Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 11/11 kur. 14-15
  • Tingatinga—Michoro Inayokufanya Utabasamu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tingatinga—Michoro Inayokufanya Utabasamu
  • Amkeni!—2011
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mawazo ya Kuchora Yanatoka Wapi?
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2011
  • Usanii Ni Nini?
    Amkeni!—1995
  • Maisha Yangu Nikiwa Mchoraji
    Amkeni!—2001
  • Kutumikia Msanii Aliye Mkubwa wa Wote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2011
g 11/11 kur. 14-15

Tingatinga​—Michoro Inayokufanya Utabasamu

“TINGATINGA ni michoro inayotukumbusha jinsi tulivyouona ulimwengu tulipokuwa watoto. Tuliuona kuwa wenye kufurahisha na wenye rangi za kuvutia,” anaandika Daniel Augusta, meneja wa Sosaiti ya Ushirika wa Wasanii wa Tingatinga. Michoro ya Tingatinga huonyesha wanyama na tamaduni za Afrika, hasa zile za Tanzania, chimbuko la sanaa hiyo.

Sanaa hiyo ilipewa jina la mwanzilishi wake, Edward Said Tingatinga aliyezaliwa mnamo 1932. Edward alipokuwa akikua, bila shaka alivutiwa sana na eneo la porini na wanyama mwitu waliokuwa karibu na kijiji chao kusini mwa Tanzania. Alipokuwa na umri wa miaka 25 hivi, aliondoka nyumbani kwenda kutafuta kazi na maisha bora. Baadaye, alihamia kwenye mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam, na akaajiriwa kuwa mtunza-bustani. Wakati wa jioni, kipawa chake kilijidhihirisha kupitia kuimba na kucheza dansi; hata alikuja kujulikana sana kama mtumbuizaji.

Maisha ya Edward yalibadilika ghafula mwaka wa 1968. Alipata kazi ya kuwasaidia wauguzi na madaktari katika hospitali ya umma ya Muhimbili mjini Dar es Salaam. Akiwa huko, alianza kuchora kumbukumbu na mambo yaliyomvutia utotoni kwa kutumia aina ya uchoraji aliobuni mwenyewe. Na hapo ndipo sanaa ya Tingatinga ilianzia. Hakukuwa na maduka yenye vifaa vya kuchorea kama vile brashi maalumu, rangi za kawaida na zile za asili, na vifaa vingine ambavyo Edward angeweza kutumia. Kwa hiyo, alitumia vifaa ambavyo kila mtu angeweza kununua katika duka linalouza vifaa vya ujenzi. Kwa mfano alitumia rangi inayong’aa ya kupaka baiskeli, na ubao wa aina fulani ambao upande wake mmoja ulikuwa laini na uling’aa, na ambao ulifaa kabisa kuchorea picha zinazometameta.

Mtindo wa kuchora wa Edward ulikuwa sahili. Kwanza alipaka rangi moja au mbili kwenye ubao wote kisha akachora mchoro wa kitu kimoja tu—mnyama wa Afrika aliyepakwa rangi nyangavu na ambaye sehemu fulani yake ilichorwa kwa njia iliyotiliwa chumvi. Hakuongeza mandhari au kitu kingine.

Edward aliwaruhusu baadhi ya rafiki zake wa karibu na watu wa ukoo watazame alipokuwa akichora. Upesi wengi wao wakajifunza mbinu hiyo ya kuchora na mtindo wake ukaanza kuwa maarufu.

Kuanzia na mchoro wake wa kwanza kabisa, sanaa ya Tingatinga imekuwa ikitumia rangi nyangavu na maumbo sahili. Hata hivyo, kadiri ambavyo miaka imepita, mtindo huo umeboreshwa na sasa kila picha ina madoido na maumbo kadhaa. Wasanii fulani huchora watu, wanyama, na vitu vingine vingi.

Mawazo ya Kuchora Yanatoka Wapi?

Hakuwezi kuwa na mwisho wa vitu vya kuchora kwa kutumia sanaa ya Tingatinga kwa kuwa kuna aina nyingi sana za mimea na wanyama wanaopatikana Afrika: swala, nyati, ndovu, twiga, viboko, simba, tumbili, pundamilia, na wanyama wengine, pia maua, miti, ndege, na samaki—hasa wale wenye rangi maridadi. Sehemu ya nyuma ya michoro iliyo maarufu sana iko na ule mlima mrefu zaidi Afrika, Mlima Kilimanjaro, ulioko kaskazini-mashariki mwa Tanzania.

Michoro ya kisasa ya Tingatinga hujaribu pia kuonyesha watu wa Afrika na tamaduni zao. Mchoro unaweza kuonyesha pilkapilka kwenye soko lenye shughuli nyingi, wagonjwa kwenye zahanati, au maisha ya kawaida kijijini.

Tangu ilipoanzishwa, sanaa ya Tingatinga imewapa watu wa Afrika wenye vipawa vya kuchora nafasi ya kueleza wanachofikiri, na wakati huohuo wakijiletea mapato ya ziada. Wasanii wa Tingatinga wameunda muungano wa ushirika wa wasanii ambao makao yake makuu yako mjini Dar es Salaam. Baadhi yao bado wamedumisha utamaduni wa kuchora kwa kutumia rangi ngumu za kupaka baiskeli. Ikiwa Edward Tingatinga angekuwa hai leo (alikufa 1972), uso wake ungekuwa na tabasamu kubwa kwa sababu ya umaarufu wa sanaa aliyoanzisha.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki