Yabisi-kavu Ni Ugonjwa Unaolemaza
“IWAPO HUJAWAHI KUUGUA UGONJWA HUO HUTAWEZA KUWAZIA ULE UCHUNGU UNAOSABABISHWA NAO. NILIFIKIRI NI KIFO PEKEE AMBACHO KINGEWEZA KUMALIZA MAUMIVU YANGU.” —SETSUKO, JAPANI.
“UGONJWA HUO UMEHARIBU UJANA WANGU KWA SABABU NIMEKUWA NAO TANGU NILIPOKUWA NA UMRI WA MIAKA 16.”DARREN, UINGEREZA.
“NIMEPOTEZA MIAKA MIWILI YA MAISHA YANGU KWA KUWA NILIKUWA MGONJWA KITANDANI KWA MUDA HUO.”— KATIA, ITALIA.
“VIUNGO VYANGU VYOTE VILIPOANZA KUUMA, NILIHISI MAUMIVU MATUPU.”—JOYCE, AFRIKA KUSINI.
HAYO ni maelezo yenye kuhuzunisha ya wagonjwa wanaougua yabisi-kavu (arthritis). Kila mwaka mamilioni ya wagonjwa huenda kwa madaktari ili wapate kitulizo cha maumivu, kukakamaa, na ulemavu unaosababishwa na ugonjwa huo.
Zaidi ya watu milioni 42 wanaugua ugonjwa wa yabisi-kavu nchini Marekani pekee, na mtu 1 kati ya watu 6 hulemazwa na ugonjwa huo. Ugonjwa wa yabisi-kavu ni kisababishi kikuu cha ulemavu katika nchi hiyo. Shirika la Taifa la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa linasema kwamba ugonjwa huo huathiri uchumi kama vile ‘kushuka kwa uchumi kunavyofanya,’ kwa kuwa Wamarekani hupoteza zaidi ya dola bilioni 64 kila mwaka kwa matibabu na kwa sababu ya upungufu wa uzalishaji. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, uchunguzi mbalimbali uliofanywa katika nchi zinazoendelea kama vile Brazili, Chile, China, India, Indonesia, Malaysia, Mexico, Pakistan, Thailand, na Ufilipino ulionyesha kwamba ugonjwa wa yabisi-kavu na magonjwa mengine aina ya baridi-yabisi huathiri nchi hizo karibu “sawa na vile yanavyoathiri nchi zilizoendelea.”
Si wazee pekee wanaoshikwa na yabisi-kavu. Ni kweli kwamba wazee ndio wanaoathiriwa zaidi na ugonjwa huo. Hata hivyo, watu wengi wanaougua ugonjwa wa baridi-yabisi (rheumatoid arthritis), ambao ni aina moja ya yabisi-kavu, ni watu wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 50. Nchini Marekani, karibu watu 3 kati ya 5 wanaougua yabisi-kavu wana umri unaopungua miaka 65. Hali kadhalika, huko Uingereza, wagonjwa milioni 1.2 kati ya milioni 8 wana umri unaopungua miaka 45. Zaidi ya watoto 14,500 wanaugua ugonjwa huo.
Idadi ya wagonjwa wanaougua yabisi-kavu inaongezeka kila mwaka. Watu milioni moja watapata ugonjwa huo nchini Kanada katika miaka kumi ijayo. Ingawa ugonjwa wa yabisi-kavu ni wa kawaida zaidi huko Ulaya kuliko katika bara la Asia na Afrika, unaendelea kuenea katika mabara hayo pia. Kwa hiyo, kipindi cha mwaka wa 2000 hadi 2010 kimetangazwa na Shirika la Afya Ulimwenguni kuwa Mwongo wa Mifupa na Viungo. Katika kipindi hicho madaktari na wataalamu wanaotunza afya ulimwenguni pote watashirikiana kuboresha maisha ya watu wanaougua magonjwa yanayoathiri mifupa na misuli, kama vile yabisi-kavu.
Tunajua nini kuhusu ugonjwa huo unaosababisha maumivu makali? Ni nani hasa wanaoweza kuupata? Wale wanaolemazwa na ugonjwa huo wanaweza kukabiliana na ulemavu wao jinsi gani? Je, tunaweza kutarajia tiba? Maswali hayo yatajibiwa katika sehemu zinazofuata.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Picha ya eksirei: Used by kind permission of the Arthritis Research Campaign, United Kingdom (www.arc.org.uk)