Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 3/13 kur. 14-15
  • Robert Boyle

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Robert Boyle
  • Amkeni!—2013
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MWANAMUME ALIYEPENDA SAYANSI
  • MWANAMUME MWENYE IMANI
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2013
  • Biblia ya Bedell
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Mjue “Wolfhound” wa Ireland
    Amkeni!—1999
  • Dini Yangu Ilikuwa Sayansi
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2013
g 3/13 kur. 14-15

TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Robert Boyle

Watu wanaopendezwa sana na historia huenda wanamkumbuka Robert Boyle kuwa mwanasayansi aliyetunga ile inayoitwa kanuni ya Boyle—sheria ya asili inayoeleza uhusiano uliopo kati ya shinikizo na kiasi cha gesi. Ugunduzi huo muhimu ulifungua njia ya maendeleo mengi ya kisayansi baada ya hapo. Lakini Robert Boyle hakuwa tu mwanasayansi stadi. Anatambuliwa pia kwa sababu ya imani yake yenye nguvu katika Mungu na katika Neno Lake, Biblia, lililoongozwa kwa roho.

BOYLE alizaliwa mnamo mwaka wa 1627 katika familia tajiri kwenye Kasri la Lismore, huko Ireland. Kipindi hicho kilikuwa karibu na mwanzo wa kile ambacho wanasayansi wanakiita enzi ya kutumia akili—kipindi cha wakati ambapo watu wengi wenye akili na wanaopendezwa na matukio na masuala muhimu walijaribu kuwafanya wanadamu waache kukazia fikira maoni yasiyo na msingi yaliyokuwa yamewapumbaza kwa karne nyingi. Boyle alishiriki katika jitihada hizo. Katika maelezo kuhusu maisha yake ya mapema, alijiita Philaretus, yaani “Mpenda Ukweli.”

Tamaa ya Boyle ya kujifunza ukweli ililingana na tamaa yake ya kuwaeleza wengine mambo yote aliyokuwa amejifunza. Aliandika vitabu vingi ambavyo vilikuwa na uvutano mkubwa kwa wanasayansi wengi wa wakati wake, kutia ndani mwanasayansi maarufu Sir Isaac Newton. Mnamo mwaka wa 1660, Boyle akawa mmoja kati ya waanzilishi wa taasisi ya Royal Society, taasisi ya kisayansi ambayo bado iko huko London, Uingereza.

MWANAMUME ALIYEPENDA SAYANSI

Boyle amesemekana kuwa baba wa kemia. Alikuwa na maoni tofauti kabisa na yale ya wanakemia wa siku zake. Wanakemia hao walificha ugunduzi wao au waliuandika kwa maneno yasiyoeleweka ambayo ni watu wachache sana wasio wanakemia wangeweza kuelewa. Tofauti na hilo, Boyle alichapisha waziwazi habari zote kuhusu kazi yake. Isitoshe, badala ya kukubali tu dhana zilizokubaliwa kwa muda mrefu, aliamini kwamba ni sahihi zaidi kufanya majaribio katika maabara ili kuthibitisha mambo hakika.

Majaribio ya Boyle yaliunga mkono wazo la kwamba mata imefanyizwa na kile alichokiita corpuscles, yaani chembechembe za aina fulani, zilizoungana kwa njia tofauti tofauti kufanyiza vitu mbalimbali.

Maoni ya Boyle kuhusu utafiti wa kisayansi yanaelezwa katika kitabu chake maarufu The Sceptical Chymist. Katika kitabu hicho anapendekeza kwamba wanasayansi waepuke kuwa na kiburi au kushikilia sana kauli yao na badala yake wawe tayari kukubali makosa yao. Boyle alisisitiza kwamba wale waliokuwa na msimamo mkali kuelekea mambo walipaswa kutofautisha kati ya mambo waliyoyajua kuwa kweli na mambo waliyodhani kuwa kweli.

Boyle alisisitiza kwamba wale waliokuwa na msimamo mkali kuelekea mambo walipaswa kutofautisha kati ya mambo waliyoyajua kuwa kweli na mambo waliyodhani kuwa kweli

MWANAMUME MWENYE IMANI

Boyle alikuwa na maoni hayohayo kuhusu mambo ya kiroho. Mambo aliyogundua kuhusu ulimwengu na muundo wa ajabu wa viumbe hai yalimthibitishia kwamba lazima kuwe na Mbuni na Muumba. Kwa hiyo, alipinga maoni ya kwamba hakuna Mungu yaliyokuwa yakienea kati ya wasomi wa siku zake. Boyle alifikia mkataa kwamba hakuna mtu anayetumia uwezo wake wa kufikiri kwa unyoofu, ambaye angeweza kukosa kumwamini Mungu.

Hata hivyo, Boyle hakudhani kwamba kutumia tu uwezo wake wa kufikiri kungemsaidia mwanadamu kufahamu ukweli wa kidini. Aliona uhitaji wa kupata ufunuo fulani kutoka kwa Mungu. Naye alisema kwamba ufunuo huo ni Neno la Mungu, Biblia.

Boyle alisikitika sana kuona kwamba watu wengi hawakufahamu mafundisho ya Biblia na walionekana kuwa hawana msingi imara wa imani yao ya kidini. Inawezekanaje, aliuliza, kwamba imani ya kidini ya mtu itegemee tu kile ambacho wazazi wake waliamini au mahali mtu alipozaliwa? Boyle alitamani sana kuwasaidia watu wapate ujuzi zaidi wa Biblia.

Ili kutimiza jambo hilo, Boyle alitoa pesa ili kufadhili kuchapishwa kwa Biblia katika lugha nyingi. Lugha hizo zilitia ndani baadhi ya lugha za Wenyeji wa Asili wa Amerika Kaskazini, na pia Kiarabu, Kiailandi, Kimalay, na Kituruki. Kwa sababu hiyo, Robert Boyle akathibitika kuwa mwanamume mwenye vipawa lakini mnyenyekevu na aliyetamani sana kujua ukweli wa mambo yote na kuwasaidia wengine kufanya hivyo.

TAARIFA FUPI:

  • Alizaliwa nchini Ireland katika mwaka wa 1627.

  • Aliitwa baba wa kemia.

  • Mwanasayansi maarufu wa kwanza kuandika ufafanuzi wa kina kuhusu mbinu zake za kufanya majaribio katika maabara.

  • Maandishi yake yalikuwa na uvutano mkubwa sana kwa Sir Isaac Newton, aliyeishi katika kipindi hicho lakini alikuwa mchanga zaidi.

  • Alifadhili kazi ya kutafsiriwa kwa Biblia katika lugha nyingi.

  • Alikufa nchini Uingereza katika mwaka wa 1691 akiwa na umri wa miaka 64.

BIBLIA KATIKA KIAILANDI

Robert Boyle alijua kwamba tangu mwaka wa 1573, kikundi fulani cha wasomi kilikuwa kimeanza kutafsiri sehemu za Biblia katika Kiailandi. Katika mwaka wa 1602 walichapisha katika Kiailandi sehemu ambayo inajulikana kama Agano Jipya. Baadaye, katika mwaka wa 1640, kutafsiriwa kwa sehemu inayosalia ya Biblia katika Kiailandi kulikamilika. Tafsiri hiyo haikuchapwa hadi mwaka wa 1685, baada ya Boyle kutoa pesa kwa ajili ya mradi huo. Miaka mitano baadaye, kupitia ufadhili wa kifedha wa Boyle, Biblia kamili ya Kiailandi ilichapishwa. Vitabu vya Apokrifa vilikuwa pia vimetafsiriwa katika Kiailandi. Apokrifa ni mojawapo ya mkusanyo wa maandishi yasiyopatana na Biblia ambayo mara nyingi huunganishwa pamoja na Biblia na kuchapishwa kama kitabu kimoja. Hata hivyo, kwa sababu Boyle alikuwa mpenda kweli, alikataa kuchapisha vitabu hivyo vya uwongo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki