Ekuado—Nchi Inayovuka Ikweta
TUKIWA wageni kutoka Ulaya, kitu cha kwanza ambacho mimi na mke wangu tulitambua kuhusu Ekuado kilikuwa ikweta. Kweli, ni mstari usioonekana, lakini uvutano wake juu ya Ekuado ni dhahiri.
Ekuado ni jina la Kihispania limaanishalo “ikweta.” Huenda wengine wakafikiri kwamba ikweta hudhibiti tabia ya nchi ya Ekuado. Hata hivyo, mara baada ya kuwasili, tuligundua ya kwamba halihewa yenye joto au baridi ilihusiana zaidi na usawa wa bahari kuliko wakati wa mwaka. Kwa kuwa jua huzunguka-zunguka juu mwaka mzima katika latitudo hizi, kimo juu ya usawa wa bahari ni mojawapo ya mambo yawezayo kukuongoza kuamua ni mavazi mangapi utakayovalia.
Huku ikweta ikifananisha Ekuado, Andes hufanyiza mandhari za nchi hiyo. Milima hii yenye fahari huivuka nchi hiyo ikiwa sehemu ya msingi na kutokeza unamna-namna wa mandhari zisizokoma.
Rangi za Namna Nyingi
Jambo la pili lililotuvutia katika Ekuado lilikuwa rangi. Asubuhi moja mara baada ya kuwasili, tuliketi chini ya kivuli cha miti fulani mikubwa. Tulikaribishwa na muziki wa ndege, muziki kama wa filimbi wa kiambizi, makelele yenye kuendelea ya wren ndege wadogo, na makelele ya sauti za muziki wa antpitta walio shupavu. Lakini rangi zao zilivutia hata zaidi kuliko sauti.
Kwa mwako mwekundu, shore aina ya vermilion aliruka kutoka kwenye makao yake ili kunyakua mbu. Kundi la kasuku wadogo wenye rangi nyangavu ya kijani kibichi walivutia uangalifu huku wakimpigia makelele turkey vulture aliyekuwa akipaa juu yao. Viambizi wenye rangi nyangavu ya manjano na nyeusi na vipepeo wenye rangi ya upindemvua waliongezea kukandika rangi zao kwenye mandhari isiyosahaulika.
Tulipokuwa tukisafiri katika nchi, tuliona kwamba zile rangi nyangavu za ndege na vipepeo zilionekana katika mavazi na kwenye vitu vilivyofanyizwa kwa mikono vya Ekuado. Kwa mfano, ule wekundu wa shore, ulilingana na zile skati nyekundu-nyangavu za wanawake Wahindi wa mkoa wa Cañar. Na vile vitambaa vilivyofumwa kwa sufi vyenye kung’aa vya Wahindi wa Otavalo vilionekana kuwakilisha rangi zote za Ekuado.
Tabia ya Nchi Iliyo Tofauti-Tofauti
Ikweta na ile Andes hushirikiana ili kutokeza tabia ya nchi iliyo tofauti-tofauti katika Ekuado. Ndani ya kilometa chache—umbali unaoweza kupimwa katika mstari ulionyooka—tabia ya nchi yaweza kubadilika kutoka kuwa joto lenye unyevunyevu la kitropiki la Amazon hadi kufikia theluji za vilele vya milima.
Siku moja, tulisafiri kutoka sehemu ya chini ya vilima vilivyo karibu na sehemu za juu za Amazon kufikia milima ya juu kuzunguka Quito. Gari letu lilipopanda, tuliona jinsi msitu wa mvua wa kitropiki ulivyobadilika hatua kwa hatua kufikia msitu wa wingu, hatimaye mandhari ilibadilika kuwa pori ya mbuga, au uwanda. Mabadiliko yenye kutokeza ya mandhari yaliyotupatia wazo la kwamba tulikuwa tumesafiri kutoka Afrika ya ikweta kufikia nyanda za juu za Scotland kwa muda wa saa chache.
Miji na majiji mengi ya Ekuado yanapatikana katika mabonde yanayokingwa na milima, ambapo tabia ya nchi inafafanuliwa kuwa kama masika kotekote katika mwaka. Hata hivyo, miji iliyo juu katika Andes yaweza kupata yoyote ya yale majira manne wakati wowote—na nyakati nyingine yote manne katika siku ileile! Kama vile msafiri mmoja mwenye uzoefu alivyoeleza, “kitu kimoja kilicho hakika kuhusiana na halihewa ya Ekuado ni hali yake ya kutoweza kutabirika.”
Ndege-Mvumi na Tai Wakubwa
Unamna-namna wa tabia za nchi hutokeza wanyama na mimea ya aina zote kwa wingi. Ekuado ina zaidi ya spishi 1,500 za ndege, ambazo ni mara mbili ya jumla yote ya Marekani na Kanada na sehemu ya sita ya spishi zote zinazojulikana ulimwenguni. Zote hizi hupatikana katika nchi ambayo ni ndogo kuliko Italia.
Jambo lililotuvutia mahususi lilikuwa ni wale ndege-wavumi wadogo mno—kuna spishi zipatazo 120 katika Ekuado. Kwanza tuliwaona kwenye bustani za jiji, wakiwa na shughuli nyingi katika kupiga doria kwenye viraka vya vichaka vilivyoota maua mapema asubuhi. Wanapatikana katikati ya msitu wa mvua wa Amazon na hata kwenye miteremko iliyo na mkondo wa upepo wenye nguvu juu katika Andes.
Katika mji wa Baños, tulitumia muda wa saa nzima tukitazama ndege-mvumi anayeitwa sikio-urujuani akilisha kwenye kichaka cha haibiskasi chenye maua mekundu. Wakati ambapo alikuwa akizunguka-zunguka angani bila kuchoka mbele ya ua moja baada ya jingine, akionja kwa ustadi nekta yenye thamani, mshindani alikuja kandokando na kumkaribia bila wasiwasi. Alikuwa ni ndege mwenye mkia mweusi mshika-mkia, aliyepewa jina hilo kwa sababu ya mkia wake mweusi na mrefu ambao unamfanya aonekane kama nyotamkia nyeusi wakati inapovuma kuzunguka eneo lake, ikifukuzia mbali washindani wake. Badala ya kuzunguka-zunguka hewani, huyu ndege-mvumi alitua kwenye shina na kudunga maua kutoka nyuma kusudi azidue nekta.
Si ndege wote wa Ekuado walio wadogo sana. Yule tai mkubwa mwenye fahari, aliye mkubwa zaidi kati ya ndege wote wawindaji, bado hupaa juu ya Andes, ijapokuwa kwa idadi iliyopungua sana. Daima tulichunguza kikamili vilele vilivyoinuka sana, tukitumaini kuona umbo lake jeusi lililo dhahiri, lakini bila mafanikio. Katika eneo la Amazon, yule tai mkendege—ndege mwindaji aliye na nguvu nyingi zaidi ulimwenguni—vilevile ni vigumu kumwona. Wakati mwingi wa mchana, hutua kwa kutoonekana kwa urahisi juu ya tawi la mti mkubwa katika msitu wa mvua uliotulia, akingojea kushuka kwa kasi juu ya mamalia mwenye kutembea polepole wa Amerika Kusini asiyeshuku au tumbili.
Mimea Iwezayo Kuponya
Mimea mingi ipatikanayo Ekuado yaweza kutumika kama dawa vilevile kwa kupamba. Wakati wa ziara yetu kwenye Mbuga ya Taifa ya Podocarpus, katika kusini ya nchi, kiongozi wetu alituonyesha mti mdogo wenye kokwa nyekundu. “Ule ni mti cascarilla,” akaeleza. “Ganda lake limekuwa chanzo cha kwinini kwa karne kadha.” Miaka mia mbili iliyopita, katika Loja ulio karibu, kwinini iliokoa maisha ya mwanamke kabaila Mhispania aliyekuwa akifa kwa malaria. Sifa yake, ambayo imejulikana na Wainka kwa muda mrefu, punde si punde ilienea ulimwenguni pote. Ijapokuwa ule mti cascarilla huonekana kuwa duni unapoutupia jicho kwa mara ya kwanza, dawa inayoziduliwa kutoka kwenye ganda lake imeokoa uhai mwingi.
Msitu wa wingu ambapo mti huo husitawi pia huwa makao ya miti mingi ya kale, ambayo matawi yake yaliyojipindapinda yametungishwa maua na spiky bromeliads, mingine yake ikiwa imechanua maua mekundu mangavu. Misitu hii iliyotengana pia huwa kimbilio la dubu wenye madoa, paka-mwitu wa Marekani, na puma, vilevile spishi zisizohesabika za mimea ambazo wanabotania bado wanajaribu kuziingiza katika orodha.
Wanasayansi wanachunguza kwa makini chura mdogo sana wa Ekuado, wakiwa na matumaini ya kupata madawa yaliyo bora ya kutuliza maumivu. Ngozi ya chura huyu mwenye sumu kwa ghafula hutoa kituliza-maumivu kinachosemekana kuwa chenye nguvu mara 200 zaidi kuliko afyuni.
Juu katika Andes, tuliona mimea fulani isiyofanana na yoyote tuliyopata kuona wakati wowote. Ile Puya, aina ya mitishamba ambayo huvutia ndege-mvumi, ilitukumbusha ufagio mkubwa wa kikale, unaongojea tu kuchukuliwa na kuanza kutumiwa kufagia mandhari inayouzunguka hapo. Katika sehemu zilizobonyeka zilizo wazi za nyanda zilizotengwa kuna misitu quinoa yenye miti mifupi, mti uwezao kustahimili hali zisizofaa unaokua kwenye mwinuko sawa na misonobari ya Himalaya. Miti hii ya vichakani, yenye urefu wa meta mbili hadi tatu, hufanyiza vichaka visivyoingilika ambavyo huwa mahali salama pa ndege na wanyama.
Hata hivyo, katika msitu wa mvua wa Amazon, miti ni mirefu na yenye kusitawi sana. Wakati wa ziara kuelekea kwenye Kituo cha Biolojia cha Jatun Sacha, tulisimama chini ya mti mkubwa wa msitu, wenye urefu unaozidi meta thelathini. Kwa ghafula, mtetemo mdogo karibu na mizizi yake mikubwa yenye kuutegemeza ulitushtua. Ndipo tulipotambua kwamba moja ya mianya katika mizizi ulikuwa makao ya familia ya popo wadogo sana. Jambo hili tulilokutana nalo lilitukumbusha kwamba msitu huo hutegemea mahusiano haya mengi yenye kutegemeana. Popo, wagawanyaji na wachavusha-mbegu wakuu wa msitu wa mvua, ni wasaidizi wa maana wa miti ambayo huwatolea kinga.
Masoko Katika Milima
Karibu asilimia 40 ya watu wa Ekuado inafanyizwa na makabila ya Kihindi. Vikundi vya kikabila vilivyo tofauti—kila kimoja kikiwa na vazi rasmi la kujitofautisha—ni vyenye kufanyiza sehemu kuu ya mabonde mengi ya Andes. Mara nyingi, tuliwaona wanawake Wahindi wakipanda vijia vyenye mwinuko mkali kwenye miteremko ya mlima, wakisokota sufu ya kondoo walipotembea. Ilionekana kana kwamba hakuna mteremko wowote uliokuwa wima sana kulimwa nao. Tulichunguza shamba moja la mahindi, lililokadiriwa kuwa limeinama kwa angalau digrii 45!
Masoko ya Ekuado, kama lile la Otavalo, yamekuwa maarufu. Ni vituo ambavyo wenyeji wa huko wanaweza kununua au kuuza wanyama na mazao ya shamba na vilevile vikorokoro vilivyofumwa vya kitamaduni au vitu vingine vilivyotengenezwa kwa mkono. Kwa kuwa wenyeji wa huko huenda sokoni wakiwa wamevalia kiasili, pindi hiyo huwa tamasha ambayo huvutia watalii wengi. Mashahidi wa Yehova pia hutumia kwa manufaa siku za soko kushiriki ujumbe wa Biblia pamoja na watu.
Uvutio wa kazi ya mfumaji ni mambo ya kale na uhuru wa kutumia rangi za kitamaduni na motifu. Watu wa Andes walikuwa wakifuma majoho yao maarufu muda mrefu kabla Wahispania hawajawasili. Ijapokuwa mbinu yao imefanywa kuwa ya kisasa, Wahindi hawa wenye kufanya kazi kwa bidii bado hutokeza nguo na vitambaa vizuri vilivyofumwa.
Milima Iliyo Katika Ukungu
Kuendesha gari kupitia Andes hakuwezi kufaa kwa mtu anayepatwa na kigegezi. Barabara hupindika na kugeuka, hupanda na kutumbukia, zinapoambaa kwenye pande za mabonde yanayojipinda-pinda. Msafiri hodari huthawabishwa na mandhari inayobadilika daima, ambayo inaweza kufafanuliwa tu kuwa yenye kutia kicho.
Tulipokuwa tukipanda kwa gari kuingia ndani ya Andes kwa mara ya kwanza, ukungu—karibu kuwa mwandamani wetu wa daima—ulijaa na kufunika gari letu. Nyakati nyingine tuliibuka kutoka kwenye ukungu na tungeweza kuona ukitandaa kwa umbali wimbi baada ya wimbi la mabonde yaliyojaa ukungu. Tulipokuwa tukisafiri kandokando ya safu ya milima Andes ukungu ulionekana kuwa ukitutania. Dakika moja, kijiji tulichokipitia kingekuwa kimefunikwa kabisa. Dakika chache baadaye, kijiji kilichofuata kingekuwa kimejianika kwenye mwanga wa jua jangavu.
Nyakati nyingine ukungu ulizunguka-zunguka juu kutoka chini; nyakati nyingine ulishuka chini kutoka kwenye vilele vya milima vilivyo juu. Ingawa iliudhi kuona mandhari nzuri ikiwa imefunikwa, ukungu ulitokeza utukufu mwingi na fumbo kwa vilele vilivyoinuka kama mnara juu yake. La maana zaidi, unafanya msitu wa mawingu uvutie, ambao hupata unyevu wenye thamani sana kutokana nao.
Kwenye asubuhi yetu ya mwisho katika Ekuado, ukungu uliisha. Kwa muda wa saa kadhaa tulijionea mandhari yenye fahari ya Cotopaxi—pia ambayo karibu imefunikwa kikamili na theluji. Volkano hii tendaji, iliyo ndefu zaidi ulimwenguni, imefanywa kuwa pambo la katikati la mbuga ya taifa. Wakati tulipokaribia kilele, tulishangaa kuona barafuto kubwa ambayo ilikuwa inajongea kidogo-kidogo kwenye moja ya miteremko yake ya juu. Kwenye mwinuko wa karibu meta 6,000, inafanikiwa kustahimili jua la ikweta lenye kuwaka sana.
Siku iliyofuata, ndege yetu ilipotoka Quito kwa safari ya kuelekea nyumbani, tuliona kwa mara ya mwisho mandhari ya Ekuado. Katika nuru ya asubuhi, tuliona Cayambe, volkano nyingine yenye kufunikwa na theluji, ikijisukuma juu ya ukungu na kumetameta kama dhahabu iliyo katika mwanga wa jua. Volkano hii, ambayo kilele chake kiko karibu na ikweta kabisa, ilionekana kuwa ishara yenye kufaa ya kuaga ya nchi yenye kuvutia sana tuliyokuwa tumezuru. Kama Cayambe, Ekuado hukaa juu ya ikweta kwa fahari.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mandhari ya Andes, na volkano Cotopaxi ikiwa katika mandharinyuma
Mhindi muuza-maua
[Picha katika ukurasa wa 26]
1. Mgomba-mwitu
2. Ndege mla-matunda wa tropiki
[Hisani]
Picha: Zoo de Baños