Adamu na Hawa
Maana: Adamu ndiye aliyekuwa kiumbe cha kwanza cha kibinadamu. Neno la Kiebrania ‘a·dhamʹ linatafsiriwa pia kwa kufaa “mwanadamu,” “mtu wa udongo,” na “binadamu.” Hawa, mwanamke wa kwanza, alikuwa mke wa Adamu.
Je, Adamu na Hawa walikuwa watu wa kubuniwa tu (wa hadithi)?
Je, ni jambo lisilopatana na akili kuamini kwamba sote tulitokana na wazazi walewale wa kwanza?
“Sasa sayansi inathibitisha yale ambayo dini nyingi zilizo kubwa zimekuwa zikihubiri kwa muda mrefu: Wanadamu wa jamii zote . . . walitokana na mtu yuleyule wa kwanza.”—Heredity in Humans (Philadelphia na New York, 1972), Amram Scheinfeld, uku. 238.
“Masimulizi ya Biblia juu ya Adamu na Hawa, baba na mama wa jamii nzima ya kibinadamu, yalisimulia karne nyingi zilizopita ukweli uleule ambao sayansi imeonyesha leo: kwamba watu wote wa dunia ni familia moja na wana asili moja.”—The Races of Mankind (New York, 1978), Ruth Benedict na Gene Weltfish, uku. 3.
Mdo. 17:26: “[Mungu] alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso wa dunia nzima.”
Je, Biblia inasimulia Adamu kuwa mtu wa kubuniwa tu anayewakilisha wanadamu wote wa kwanza?
Yuda 14: “Enoko, wa saba kutoka kwa Adamu, alitoa unabii.” (Enoko hakuwa mtu wa saba kutoka kwa wanadamu wote wa kwanza.)
Luka 3:23-38: “Yesu mwenyewe, alipoanza kazi yake, alikuwa na umri wa karibu miaka 30, akiwa . . . mwana wa Daudi . . . mwana wa Abrahamu . . . mwana wa Adamu.” (Daudi na Abrahamu ni watu wa kihistoria wanaojulikana sana. Je, si jambo linalopatana na akili kukata kauli kwamba Adamu alikuwa mtu halisi?)
Mwa. 5:3: “Adamu akaishi miaka 130. Ndipo akazaa mwana kwa mfano wake, kwa sura yake. Akamwita jina lake Sethi.” (Sethi hakuzaliwa na watu wote wa kwanza, wala watu wote wa kwanza hawakuzaa wana wakiwa na umri wa miaka 130.)
Je, yale mazungumzo kati ya nyoka na Hawa yanathibitisha kwamba masimulizi hayo ni hadithi tu?
Mwa. 3:1-4: “Basi nyoka alikuwa mwenye kujihadhari kuliko wanyama wote wa mwituni ambao Yehova Mungu alikuwa amewafanya. Kwa hiyo akaanza kumwambia mwanamke: ‘Je, ni kweli kwamba Mungu alisema msile matunda ya kila mti wa bustani?’ Mwanamke akamjibu na kumwambia nyoka: ‘ . . . Mungu amesema, “Msiyale, wala msiyaguse ili msife.”’ Ndipo nyoka akamwambia mwanamke: ‘Hakika hamtakufa.’”
Yoh. 8:44: “[Yesu akasema:] Ibilisi . . . ni mwongo na ndiye baba ya uwongo.” (Kwa hiyo, Ibilisi ndiye aliyekuwa chanzo cha ule uwongo wa kwanza uliosemwa katika Edeni. Alimtumia nyoka kama msemaji wake. Masimulizi ya Mwanzo hayatumii viumbe wa kubuniwa tu ili kufundisha somo. Ona pia Ufunuo 12:9.)
Mfano: Si ajabu kwa mtu mwenye ustadi kufanya ionekane kana kwamba sauti yake inatoka katika chanzo kingine. Linganisha na andiko la Hesabu 22:26-31, linalosema kwamba Yehova alimfanya punda-jike wa Balaamu aseme.
Ikiwa “mtu wa kwanza Adamu” alikuwa mtu wa kubuniwa tu, vipi yule “Adamu wa mwisho,” Yesu Kristo?
1 Kor. 15:45, 47: “Hata imeandikwa hivi: ‘Mtu wa kwanza Adamu akawa nafsi hai.’ Adamu wa mwisho akawa roho inayotoa uhai. Mtu wa kwanza ni wa kutoka duniani na amefanywa kwa mavumbi; mtu wa pili ni wa kutoka mbinguni.” (Kwa hiyo, mtu anapodai kwamba Adamu hakuwa mtu halisi aliyemtendea Mungu dhambi, inaonyesha kwamba mtu huyo anatilia shaka utambulisho wa Yesu Kristo. Dai hilo humfanya mtu akatae sababu iliyomlazimu Yesu autoe uhai wake kwa ajili ya wanadamu. Kukataa huko ni kukana imani ya Kikristo.)
Yesu mwenyewe aliyaonaje masimulizi ya Mwanzo?
Mt. 19:4, 5: “[Yesu] akasema: ‘Je, hamkusoma [katika Mwanzo 1:27; 2:24] kwamba yeye aliyewaumba hao [Adamu na Hawa] kutoka mwanzo aliwafanya mwanamume na mwanamke na kusema, “Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja”?’” (Kwa kuwa Yesu aliamini kwamba masimulizi ya Mwanzo yalikuwa ya kweli, je, sisi pia hatupaswi kuyaamini?)
Mtu Akisema—
‘Dhambi ya Adamu ilikuwa mapenzi ya Mungu, mpango wa Mungu.’
Unaweza kujibu hivi: ‘Watu wengi wamesema hivyo. Lakini ikiwa ningefanya jambo ambalo ulitaka nifanye, je, ungenihukumu nikilifanya? . . . Basi, ikiwa dhambi ya Adamu ilikuwa mapenzi ya Mungu, kwa nini Adamu alifukuzwa kutoka Edeni akiwa mtenda-dhambi? (Mwa. 3:17-19, 23, 24)’
Au unaweza kusema: ‘Hilo ni jambo lenye kupendeza, na kwa kweli jibu linatia ndani Mungu ni mtu wa aina gani. Je, lingekuwa jambo la haki au la upendo kumhukumu mtu kwa kufanya jambo ambalo wewe mwenyewe ulimpangia afanye?’ Kisha unaweza kuongezea: (1) ‘Yehova ni Mungu wa upendo. (1 Yoh. 4:8) Njia zake zote ni haki. (Zab. 37:28; Kum. 32:4) Hayakuwa mapenzi ya Mungu Adamu afanye dhambi; alimwonya Adamu. (Mwa. 2:17)’ (2) ‘Mungu alimruhusu Adamu, kama anavyoturuhusu sisi, kuwa na uhuru wa kuchagua jambo ambalo angefanya. Ukamilifu haukuondoa uhuru wa kuchagua kutotii. Adamu alichagua kumwasi Mungu, ingawa alikuwa ameonywa kwamba matokeo yangekuwa kifo.’ (Ona pia ukurasa wa 172, 173.)