Yabisi-kavu Ni Ugonjwa wa Aina Gani?
“NINAPOENDA KULALA USIKU, MIMI HULIA MACHOZI NINAPOTAZAMA MIGUU NA MIKONO YANGU ILIYOHARIBIKA UMBO.”—MIDORI, JAPANI.
UGONJWA wa yabisi-kavu umeathiri wanadamu kwa karne nyingi. Maiti za kale zilizohifadhiwa huko Misri zinathibitisha jambo hilo. Yaelekea, mvumbuzi Christopher Columbus alikuwa na ugonjwa huo. Na mamilioni wanateseka leo. Ugonjwa huo wenye kulemaza ni ugonjwa wa aina gani?
Jina la Kiingereza la ugonjwa huo, “arthritis,” linatokana na maneno ya Kigiriki yanayomaanisha “viungo vilivyovimba,” nalo larejezea magonjwa na hali mbalimbali za yabisi zaidi ya 100.a Mbali na kuathiri viungo, magonjwa hayo yanaweza kuathiri pia misuli, mifupa, na kano (mishipa inayounganisha misuli na mifupa) mbalimbali zinazotegemeza viungo. Aina fulani za yabisi-kavu zinaweza kuathiri ngozi yako, maungo ya ndani ya mwili, na hata macho yako. Tutachunguza hasa magonjwa mawili ya aina ya yabisi-kavu, yaliyo ya kawaida sana—ugonjwa wa osteoarthritis na baridi-yabisi.
Muundo wa Viungo
Kiungo ni mahali ambapo mifupa miwili imeunganishwa. Mfuko unaonyumbuka hufunika viungo fulani vinavyolainishwa na umajimaji mzito. Mfuko huo huvilinda viungo hivyo na kuvitegemeza. (Tazama picha kwenye ukurasa wa 4.) Mfuko huo una utando wa ndani unaotokeza umajimaji huo wenye kulainisha. Ncha ya mifupa iliyomo ndani ya mfuko huo zimefunikwa kwa mfupa mwororo unaoitwa gegedu. Gegedu hiyo inazuia mifupa yako isisuguane. Nayo hulinda viungo vyako kwa kupunguza shinikizo na kwa kufanya mifupa yote ihimili shinikizo kwa usawa.
Kwa mfano, unapotembea, kukimbia, au kuruka, shinikizo kwenye viuno na magoti yako linaweza kuwa mara nne hadi mara nane ya shinikizo la uzito wako! Ijapokuwa misuli na kano za sehemu hiyo zinaweza kupunguza shinikizo hilo, gegedu husaidia mifupa yako kuhimili uzito huo inaposhinikizwa.
Baridi-Yabisi
Mtu anaposhikwa na ugonjwa wa baridi-yabisi, mfumo wa kinga wa mwili huanza kushambulia viungo vyake kwelikweli. Kwa sababu isiyojulikana, chembe nyingi za damu—kutia ndani chembe za T, ambazo ni chembe muhimu katika mfumo wa kinga wa mwili—huingia ghafula katika vitundu vya kiungo. Jambo hilo husababisha utendaji mwingi wa kemikali ambao hufanya kiungo kifure. Huenda chembe zinazotokeza umajimaji zianze kuongezeka kwa wingi sana, na kusababisha uvimbe unaoitwa pannus. Kisha uvimbe huo hutokeza vimeng’enya vinavyoharibu gegedu. Sasa kwa sababu mifupa inaweza kugusana, inakuwa vigumu kusogeza kiungo na hiyo husababisha maumivu makali sana. Misuli na kano pia hupoteza nguvu. Hiyo inafanya kiungo kianze kulegea na kuteguka kwa kadiri fulani, na mara nyingi kuharibika umbo. Kwa kawaida ugonjwa wa baridi-yabisi huathiri viwiko, magoti, na miguu kwa wakati mmoja. Asilimia 50 hivi ya wagonjwa wanaougua baridi-yabisi hupata pia uvimbe au vinundu chini ya ngozi. Wengine wana upungufu wa damu, na wanaumwa na koo na macho makavu. Uchovu na dalili za mafua, kama vile homa na maumivu ya misuli, ni dalili nyingine za baridi-yabisi.
Si wagonjwa wote wanaougua baridi-yabisi walio na dalili zilezile, na hata muda ambao wagonjwa huugua hutofautiana vilevile. Huenda mtu mmoja akaanza kuumwa na kukakamaa polepole kwa muda wa majuma kadhaa au hata miaka. Lakini mtu mwingine anaweza kuwa mgonjwa ghafula. Baadhi ya watu huugua baridi-yabisi kwa muda wa miezi michache tu kisha wanapona kabisa. Wengine wanaweza kujisikia vibaya sana wakati fulani na kujisikia nafuu wakati mwingine. Na wengine wanaugua kwa miaka mingi, wakiendelea kulemazwa.
Ni nani hasa wanaoweza kupata ugonjwa wa baridi-yabisi? Dakt. Michael Schiff anasema kwamba “hasa wanawake wa makamo wanapata ugonjwa huo.” Hata hivyo, Schiff anasema pia kuwa “mtu yeyote wa umri wowote ule, watoto, na vilevile wanaume, wanaweza kupata ugonjwa huo.” Wale walio na watu wa ukoo wenye baridi-yabisi, wanakabili hatari ya kuupata kuliko watu wengine. Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba kuvuta sigara, kunenepa kupita kiasi, na kutiwa damu mishipani huzidisha hatari ya kushikwa na ugonjwa huo.
Yabisi-Kavu Aina ya Osteoarthritis
Jarida la Western Journal of Medicine lasema kwamba “ugonjwa wa osteoarthritis hufanana na hali ya hewa kwa njia nyingi—upo kila mahali, mara nyingi hautiliwi maanani, na nyakati nyingine una athari mbaya sana.” Ugonjwa wa osteoarthritis (OA) hutofautiana na baridi-yabisi kwa kuwa hauenei hadi sehemu nyingine za mwili bali huathiri kiungo kimoja tu au viungo vichache. Gegedu inapoharibika hatua kwa hatua, mifupa huanza kusuguana. Wakati huohuo mifupa mipya inayotokeza huanza kukua karibu na kiungo. Uvimbe unaweza kutokea, na mfupa ulio chini ya gegedu huwa mzito na kuharibika umbo. Dalili nyingine za ugonjwa huo ni, vinundu kwenye viungo vya vidole, sauti ya kusugua katika viungo vilivyoathiriwa, mishtuko ya ghafula ya misuli, na vilevile maumivu, kukakamaa, na kushindwa kusogeza viungo.
Zamani, ilidhaniwa kwamba ugonjwa huo ulitokea tu kwa sababu ya uzee. Hata hivyo, wataalamu wametupilia mbali dhana hiyo ya kale. Jarida la The American Journal of Medicine lasema hivi: “Hakuna uthibitisho wowote kwamba kiungo cha kawaida kinachofanya kazi ya kawaida tu kitaharibika katika kipindi cha maisha.” Basi, kisababishi cha ugonjwa huo wa osteoarthritis ni nini? Gazeti la Uingereza la The Lancet linasema kwamba jitihada za kuelewa kisababishi cha ugonjwa huo “zimetokeza ubishi mwingi.” Baadhi ya wachunguzi wanafikiri kwamba huenda mfupa ulikuwa umejeruhiwa mbeleni bila kugunduliwa. Halafu, huenda madhara hayo yakasababisha ule ukuzi wa mfupa unaotokeza na vilevile kuharibika kwa gegedu. Wengine wanadhani kwamba ugonjwa huo huanzia katika gegedu yenyewe. Wanafikiri kwamba gegedu hiyo inapoharibika na kuchakaa, shinikizo kwenye mfupa unaokinzwa na gegedu hiyo huzidi. Mabadiliko katika viungo hutokea mwili unapojaribu kutengeneza gegedu iliyoharibika.
Ni nani hasa anayeweza kupata ugonjwa huo? Ijapokuwa si uzee unaosababisha ugonjwa huo, uharibifu wa gegedu huwaathiri hasa wazee. Wengine wanaoweza kupata ugonjwa huo ni watu ambao wana kasoro fulani katika viungo vyao, au wale wenye misuli dhaifu ya miguu na mapaja, miguu isiyo na urefu sawa, au kasoro katika uti wa mgongo. Kiungo kilichojeruhiwa katika aksidenti, au kutumia kiungo fulani kupita kiasi kazini kunaweza pia kusababisha ugonjwa huo. Baada ya uharibifu wa gegedu kuanza, kunenepa kupita kiasi kunaweza kuuzidisha.
Dakt. Tim Spector anasema hivi: “Osteoarthritis ni ugonjwa tata ambao mara nyingi husababishwa na hali ya mazingira tunamoishi lakini hurithiwa vilevile.” Hasa wanawake wa makamo na wanawake wazee walio na watu wa ukoo wenye ugonjwa huo wanakabili hatari ya kuupata. Ni watu walio na mifupa migumu hasa wanaopata ugonjwa wa osteoarthritis, tofauti na ugonjwa wa osteoporosis unaodhoofisha mifupa. Watafiti fulani wanasema pia kwamba madhara yanayosababishwa na molekuli ya oksijeni yenye idadi ya elektroni isiyogawanyika kwa mbili, na upungufu wa vitamini C na D, unaweza kusababisha ugonjwa huo.
Matibabu
Matibabu ya yabisi-kavu kwa kawaida huhusisha kutumia dawa, mazoezi ya mwili, na kubadili namna ya kuishi. Huenda tabibu wa maungo akaanzisha matibabu ya mazoezi ya mwili. Mazoezi hayo yanaweza kuhusisha mazoezi ya kukaza misuli, mazoezi yanayoboresha mfumo wa kupumua na mzunguko wa damu, kama vile kutembea au kukimbia, na mazoezi ya misuli ya kuinua vitu vizito. Mazoezi hayo yamesaidia sana kupunguza dalili nyingi kama vile uvimbe na maumivu ya viungo, unyong’onyevu, uchovu, na kushuka moyo. Mazoezi hayo hunufaisha hata wale walio wazee sana. Mazoezi yanaweza pia kuzuia kudhoofika kwa mifupa. Watu fulani wanadai kwamba maumivu yanaweza kupunguzwa kwa matibabu mbalimbali ya maungo kwa kutumia joto na baridi na kwa tiba ya vitobo.b
Kupunguza unene kunaweza kusaidia sana kutuliza maumivu ya viungo yanayosababishwa na yabisi-kavu. Inasemekana kwamba chakula kinachoweza kupunguza unene na vilevile maumivu ni chakula chenye kalisi nyingi kama vile mboga, matunda, na samaki wanaoishi katika bahari zenye maji baridi sana wenye asidi-mafuta nyingi inayoitwa omega-3. Chakula kilichotayarishwa katika viwanda na chakula chenye mafuta yenye asidi nyingi kiepukwe. Vyakula hivyo maalumu vinasaidia vipi? Inasemekana kwamba vyakula hivyo huzuia uvimbe. Wengine wanasema kwamba wamesaidiwa kwa kutokula nyama, vyakula vinavyotengenezwa kwa maziwa, ngano, na jamii ya mboga za mtunguja, nyanya, viazi, pilipili, na biringani.
Baadhi ya wagonjwa wanapendekezewa upasuaji unaohusisha kuingiza chombo fulani ndani ya kiungo chenyewe, na kuondoa utando unaotokeza vimeng’enya vinavyoharibu gegedu. Hata hivyo, mara nyingi uvimbe hurudi baada ya upasuaji huo. Upasuaji wenye matokeo ya mara moja unahusisha kuondoa kiungo kizima (mara nyingi nyonga au goti) na kuweka kiungo kingine cha bandia. Mara nyingi maumivu huisha kabisa baada ya upasuaji huo, na viungo vya bandia hudumu kwa miaka 10 hadi 15.
Hivi majuzi madaktari wamejaribu matibabu ya kuingiza asidi fulani ndani ya kiungo. Magoti hasa hutibiwa kwa njia hiyo. Kulingana na uchunguzi mbalimbali huko Ulaya, matibabu ya kuingiza umajimaji mbalimbali unaotibu gegedu yamekuwa na manufaa kwa kadiri fulani pia.
Ijapokuwa ugonjwa wa yabisi-kavu hauna dawa, kuna dawa nyingi za kutuliza maumivu na uvimbe, na yaelekea baadhi ya hizo zinaweza kuzuia kwa kadiri fulani ugonjwa usizidi. Dawa zifuatazo ni dawa ambazo hutumiwa kutuliza dalili za yabisi-kavu: Dawa za kutuliza maumivu, dawa mbalimbali za cortisone, dawa zisizo na steroidi za kutibu uvimbe (NSAID), dawa za kupunguza dalili za ugonjwa zisizo za kutuliza maumivu (DMARD), dawa zinazozuia utendaji wa mfumo wa kinga za aina mbalimbali, na dawa nyinginezo. Hata hivyo, dawa hizo zote zinaweza kuwa na athari mbaya sana. Si jambo rahisi kwa daktari na mgonjwa kuchagua dawa inayofaa.
Baadhi ya wale ambao wameugua ugonjwa wa yabisi-kavu wamewezaje kuvumilia ugonjwa huo mkali?
[Maelezo ya Chini]
a Kati ya hayo kuna ugonjwa wa osteoarthritis, baridi-yabisi, systemic lupus erythematosus (ugonjwa wa mfumo wa kinga wa mwili), ugonjwa wa baridi-yabisi wa watoto, jongo, bursitis (uvimbe wa bega au wa kiwiko cha mkono), homa ya baridi-yabisi, maradhi ya Lyme, maumivu na kudhoofika kwa kiganja cha mkono, fibromyalgia (uyabisi wa misuli na kano za mwili), ugonjwa wa Reiter, na ugonjwa wa baridi-yabisi wa uti wa mgongo.
b Gazeti la Amkeni! halipendekezi matibabu, dawa, wala upasuaji wowote. Kila mgonjwa ana daraka la kuchunguza na kuelewa manufaa na athari za matibabu yanayopatikana.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
KUNENEPA KUPITA KIASI, KUVUTA SIGARA, NA KUTIWA DAMU MISHIPANI KUNAWEZA KUZIDISHA UWEZEKANO WA KUPATA UGONJWA WA BARIDI-YABISI
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
MATIBABU YA BADALA
Dawa fulani ambazo hazipendekezwi na madaktari mara nyingi zinadhaniwa kuwa na athari chache kuliko zile za kawaida. Kati ya dawa hizo kuna protini aina ya type II collagen, ambayo baadhi ya watafiti wanasema inapunguza uvimbe na maumivu ya viungo yanayosababishwa na baridi-yabisi. Dawa hiyo inafanya kazi jinsi gani? Inazuia protini zinazosababisha uvimbe zinazoitwa interleukin-1 na tumor necrosis factor α zisiongezeke. Imeripotiwa kwamba baadhi ya virutubishi katika chakula pia vinaweza kuzuia protini hizo. Baadhi ya virutubishi hivyo ni: vitamini E, vitamini C, niacinamide, mafuta ya samaki yenye asidi nyingi aina ya eicosapentaenoic, na asidi ya gammalinolenic, mafuta ya mbegu za mmea wa borage, na mafuta ya ua la evening primrose. Huko China miti-shamba aina ya Tripterygium wilfordii Hook F, imetumiwa kwa miaka mingi. Inasemekana kwamba imesaidia baadhi ya wagonjwa wenye baridi-yabisi kupata nafuu.
[Mchoro katika ukurasa wa 4, 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KIUNGO KISICHOATHIRIWA NA UGONJWA
“BURSA”
MSULI
GEGEDU
UKANO
MFUKO WA KIUNGO
UTANDO UNAOTOKEZA UMAJIMAJI
MFUPA
UMAJIMAJI WA KULAINISHA
KIUNGO KILICHOATHIRIWA NA BARIDI-YABISI
UWAZI UNAOPUNGUA
UHARIBIFU WA MFUPA NA GEGEDU
UTANDO ULIOVIMBA UNAOTOKEZA UMAJIMAJI
KIUNGO KILICHOATHIRIWA NA UGONJWA WA “OSTEOARTHRITIS”
VIPANDE VYA GEGEDU ILIYOHARIBIKA
GEGEDU INAYOHARIBIKA
MFUPA UNAOKUA ISIVYO KAWAIDA
[Hisani]
Source: Arthritis Foundation
[Picha katika ukurasa wa 7]
Watu wenye umri wowote ule wanaweza kuathiriwa na ugonjwa wa yabisi-kavu
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mazoezi ya mwili na chakula kinachofaa kinaweza kupunguza maumivu