa, ambayo ndiyo sehemu ya dunia iliyo chini kabisa na yenye chumvi nyingi zaidi, inatoweka haraka. Katika mwaka wa 1965 uso wa Bahari Iliyokufa ulikuwa meta 395 chini ya usawa wa bahari. Sasa uso wa bahari hiyo upo meta 413 chini ya usawa wa bahari, na kisehemu kidogo cha ardhi kavu kimejitokeza ambacho kinagawanya bahari hiyo mara mbili. Hoteli zilizojengwa kwenye kingo za maji hayo sasa ziko mbali. “Kiwango cha maji yake kinapungua kwa sentimeta 80 kwa mwaka, hakukuwa na maji ya kutosha yaliyotiririka ndani ya Bahari Iliyokufa kwa sababu ya mahitaji ya watu na ya siasa,” lasema The Dallas Morning News. “Uwezekano wa kufa kwa Bahari Iliyokufa waonyesha ukubwa wa uhaba wa maji katika eneo hilo, huku mambo yanayozuia utatuzi yakionyesha jinsi maji na amani yanavyohusiana katika Mashariki ya Kati iliyo kavu. . . . Leo, chanzo kikuu cha maji ya Bahari Iliyokufa, Mto Jordan, karibu umeelekezwa kwingineko kabisa . . . na Israeli, Siria na Yordani.” Kuhusu historia ya Bahari Iliyokufa, makala hiyo yasema: “Kwa kiwango kikubwa simulizi lililo dhahiri ni lile la Kibiblia juu ya jinsi Majiji ya Nyanda yalivyokaa katika eneo lenye rutuba mpaka wakati Mungu, alipokatishwa tumaini na uvunjaji maadili wa watu hao, ‘akanyesha salfa na moto juu ya Sodoma na Gomora’ na kuyaangamiza.”