Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 12/8 kur. 7-10
  • Kutafuta Maisha ya Hali ya Juu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutafuta Maisha ya Hali ya Juu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ‘Mlifanikiwaje Hapo Awali . . . ?’
  • Ufuatiaji Raha
  • “Kujiburudisha Kupita Kiasi”
  • “King’aacho . . .”
  • Badiliko Muhimu Litakalokuwa Bora
    Amkeni!—1999
  • ‘Mabadiliko Makubwa Zaidi’
    Amkeni!—1999
  • Utalii Biashara ya Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2002
  • Je, Ni Mapema Sana au Ni Kuchelewa Mno?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 12/8 kur. 7-10

Kutafuta Maisha ya Hali ya Juu

“Karne ya ishirini ilipoendelea, maisha ya kila siku ya watu wengi . . . yalibadilishwa na maendeleo ya kisayansi na ya kitekinolojia.”—The Oxford History of the Twentieth Century.

MOJAWAPO ya mabadiliko makubwa katika enzi hii yahusu idadi ya watu. Hakuna karne nyingine ambayo imekuwa na ongezeko kubwa la watu kadiri hiyo. Lilifikia takriban bilioni moja mapema katika miaka ya 1800 na takriban bilioni 1.6 kufikia miaka ya 1900. Mwaka wa 1999, idadi ya watu ulimwenguni ilifikia bilioni sita! Na wengi wa watu hao wanaoongezeka wametaka vile vinavyoitwa eti vitu bora maishani.

Maendeleo katika tiba na kupatikana kwa utunzaji wa afya kumechangia ongezeko hilo la watu. Matarajio ya muda wa kuishi kwa wastani yaliongezeka katika sehemu kama vile Australia, Japani, Marekani na Ujerumani—kutoka miaka inayopungua 50 mwanzoni mwa karne hii hadi kufikia zaidi ya 70 sasa. Hata hivyo, mwelekeo huo unaofaa si mkubwa sana kwingineko. Watu wanaoishi katika angalau nchi 25 bado wana matarajio ya muda wa kuishi wa miaka 50 au inayopungua hiyo.

‘Mlifanikiwaje Hapo Awali . . . ?’

Nyakati fulani vijana hawaelewi jinsi babu zao wa zamani walivyofanikiwa bila ndege, kompyuta, televisheni—vitu ambavyo sasa vinaonwa kuwa vya kawaida na hata vya lazima na watu fulani katika nchi tajiri zaidi. Kwa mfano, fikiria jinsi ambavyo gari limebadili maisha yetu. Lilivumbuliwa mwishoni mwa karne ya 19, lakini hivi karibuni gazeti Time lilisema: “Gari ni mojawapo ya uvumbuzi uliotofautisha karne ya 20 kuanzia mwanzo hadi mwisho.”

Mnamo mwaka wa 1975 ilikadiriwa kwamba mtu mmoja kati ya kumi miongoni mwa wafanyakazi Wazungu angekosa kazi iwapo magari yangetoweka ghafula. Licha ya matokeo yaliyo wazi katika viwanda vya magari, mikahawa ambako watu huingia na magari yao, na biashara nyingine zinazotegemea wateja wenye magari zingefungwa. Wakulima wakikosa namna ya kupeleka bidhaa zao sokoni, mifumo ya ugawanyaji chakula ingekoma. Wafanyakazi wa jijini wanaoishi kwenye vitongoji wangekosa kufika kazini. Barabara kuu zinazovuka nchi hazingetumiwa tena.

Ili kuongeza utengenezaji wa magari na kupunguza gharama, mashine za kufanya kazi hatua kwa hatua katika kuunda vitu ambavyo sasa ni vya kawaida katika viwanda vingi, zilianzishwa mapema katika karne hii. (Mashine za kufanya kazi hatua kwa hatua katika kuunda vitu ziliwezesha kutokezwa kwa wingi kwa bidhaa nyingine, kama vile vyombo vya jikoni.) Mwanzoni mwa karne, gari lilionwa kuwa chombo cha anasa cha matajiri katika nchi chache tu, lakini sasa ndiyo namna ya usafiri kwa watu wa kawaida katika sehemu nyingi za ulimwengu. Kama mtungaji mmoja alivyosema, “ni kama sasa haiwezekani kuwazia maisha bila magari katika karne ya 20.”

Ufuatiaji Raha

Kusafiri kulimaanisha kwenda mahali ulipolazimika kwenda. Lakini katika karne ya 20, mambo yalibadilika—hasa katika nchi zilizositawi. Kazi zenye mshahara mkubwa zilipozidi kupatikana na saa za kufanya kazi zilipopungua kufikia saa 40 au zinazopungua hizo, watu walikuwa na pesa na wakati wa kusafiri. Sasa kusafiri kulimaanisha kwenda mahali ulipotaka kwenda. Magari, mabasi, na ndege ziliwezesha watu kwenda tafrija mahali pa mbali. Utalii wa watu wengi ukawa biashara kubwa.

Kulingana na The Times Atlas of the 20th Century, utalii “uliathiri sana nchi zilizopokea watalii na nchi walikotoka.” Kumekuwa na athari fulani isiyofaa. Mara nyingi sana watalii wamechangia pia kuharibu vitu vyenye kuvutia walivyokuja kuviona.

Sasa watu walikuwa na wakati zaidi wa kufuatilia michezo. Wengi wakaanza kuishiriki; wengine wakaridhika kuwa mashabiki sugu na wakati mwingine wakitokeza ghasia kwa ajili ya timu na wanariadha wanaowapenda zaidi. Televisheni ilipotokea, matukio ya michezo yakawa yanafikia karibu kila mtu. Michezo ya nchini na ya kimataifa ilivutia mamia ya mamilioni ya watazamaji wa televisheni wenye shauku.

“Michezo na filamu iliweka msingi wa biashara kubwa ya vitumbuizo, ambayo sasa ni mojawapo ya sekta za biashara ambazo zimeajiri watu wengi sana na hupata faida kubwa sana,” chasema kichapo The Times Atlas of the 20th Century. Kila mwaka watu hutumia mabilioni ya dola kwa vitumbuizo, kutia ndani kucheza kamari, aina ya tafrija inayopendwa na wengi. Kwa mfano, uchunguzi mmoja wa mwaka wa 1991 uliorodhesha kucheza kamari kuwa biashara namba 12 kwa ukubwa katika Jumuiya ya Ulaya, yenye faida ya kila mwaka ya angalau dola za Marekani bilioni 57.

Tafrija hiyo ilipokuwa jambo la kawaida, watu walianza kutafuta mambo mapya ya kuwasisimua. Kwa mfano, majaribio yao ya dawa za kulevya, yalienea sana hivi kwamba kufikia katikati ya miaka ya 1990, biashara ya dawa za kulevya haramu ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 500 kwa mwaka na kuifanya kuwa, kama kichapo kimoja kisemavyo, “sekta pekee ya biashara yenye faida kubwa zaidi ulimwenguni.”

“Kujiburudisha Kupita Kiasi”

Tekinolojia ilisaidia kugeuza ulimwengu kuwa kijiji kimoja cha dunia nzima. Sasa watu huathiriwa karibu mara moja na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni. “Kwa wazi, kumekuwa na nyakati fulani maishani ambapo mabadiliko makubwa yalifanyiza historia,” akasema Profesa Alvin Tofller, mtungaji wa Future Shock, mnamo mwaka wa 1970. Aliongezea: “Lakini mambo hayo yenye kushtua na mabadiliko makubwa yaliathiri tu kikundi kimoja au vikundi vya jamii zinazoishi karibu-karibu. Ilichukua vizazi kadhaa, hata karne kadhaa, ili kuathiri sehemu zilizo ng’ambo ya mipaka hiyo. . . . Leo mifumo ya ushirikiano wa kijamii imefungamanishwa sana hivi kwamba matokeo ya matukio ya wakati uleule huenea mara moja ulimwenguni pote.” Televisheni za setilaiti na Internet pia zimechangia fungu fulani katika kuathiri watu ulimwenguni pote.

Wengine wanasema kwamba televisheni imekuwa chombo chenye uvutano zaidi cha karne ya 20. Mwandikaji mmoja alisema: “Ingawa watu fulani huchambua mambo yaliyomo katika televisheni, hakuna yeyote anayebisha juu ya uwezo wake.” Lakini televisheni si bora kuliko wanadamu ambao hutokeza vipindi hivyo. Hivyo pamoja na uwezo wake wa kuathiri watu kwa njia inayofaa, ina uwezo wa kuathiri watu kwa njia isiyofaa. Ingawa programu zenye mambo yasiyofaa, zilizojaa jeuri na ukosefu wa adili, zina mambo ambayo watu fulani wanataka kuona, programu hizo zilishindwa kuboresha uhusiano wa kibinadamu na mara nyingi kuuzorotesha zaidi.

Neil Postman, katika kitabu chake Amusing Ourselves to Death, ataja hatari nyingine, akisema: “Tatizo si kwamba televisheni hututolea mambo ya kutumbuiza bali kwamba mambo yote huonyeshwa kuwa yenye kutumbuiza . . . Bila kujali ni nini kinachoonyeshwa au ni kwa kutegemea maoni gani, sababu kuu ni kwamba kiko hapo ili kututumbuiza na kutufurahisha.”

Watu walipozidi kutanguliza raha, kanuni za kiroho na za kiadili zilizorota haraka sana. “Dini nyingi za ulimwengu zilizopangwa kitengenezo zimepoteza uvutano katika karne ya 20,” chasema kichapo The Times Atlas of the 20th Century. Huku hali ya kiroho ikididimia, utafutaji anasa ulitangulizwa kupita kiasi kuliko ulivyostahili.

“King’aacho . . .”

Mabadiliko mengi yanayofaa yanabainisha karne ya 20, lakini, kama msemo usemavyo, “King’aacho usidhani ni dhahabu.” Ingawa watu wamenufaika na kurefushwa kwa muda wa maisha, kuongezeka kwa idadi ya watu ulimwenguni kumetokeza matatizo mapya makubwa. Hivi majuzi gazeti National Geographic lilisema: “Huenda ikawa ukuzi wa idadi ya watu ndilo suala la hima zaidi tunalokabili tuingiapo milenia mpya.”

Magari ni yenye mafaa na yanafurahisha lakini pia ni ya kufisha, kama ithibitishwavyo na takriban vifo robo milioni kila mwaka vinavyosababishwa na aksidenti za magari ulimwenguni pote. Na magari ndiyo kisababishi kikuu cha uchafuzi. Watungaji wa kitabu 5000 Days to Save the Planet wasema kwamba uchafuzi “sasa unatukia tufeni pote, ukiharibu au kudhoofisha uwezo wa mifumikolojia kutoka kizio kimoja hadi kingine.” Wanaeleza: “Tumevuka mipaka ya kuharibu mifumikolojia na sasa tunavuruga mambo yanayohitajiwa hasa ili kudumisha Dunia ikiwa mahali panapofaa wanyama wa hali ya juu.”

Katika karne ya 20, uchafuzi umekuwa tatizo ambalo halikujulikana katika karne zilizotangulia. “Hadi hivi majuzi hakuna mtu aliyejua kwamba utendaji wa kibinadamu ungeweza kuathiri ulimwengu kwa kiwango cha tufeni pote,” lasema National Geographic. “Sasa wanasayansi fulani wanaamini kwamba kwa mara ya kwanza katika historia iliyorekodiwa mabadiliko hayo yanatokea.” Kisha laonya: “Athari ya kibinadamu kwa ujumla ni kubwa kiasi cha kwamba kutoweshwa kwa kiwango kikubwa kungeweza kutukia katika kizazi kimoja cha kibinadamu.”

Kwa kweli karne ya 20 imekuwa ya pekee. Watu waliobarikiwa na fursa zisizo na kifani za kufurahia maisha ya hali ya juu sasa wanaona uhai wenyewe ukiwa hatarini!

[Chati/Picha katika ukurasa wa 8, 9]]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

1901

Marconi apeleka ishara ya kwanza ya redio inayovuka Atlantiki

1905

Einstein achapisha nadharia yake ya pekee ya uwiano wa vipimo vya mwendo, nafasi na wakati

1913

Ford afungua kiwanda cha kutengeneza gari aina ya Ford T

1941

Kituo cha televisheni cha kibiashara chaanzishwa

1969

Mwanadamu atembea kwenye mwezi

Utalii wa watu wengi wawa biashara kuu

Internet yazidi kupendwa

1999

Idadi ya watu ulimwenguni yafikia bilioni sita

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki