Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/8 kur. 16-18
  • Maua Huonyesha Kwamba Mtu Fulani Anajali

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maua Huonyesha Kwamba Mtu Fulani Anajali
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vibanda vya Kuoteshea Vilivyofunikwa na Plastiki na Maziwa Bandia
  • Ukuzaji Wapangwa Kimbele
  • Kazi Ngumu Katika Msimu wa Uhitaji
  • Ujumbe Wenye Kupendeza na Wenye Harufu Nzuri
  • Yule Ambaye Hujali Kikweli
  • Waridi Maridadi Kutoka Afrika
    Amkeni!—2007
  • Ni Maridadi na Matamu!
    Amkeni!—2004
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • “Tupeleke Kadi”
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/8 kur. 16-18

Maua Huonyesha Kwamba Mtu Fulani Anajali

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KOLOMBIA

MTOTO mchanga aliyevutiwa akusanya shada la maua aina ya kombemtindi katika viganja vyake vinene vilivyokunjwa na kumkimbilia mama akiwa na maua hayo yenye thamani aliyopata. Kwenye kibanda cha kando ya barabara, mume mwenye upendo achagua makumi ya waridi kwa ajili ya mke wake, ili kumwonyesha jinsi anavyojali. Mwana mwenye uthamini apigia simu mwuzaji maua wa ujiranini ili apate maua aina ya dalia zilizokatwa karibuni amfurahishe mama yake. Mke-nyumbani mwenye ujitoaji aweka shada la maua yenye rangi nyingi aina ya “carnation” katika kigari cha kuwekea vitu alivyonunua dukani. Yataongezea mambo machache kwa nyumba yake iliyopambwa vyema.

MAUA huchangamsha mioyo ya wachanga na vilevile wazee. Hayo ni njia nzuri sana ya kuwasilisha hisia ya kwamba “Mtu fulani anajali.” Methali moja ya Kihispania husema: “Yeyote asiyekuwa na shukrani kwa waridi hatakuwa na shukrani kwa chochote.” (Quien no agradece una rosa, no agradecerá ninguna cosa.)

Mauzo ya maua yanaongezeka kwa haraka sana kuliko wakati uliopita. Katika muhula huu wa uchukuzi wa hewani wenye haraka, maua yaweza kukuzwa mbali sana na maduka, maduka makubwa, na vibanda vya kando ya barabara ambapo huvutia macho ya wapita-njia. Gazeti Time lilitaarifu kwamba biashara ya maua “inaongezeka haraka na kubadilika haraka hata zaidi: yanakuzwa zaidi sana katika kizio cha kusini—hasa Kolombia, ambayo imekuja kuwa mwuzaji-nje wa pili mkubwa zaidi kufuatia Holland.”

Vibanda vya Kuoteshea Vilivyofunikwa na Plastiki na Maziwa Bandia

Ikiwa na zaidi ya miaka 25 katika biashara hii, Kolombia huongoza ulimwenguni katika uuzaji-nje wa maua aina ya carnation, huku ikiwa ya pili kwa mauzo ya jumla ya maua. Katika 1964 mwanafunzi wa chuo kikuu katika California, Marekani, alifanya uchunguzi wa kompyuta ili kupambanua mahali palipo na mazingira yafaayo kwa ukuzaji wa maua wakati wote mwakani. Alipata kwamba tabia ya nchi na kimo cha bonde la uwanda wa juu ambapo mji wa Bogotá upo, kaskazini tu ya ikweta na karibu futi 9,000 juu katika Milima Andes, palikuwa na hali zifaazo.

Savana ya kijani sana ya Santa Fe de Bogotá, ambapo asilimia 92 ya ukuzaji wa maua ya kuuzwa nje katika Kolombia upo, kumetapakaa maziwa bandia na vibanda ya kuoteshea vilivyofunikwa na plastiki. Ndani ya vibanda hivi vilivyotengenezwa kwa mbao na fremu za chuma, mazingira ya wakati wa masika yaliyodhibitiwa kwa uangalifu huwezesha ukuzi wa mamilioni ya carnation, dalia, waridi, kipangusi, alstroemerias, na namna nyinginezo nyingi, ambazo baada ya muda mfupi zitakatwa na kupakiwa kwa ajili ya kusafirishwa hadi Amerika Kaskazini, Ulaya, na Asia.

Halijoto kwa ajili ya ukuzaji wa maua huanzia kati ya digrii 18 hadi 20 Selsiasi, halijoto ya kawaida ya mchana wakati wote mwakani katika savana. Hapa, kuna maji mengi ya mvua, udongo una rutuba sana, na kuna wafanyakazi wa vibarua wanaolipwa kwa gharama ya chini. Wakati wa usiku, halijoto zaweza kushuka hadi karibu kiwango cha ugandaji na mara kwa mara hadi digrii mbili Selsiasi chini ya sufuri. Vyungu vyenye kutoa moshi, balbu za taa zenye nguvu nyingi, au mirashi hulinda dhidi ya baridi. Balbu hizo za taa pia hutumika kuongezea saa za mchana, hivyo ikifanya mimea fulani ibaki ikiwa yenye utendaji na kuharakisha ukuzi wayo.

Ukuzaji Wapangwa Kimbele

Zaidi ya wafanyakazi 120,000 katika Kolombia huhusika katika hatua fulani ya biashara ya maua. Miongoni mwao mna Mashahidi wa Yehova wengi ambao huishi katika jumuiya zilizotapakaa katika savana. Benito Quintana, mzee Mkristo katika moja ya makutaniko yaliyoko Facatativá, hufanya kazi akiwa msimamizi wa utokezaji katika bustani moja. Yeye aeleza: “Miezi kadhaa mapema, ni lazima tupange utokezaji ili utosheleze mahitaji ya soko ya kimsimu. Mimea ambayo kutoka kwayo maua ya carnation hukua huletwa kutoka Uholanzi au Italia, dalia kutoka Florida. Wanawake hukata machipukizi madogo kwa uangalifu, wakiyapanda katika mafungu ya mchanga yaliyopigwa safu katika kibanda cha kuoteshea chenye ujoto ambapo hutiwa maji na ukungu ulio kama wingu hadi yanapotia mizizi. Dalia huchukua siku 12 kwa digrii 20 hadi 35 Selsiasi, kukiwa na saa za ziada za nuru wakati wa usiku. Maua ya carnation huchukua siku 23 kwa halijoto ya kati ya digrii 15 hadi 25 Selsiasi, bila nuru wakati wa usiku. Kisha sisi huhamisha mimea midogo hadi kwenye mashamba katika vibanda vingine vya kuoteshea ambapo hurutubishwa, kufukizwa, na kutiwa maji hadi inapochanua maua, miezi sita baadaye kwa carnation na miezi mitatu kwa dalia.”

Kazi Ngumu Katika Msimu wa Uhitaji

Wakati wa kukata maua ufikapo, ni wanawake wafanyao kazi hiyo vyema zaidi, yapendekezwa bila glavu na kwa mikono safi sana. Mashine haziwezi kuamua kiwango ambacho machipukizi yamefunuka au kunyooka kwa mashina, mambo ambayo huamua ubora wa ua.

Judith Corredor, kutoka Facatativá, aeleza: “Wanawake wana subira na mguso mwororo na vilevile kasi na ustadi uhitajiwao. Tuingiapo katika vibanda vya kuoteshea mchana,” Judith aendelea, “savana mara nyingi huwa imefunikwa na ukungu; kwaweza kuwa na baridi sana, hata kufikia kuganda. Wasichana wengi huvaa skafu. Wakati wa mchana kunakuwa na joto, nyakati fulani hata kufikia digrii 32 selsiasi. Ni kazi ngumu hasa katika msimu wenye shughuli nyingi wakati tunaharakishwa na kulazimika kufanya ovataimu.”

Ujumbe Wenye Kupendeza na Wenye Harufu Nzuri

Baada ya kukatwa, maua hayo hupelekwa kwenye chumba cha pekee ambapo kuna hewa na nuru nyingi. Hapa, wanawake huchagua na kuainisha maua kulingana na ubora wa michanuo na jinsi yalivyonyooka, unene, na urefu wa mashina. Kisha maua hayo hufungwa katika plastiki iwezayo kupenywa na nuru, maua 25 katika kila shada, tayari kwa upakizi. Yaliyo bora zaidi ndiyo huteuliwa kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi.

Wanaume hupakia maua hayo katika visanduku vya kipekee vyenye mikunjo-kunjo vilivyo na jina la bustani yalipokuzwa—mashada 24 ya carnation, kwa kisanduku. Ndugu ya Benito, Alejandro Quintana, ambaye hufanya kazi katika upakizi, asema: “Ni lazima tufanye kazi haraka, kwa kuwa maua ni miongoni mwa mazao yaharibikayo upesi sana. Kampuni yetu ina pampu mbili ambazo huvuta hewa yenye ujoto kutoka visanduku hivyo, visanduku 112 kwa wakati mmoja, huku zikishindilia hewa baridi kwa muda wa saa mbili, hivyo zikishusha halijoto ya maua hadi digrii chache juu ya kuganda. Kisha matundu katika visanduku hivyo yazibwa, na maua yawekwa mahali palipo baridi hadi yanapoingizwa katika malori kwa ajili ya kusafirishwa hadi uwanja wa ndege.”

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa El Dorado wa Bogotá, maua hayo hupitia uchunguzi wa usafirishaji wa kwenda nje kisha huhifadhiwa mahali palipo na baridi kwa saa chache hadi bidhaa hizo ziingizwapo katika ndege kubwa ili kusafirishwa hadi mahali pa usabambazaji ng’ambo. Kwa kipindi cha siku chache tu, maua haya yatakuwa yakifunua petali zayo katika nyumba, maofisi, vyumba vya wagonjwa, na mahali penginepo, yakiwasilisha ujumbe wenye kupendeza na wenye harufu nzuri kwamba mtu fulani anajali.

Yule Ambaye Hujali Kikweli

Karibu kila mahali tuendapo duniani, tunapata maua kwa ajili ya furaha yetu. Hayo hupatikana katika milima yenye kimo cha juu kwenye kingo za nyanda zenye barafu na barafuto, katika misitu na nyanda zenye nyasi, kandokando ya vijito na mito, kando ya ufuo wa bahari, na hata katika majangwa yenye joto, yaliyokauka. Maua yamekuwapo hapa wakati mrefu kabla ya mwanadamu kutokea duniani. Wanabotania husisitiza kwamba ‘mimea yenye kuchanua maua ndiyo msingi wa uhai wote wa mnyama na mwanadamu. Bila hiyo, wanyama na mwanadamu hawangeweza kuwapo.’

Kwa ufahamu wenye kina, Mfalme Sulemani alitangaza: ‘Mungu amefanya kila kitu kizuri kwa wakati wake.’ (Mhubiri 3:11) Hii yatia ndani zawadi ya Mungu ya maua katika namna zayo zote na uzuri. Tangu wakati usiojulikana yamechangamsha mioyo ya wachanga na vilevile wazee. Kwa hakika, Mungu hujali kweli!

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Kufanya Maua Yadumu Muda Mrefu Zaidi

• Kata mashina kimlazo chini ya maji kabla ya kuyaweka katika chungu cha kuwekea maua. Matone ya maji yajishikanishayo kwenye ncha za mashina yazuia hewa kuingia hivyo yakizuia kuingia kwa maji na virutubisho tena.

• Gazeti GeoMundo hunukuu wakulima wa bustani wa Kolombia wakisema kwamba tembe ya aspirin, kijiko kidogo cha sukari, au cola kidogo iliyoongezwa kwenye maji itafanya maua yadumu kwa muda mrefu yakiwa katika hali nzuri. Badilisha maji baada ya kila siku mbili au tatu, ukitumia maji safi yaliyo na halijoto ya chumba, ingawa maji yenye ujoto yaweza kutumiwa kufanya machipukizi yafunuke upesi zaidi.

• Michanuo iliyonyauka kidogo yaweza kuhuishwa kwa kutumbukiza mashina katika maji ya moto kwa dakika kumi huku ukinyunyizia petali maji baridi. Weka maua mbali na vyanzo vya joto, mbali na chombo cha kusawazisha mwingio wa hewa, na mbali na nuru ya jua ya moja kwa moja.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki