Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 6/13 kur. 10-11
  • Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita Kiasi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita Kiasi
  • Amkeni!—2013
  • Habari Zinazolingana
  • Naweza Kutumiaje Pesa Zangu Vizuri?
    Amkeni!—2006
  • Kadi za Mkopo—Je, Zitakutumikia au Zitakutumikisha?
    Amkeni!—1996
  • Ninaweza Kupangaje Matumizi ya Pesa Zangu?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Je, Napaswa Kuchukua Kadi ya Mkopo?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2013
g 6/13 kur. 10-11

Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita Kiasi

Mbali na kushinikizwa na wauzaji bidhaa, hisia zetu pamoja na mazoea yetu yanaweza kutuchochea kununua vitu kupita kiasi. Yafuatayo ni madokezo sita yatakayokusaidia kudhibiti ununuzi wako.

  1. Epuka kununua vitu ambavyo hukupangia. Je, wewe hufurahia msisimuko unaotokana na kununua vitu, hasa vile vilivyopunguzwa bei? Ikiwa ndivyo, huenda ukawa na mwelekeo wa kununua vitu ambavyo hukupangia. Ili kuepuka tabia hiyo, tua na ufikirie matokeo ya kununua, kumiliki, na kudumisha kitu unachotaka kununua. Fikiria kuhusu vitu ulivyonunua bila kupangia na baadaye ukajuta kwamba ulivinunua. Chukua muda kufikiria kwa uzito kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

  2. Epuka kununua vitu ili tu ujihisi vizuri. Kununua vitu kunaweza kukutuliza kwa muda unapohisi kuwa umeshuka moyo. Lakini hisia zisizofaa zinaporudi, huenda ukahisi kwamba unahitaji kununua vitu vingine ili upate kitulizo. Badala ya kununua vitu ili ujihisi vizuri, zungumza na marafiki wanaoweza kukusaidia au jihusishe katika utendaji fulani kama vile kwenda matembezi.

  3. Usifanye ununuzi wa vitu kuwa tafrija. Maduka makubwa ya kifahari yamefanya ununuzi wa vitu kuwa burudani. Ingawa huenda lengo lako la kwenda madukani au kutazama bidhaa kwenye Intaneti likawa ni kufurahisha macho tu, vitu unavyoona vimekusudiwa kuchochea tamaa yako ya kununua. Nenda madukani wakati tu unahitaji kununua kitu fulani hususa, na ununue kitu hicho tu.

  4. Uwe mwangalifu unapochagua marafiki. Mtindo wa maisha na mazungumzo ya marafiki wako yanaweza kuchochea tamaa yako. Ikiwa unanunua vitu vingi kupita kiasi ili tu ufanane na marafiki wako, basi chagua marafiki ambao hawakazii sana pesa au mali.

  5. Chukua mikopo kwa hekima. Ni rahisi kuchukua mikopo bila kufikiria matokeo. Iwe unatumia njia gani kuchukua mkopo, jaribu kulipa kiasi fulani cha mkopo huo kila mwezi. Jua ni kiasi gani cha riba utakachotozwa kwa mkopo unaochukua. Jihadhari na mashirika ya kifedha yanayotoa mkopo wa kiasi kikubwa cha pesa bila masharti mengi. Badala ya kuchukua mkopo au kununua vitu kwa mkopo, weka pesa akiba hadi utakapoweza kununua kitu unachohitaji kwa pesa taslimu.

  6. Fahamu hali yako ya kifedha. Ni rahisi kutumia pesa kupita kiasi kwa sababu hujui hali yako ya kifedha. Weka rekodi ya matumizi yako na ujue hali yako ya kifedha kwa ujumla. Panga bajeti ya matumizi ya kila mwezi ikitegemea mapato yako na matumizi ya wakati uliopita. Linganisha matumizi yako na bajeti uliyopanga. Mwombe rafiki unayemwamini akusaidie kuelewa mambo ya kifedha ambayo hujui.

Walinde Watoto Wako Wasinaswe na Mtego wa Kununua Vitu Kupita Kiasi

Matangazo ya kibiashara huwalenga hasa watoto, na kwa sababu nzuri. Vijana leo wananunua vitu vingi kuliko wakati mwingine wowote. Nchini Marekani, vijana hutumia mabilioni ya dola kila mwaka kununua vitu.

Hata hivyo, mtafiti Juliet Schor anasema kwamba ni rahisi zaidi kwa watoto ambao hununua vitu kupita kiasi kupatwa na mshuko wa moyo na wasiwasi na wana uhusiano mbaya na wazazi wao. Unaweza kuwalindaje watoto wako? Fikiria njia ambazo wazazi fulani wametumia ili kuwalinda watoto wao.

WAELIMISHE: “Huwezi kuwalinda watoto wasiathiriwe na matangazo ya kibiashara kwa sababu yako kila mahali. Kwa hiyo sisi huwaambia binti zetu kwamba mashirika yanayotumiwa kutangaza bidhaa yana lengo fulani na makampuni yaliyowaajiri yanataka kupata pesa. Hayajali masilahi yao.”—James na Jessica.

USILEGEZE MSIMAMO: “Watoto humshinikiza mzazi awanunulie kitu fulani, nao hawaachi hadi awanunulie. Lakini usikubali kushindwa. Mwishowe watajifunza kwamba si lazima wapate kila kitu wanachotaka. Tulipokuwa tukimlea binti yetu, tulizungumza pamoja tukiwa wazazi kuhusu kuwa na usawaziko na mipaka ambayo tungemwekea.”—Scott na Kelli.

PUNGUZA MUDA WA KUTAZAMA MATANGAZO YA KIBIASHARA: “Familia yetu hutumia wakati mchache sana kutazama televisheni. Si kawaida yetu kutazama televisheni. Badala ya kutazama televisheni sisi hutumia wakati huo kufanya mambo mengine. Sisi hupika na kula pamoja, na wavulana wetu hupenda sana kusoma.”—John na Jenniffer.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki