“Kiumbe Kipya” Chaanza Kutenda!
(Funzo la Kitabu)
1, 2. (a) Ni uumbaji gani, wa miaka inayopungua elfu mbili iliyopita, uliokuwa mzuri sana kuliko ule wa mwanamume na mwanamke? (b) Kulingana na maneno ya Yesu katika Luka 24:46-48 na Matendo 1:8 kutiwa mafuta kwa “kiumbe kipya” kulikuwa kwa Kusudi gani?
KUUMBWA kwa mwanamume na mwanamke wa kwanza yapata miaka elfu sita iliyopita lilikuwa jambo zuri sana. (Mwa. 1:26-28) Kuzaliwa kwa “kiumbe kipya” miaka isiyozidi elfu mbili iliyopita lilikuwa jambo zuri hata zaidi, na la maana zaidi kwa wanadamu wote. Kuzaliwa huko kulitukia katika siku ya Pentekoste ya mwaka 33 W.K. lilipozaliwa kundi la wanafunzi wa Kristo, wote wakiwa wametiwa mafuta kwa roho takatifu kusudi watangaze ufalme wake wa Kimasihi.
2 Juma zinazopungua mbili kabla ya siku hiyo yenye kutokeza ya Pentekoste, Yesu Kristo aliyefufuliwa aliwaambia wanafunzi wake hivi:
“Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.” (Luka 24:46-48) “Mtapokea nguvu, [ikiisha kuwajilia juu yenu roho takatifu]; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa [dunia].”—Matendo 1:8.
3. Huo mgawo wa eneo ulikuwa mkubwa kadiri gani nao wanafunzi walianza kulitolea ushuhuda wakati gani na tangu wapi?
3 Je! kungeweza kuwa na mgawo wa eneo la kutolea ushuhuda kubwa kuliko hili? Lilikuwa ulimwengu wote. Namna gani juu ya kufikia eneo lote hili na ushuhuda wa Kimasihi? Jambo hili lingehitaji wakati, ndiyo, jitihada yenye ujasiri na yenye kudumu. Hata hivyo, muda si muda baada ya roho takatifu kuwajilia siku ya Pentekoste, walianza kutenda kama mashahidi kwa wengine kwanza huko Yerusalemu.
4. Mambo yalianza kutendeka namna gani wakati wa siku hiyo ya Pentekoste kama vile Yoeli 2:28, 29 lilivyokuwa limetabiri?
4 Mambo yalitukia kama vile tu yalivyokuwa yametabiriwa katika Yoeli 2:28, 29; wanafunzi hao wenye kujawa na roho takatifu walianza kutabiri, hata katika lugha za kigeni, kimwujiza! Maelfu ya Wayahudi waliokuwako Yerusalemu kusudi washerehekee sikukuu ya Pentekoste walikusanyika ili washuhudie tamasha hii. Walilisikia kundi hili dogo la wanafunzi wa Kristo ‘likizungumza,’ kama vile walivyosema, “kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”—Matendo 2:11.
5. Petro alitumiaje ufunguo wa kwanza wa ‘zile funguo za ufalme wa mbinguni’ wakati wa siku hiyo ya Pentekoste?
5 Ili kulieleza tukio hili, mtume Petro alitumia ufunguo wa kwanza wa zile “funguo za ufalme wa mbinguni” kwa kuongoza katika kuwahubiri watu wenye kuuliza maulizo. (Mt. 16:19) Alimshuhudia Yesu kuwa Masihi, yule ambaye alikataliwa na kuuawa na viongozi wa Kiyahudi lakini akafufuliwa siku ya tatu na sasa ametukuzwa kwenye mkono wa kuume wa Mungu. Wayahudi wenye kuchomwa na dhamiri sasa wakauliza hivi: “Tutendeje ndugu zetu?” Jibu la Petro lilikuwa hili: “Tubuni mkabatizwe kila mmoja [wenu] kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha [roho takatifu]. Kwa kuwa ahadi hii [ya Yoeli 2:28, 29] ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na [Yehova] Mungu wetu wamjie.”—Matendo 2:14-39.
6. Wayahudi waliotubu na kubatizwa walipatwa na tukio gani, nao waliokolewa kutokana na nini?
6 Wale waliomkubali Yesu kuwa Masihi au Kristo kwa kutii walibatizwa katika maji. Kwa hiyo siku hiyo watu wapata elfu tatu walibatizwa. Yesu Kristo aliyetukuzwa aliwabatiza kwa roho takatifu, wakazaliwa kwa mara ya pili wakawa wana wa kiroho wa Mungu. Walitolewa kutoka katika agano la Torati ya Musa na kuletwa katika agano jipya lililopatanishwa na Yesu Kristo. Katika njia hii walitii shauri la Petro lenye uharaka kwamba ‘waokolewe kutokana na kizazi hiki kipotovu.’ Kwa kufanya hivi, walipona kubatizwa kwa moto wakati Yerusalemu ulipoharibiwa katika mwaka 70 W.K. na watekaji Warumi chini ya Jemedari Tito.—Matendo 2:40; Luka 3:16, 17.
7. Watiwa mafuta wangemwiga Yesu Kristo katika njia gani, nako kuifanya kazi aliyotabiri kulifungulia waamini njia kwenye nini?
7 Tangu siku hiyo ya Pentekoste na kuendelea, wengi zaidi na zaidi wa wale waliomwamini Yesu kuwa Masihi walitiwa mafuta kwa roho takatifu ilipokuja juu yao. Sasa wafanye nini? Kama watiwa mafuta, walikuwa na daraka la kuuiga mfano wa Yesu Kristo. Yeye alifanya nini baada ya kutiwa mafuta katika Mto Yordani? Alikwenda kote kote nchini na kuhubiri ufalme wa Mungu. (Mt. 4:12-17) Kuhubiriwa kwa ufalme wa Mungu kusingekoma wakati wa kufa kwake. Siku chache kabla ya kufia imani huko Yerusalemu, alitabiri kuharibiwa kwa mji huo na Warumi walakini akasema kwamba, hata kabla ya msiba huo wa taifa zima, “habari njema hizi za ufalme zitahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa na watu kuwa ushuhuda kwa mataifa yote.” (Mt. 24:14-22, NW) Ikaja Pentekoste, ikifuatana na kutiwa mafuta kwao kwa roho takatifu, watiwa mafuta hao hawakupoteza wakati katika kuanza kazi! Kuhubiri huku kwa Ufalme kuliwafungulia njia waamini hao wapate kuwa warithi pamoja na Yesu Kristo katika ufalme wake wa kimbinguni.
8. Kuhubiri Ufalme kulielekezwaje kwa Wasamaria, nako kukiwa na matokeo gani?
8 Yakatokea mateso makali. Wanafunzi hao wakatawanywa kutoka Yerusalemu. Walakini kutawanywa huku kwa kundi hilo kulitokeza tu kuenezwa kwa Ufalme. Kama vile ilivyokuwa imetabiriwa, ushuhuda huo ukapelekwa katika jimbo la Samaria. Akiwa amelazimishwa kutoroka kutoka Yerusalemu, mwanafunzi Filipo alielekeza fikira zake kwa Wasamaria. “Walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.” Baadaye, wakati wa ziara ya Petro na Yohana huko Samaria, Wasamaria hawa waliobatizwa wakapokea roho takatifu kupitia kwa mitume hao.—Matendo 8:1-17.
9. (a) Ni kuongolewa gani kusikotazamiwa ambako sasa kulitukia kati ya Wayahudi? (b) Petro aliutumiaje ufunguo mwingine wa ‘zile funguo za ufalme wa mbinguni?
9 Kwa ghafula sasa, ajabu kubwa yatokea! Kiongozi wa watesi wa Wakristo ageuka kuwa Mkristo. Sauli wa Tarso ageukia Ukristo. Akawa mtangazaji mkuu wa ufalme wa Mungu kupitia kwa Yesu, Masihi. (Matendo 9:1-30) Aacha jina lake la kwanza, Sauli, akaja kujulikana kama mtume Paulo. Baada ya kugeuka huko kwenye kutokeza, kukaja kugeuka kwingine kwenye kutokeza kwa namna nyingine. Kulikuwa kugeuka kwa Mtaifa wa kwanza asiyetahiriwa au mtu asiye Myahudi. Jambo hili lilitukia wakati roho takatifu ilipomwongoza mtume Petro atumie ufunguo mwingine wa zile “funguo za ufalme wa mbinguni.” (Mt. 16:19) Petro alifanya hivyo kwa kuhubiri katika nyumba ya akida Mwitalia Komelio katika Kaisaria. Katika Matendo 10:44-48 twasoma hivi:
“Petro alipokuwa akisema maneno hayo [roho takatifu] [i]kawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha [roho takatifu]. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea [roho takatifu] vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo.”
10, 11. (a) Kutoka kwa nyumba ya Kornelio, kuhubiriwa kwa ufalme kulienea mbali kadiri gani, na kwa faida ya nani? (b) Ingawa Petro ndiye aliyepainia njia kwenye ulimwengu wa mataifa, namna gani na sababu gani Paulo alimzidi?
10 Kutoka kwa nyumba ya akida Mtaifa Kornelio habari njema zikahubiriwa na kuenea ‘mpaka miisho ya [dunia].’ Hii ilikuwa kwa faida ya Mataifa na vile-vile ya Wayahudi wa asili.
11 Ijapokuwa Petro alipainia njia katika ulimwengu wa Mataifa, mtume Paulo aliwazidi wengine wote katika kuhubiri Neno la Mungu kwa Mataifa wasiotahiriwa, katika siku zake. Yeye hakuona aibu kujiita “mtume kwa watu wa mataifa.” Hakulifanya jambo hili la hakika kuwa dogo. Aliutukuza utumishi huu wake na kwa hiyo aliufanyia bidii.—Rum. 11:13.
12. Paulo alitaka kwenda kuhubiri kwenye sehemu gani ya mbali, walakini kuelekea upande huo alifika mbali kadiri gani nako huko alifanya nini?
12 Paulo alitaka kufika hata mpaka Spania, walakini mara ya mwisho tunapomsikia ilikuwa wakati wa kuzuiliwa kwake katika Rumi, Italia. Kwa habari ya kukamatwa kwake kwa mara ya kwanza na kuzuiliwa katika nyumba yake mwenyewe aliyokuwa amepanga katika Rumi, twasoma hivi: “Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.”—Matendo 28:30, 31; Rum. 15:24, 28.
Kutoka Holy Spirit—The Force Behind the Coming New Order Sura ya 7.