Waridi Maridadi Kutoka Afrika
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA
“Ndiyo maua yenye kuvutia zaidi ambayo nimewahi kuona!” “Zawadi bora zaidi unayoweza kumpa rafiki mpendwa.” “Ni njia ya kusema, ‘Mtu fulani anakujali.’”
HUENDA una maoni kama hayo yaliyoonyeshwa hapo juu ya wakazi wa Nairobi, Kenya. Huenda hakuna ua maarufu ulimwenguni kuliko waridi kati ya mimea yote ya maua ambayo inakua msituni na inayokuzwa na watu. Ua hilo limewazuzua wanadamu kwa karne nyingi. Washairi wameandika kulihusu nao wasanii wamelichora mara nyingi. Mwandishi Shakespeare alilisifu kwa maneno haya yanayojulikana sana katika kitabu Romeo and Juliet: “Jina ni muhimu kadiri gani? Kile tunachokiita waridi bado kingenukia vizuri hata kama kingeitwa kwa jina lingine lolote.” Waridi limesaidia kuanzisha urafiki na kuuimarisha, limepatanisha watu waliotofautiana, nalo limewatia moyo wagonjwa wengi.
Kuongezea mambo hayo, waridi lina faida kubwa za kiuchumi. Katika nchi nyingi ambako hali ya hewa ni nzuri kwa ukuzaji wa maua, ua la waridi husaidia sana nchi hiyo kupata pesa za kigeni. Kwa mfano, katika mwaka mmoja hivi karibuni zaidi ya asilimia 70 ya mamilioni ya maua yaliyosafirishwa kutoka nchini Kenya yalikuwa ya waridi na hivyo kuifanya Kenya kuwa moja ya nchi zinazokuza waridi zaidi ulimwenguni.
Zamani, kabla wanadamu hawajagundua sifa zenye kupendeza za ua hilo, mimea ya waridi ilikuwa ikiota porini. Leo, mbinu za kuchanganya zaidi ya aina 100 za mbegu za maua ya waridi ya mwituni zimetokeza maelfu ya aina za waridi zinazojulikana. Kwa sababu hiyo, ua hilo limekuwa maarufu ulimwenguni pote na linapatikana katika karibu kila nchi duniani. Ua la hybrid tea rose ndilo linalojulikana na kupandwa zaidi duniani.
Kutoka Shambani Hadi Nyumbani
Watu wengi hununua waridi kutoka kwa wauzaji wa maua au dukani. Maua hayo hukuzwa katika mashamba makubwa na yanahitaji uangalifu mkubwa kuliko yale yanayopandwa katika bustani ya nyumbani. Tulipotembelea shamba moja karibu na Nairobi tuliona uangalifu wa ziada unaohitajika kutayarisha maua hayo ili yauzwe.
Huko, kama katika maeneo mengine ya Kenya, mabanda ya kukuzia maua yanatambulisha shamba kubwa la kukuzia maua ya waridi. (Ona picha kwenye ukurasa wa 26.) Mabanda hayo hutumiwa kwa makusudi mengi. Maua ya waridi yaliyopandikizwa karibuni yanahitaji kulindwa kutokana na hali mbaya ya hewa. Mvua kubwa, upepo, au jua linapoyapiga moja wa moja linaweza kuyaharibu. Ili kudumisha hali sawa ya joto, ni muhimu kwamba hewa baridi iingizwe ndani ya mabanda hayo kwa urahisi na hewa yenye joto iondolewe.
Ndani ya mabanda ya kukuzia maua hayo kuna mistari ya maua yaliyo katika hatua mbalimbali za ukuzi. Katika shamba hilo aina mbalimbali za waridi hukuzwa, kuanzia ua maarufu linaloitwa hybrid tea rose, lenye urefu wa sentimita 70 hivi, kufikia ua linaloitwa sweetheart rose lenye urefu wa sentimita 35 ambalo limezalishwa kutokana na waridi linaloitwa tea rose. Ekari mbili na nusu za shamba hilo zinaweza kuwa na mimea 70,000 hivi.
Mimea hiyo hupataje virutubisho? Udongo wa kawaida hautumiwi. Maua hayo hukuzwa kwenye mawe ya volkano yaliyolazwa juu ya karatasi za plastiki. Hiyo ndiyo mbinu inayofaa zaidi kwani mawe hayo hayana magonjwa mengi yanayopatikana katika udongo. Mbinu fulani ya kunyunyizia maji hutumiwa ili kuipatia mimea maji. Katika mbinu hiyo, mabomba madogo yanaelekezwa kwenye maua na kutoa maji na virutubisho kwa kiwango kinachofaa. Udongo huo wa volkano una matundu madogo-madogo yanayoweza kuruhusu maji yapite, yakusanywe, na kutumiwa tena.
Licha ya utunzaji wa hali ya juu unaotolewa, maua ya waridi yanaweza kuambukizwa magonjwa mbalimbali, hasa yale yanayosababishwa na kuvu. Yanatia ndani botrytis na ukungu, ambao huvamia majani na mashina ya mimea. Yasipochunguzwa, magonjwa hayo yanaweza kuathiri ubora wa maua. Kutumia dawa za kuua wadudu husaidia kudhibiti tatizo hilo.
Wakati unapopita, rangi fulani nyangavu huanza kutokea, na hilo huonyesha wazi kwamba maua ya waridi yako tayari kuchumwa. Maua hayo hukatwa kwa uangalifu kabla matumba hayajafunguka. Wakati huo bado petali huwa hazijafunguka. Yanapochumwa wakati huo, hayanyauki upesi na vilevile rangi yake hudumu kwa muda mrefu. Hata hivyo, huenda wakati wa kuchumwa ukatofautiana kwa kutegemea aina ya ua. Ni muhimu kuchuma maua hayo asubuhi au jioni, wakati ambapo kuna unyevu na hayanyauki upesi. Maua yaliyochumwa hupelekwa kwenye chumba cha baridi ambako yanapunguzwa joto. Hilo pia huhakikisha kwamba maua hayo yanadumu kwa muda mrefu zaidi yakiwa yanapendeza.
Baada ya hapo maua yatapitia hatua nyingine muhimu ya kupangwa. Katika hatua hii yatatenganishwa kulingana na rangi na ukubwa. Maua yanafungwa kulingana na matakwa ya mnunuzi. Mwishowe, maua yako tayari kuuzwa. Kutoka katika shamba hilo yanapelekwa hadi uwanja mkuu wa ndege jijini Nairobi, na kutoka hapo yatasafirishwa hadi Ulaya, umbali wa maelfu ya kilomita. Kwa sababu maua huharibika haraka, lazima yafikishwe sokoni ndani ya muda wa saa 24 baada ya kuvunwa, iwe soko hilo ni la karibu au la kimataifa.
Kwa hiyo, wakati ujao ukipokea zawadi ya maua au ukiyanunua, tua ufikirie mwendo mrefu ambao yamesafiri, huenda hata ni ya Afrika. Labda hilo litakufanya umthamini zaidi Muumba, Yehova Mungu.—Zaburi 115:15.
[Sanduku/ Picha katika ukurasa wa 26]
Kutakuwa na Waridi la Bluu?
Maua ya waridi yamebadilika sana na kuna aina nyingi mpya zinazovumbuliwa. Mbinu mpya za kuchanganya mbegu zimeanza kutumiwa. Ni maua machache yaliyo na rangi nyingi kama ua la waridi. Wewe unapendezwa na rangi gani zaidi? Je, ni rangi nyeupe, waridi, nyekundu iliyoiva, au nyekundu nzito? Rangi nyingi kati ya hizo zimetokezwa kwa kutumia mbinu mbalimbali za kuchanganya mbegu.
Kwa mfano, je, ulijua kwamba hata ingawa watu huzungumzia ua “jekundu” la waridi, ukweli ni kwamba hakukuwa na maua mekundu ya waridi? Jamii hiyo haikuwa na chembe za urithi zinazotokeza rangi nyekundu. Rangi nyekundu ilitokana na mabadiliko ya chembe za urithi mnamo 1930, na hilo mwishowe limetokeza maua mekundu ya waridi tunayoona leo. Kati ya aina zote za waridi hakukuwa na yoyote ya rangi ya bluu. Chembe za urithi za kiasili zinazotokeza rangi ya bluu, delphinidin, hazipatikani katika jamii ya waridi. Hata hivyo, baada ya miaka mingi ya ushirikiano wa kufanya utafiti kati ya kampuni ya Australia na ya Japani, ua la waridi la “bluu” lilitokezwa mnamo 2004 kwa kubadili maumbile ya chembe za urithi. Hata hivyo, kazi nyingi zaidi inahitajiwa ili kutokeza ua lenye rangi ya bluu zaidi.
[Picha]
Banda la kukuzia maua
[Picha katika ukurasa wa 25]
Tayari kuchumwa