Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 2/8 kur. 16-19
  • Matterhorn wa Kipekee

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Matterhorn wa Kipekee
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Makazi ya Mapema
  • Upendezi Wenye Kuongezeka Katika Sayansi ya Asili
  • Matterhorn Wapandwa!
  • Gharama ya Juu Mno
  • Hatari
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1996
  • Mimi Nilipanda Mlima Ulio Mzuri Kupita Yote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Barafu Juu ya Ikweta
    Amkeni!—2005
  • Kilimanjaro—Kilele cha Afrika
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 2/8 kur. 16-19

Matterhorn wa Kipekee

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA USWISI

“KUNA Matterhorn MOJA tu duniani kote; mlima MMOJA tu wenye sehemu zilizosawazika sana. Mandhari nzuri ajabu!” Ndivyo alivyosema Guido Rey, Mpanda-milima Mwitalia.

Kwa kweli, Matterhorn ni kilele kisicho cha kawaida, mmoja wa milima ijulikanayo sana ulimwenguni. Yaelekea picha kwenye kurasa hizi siyo ya kwanza ambayo umepata kuona ya mlima huu wenye kutokeza.

Matterhorn ulio kama piramidi uko mpakani mwa Italia na Uswisi, kilometa kumi kusini-magharibi mwa kijiji Zermatt, Uswisi, mji ambao jina lao lilipewa hicho kilele. Hufika kimo cha meta 4,478 angani na una vilele viwili ambavyo vimetengana kwa meta 100.

Ingawa huo ni sehemu ya Alps ya Kati, Matterhorn husimama peke yao, bila majirani wa karibu. Hili hufanyiza mwono wenye kutokeza wa mlima huo kutoka pande zote na huufanya ufae sana kupigwa picha.

Wengine kwa kufaa wamefafanua Matterhorn kuwa na umbo kama la nguzo ndefu iliyochongoka juu. Hufunua pande zao nne kwa zile ncha kuu nne, kila upande ukitenganishwa kipekee na ncha.

Matterhorn, licha ya kimo chao, sikuzote haufunikwi na barafu. Mwishoni-mwishoni mwa masika kuta zao za mwamba zilizochongoka sehemu ya juu hutoa theluji na barafu kwa joto la jua. Chini zaidi, barafuto upande wa mashariki na kaskazini-magharibi hukaa kwa utulivu dhidi ya mlima mwaka mzima kama ukanda kuzunguka kiuno chao.

Watu wengi wenye kuvutiwa wameshangaa jinsi mlima huu usio na kifani ulivyotokea. Hakuna mrundiko wa vipande-vipande kuzingira upande wa chini uwezao kuonekana ukiwa mabaki ya kitu ambacho mlima huo ulichongwa kutoka kwacho. Mrundiko wowote kama huo lazima uliondoshwa wakati wa maelfu ya miaka yasiyojulikana ya kuwapo kwao. Ni kani za asili zilizo na uwezo kama nini ambazo ni lazima zilichangia kutokeza mandhari hii nzuri!

Makazi ya Mapema

Bonde la alpine linaloongoza hadi kwenye sehemu ya chini ya Matterhorn tayari lilikuwa limekaliwa wakati wa Milki ya Kiroma. Historia huripoti kwamba katika mwaka 100 K.W.K., jenerali Mroma Mario alivuka Kipito cha Theodul, mashariki mwa Matterhorn, kwenye kimo cha meta 3,322. Njia hii ya mlimani ilitumiwa pia wakati wa Enzi za Kati kwa kusafirisha mizigo kutoka kusini hadi kaskazini.

Katika nyakati hizo wakazi waliuheshimu sana Matterhorn, hata kwa hofu ya kishirikina. Hawangejaribu kamwe kuupanda huo mlima, ambao walifikiria kuwa ulikaliwa na Ibilisi mwenyewe! Ni nani mwingine angekuwa akivurumisha barafu na maporomoko ya theluji na miamba mikubwa kama nyumba ikiwa siye?

Upendezi Wenye Kuongezeka Katika Sayansi ya Asili

Kile ambacho watu hao wanyenyekevu walikiepuka kwa sababu ya hofu baadaye kilikuja kupendwa na tabaka ya juu ya waanzilishi wa mitindo katika Uingereza. Upendezi wa kisayansi ukaanza kukua, ukisababisha wavumbuzi wapande milima kwa ajili ya uchunguzi katika nyanja za ujuzi kama vile jiolojia, topografia, na botania.

Kwa hakika, katika 1857 Klabu cha Alpine kilianzishwa London, na Waingereza wengi matajiri walisafiri hadi Ufaransa, Italia, au Uswisi ili kushiriki katika kufaulu kupanda milima Alps. Wajasiria hao walipanda kilele baada ya kilele, kutia ndani Mont Blanc. Ingawa mlima huu ndio wenye kimo cha juu kuliko yote Ulaya, wenye kimo kipatacho meta 4,807, hautokezi ugumu mwingi kwa wapanda-milima kuliko Matterhorn.

Si jitihada zote hizi zilifanywa kabisa kwa sababu ya sayansi ya asili. Kujitakia umashuhuri kuliingia. Sifa ya kuwa wa kwanza, mwenye ujasiri kuliko wote, mgumu kuliko wote, ilikuwa jambo la maana zaidi. Wakati huo katika Uingereza, neno “mchezo” halikumaanisha kitu kingine ila upandaji milima.

Kiangazi cha 1865 kilikuwa chenye shughuli nyingi mno za upandaji milima, hasa kuhusiana na Matterhorn. Piramidi hii yenye kuvutia ilikuwa moja ya vilele vya mwisho vilivyobaki kupandwa. Ilifikiriwa kuwa isiyoweza kufikilika na waongozi wa mahali hapo walikataa hata kujaribu. Mtazamo wao ulikuwa, ‘Kama ni mlima mwingine wowote sawa—lakini si Matterhorn.’

Hata hivyo, kupandwa kwa Matterhorn kulikuwa kuwezekane. Katika miaka ya mapema ya 1860, watu walipanda vilele kadhaa vya alpine. Wapandaji walijifunza kutokana na uzoefu nao wakakuza ufundi mpya. Alipokuwa na umri wa miaka 20, Edward Whymper kutoka Uingereza alitumwa Uswisi na mhariri fulani wa London achore picha za mandhari za alpine kwa ajili ya picha za kitabu fulani juu ya habari hiyo. Whymper alivutiwa na hiyo milima, na kupanda milima kukawa hamu yake kuu. Yeye alipanda vilele vingi mno kote katika Ufaransa na Uswisi naye alifanya majaribio kadhaa ya kupanda Matterhorn. Lakini alishindwa.

Matterhorn Wapandwa!

Mwishowe, katika Julai 1865, ilitukia kwamba vikundi vitatu tofauti vya kupanda milima vilikutana katika Zermatt—vyote vitatu vikiwa tayari kupanda Matterhorn. Vikiwa na haraka kwa sababu ya wakati, kwa kuwa kikundi cha Italia huenda kingefika mbele yao, vikundi hivyo vitatu viliamua kuungana kuwa cordée moja, au msitari wa wapanda-milima waliojifunga kamba. Hicho kikundi kilikuwa na wanaume saba—Edward Whymper na Lord Francis Douglas, Charles Hudson na rafiki yake mchanga Hadow—wote Waingereza—kuongezea Waswisi wawili na mwongozi mmoja Mfaransa ambaye walifaulu kumwajiri.

Wakiondoka Zermatt asubuhi ya Julai 13, walikaribia huo mlima bila haraka kutoka mashariki na kupata kwamba kwa kulinganisha sehemu za chini zaidi zilikuwa rahisi kupanda. Walipiga hema yao kwenye kimo cha meta 3,300 hivi na kufurahia sehemu iliyobaki ya siku hiyo yenye jua.

Asubuhi iliyofuata, Julai 14, kabla ya kupambazuka, walianza kupanda. Kamba ilihitajiwa mara kwa mara tu. Sehemu fulani zilikuwa ngumu kuliko nyinginezo, lakini mara nyingi walipata njia ya kupita kuzunguka vipingamizi vigumu zaidi. Baada ya vipindi viwili vya kupumzika, walifika sehemu ngumu kuliko zote. Meta 70 za mwisho zilikuwa na theluji tupu, na saa 7:45 alasiri, walifika kileleni. Matterhorn ulipandwa!

Hicho kilele hakikuonyesha kuwapo kwa wageni wa kibinadamu, kwa hiyo kwa wazi walikuwa wa kwanza. Ilikuwa hisia iliyoje! Kwa muda wa saa nzima hivi, hicho kikundi chenye ushindi kilifurahia mwono wa ajabu wa kila upande, kisha kikajitayarisha kuteremka. Wapanda-milima Waitalia wakijaribu kupanda siku iyo hiyo walibaki nyuma sana kisha wakarudi walipotambua kwamba walikuwa wamepoteza hilo shindano.

Gharama ya Juu Mno

Hata hivyo, ushindi wa wapandaji hao ulikuwa uwagharimu sana. Walipofika kipito kigumu kwenye mteremko, walijifunga kamba pamoja, mwongozi mwenye uzoefu zaidi akiongoza. Licha ya tahadhari yao, mshiriki mchanga zaidi aliteleza na kumwangukia mwanamume aliyekuwa chini yake, akimvuta na wale wengine waliokuwa juu. Wakitahadharishwa kwa yowe, wanaume watatu waliobaki waliweza kujishikilia kwenye miamba. Hata hivyo kamba ilikatika, na kwa kipindi kifupi mno, wanaume wanne wa kwanza walitokomea chini bondeni.

Wakiwa wamekufa ganzi, Edward Whymper na wale waongozi wawili Waswisi walibaki katika hali mbaya mno. Iliwalazimu kupiga kambi ya muda kwa usiku huo na kurudi Zermatt siku iliyofuata. Kwa hiyo utukufu wa hiyo siku uligeuka mara moja kuwa msiba ambao uliwaachia alama waliosalimika kwa muda wote wa maisha yao.

Miili mitatu kati ya minne ilitolewa baadaye kutoka katika barafuto meta 1,200 chini kutoka mahali pa aksidenti. Mwili wa nne, Lord Douglas, haukupatikana kamwe.

Hawa hawakuwa majeruhi wa mwisho kwenye miinamo ya Matterhorn. Licha ya uhakika wa kwamba kamba nyingi zimewekwa kwa uthabiti ndani ya miamba katika njia nyingi za kupanda na kuvuka kuta za miamba na nyufa nyembamba na licha ya uzoefu ulioongezeka na vifaa vilivyoboreshwa mno vya wapanda-milima, kumekuwa na vifo 600 hivi kwenye mlima huu pekee.

Hatari

Jambo moja ambalo huchangia sana hatari ni halihewa. Inaweza kubadilika haraka sana. Huenda siku ikaanza ikiwa yenye kupendeza, lakini kabla ya mtu kutambua, ukungu mnene au mawingu meusi mno yaweza kufunika ile piramidi na dhoruba yenye kutisha yaweza kutokea. Hilo laweza kuambatana na umeme wenye kutia hofu na radi, pamoja na pepo kali za ghafula, na kumalizikia kwa mmwagiko mkuu wa theluji. Na yote hayo katika siku yenye kupendeza ya wakati wa kiangazi!

Wapandaji wakipatwa na badiliko hilo la hali, huenda wakalazimika kupitisha usiku wakiwa mahali wazi, labda kwenye jukwaa dogo lisiloweza kuwaruhusu kusimama vizuri. Halijoto zaweza kuwa chini ya kiwango cha kuganda. Chini kuna bonde lenye kina sana. Ndipo huenda mtu akatamani angetazama Matterhorn akiwa mbali!

Hatari nyingine ni mawe yanayoanguka. Nyakati fulani wapandaji wasiofikiri huangusha mawe wenyewe. Hata hivyo, katika visa vingi, visababishi ni vya kiasili. Mabadiliko ya halijoto, barafu na theluji, mvua, na jua kali, na vilevile pepo zenye nguvu zinazofukuzana kuzunguka Matterhorn, hali zote hizo hutenda juu ya miamba, zikisababisha vipande vikubwa kuvunjika. Nyakati nyingine hivyo hubaki kwa miaka mingi, kama rundamano kubwa la sahani, lakini maporomoko ya theluji huenda hatimaye yakavifanya visonge na kuanguka.

Wapandaji wengi wamestaajabu kwamba hali hii imeendelea kwa maelfu ya miaka na bado huo mlima umebaki na umbo lao jembamba kama nguzo ndefu bila kuonyesha ishara za badiliko katika umbo lao. Ingawa hivyo, yakilinganishwa na meta kyubiki bilioni 2.5 za huo mlima, mawe yanayoanguka si ya maana vya kutosha kubadili umbo lao. Hata hivyo, hayo husababisha majeraha na potezo la uhai.

Kwa wakati huohuo, kupanda Matterhorn kumependwa na wengi. Waongozi fulani wamekuwa katika kilele chao mamia ya mara. Pia, wanaume na wanawake wengi hurudia tendo hilo, wakichagua njia nyingine kila wakati.

Lakini kuna wale pia ambao hujaribu kuupanda, lakini ambao huja kutambua kwamba ama hali hazifai, au hawana uwezo, hali za kimwili, au hawakufanya mazoezi ya kutosha. Kwa hiyo hawaendelei kupanda, lakini wao huacha kusababu kuzuri kushinde sifa ya kwamba walifaulu kupanda Matterhorn.

Hata hivyo, iwe umeona mlima huu wenye kutazamisha pichani au sinemani au umesimama karibu nao kwa kicho ukivutiwa na wangavu wao wenye fahari wakati wa maawio au machweo, huenda ulikumbushwa juu ya Mchongaji Mkuu Kuliko Wote. Kwa staha ya kina kwa kazi yake, huenda moyo wako uliyarudia maneno yaliyo kwenye Zaburi 104:24: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki