Maoni ya Biblia
Je, Wakristo Wanapaswa Kushiriki Desturi ya Fêng Shui?
BARANI Asia, desturi hiyo hutumiwa kuchagua makaburi. Majengo hujengwa na kupambwa kulingana na desturi hiyo. Mali hununuliwa na kuuzwa kwa kutegemea desturi hiyo. Desturi hiyo huitwa fêng shui katika Kichina, nayo ni aina fulani ya ubashiri. Japo desturi ya fêng shui imefuatwa kwa karne nyingi katika nchi za Asia, katika miaka ya karibuni imeenea katika nchi za Magharibi. Baadhi ya wasanifu-ujenzi huitumia kuunda majengo marefu, ofisi, na nyumba. Wanawake fulani huitumia kupamba nyumba zao. Vitabu na vituo vingi vya Internet huendeleza na kufundisha desturi hiyo.
Kwa nini desturi hiyo inazidi kupendwa na wengi? Kulingana na mtu mmoja anayeiunga mkono, desturi ya fêng shui, yaweza “kuboresha maisha, afya, ndoa au mahusiano, kuleta utajiri mwingi, na amani ya akili.” Ingawa mambo hayo yanatamanika, desturi hiyo ni nini hasa, na Wakristo wanapaswa kuiona kwa njia gani?
Desturi Hiyo Ni Nini?
Maneno ya Kichina fêng shui humaanisha “upepo-maji” yanapotafsiriwa neno kwa neno. Desturi ya fêng shui ilianza maelfu ya miaka iliyopita wakati falsafa nyingi za Mashariki zilipobuniwa. Falsafa moja ilikuwa juu ya usawaziko wa kanuni ya yin na kanuni ya yang (giza na nuru, joto na baridi, mabaya na mazuri). Wazo la yin na yang liliunganishwa na wazo la chʼi, ambalo likitafsiriwa neno kwa neno linamaanisha “hewa” au “pumzi.” Kanuni ya yin, yang, na chʼi, pamoja na vile vitu vitano vya asili, yaani, mbao, udongo, maji, moto, na metali, ni muhimu sana katika dhana ya fêng shui. Watu wanaofuata desturi ya fêng shui huamini kwamba nishati yenye nguvu hupita kwenye maeneo yote. Kusudi la desturi hiyo ni kutambua mahala ambapo inawezekana kusawazisha nishati, au chʼi, ya nchi kavu na anga. Hilo huwezekana kwa kufanya mabadiliko fulani ndani ya jengo au kwenye eneo lenyewe. Inadhaniwa kwamba watu wanaofanya kazi au kuishi mahala ambapo mabadiliko hayo hufanywa, hupata mafanikio kupitia usawaziko huo.
Kwa kawaida, wabashiri wa desturi ya fêng shui hutumia dira ya kubashiri.a Hiyo ni dira ndogo ambayo huwekwa katikati ya chati ya unajimu. Dira hiyo imechorwa duara zenye kitovu kimoja ambazo zimegawanywa na mistari. Dira hiyo ina habari kuhusu makundi ya nyota, majira, na wakati ambapo utendaji muhimu wa jua hujirudia-rudia. Jengo au eneo fulani linapokaguliwa, habari mbalimbali zinazoonyeshwa kwenye dira hiyo hurekodiwa. Mbashiri wa fêng shui hutazama mahala ambapo dira inakutana na mistari na duara za nje. Kisha, kwa kutumia habari hiyo anatambua kinachohitajiwa ili “kutibu” eneo hilo.
Mandhari ya eneo, mito, mabomba ya maji machafu, na mpangilio wa madirisha na milango katika jengo unaweza kutiliwa maanani wakati wa kusawazisha eneo fulani la ujenzi. Kwa mfano, mwuza-duka mmoja huko Kanada alitundika kioo kwenye mlango wa nyuma wa duka lake kwa sababu milango haikuwa mahala panapofaa. Ili kusawazisha jengo au chumba, huenda mbashiri akapendekeza mimea au fanicha ihamishwe, kubadilisha picha, kuweka kengele ndogondogo ambazo hulia zinapopigwa na upepo, au kuweka chombo cha kufuga samaki.
Maoni ya Kikristo
Maktaba nyingi huorodhesha vitabu vya fêng shui pamoja na vitabu vya unajimu na ubashiri. Hata vitabu fulani vya marejeo hufafanua ubashiri kuwa uaguzi wa kutumia namba au mistari au mandhari za kijiografia. Hivyo, watu wengi hukubali kwamba desturi ya fêng shui ni aina fulani ya ubashiri. Inahusisha uaguzi na mazoea ya kuwasiliana na roho waovu ambayo yalianza kale.
Waisraeli walipotoka Misri na kuingia mwishowe katika nchi ya Kanaani katika karne ya 15 K.W.K., uaguzi wa kila aina ulikuwa umeenea sana katika nchi hizo mbili. Kama ilivyoandikwa kwenye Kumbukumbu la Torati 18:14, Mungu alisema hivi kupitia Musa: “Mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao [“wanaotumia uaguzi,” Zaire Swahili Bible]; bali wewe, BWANA, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.” Aina nyingi za uaguzi za Misri na Kanaani zilianza katika Babiloni ya kale. Yehova alipovuruga lugha ya watu wa Babiloni, watu hao walisambaa kwenye sehemu nyingine, na wakaendeleza desturi hizo za Babiloni za uaguzi na za kuwasiliana na roho waovu mahala walipokwenda.—Mwanzo 11:1-9.
Yehova Mungu aliwaonya vikali Waisraeli tena na tena kwamba wasifuate desturi za uaguzi za mataifa mengine, kwa kusema hivi: “Asionekane kwako mtu . . . atazamaye bao [“anayetumia maaguzi,” ZSB] wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri . . . Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.” (Kumbukumbu la Torati 18:9-12; Mambo ya Walawi 19:26, 31) Watu walioshiriki desturi ya uaguzi walipaswa kuuawa.—Kutoka 22:18; Mambo ya Walawi 20:27.
Mbona uaguzi ulishutumiwa vikali hivyo? Andiko la Matendo 16:16-19 husema kuhusu mwanamke aliyekuwa na “roho mwovu wa uaguzi.” Naam, uaguzi unahusiana kabisa na ibada ya roho waovu. Hivyo, mtu anaposhiriki aina yoyote ya uaguzi anashirikiana na Shetani na mashetani wake! Jambo hilo laweza kumwangamiza kiroho.—2 Wakorintho 4:4.
Huenda hapo awali mitindo fulani ya mapambo na ya kutengeneza bustani, ya Mashariki au Magharibi, ilihusiana na desturi za dini za uwongo kama vile fêng shui. Hata hivyo, mitindo mingi kama hiyo imeacha kuhusianishwa na dini. Ingawa hivyo, kutumia desturi ya fêng shui ili kubashiri mambo ya wakati ujao au kupata bahati njema au afya njema ni kuvunja sheria ya Mungu waziwazi. Kufanya hivyo ni kuvunja amri ya Biblia iliyo wazi ya kuepuka kugusa kitu chochote “kisicho safi.”—2 Wakorintho 6:14-18.
[Maelezo ya Chini]
a Katika nchi za Magharibi, wabashiri wamejaribu kufanya desturi ya fêng shui ionekane kuwa ya kisayansi. Wengine hata hutumia kompyuta ili ziwasaidie kukagua maeneo mbalimbali.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Dira ya kubashiri
[Hisani]
Ukurasa wa 2 na wa 23: Hong Kong Tourism Board