Matibabu Mengine Bora Badala ya Damu
Huenda wewe ukahisi, ‘Utiwaji-damu mishipani ni hatari, lakini je! kuna matibabu mengine yaliyo bora?’ Hilo ni swali zuri, na angalia neno hilo “bora.”
Kila mmoja, kutia na Mashahidi wa Yehova, hutaka utunzaji wa kitiba wa hali bora wenye mafanikio. Dakt. Grant E. Steffen aliandika juu ya mambo mawili: “Utunzaji wa kitiba wa hali bora ni uwezo wa mambo ya utunzaji huo ili kufikia miradi halali ya kitiba na isiyo ya kitiba.” (The Journal of the American Medical Association, Julai 1, 1988) ‘Miradi isiyo ya kitiba’ ingetia ndani kutohalifu dhamiri ya mgonjwa yenye msingi wa Biblia.—Matendo 15:28, 29.
Je! kuna njia halali na zenye mafanikio za kumaliza matatizo mazito ya kitiba bila kutumia damu? Kwa furaha, jibu ni ndiyo.
Ingawa matabibu walio wengi wamedai kwamba waliwapa wagonjwa damu wakati tu ilipokuwa inahitajiwa kabisa, baada ya kutokea ugonjwa wa UKIMWI wenye kuenea sana utumizi wao wa damu ulishuka kwa haraka sana. Tahariri moja katika Mayo Clinic Proceedings (Septemba 1988) ilisema kwamba “mojapo manufaa za ugonjwa huo wenye kuenea sana” ilikuwa kwamba “ilitokeza mbinu mbalimbali upande wa wagonjwa na matabibu kuepuka utiaji-damu mishipani.” Ofisa wa benki ya damu alieleza hivi: “Jambo ambalo limebadilika ni mkazo wa ujumbe, kupokewa kwa ujumbe huo na madaktari (kwa sababu walifahamu hatari yenye kuongezeka), na dai la ufikirio wa matibabu mengine.”—Transfusion Medicine Reviews, Oktoba 1989.
Angalia kwamba, kuna matibabu mengine! Hilo linapata kuwa lenye kueleweka wakati tunapopitia sababu kwa nini utiaji-damu mishipani unafanywa.
Hemoglobini iliyo katika chembe nyekundu hupeleka oksijeni inayohitajiwa kwa ajili ya afya njema na uhai. Hivyo ikiwa mtu amepoteza damu nyingi, huenda ikaonekana kuwa jambo la akili ni kumtia tu nyingine badala ya hiyo iliyopotezwa. Kwa kawaida wewe una gramu zapata 14 au 15 za hemoglobini katika kila kyubiki sentimeta 100 za damu. (Kipimio kingine cha kupimia ni hematokriti, ambacho kwa kawaida huwa karibu asilimia 45.) “Kanuni” iliyopokewa ilikuwa kumtia mgonjwa damu kabla ya upasuaji ikiwa hemoglobini yake ilikuwa chini ya 10 (au hematokriti asilimia 30). Jarida la Uswisi Vox Sanguinis (Machi 1987) liliripoti kwamba “asilimia 65 ya [waanesthesiolojia (wataalamu wa nusukaputi)] walitaka wagonjwa wawe na hemoglobini ya gm/dl 10 kabla ya upasuaji kwa ajili ya upasuaji wa kujichagulia.”
Lakini kwenye kongamano la 1988 juu ya utiaji-damu mishipani, Profesa Howard L. Zauder aliuliza, “Sisi Tulipataje ‘Nambari ya Kimwujiza’?” Alitaarifu kwa uwazi: “Hoja ya visababisha magonjwa yenye takwa la kwamba mgonjwa awe na gramu 10 za hemoglobini (Hgb) kabla ya kupokea nusukaputi [anesthetic] ni ya kimapokeo, si dhahiri, na haikuhakikishwa na uthibitisho wa uchunguzi uliofanywa katika klinki wala wa kimajaribio.” Ebu wazia yale maelfu mengi ya wagonjwa ambao kutiwa damu mishipani kwao kulisababishwa na takwa ‘lisilo dhahiri, lisilohakikishwa’!
Huenda wengine wakauliza, ‘Kwa nini kiwango cha hemoglobini cha 14 chahitajiwa ikiwa unaweza kuendelea ukiwa na kiasi kidogo zaidi?’ Basi, kwa njia hiyo unakuwa na akiba kubwa ya uwezo wa kupeleka oksijeni hivi kwamba unakuwa tayari kwa mazoezi au kazi nzito. Machunguzi waliofanyiwa wagonjwa wenye upungufu wa damu hata yalifunua kwamba “ni vigumu kugundua upungufu katika uwezo wa kufanya kazi kwa msongamano wa hemoglobini ulio chini kiasi cha g/dl 7. Wengine wamepata uthibitisho kwamba utendaji uliharibika kwa kiasi tu.”—Contemporary Transfusion Practice, 1987.
Ingawa watu wazima wanaweza kuwa na kiwango cha chini cha hemoglobini, namna gani watoto? Dakt. James A. Stockman III asema: “Kukiwa na visa vichache vilivyo tofauti, vitoto vilivyozaliwa kabla ya wakati vitapata upungufu katika hemoglobini katika mwezi wa kwanza hadi mitatu . . . Vionyeshi vya utiwaji-damu mishipani wakiwamo nasari si dhahiri. Kweli kweli, vitoto vingi huonekana vikivumilia msongamano wa kiwango cha chini wa hemoglobini kwa njia yenye kutokeza bila magumu yenye kuonekana wazi katika uchunguzi uliofanywa katika kliniki.”—Pediatric Clinics of North America, Februari 1986.
Habari kama hizo hazimaanishi kwamba hakuna kitu kinachopasa kufanywa wakati mtu anapopoteza damu nyingi katika aksidenti au wakati wa upasuaji. Ikiwa mtu anapoteza damu nyingi sana na kwa haraka, kanieneo ya damu yake itashuka, na huenda akapatwa na mshtuko. Jambo la msingi linalohitajiwa ni kukomesha kutokwa damu na kurudisha kiasi katika mfumo wake. Jambo hilo litazuia kupatwa na mshtuko na kuendeleza katika mzunguko wa damu chembe nyekundu zinazobaki pamoja na sehemu nyingine.
Kurudisha kiasi mahali pa kilichopotezwa kwaweza kufanywa bila kutumia damu nzima au plazima ya damu.a Umajimaji mbalimbali usio damu huwa na mafanikio katika kutanua kiasi. Ulio sahili zaidi ni myeyusho-chumvi, ambao si ghali na unafaana na damu yetu pia. Vilevile kuna umajimaji ulio na vitu vya pekee, kama deksitrani, Haemaccel, na myeyusho-maziwa-chumvi wa Ringer. Hetastarchi (HES) ni kitanuzi kiasi kilicho kipya zaidi, na “kinaweza kupendekezwa kuwa salama kwa wale wagonjwa [wenye kuchomeka] wanaokataa vitu vilivyofanyizwa kwa damu.” (Journal of Burn Care & Rehabilitation, Januari/Februari 1989) Umajimaji huo mbalimbali una manufaa dhahiri. “Miyeyusho ya kristoloidi [kama myeyusho-chumvi na myeyusho-maziwa-chumvi wa kawaida wa Ringer], Deksitrani na HES haina sumu na si ghali kwa kulinganishwa, inapatikana kwa utayari, inaweza kuwekwa katika hali-joto ya chumbani, haihitaji uchunguzi ili kufaana na damu na haina hatari ya magonjwa yanayopitishwa kwa utiwaji-damu mishipani.”—Blood Transfusion Therapy—A Physician’s Handbook, 1989.
