Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 6/11 kur. 16-18
  • Svaneti—Eneo la Milimani Lenye Minara

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Svaneti—Eneo la Milimani Lenye Minara
  • Amkeni!—2011
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutembelea Eneo Hilo
  • Watu Wanaoishi Huko
  • Kuishi Ndani ya Mnara
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2011
  • Barafu Juu ya Ikweta
    Amkeni!—2005
  • Georgia—Urithi wa Kale Uliohifadhiwa
    Amkeni!—1998
  • Matterhorn wa Kipekee
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2011
g 6/11 kur. 16-18

Svaneti​—Eneo la Milimani Lenye Minara

TUKIWA tumeegemea mbele, huku tukishikilia kwa nguvu mihimili ya paa, tulitazama nje kutoka juu ya mnara wa mawe uliojengwa miaka 800 iliyopita huko Georgia. Tukiwa tumesimama hapo mita 25 hivi kutoka ardhini, tuliona minara mingine mingi ya kale ikiwa imetapakaa katika kijiji cha Mestia, mji mkuu wa eneo la Svaneti.

Tulizungukwa na milima mikubwa yenye vilele vyenye theluji na bonde lenye miteremko iliyofunikwa kwa nyasi za kijani. Tulivutiwa sana na eneo hilo la kale, tukajihisi ni kana kwamba tunaishi tena katika Enzi za Kati. Kwa kweli, lengo moja la safari yetu lilikuwa kutembelea minara ya Svaneti inayojulikana sana.

Kutembelea Eneo Hilo

Safari yetu ya kutembelea eneo hilo la milimani la Svaneti ilianzia huko Zugdidi, Georgia, karibu na Bahari Nyeusi. Hakukuwa na mawingu asubuhi hiyo, kwa hiyo tungeweza kuona vilele vyeupe maridadi kutoka Tbilisi. Tulipofika kwenye korongo lililozunguka Mto Inguri, tulianza kupanda. Eneo hilo lenye msitu lilikuwa na maua mengi ya mwituni.

Kufikia jioni, kikundi chetu kilikuwa kimefika kwenye kijiji cha Becho kilicho na mandhari maridadi. Kijiji hicho kiko chini ya Mlima Ushba unaopendeza sana ulio na minara miwili ya matale. Kama vile tu nondo huvutiwa na moto wa mshumaa, watu wanaopenda kukwea milima huvutiwa na vilele vyenye barafu vya Mlima Ushba. Mlima huo una kimo cha mita 4,710 na inasemekana kwamba unafanana na Mlima Matterhorn huko Uswisi.

Tukiwa na njaa na uchovu kutokana na safari, tulinunua kondoo kutoka kwa mchungaji mmoja kwa ajili ya chakula chetu cha jioni. Muda si muda, tukiwa tumeketi kando ya moto, tulifurahia ukarimu wa marafiki wetu Wasvan waliotupatia mtsvadi, au mshikaki. Chakula hicho kililiwa pamoja na mkate uliookwa katika jiko la udongo linalotumia kuni. Baada ya mlo, tulifurahia kunywa Saperavi, divai nyekundu inayotengenezwa huko Georgia.

Asubuhi iliyofuata, tulisafiri hadi Mestia. Hapo ndipo tulipotazama kutoka kwenye mnara uliotajwa mwanzoni mwa habari hii, na tukakata kauli kwamba Svaneti ni mojawapo ya maeneo ya milimani maridadi zaidi ulimwenguni. Kilomita 45 hivi kutoka Mestia, kuna kijiji cha Ushguli, kilicho juu kabisa milimani. Wanakijiji hao wanaishi eneo lililo mita 2,200 juu ya usawa wa bahari. Kijiji cha Ushguli kimetajwa kuwa “ndicho kijiji cha Ulaya kilicho juu zaidi ambacho hakijawahi kukosa wakazi.”

Ili kufika kwenye kijiji hicho, tulipitia barabara nyembamba isiyo na watu iliyojipindapinda milimani, na kando yake kulikuwa na jabali lenye mteremko mkali hadi kwenye mto uliokuwa chini. Hatimaye tulipofika Ushguli, tuliona mandhari maridadi ajabu. Nyumba kadhaa zilikuwa zimezunguka minara ya kale. Nyuma yake kulikuwa na Mlima Shkhara ambao ni mkubwa sana. Mlima huo maridadi uliokuwa umefunikwa kwa theluji ulionekana waziwazi kwenye anga la bluu.

Mlima Shkhara ulio na kimo cha mita 5,201 juu ya usawa wa bahari ndio mlima mrefu zaidi nchini Georgia, na ni sehemu ya ule unaoitwa Ukuta wa Bezengi, ambao ni mstari wa vilele ambavyo vimeenea kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 12 vinavyokaribia kimo cha Mlima Shkhara. Vilele hivyo ni sehemu ya safu ya milima ya Greater Caucasus yenye urefu wa kilomita 1,207. Kila mahali tulipotazama tuliona mabonde yenye nyasi na mimea mingi iliyokuwa na mandhari yenye kuvutia sana. Hata hivyo, mtu hawezi kufika kwenye mabonde hayo isipokuwa awe jasiri sana au awe mwenyeji wa Svaneti.

Watu Wanaoishi Huko

Wasvan wanaoishi sehemu ya Juu ya Svaneti wamekuwapo tangu zamani na wana lugha yao. Kwa muda mrefu wamejulikana kuwa watu ambao walikataa kutawaliwa na bwana yeyote. Katika karne ya 18, mvumbuzi mmoja alisema kwamba Wasvan walikuwa “wamefanyiza jamii bora ambapo uhuru wa mtu wa kuchagua ulipita mambo mengine yote.”

Mambo mawili yamechangia uhuru huo wa pekee wa watu wa Svaneti. Kwanza, safu za milima mirefu sana zimewatenga na ulimwengu na kuwalinda na wavamizi. Pili, minara ililinda uhuru wa kila familia. Iliwalinda kutokana na maadui na watu kutoka katika vijiji jirani ambao nyakati nyingine walikuwa na uhasama, na pia iliwalinda kutokana na maporomoko ya theluji ambayo yalifunika majengo madogo.

Kuishi Ndani ya Mnara

Tulialikwa tutembelee mnara wa familia moja ya Wasvan ambao ulijengwa katika karne ya 12. Ngome hiyo ilikuwa na sehemu mbili kuu—mnara wenyewe unaoitwa murkvam, na nyumba iliyounganishwa nao, inayoitwa kor. Kwenye orofa ya kwanza ya nyumba hiyo, kuna mahali pakubwa pa kuwashia moto ili kutoa mwangaza na joto. Pia kuna kiti cha mbao cha mzee wa ukoo, ambaye alisimamia familia yake yote kutia ndani mke wake, wana wake, na wake zao. Kila mwanamke alikuwa na zamu ya kufanya kazi za nyumbani. Kazi hizo zilitia ndani kusaga unga, kuoka mkate, kudumisha usafi, kuwalisha wanyama, na kuhakikisha kwamba moto hauzimiki.

Mnara huo mkubwa ulitengenezwa kwa mawe na kupigwa plasta kwa chokaa ngumu. Ulikuwa na orofa nne. Orofa hizo zilikuwa juu ya nyumba yenye orofa mbili iliyokuwa sehemu ya mnara huo. Tulipoingia kwenye mnara kupitia kwa nyumba hiyo, ilichukua muda kwa macho yetu kuzoea mwangaza hafifu wa mnara huo. Orofa za chini za mnara huo zilitumiwa kuhifadhi maji, unga, matunda, jibini, divai, na nyama.

Wakati wa hatari, familia ililala kwenye orofa ya chini na ya katikati ya mnara huo. Orofa ya juu kabisa, iliyokuwa imefunikwa kwa vigae, ilitumiwa kuwa mahali pa kupigana na kulikuwa na miingilio midogo ukingoni. Mtu mmoja aliyetembelea eneo hilo katika karne ya 19 alisema kwamba kwa kuwa “hakukuwa na serikali yoyote kufanya maamuzi, mara nyingi watu walitumia silaha kusuluhisha tofauti zao.” Kwa hiyo kila familia ilikuwa tayari kujipigania.

Tuliporudi nyumbani, mioyo yetu ilijawa na shukrani kwa Yehova tulipotafakari uzuri tulioona katika uumbaji wake wenye kustaajabisha wa Svaneti. Wale walioishi kwenye minara hiyo miaka mingi iliyopita wana tumaini la kuishi katika ulimwengu mpya wa Mungu. Wakati huo, hakutakuwa na uhitaji wa kujenga minara au ngome nyingine yoyote ili kujilinda. Kwa nini? Kwa kuwa Biblia inaahidi kwamba wakati huo, watu ‘wataketi, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakutakuwa na mtu yeyote atayewatetemesha.’—Mika 4:4; Waroma 8:21, 22.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Top: Paata Vardanashvili

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki