Kofia ya Panama Imetengenezewa Ekuado!
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI EKUADO
MTEJA amedanganywa? Inaonekana hivyo. Kwani mteja huyo alikuwa amelipa dola 300 za Marekani kununua kofia ya Panama. Lakini mwuzaji aliitoa katika sanduku lililokuwa limebandikwa maneno “Imetengenezewa Ekuado”! Amedanganywa? Hasha. Kwa kweli, kofia halisi ya Panama hutengenezewa Ekuado. Lakini kofia inayotengenezewa Ekuado ilipataje kuitwa kofia ya Panama? Na kwa nini kofia hiyo hugharimu mamia ya dola za Marekani?
Katikati ya miaka ya 1800, watu waliokwenda kuchimba dhahabu walimiminika California, nao walisafiri kwenda huko kupitia Shingo ya Nchi ya Panama. Hapo walinunua kofia ambazo zilikuwa zimeletwa kutoka Ekuado. Muda si muda, kofia hizo zilianza kuitwa kwa jina la mahali ziliponunuliwa badala ya mahali ambapo zilitengenezewa. Kwa vyovyote vile, kofia ya Panama ilikuja kupendwa na wengi. Kwa mfano, kofia zaidi ya 220,000 ziliuzwa nje ya Ekuado katika mwaka wa 1849. Kisha, mwanamume Mfaransa aliyeishi Panama alileta kofia hiyo kwenye onyesho la kimataifa jijini Paris katika mwaka wa 1855. Wafaransa ambao hupenda mitindo mizuri walivutiwa na kofia hiyo, hata wengine walisema kwamba imetengenezwa kwa “kitambaa cha nyasi.” Punde si punde kila mtu alivaa kofia hiyo!
Kofia ya Panama ilipata umaarufu zaidi mapema katika karne ya 20 wakati picha ya Rais wa Marekani, Theodore Roosevelt, alipokuwa amevalia kofia hiyo, ilipochapishwa katika magazeti kotekote duniani. Katika picha hiyo alikuwa amevalia fino, yaani, kofia bora ya Panama. Wengi zaidi walitaka kofia hiyo maridadi. Biashara kubwa za nguo na kofia zilianza kuziuza ulimwenguni pote. Nchini Uturuki, kofia aina ya tarbushi ilipigwa marufuku katika mwaka wa 1925 na sheria iliamuru watu kuvalia kofia ya Panama. Kufikia mwaka wa 1944, uuzaji wa kofia za Panama katika nchi za nje ulikuwa biashara kuu ya Ekuado.
Kufikia mwaka wa 1950 umaarufu wa kofia hizo ulikuwa umefifia. Lakini kofia za Panama zilizofumwa kwa ustadi huko Ekuado, bado huvutia. Wauzaji na watengenezaji wa kofia ulimwenguni hutafuta kufa na kupona kofia bora za Panama. Watu mashuhuri wa zamani na wa leo wamevutiwa na kofia hiyo maridadi. Kofia hiyo imerembesha kichwa cha Winston Churchill, Nikita Khrushchev, Humphrey Bogart, Michael Jordan, na wengineo.
Bila shaka kuna kofia za Panama za bei nafuu ambazo zimetengenezwa kwa wingi. Kofia nyingi hizo hupasuka, na nyingine hazipenywi na hewa kwa urahisi. Kofia halisi ya Panama si nzito na inapenywa na hewa ifaavyo, nayo hudumu muda wote wa maisha ya mwenyewe. Kila moja hufumwa kwa mikono, kwa hiyo kila kofia ni ya kipekee. Bei ya kofia hizo huanzia na dola chache za Marekani kwa kofia duni, kufikia zaidi ya dola 1,000 kwa kofia bora za Montecristi ziitwazo superfino. Kofia bora zimefumwa kwa ustadi zikiwa na ufumaji ulioshikamana na vilevile rangi iliyotiwa ifaavyo. Kwa vyovyote, kumbuka jambo hili: Kofia halisi ya Panama hutengenezewa nchini Ekuado tu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26, 27]
Jinsi ya Kutengeneza Kofia ya Panama
Kofia ya Panama hutengenezwaje? Mmea wa jamii ya mchikichi hutumiwa kutengeneza nyuzi zinazoitwa toquilla ambazo hutumiwa kufuma kofia hiyo. Mmea huo unasitawi sana kwenye nchi tambarare karibu na pwani ya Ekuado. Watengenezaji wa kofia wa Ekuado ni miongoni mwa wafumaji stadi ulimwenguni, nao hufanya kazi yao kwa uangalifu kama nini! Inaweza kuchukua muda wa miezi sita kumaliza kufuma kofia bora ya Montecristi inayoitwa superfino. Kila unyuzi katika kofi ni mfupi. Hata hivyo, katika kofia halisi ya Panama, huwezi kuona mahali ambapo unyuzi mmoja huishia na ule mwingine kuanza. Isitoshe, nyuzi zinafumwa na kusongwa sana hivi kwamba hata maji hayawezi kupenya!
Mji wa Montecristi unajulikana kwa sababu ya kofia zake bora zilizofumwa kwa mikono. Wafumaji stadi wa eneo la Montecristi hufuma mapema asubuhi au jioni-jioni, ili kuzuia joto kali la sehemu hiyo ya ikweta lisiathiri unyumbufu wa nyuzi. Wanaanza kufuma sehemu ya juu ya kofia. Mfumaji hufuma mviringo baada ya mviringo wa nyuzi kama wavu tata, hadi afikapo kipenyo kinachotakiwa. Halafu, sehemu hiyo ya juu ya kofia huwekwa kwenye mbao yenye umbo la duara, ili kumwezesha mfumaji kuendelea kufuma sehemu za kando za kofia akielekea chini. Baada ya majuma kadhaa kupita, ataanza kufuma ukingo wa kofia. Mambo ya kumalizia hutia ndani kuosha na kupararisha kofia, na mwishowe kofia maarufu ya Panama huwa tayari.
[Picha]
Nyuzi za majani huchemshwa na kukaushwa kabla ya kutumiwa kwa ufumaji
[Picha katika ukurasa wa 27]
Winston Churchill ni mmojawapo wa watu mashuhuri ambao wamevalia kofia ya Panama
[Hisani]
U.S. National Archives photo