Popo Mdogo Zaidi Ulimwenguni
● Katika mwaka wa 1973, mwanabiolojia Kitti Thonglongya wa Thailand, akiwa na kikundi chake kwenye mapango fulani karibu na poromoko la maji la Sai Yok, walikusanya zaidi ya popo 50 ambao hawakujulikana. Aliwapeleka popo kadhaa kwa Dakt. J. E. Hill kwenye Jumba la Makumbusho la Uingereza la Historia ya Asili huko London. Kwa kusikitisha, Kitti alikufa kabla ya kujua kwamba alikuwa amegundua jamii mpya ya popo, ambayo Hill aliiita Craseonycteris thonglongyai kwa heshima ya Kitti. Jina linalojulikana sana ni popo wa Kitti mwenye pua ya nguruwe.
Akiwa na urefu wa milimita 30 hivi na mabawa yenye upana wa milimita 127 hivi kuanzia ncha ya bawa moja hadi lingine, popo huyo ndiye mdogo zaidi anayejulikana duniani na ni mmoja kati ya wanyama wadogo zaidi wanaonyonyesha. Ni mdogo sana hivi kwamba nyakati nyingine amelinganishwa na nyuki. Sifa nyingine zinazomtambulisha ni pua yake inayofanana na ya nguruwe (kama jina lake linavyoonyesha), hana mkia, na ana masikio makubwa na mfereji wa sikio uliovimba.
Wanaishi Katika Eneo Dogo
Popo hao wanaweza kupatikana tu katika Mbuga ya Taifa ya Sai Yok nchini Thailand na katika maeneo ya karibu ya Myanmar. Kama popo wa aina nyingine, popo wa jamii hii hutegemea mawimbi ya sauti wanapowinda wadudu. Akiwa na mabawa marefu sana yanapolinganishwa na mwili wake, popo huyo anaweza kuelea angani bila kusonga, jambo linaloweza kumsaidia kukamata chakula chake katikati ya miti yenye majani mengi. Anapopumzika, popo huyo hupendelea sehemu za juu za mapango ya mawe ya chokaa yaliyoinuka juu sana na yenye sehemu nyingi, maeneo yenye ulinzi na yanayomsaidia asipoteze joto la mwili sana, jambo muhimu kwa wanyama wadogo wanaonyonyesha wenye damu moto. Kwa kweli, Muumba aliwapa viumbe hawa wadogo hisi na uwezo wa ajabu sana!—Ufunuo 4:11.
Kwa kuwa popo huyo wa Kitti mwenye pua ya nguruwe hapatikani kwa urahisi na anaishi katika eneo dogo sana, anakabili hatari ya kutoweka ikiwa hali hazitabadilika ziwe nzuri zaidi. Jitihada zaidi zinafanywa za kumlinda, lakini ukataji wa miti, ujenzi wa barabara, na utalii unamhatarisha. Tunasubiri tuone kama huyo mnyama mdogo anaweza kuokoka uvamizi wa wanadamu katika eneo lake dogo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]
MKUBWA ZAIDI NA MDOGO ZAIDI
Kuna zaidi ya aina 1,000 za popo, nao ndio wanyama wanaonyonyesha pekee ambao wanaweza kupaa. Popo wakubwa zaidi (1), wanaoitwa nundu, wanaweza kuwa na mabawa yenye upana wa zaidi ya mita 1.5 kutoka ncha ya bawa moja hadi lingine na uzito wa kilogramu moja hivi. Kwa kulinganisha, popo wa Kitti mwenye pua ya nguruwe (2) ana mabawa yenye upana wa sentimita 13 hivi kutoka ncha moja hadi nyingine na uzito wa gramu 2 tu.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
Photos: © Merlin D. Tuttle, Bat Conservation International, www.batcon.org