Hata hivyo huenda ukauliza, ‘Kwa nini umajimaji usio damu wa kurudisha kiasi cha damu mahali pa kilichopotezwa hufanya kazi ikiwa mimi nahitaji chembe nyekundu kupeleka oksijeni kotekote mwilini?’ Kama ilivyotajwa, wewe una akiba ya kupeleka oksijeni. Ukipoteza damu, mifumo ya ajabu ya kulipia huanza kufanya kazi. Moyo wako huanza kupiga damu nyingi zaidi kwa kila mpigo. Kwa kuwa umajimaji unaofaa ulitiwa mahali pa damu iliyopotezwa, ile damu ambayo sasa imechanganywa umajimaji hutiririka kwa urahisi zaidi, hata katika ile mishipa midogo. Kama tokeo la badiliko la kikemikali, oksijeni zaidi inaachiliwa iingie katika tishu. Ujipatanishaji huu mbalimbali ni wenye mafanikio sana hivi kwamba kama nusu tu ya chembe zako nyekundu ndiyo inayobaki, upelekaji oksijeni waweza kuwa asilimia 75 ya ule wa kawaida. Mgonjwa anayepumzika hutumia asilimia 25 tu ya oksijeni inayopatikana katika damu yake. Na nusukaputi nyingi inayoathiri mwili mzima hupunguza sana uhitaji wa mwili kupokea oksijeni.
MADAKTARI WAWEZA KUSAIDIAJE?
Matabibu stadi wanaweza kumsaidia mtu ambaye amepoteza damu na hivyo ana chembe nyekundu chache zaidi. Mara kiasi cha damu kikiisha kurudishwa, madaktari waweza kumtia oksijeni kwa kiwango cha juu sana. Jambo hilo linafanya ipatikane zaidi kwa ajili ya mwili na mara nyingi imekuwa na matokeo makubwa sana. Madaktari Waingereza walitumia njia hiyo kwa mwanamke aliyekuwa amepoteza damu nyingi sana hivi kwamba “hemoglobini yake ilishuka kufikia g/dlita 1.8. Alitibiwa kwa mafanikio . . . [kwa] mishindilio ya oksijeni iliyovuviwa sana na utiwaji mishipani wa myeyusho wa gelatini [Haemaccel].” (Anaesthesia, Januari 1987) Ripoti hiyo husema pia kwamba wengine wenye kupoteza damu sana wametibiwa kwa mafanikio katika machemba ya oksijeni yenye kanieneo kubwa zaidi ya kawaida.
Pia matabibu wanaweza kusaidia wagonjwa wao kufanyiza chembe nyekundu zaidi. Jinsi gani? Kwa kuwapa (misulini au mishipani) mitayarisho yenye chuma, ambayo yaweza kusaidia mwili kufanyiza chembe nyekundu kwa haraka zaidi mara tatu au nne ya kawaida. Hivi majuzi msaada mwingine umekuwa wenye kupatikana. Mafigo yako hufanyiza hormoni inayoitwa erithropoietini (EPO), inayochochea uroto kufanyiza chembe nyekundu. Sasa EPO iliyosanisiwa (kiunganisho-upya) inapatikana. Madaktari wanaweza kuwapa baadhi ya wagonjwa waliopungukiwa sana damu, na hivyo kuwasaidia wafanyize kwa haraka sana chembe nyekundu badala ya zilizopotezwa.
Hata wakati wa upasuaji, madaktari wapasuaji na wataalamu wa nusukaputi walio stadi na wenye kudhamiria wanaweza kusaidia kwa kutumia njia zilizofanyiwa maendeleo sana za kuokoa damu. Mbinu zenye uangalifu mwingi sana za upasuaji, kama vile kuchoma kwa umeme (electrocautery) ili kupunguza kutokwa damu, zapasa zisisitiziwe sana-sana. Nyakati nyingine damu inayotiririka ndani ya kidonda yaweza kufyonzwa, kuchujwa, na kuelekezwa kurudi ndani ya mzunguko.b
Wagonjwa wanaotibiwa kwa mashine ya kusaidia moyo na mapafu iliyojazwa umajimaji usio damu wanaweza kunufaika kwa tokeo la mpunguzo wa chembe na vitu vigumu katika damu (hemodilution), kukiwa na chembe nyekundu chache sana zinazopotezwa.
Na kuna njia nyingine za kusaidia. Kumpoza mgonjwa ili kupunguza uhitaji wake wa oksijeni wakati wa upasuaji. Upotezaji fahamu kwa kutumia nusukaputi ili kushusha sana kanieneo ya damu. Utibabu wa kuendeleza mgando wa damu. Desmopressin (DDAVP) ili kufupisha muda wa kutokwa damu. Leza ‘skalpeli’ (kijisu chenye mnururisho kinachotumiwa katika upasuaji). Utaona kwamba orodha ya njia za kusaidia huongezeka kadiri matabibu na wagonjwa wanavyotafuta kuepuka utiaji-damu mishipani. Sisi tunatumaini kwamba wewe hutapoteza kamwe kiasi kikubwa cha damu. Lakini ukipoteza, inaelekea sana kwamba madaktari stadi wangeweza kukutunza bila kutumia utiaji-damu mishipani, ambao una hatari nyingi sana.
UPASUAJI, NDIYO—LAKINI BILA UTIAJI-DAMU MISHIPANI
Leo watu wengi hawatapokea damu. Kwa sababu za kiafya, wao wanaomba jambo ambalo Mashahidi hutafuta sana-sana kwa msingi wa kidini: utibabu bora kwa kutumia njia nyingine zisizotumia damu. Kama tulivyoona, upasuaji mkubwa ungali unawezekana. Kama una tashwishi zinazokawia-kawia, uthibitisho mwingine kutoka fasihi za kitiba huenda ukazifukuzia mbali.
Ile makala “Kuwekwa kwa Viungo Vinne Vikubwa Badala ya Vilivyoharibika Katika Mshiriki wa Mashahidi wa Yehova” (Orthopaedic Review, Agosti 1986) ilisimulia juu ya mgonjwa mwenye kupungukiwa damu aliyekuwa na “uharibifu ulioendelea sana wa magoti na nyonga zote mbili.” Dextran ya chuma ilitumiwa kabla na baada ya upasuaji uliofanywa, ambao ulifanikiwa. Jarida British Journal of Anaesthesia (1982) liliripoti juu ya Shahidi mwenye umri wa miaka 52 aliyekuwa na kiwango cha hemoglobini kilichokuwa chini ya 10. Kwa kutumia njia ya hypotensive anesthesia (upotezaji fahamu kwa kutumia nusukaputi ili kushusha sana kanieneo ya damu) kupunguza upotezaji damu, nyonga na bega lake vilibadilishwa kabisa na kuwekwa vingine. Kikundi cha upasuaji kwenye Chuo Kikuu cha Arkansas (U.S.A.) kilitumia pia njia ii hii kubadilisha nyonga mia moja na kuweka nyingine kwa Mashahidi na wagonjwa wote wakapona. Profesa aliyekuwa akiongoza idara hiyo atoa elezo hili: “Jambo ambalo tumejifunza kutoka kwa wagonjwa hao (Mashahidi), tunatumia sasa kwa wagonjwa wetu wote ambao [tunabadilisha] nyonga kabisa.”
Dhamiri za baadhi ya Mashahidi huwaruhusu wapokee mapandikizo ya viungo yakifanywa bila damu. Ripoti moja juu ya mapandikizo 13 ya figo ilifikia mkataa huu: “Matokeo ya ujumla huonyesha kwamba upandikizaji wa mafigo unaweza kutumiwa kwa Mashahidi wa Yehova kwa usalama na kwa mafanikio.” (Transplantation, Juni 1988) Vivyo hivyo, kukataa damu hakukuzuia hata mapandikizo ya moyo yenye mafanikio.
Huenda ukauliza, ‘Namna gani upasuaji wa namna nyingine usiotumia damu?’ Jarida Medical Hotline (Aprili/Mei 1983) lilisimulia juu ya “Mashahidi wa Yehova waliopata mipasuo mikubwa ya viungo vya uzazi vya wanawake na iliyohusu mimba na kuzaa [kwenye Chuo Kikuu cha Mkoa wa Wayne, U.S.A.] bila utiaji-damu mishipani.” Karatasi-habari iliripoti hivi: “Hakukuwa na vifo na matatanisho zaidi kuliko ilivyokuwa katika wanawake waliokuwa wamepata upasuaji unaofanana na huo pamoja na utiwaji-damu mishipani.” Ndipo karatasi-habari ikatoa maelezo haya: “Matokeo ya uchunguzi huu huenda yakatoa sababu ya kuchunguza upya utumizi wa damu kwa wanawake wote wanaopata mipasuo ya viungo vya uzazi na inayohusu mimba na kuzaa.”
Kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha Göttingen (Ujeremani), wagonjwa 30 waliokataa damu walipata upasuaji wanaofanyiwa watu wengi. “Hakuna matatanisho yaliyotokea ambayo hayangaliweza kutokea pia kwa wagonjwa wanaopokea utiwaji-damu mishipani. . . . Kwamba kutumia utiaji-damu mishipani hakuwezekani hakupasi kukadiriwa kupita kiasi, na hivyo hakupasi kuongoza kwenye kuacha kufanya upasuaji unaohitajiwa kabisa na ulio haki kufanywa kwa njia ya kupasua.”—Risiko in der Chirurgie, 1987.
Hata upasuaji wa ubongo bila kutumia damu umefanywa juu ya watu wazima na watoto wengi, mathalani, kwenye Kitovu cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha New York. Katika 1989 Dakt. Joseph Ransohoff, kiongozi wa upasuaji wa neva, aliandika: “Ni wazi sana kwamba katika visa vilivyo vingi ujiepushaji na vitu vilivyofanyizwa kwa damu waweza kufikiwa kukiwa na hatari kidogo sana kwa wagonjwa walio na itikadi za kidini dhidi ya utumizi wa vifanyizo hivyo, hasa ikiwa upasuaji utafanywa mara hiyo na kwa muda mfupi wa kupasua kwa uhusianifu. Wenye kupendeza sana ni uhakika wa kwamba mimi mara nyingi husahau kwamba mgonjwa ni Shahidi mpaka wakati wa kumwachilia wanaponishukuru kwa kuwa nilistahi imani zao.”
Hatimaye, je! upasuaji mgumu unaohusu moyo na mishipa waweza kufanywa juu ya watu wazima na watoto bila damu? Dakt. Denton A. Cooley alikuwa mtangulizi katika kufanya jambo ilo hilo. Kama unavyoweza kuona katika makala ya kitiba iliyochapwa upya katika Nyongeza, katika kurasa 27-9, ukitegemea uchanganuzi wa mapema zaidi, mkataa wa Dakt. Cooley ulikuwa “kwamba hatari ya upasuaji katika kikundi cha wagonjwa Mashahidi wa Yehova haikuwa juu sana kuliko ya [vikundi] vingine.” Sasa, baada ya kufanya 1,106 ya mipasuo hii, yeye aandika: “Katika kila kisa mwafaka au mkataba wangu na mgonjwa hudumishwa,” yaani, kutotumia damu.
Madaktari wapasuaji wameona kwamba mtazamo mzuri ni jambo jingine walilo nalo Mashahidi wa Yehova. “Mtazamo wa wagonjwa hawa umekuwa kielelezo kizuri,” akaandika Dakt. Cooley katika Oktoba 1989. “Wao hawana hofu waliyo nayo wagonjwa walio wengi ya matatanisho au hata ya kifo. Wana imani yenye kina na yenye kudumu katika itikadi yao na katika Mungu wao.”
Hii haimaanishi kwamba wao husisitizia haki ya kufa. Wao hufuatia kwa bidii utunzaji bora kwa sababu wanataka kupona. Wamesadikishwa kwamba kutii sheria ya Mungu juu ya damu ni jambo la hekima, jambo ambalo linakuwa na uvutano chanya katika upasuaji usiotumia damu.
Profesa Dakt. V. Schlosser, wa hospitali ya upasuaji kwenye Chuo Kikuu cha Freiburg (Ujeremani), aliandika: “Miongoni mwa wagonjwa wa kikundi hiki, tukio la kutokwa damu wakati wa pindi ya upasuaji halikuwa la juu zaidi; kwa vyovyote, matatanisho yalikuwa machache zaidi. Yale maoni ya pekee juu ya ugonjwa, waliyo nayo Mashahidi wa Yehova, yalikuwa na uvutano chanya wakati wa pindi ya upasuaji.”—Herz Kreislauf, Agosti 1987.
[Maelezo ya Chini]
a Mashahidi wa Yehova hawapokei kutiwa mishipani damu nzima, chembe nyekundu, chembe nyeupe, visahani-damu, au plazima ya damu. Kwa habari ya visehemu vidogo, kama vile globyulini za kinga, ona Mnara wa Mlinzi wa Juni 1, 1990, kurasa 30-1.
b Mnara wa Mlinzi wa Machi 1, 1989, kurasa 30-1, huzungumzia kanuni za Biblia zinazohusu njia za kuokoa damu na vifaa vya kuzungushia damu (nje ya mwili).
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
‘‘Lazima sisi tukate kauli kwamba kwa sasa kuna wagonjwa wengi wanaopokea sehemu za damu wasio na nafasi ya kunufaishwa na utiwaji-damu mishipani (damu haihitajiwi) na hata hivyo wana hatari kubwa ya kuwa na athari isiyotakwa. Hakuna tabibu ambaye kwa kujua angemweka mgonjwa katika hali ya kupata utibabu usioweza kusaidia bali uwezao kudhuru, lakini hivyo ndivyo inavyotukia hasa wakati damu inapotiwa mishipani bila kuhitajiwa kabisa.”—“Transfusion-Transmitted Viral Diseases,” 1987.
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
‘‘Baadhi ya watungaji wametaarifu kwamba hemoglobini ya kiasi cha chini kama vile gm. 2 hadi 2.5/100ml. huenda ikapokeleka. . . . Mtu mwenye afya huenda akavumilia kupoteza asilimia 50 ya tungamo la chembe nyekundu za damu na awe karibu bila dalili zozote za ugonjwa ikiwa kupoteza damu huko kwatukia kwa kipindi fulani cha wakati.”—“Techniques of Blood Transfusion,” 1982.
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
‘‘Dhana za kale juu ya usafirishaji wa oksijeni kwenye tishu, kuponesha vidonda, na ‘thamani ya ulishaji mwili’ ya damu zinaachwa. Yaliyoonwa katika kushughulika na wagonjwa Mashahidi wa Yehova huonyesha kwamba upungufu mkubwa sana wa damu unavumiliwa vema.”—“The Annals of Thoracic Surgery,” Machi 1989.
[Sanduku katika ukurasa wa 16]
Watoto wadogo pia? “Mipasuo 48 ya moyo iliyohusu watoto wadogo ilifanywa kwa mbinu za kutotumia damu bila kujali hali ya utata wa njia ya kupasua.” Watoto hao walikuwa wadogo kama kilo 4.7. “Kwa sababu ya fanikio lenye kuendelea katika Mashihidi wa Yehova na uhakika wa kwamba utiaji-damu mishipani huwa na hatari ya matatanisho mabaya, kwa sasa tunafanya iliyo mingi ya mipasuo yetu ya moyo kwa watoto bila utiaji-damu mishipani.”—“Circulation,” Septemba 1984.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mashine ya kusaidia moyo na mapafu imekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wa upasuaji wa moyo ambao hawataki damu