Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • sh sura 14 kur. 329-343
  • Kutokuamini kwa Kisasa—Je! Jitihada ya Kutafuta Yapasa Kuendelea?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutokuamini kwa Kisasa—Je! Jitihada ya Kutafuta Yapasa Kuendelea?
  • Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo Mabaya ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini
  • Shambulizi la Sayansi na Falsafa
  • Mridhiano Mkubwa
  • Msingi wa Imani Katika Mungu
  • Kwa Njia ya Nasibu au kwa Njia ya Ubuni?
  • Uthibitisho Tele Kutuzunguka Sisi
  • Biblia—Je! Waweza Kuiamini?
  • Kukabili Tatizo la Kutokuamini
  • Chanzo cha Ulimwengu na Uhai Ni Nini?
    Amkeni!—2002
  • Unaweza Kupata Wapi Majibu?
    Amkeni!—2004
  • Sayansi, Dini, na Jitihada ya Kutafuta Kweli
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Chanzo Kisicho na Kifani cha Hekima Bora
    Ni Nini Lililo Kusudi la Uhai?
Pata Habari Zaidi
Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
sh sura 14 kur. 329-343

Sura 14

Kutokuamini kwa Kisasa—Je! Jitihada ya Kutafuta Yapasa Kuendelea?

“Mungu si jambo la kawaida tena la kuhangaikiwa na wanadamu. Wanamkumbuka tu mara chache-chache wanapoendelea na shughuli za siku zao au wanapofanya maamuzi yao. . . . Mahali pa Mungu pamechukuliwa na mapendezi mengine: mapato na uzalishaji bidhaa. Huenda wakati mmoja akawa alionwa kuwa chanzo cha maana kwa ajili ya utendaji wote wa kibinadamu, lakini leo amehamishwa akapelekwa chini kwenye magereza ya siri ya historia. . . . Mungu ametokomea katika fahamu za jamii ya binadamu.”—The Sources of Modern Atheism.

1. (Tia ndani utangulizi.) (a) Kitabu The Sources of Modern Atheism chaelezaje imani katika Mungu miongoni mwa watu leo? (b) Ukosefu wa kisasa wa imani unatofautianaje sana na hali zilizokuwako si miaka mingi iliyopita?

SI MIAKA mingi iliyopita Mungu alipokuwa sehemu kubwa sana ya maisha za watu wa ulimwengu wa Magharibi. Ili mtu akubalike kijamii, alipaswa kutoa thibitisho la imani katika Mungu, hata ikiwa si kila mtu aliyezoea kwa juhudi yale aliyodai kuamini. Mtu akiwa na shaka na tashwishi zozote alijitunzia mwenyewe kwa busara. Kuzisema hadharani kungeshtua na labda hata kumfanya mtu alaumiwe.

2. (a) Ni kwa nini watu wengi wameacha kutafuta Mungu? (b) Ni maswali gani lazima yaulizwe?

2 Hata hivyo, leo, mambo yamebadilika. Kuwa na usadikisho wowote wenye nguvu wa kidini huonwa na wengi kuwa ni akili kidogo, maneno makavu, hata ushupavu wa kidini. Katika mabara mengi, twaona ubaridi, au ukosefu mkubwa wa kutopendezwa na Mungu na dini. Watu walio wengi hawatafuti Mungu tena kwa sababu hawaamini yupo au hawana hakika juu ya hilo. Kwa kweli, wengine wametumia usemi “baada ya Ukristo” ili kueleza muhula wetu. Kwa hiyo, lazima maswali fulani yaulizwe: Wazo la Mungu lilikujaje kuondoshwa mbali maishani mwa watu? Ni kani zipi zilizotokeza badiliko hilo? Je! kuna sababu timamu za kuendelea kutafuta Mungu?

Matokeo Mabaya ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini

3. Tokeo moja la Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Uprotestanti lilikuwa nini?

3 Kama tulivyoona katika Sura 13, Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Uprotestanti ya karne ya 16 yalitokeza badiliko kubwa katika namna ambayo watu waliona mamlaka, ya kidini au nyingineyo. kujidai na uhuru wa kujieleza vikachukua mahali pa utii na unyenyekeo. Ingawa watu walio wengi walibakia katika mwundo wa dini ya kimapokeo, wengine walisonga kwenye upande wa kutaka mapinduzi zaidi, wakitilia shaka imani zisizo na msingi na mafundisho ya kimsingi ya makanisa yaliyoimarishwa. Bado wengine, kwa kuona sehemu ambayo dini ilikuwa imeshiriki katika kufanyiza vita, taabu, na ukosefu wa haki katika historia yote, wakawa wanatilia shaka dini kwa ujumla.

4. (a) Maandishi ya wakati huo yalisimuliaje kadiri ya uatheisti katika Uingereza na Ufaransa katika karne za 16 na 17? (b) Ni nani waliojitokeza wazi kama tokeo la jitihada zilizofanywa wakati wa Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya kutupilia mbali kongwa la kipapa?

4 Mapema katika 1572, ripoti moja yenye kichwa Discourse on the Present State of England ilisema: “Milki hii imegawanywa kuwa vyama vitatu, Wapapa, Waatheisti, na Waprotestanti. Vyote vitatu vyapendelewa kwa kadiri ile ile: kile cha kwanza na cha pili kwa sababu, vina wengi, hatuthubutu kuvipendeza.” Na kadirio jingine lilitoa tarakimu ya 50,000 kuwa hesabu ya waatheisti katika Paris mwaka 1623, ingawa usemi huo ulitumiwa bila usahihi mno. Vyovyote vile, ni wazi kwamba Mapinduzi Makubwa ya Kidini, katika jitihada yayo ya kuondoa upigaji ubwana wa mamlaka ya kipapa, yalikuwa yametokeza wazi pia wale waliopinga cheo cha dini zilizoimarishwa. Ni kama walivyosema Will na Ariel Durant katika The Story of Civilization: Part VII—The Age of Reasons Begins: “Wenye kufikiri wa Ulaya—watangulizi wa akili ya Kiulaya—hawakuwa tena wakizungumza juu ya mamlaka ya papa; walikuwa wakijadili kuwapo kwa Mungu.

Shambulizi la Sayansi na Falsafa

5. Ni kani gani zilizoharakisha kutokea kwa ukosefu wa imani katika Mungu?

5 Kuongezea farakano la Jumuiya ya Wakristo yenyewe, kulikuwako kani nyingine zenye kufanya kazi ambazo zilidhoofisha zaidi msimamo wayo. Sayansi, falsafa, kufuatia mambo ya kilimwengu, na kufuatia mali vilitimiza mafungu yavyo katika kutokeza shaka na kusitawisha shaka juu ya Mungu na dini.

6. (a) Mpanuko wa maarifa ya kisayansi uliathirije mengi ya mafundisho ya kanisa? (b) Wengine waliojiona kuwa wa kisasa walifanya nini?

6 Mpanuko wa maarifa ya kisayansi ulitilia shaka mafundisho mengi ya kanisa ambayo msingi wayo ulikuwa ufasiri wenye kosa wa vifungu vya Biblia. Kwa kielelezo, mavumbuzi ya nyota ya watu kama Koperniko na Galileo yalibisha moja kwa moja fundisho la kanisa la kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu wote mzima. Kuongezea hayo, kuelewa sheria za asili zinazoongoza taratibu za ulimwengu wa halisi kukafanya isiwe lazima tena kuhesabu yaliyokuwa mpaka wakati huo ni maajabu ya kifumbo, kama vile radi na umeme au hata kutokea kwa nyota fulani na zile zenye mkia, kuwa ni mkono au tendo la Mungu. “Miujiza” na “kujiingiza kimungu” katika mambo ya kibinadamu pia vikaja kutiliwa shaka. Kwa ghafula, Mungu na dini vikaonekana kuwa vitu vya kikale kwa wengi, na baadhi ya wale waliojiona kuwa watu wa kisasa wakampa Mungu kisogo upesi na kumiminika kwenye ibada ya ng’ombe mtakatifu wa sayansi.

7. (a) Bila shaka ni nini lililokuwa pigo kali zaidi kwa dini? (b) Itikio la makanisa kwa nadharia ya Darwin lilikuwa nini?

7 Pigo kali zaidi kwa dini, bila shaka, lilikuwa ni nadharia ya mageuzi. Katika 1859 yule Mwingereza Charles Darwin (1809-82), mchunguzi wa maumbile, alichapisha kitabu chake Origin of Species na kutokeza ubishi wa moja kwa moja kwa fundisho la uumbaji wa Mungu la Biblia. Itikio la makanisa lilikuwa nini? Hapo kwanza makasisi wa Uingereza na kwingineko walishutumu vikali nadharia hiyo. Lakini upesi upinzani ukafifia. Ikaonekana kama kwamba madhanio ya Darwin ndiyo udhuru uliotafutwa na makasisi wengi waliokuwa na shaka kisiri. Kwa hiyo, katika muda wa maisha ya Darwin, “makasisi wenye kufikiri zaidi na wenye kusema sana walikuwa wamefikia mkataa wa kwamba mageuzi yalipatana kabisa na kuelewa kulikonurishwa kwa andiko,” chasema The Encyclopedia of Religion. Badala ya kutetea Biblia, Jumuiya ya Wakristo ilishindwa na mkazo wa rai ya kisayansi ikafuata kilichopendwa na wengi. Katika kufanya hivyo, ilibomoa imani katika Mungu.—2 Timotheo 4:3, 4.

8. (a) Wahakiki wa dini wa karne ya 19 walitilia shaka nini? (b) Ni nini baadhi ya nadharia zenye kupendwa na wengi zilizopendekezwa na wahakiki wa dini? (c) Ni kwa nini watu wengi walikubali kwa upesi mawazo ya kupinga dini?

8 Kwa kadiri karne ya 19 ilivyoendelea, wahakiki wa dini wakawa wajasiri zaidi katika shambulizi lao. Wakiwa hawatosheki tu na kutaja kasoro za makanisa, walianza kutilia shaka msingi wenyewe wa dini. Walitokeza maswali kama haya: Mungu ni nini? Kwa nini kuna uhitaji wa Mungu? Imani katika Mungu imekuwa na tokeo gani kwa jamii ya kibinadamu? Wanaume kama vile Ludwig Feuerbach, Karl Marx, Sigmund Freud, na Friedrich Nietzsche walitoa hoja zao katika semi za kifalsafa, kisaikolojia, na kisosholojia. Nadharia kama vile ‘Mungu si kitu ila ni ubuni wa mawazio ya binadamu,’ ‘Dini ni kasumba ya watu,’ na ‘Mungu ni mfu’ zote zilisikika kuwa mpya na zenye kusisimua kwa kulinganisha na mafundisho yasiyo na msingi na mapokeo yasiyoeleweka ya makanisa. Ilionekana kama kwamba hatimaye watu wengi walikuwa wamepata njia ya kiakili ya kueleza shaka na tuhuma ambazo zilikuwa zimejibanza katika akili zao. Upesi na kwa nia wakakubali mawazo hayo kuwa kweli mpya ya gospeli.

Mridhiano Mkubwa

9. (a) Makanisa yalifanya nini yalipokuwa chini ya shambulizi la sayansi na falsafa? (b) Matokeo ya mridhiano wa makanisa yalikuwa nini?

9 Chini ya shambulizi na upekuzi wa sayansi na falsafa, makanisa yalifanya nini? Badala ya kuchukua msimamo kwa ajili ya yale ambayo Biblia hufundisha, walikubali kushindwa na mikazo wakaridhiana hata katika kanuni za kimsingi za imani kama vile uumbaji wa Mungu na uasilia wa Biblia. Tokeo likawa nini? Makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yalipoteza sifa, na watu wengi wakaanza kupoteza imani. Kushindwa kwa makanisa kujitetea kuliacha mlango wazi kabisa kwa umati wa watu utoke nje. Kwa watu wengi, dini ikawa ni kikumbusho tu cha kisosholojia, kitu cha kutia alama ya mambo makubwa maishani mwa mtu—kuzaliwa, ndoa, kifo. Wengi kwa ujumla waliacha kutafuta Mungu wa kweli.

10. Ni maswali gani ya uharaka ambayo lazima yachunguzwe?

10 Kwa sababu ya yote hayo, ni jambo la kusababu kuzuri kuuliza: Je! sayansi na falsafa kwa hakika zimeua imani katika Mungu? Je! kushindwa kwa makanisa kwamaanisha kushindwa kwa kile wanachodai kufundisha, yaani, Biblia? Naam, je! jitihada ya kutafuta Mungu yapasa iendelee? Acheni tuchunguze kifupi masuala haya.

Msingi wa Imani Katika Mungu

11. (a)  Ni vitabu gani viwili ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa msingi wa imani katika Mungu? (b) Vitabu hivi vimekuwa na matokeo gani juu ya watu?

11 Imesemwa kwamba kuna vitabu viwili vinavyotuambia juu ya kuwapo kwa Mungu—“kitabu” cha uumbaji, au maumbile yanayotuzunguka, na Biblia. Vimekuwa ndivyo msingi wa imani kwa mamilioni ya watu wa wakati huu na uliopita. Kwa kielelezo, mfalme mmoja wa karne ya 11 K.W.K., kwa kustaajabishwa na aliyoona katika mbingu zenye nyota, alipaaza sauti kishairi hivi: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.” (Zaburi 19:1) Katika karne ya 20, mwanaanga mmoja, akitazama sura yenye uzuri wa ajabu ya dunia akiwa kwenye chombo chake cha angani kilipokuwa kikizunguka mwezi, alichochewa akariri: “Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.”—Mwanzo 1:1, KJ.

12. Kitabu cha uumbaji na Biblia vimekuwaje chini ya shambulizi?

12 Hata hivyo, vitabu viwili hivi vinashambuliwa na wale wasiodai kuwa na imani katika Mungu. Wanasema kwamba uchunguzi wa kisayansi wa ulimwengu unaotuzunguka umethibitisha kwamba uhai ulitokea si kwa uumbaji wa mwenye akili bali kwa nasibu tu na hatua ya hobelahobela ya mageuzi. Kwa hiyo, hutoa hoja kwamba hakukuwako Muumba na kwamba kwa hiyo suala la Mungu halizuki. Zaidi ya hayo, wengi wao huamini kwamba Biblia ni ya kikale na haipatani na kufikiri kuzuri, kwa hiyo, haistahili kuaminiwa. Kwa hiyo, kwa upande wao, hakuna tena msingi wowote wa imani katika kuwapo kwa Mungu. Je! yote hayo ni kweli? Mambo ya hakika yaonyesha nini?

Kwa Njia ya Nasibu au kwa Njia ya Ubuni?

13. Ni nini kingepaswa kutukia ili uhai utokee kwa nasibu?

13 Ikiwa hakungalikuwako Muumba, basi lazima uhai uwe ulijitokeza wenyewe kwa nasibu. Ili uhai ujitokeze, kwa namna fulani kemikali zinazofaa zingalipaswa kuungana kwa vipimo vinavyofaa, katika vipimo vinavyofaa vya joto na kanieneo na mambo mengine yenye kudhibiti, na vyote hivyo vingalipasa kudumishwa kwa urefu sahihi wa wakati. Zaidi ya hayo, ili uhai uanze na kuendelezwa juu ya dunia, matukio hayo ya nasibu yangalipaswa kurudiwa mara maelfu. Lakini uwezekano wa tukio hata moja hilo kutokea ni nini?

14. (a) Uwezekano wa kwamba molekyuli-protini sahili moja ya protini itafanyizwa kwa nasibu ni mdogo sana kadiri gani? (b) Kadirio la kihisabati laathirije wazo la uhai kujitokeza wenyewe?

14 Wanamageuzi hukubali kwamba uwezekano wa atomi na molekyuli zinazofaa kuanguka mahali pazo ili kufanyiza molekyuli-protini sahili moja tu ni 1 katika 10113, au 1 ikifuatwa na sifuri 113. Hesabu hiyo ni kubwa zaidi ya jumla ya hesabu iliyokadiriwa ya atomi katika ulimwengu wote mzima! Wataalamu wa hisabati husema halitokei kamwe lolote ambalo lina uwezekano wa kutokea unaopungua 1 katika 1050. Lakini nyingi zaidi ya molekyuli moja sahili ya protini zahitajiwa kwa ajili ya uhai. Protini tofauti 2,000 hivi zahitajiwa ili tu chembe moja idumishe utendaji wayo, na uelekeo wa kwamba zote zitajitokeza kwa nasibu tu ni 1 katika 1040,000! “Ikiwa mtu hasukumwi na imani za kijamii au mazoezi ya kisayansi asadiki kwamba uhai ulikuwa na chanzo [cha kujitokeza tu] Duniani, kadirio hili rahisi lafanya kabisa wazo hilo lisifae kujadiliwa,” asema mtaalamu wa anga na nyota Fred Hoyle.

15. (a) Wanasayansi wamevumbua nini katika uchunguzi wao wa ulimwengu halisi? (b) Profesa mmoja wa fizikia alisema nini juu ya sheria katika maumbile?

15 Kwa upande mwingine, kwa kuchunguza ulimwengu wa halisi, tangu visehemu vidogo sana vya kitone cha atomi hadi magalaksi makubwa, wanasayansi wamegundua kwamba ajabu zote za asili zinazojulikana yaelekea hufuata sheria fulani za msingi. Maana yake, wamegundua hoja na utaratibu katika kila jambo linalotukia katika ulimwengu wote mzima, nao wameweza kueleza kufikiri kuzuri na utaratibu huo katika semi sahili za kihisabati. “Ni wanasayansi wachache wanaoweza kukosa kuvutiwa na usahili na ustadi wa sheria hizi ambao karibu uwe usioweza kuwazika,” aandika profesa mmoja wa fizikia, Paul Davies, katika gazeti New Scientist.

16. (a) Ni nini baadhi ya vitu visivyobadilika vya kimsingi katika sheria za asili? (b) Ni nini kingetokea kama kanuni za vitu hivyo visivyobadilika zingebadilishwa kidogo sana tu? (c) Profesa mmoja wa fizikia alikataje maneno juu ya ulimwengu wote mzima na kuwapo kwetu?

16 Hata hivyo, uhakika wenye kuvutia sana juu ya sheria hizo ni kwamba katika hizo kuna mambo fulani hakika ambayo kanuni zayo lazima ziwekwe barabara kwa ajili ya ulimwengu wote mzima, kama tuujuavyo, ili uwepo. Miongoni mwa mambo hayo ya msingi yasiyobadilika ni kizio cha chaji ya umeme kwenye protoni, msongamano wa masi (matungamo) za vichembe fulani vya msingi, na uvutano usiobadilika uliovumbuliwa na Newton wa ulimwengu wote mzima, ambao kwa kawaida huwakilishwa na herufi G. Kuhusu hilo Profesa Davies aendelea hivi: “Hata vigeu-geu vidogo katika kanuni za baadhi yazo vingebadilisha sana sura ya Ulimwengu Wote Mzima. Kwa kielelezo, Freeman Dyson ametaja kwamba kama kani kati ya nyukleoni (protoni na nyutroni) ingekuwa na nguvu zaidi kwa asilimia chache, Ulimwengu Wote Mzima ungekosa haidrojeni. Nyota kama Jua, licha ya maji, hazingekuwapo. Uhai, angalau kama tuujuavyo, ungekuwa hauwezekani. Brandon Carter ameonyesha kwamba mabadiliko madogo zaidi ya G yangebadili nyota zote kuwa blue giants (hatua ambayo nyota hufikia upevu wayo) au red dwarfs (hatua ambayo nyota hudidimia na kulipuka), na kuwe matokeo mabaya kama hayo juu ya uhai.” Kwa hiyo, Davies amalizia hivi: “Katika kisa hiki yawazika kwamba kwaweza kuwako Ulimwengu Wote Mzima mmoja tu. Ikiwa ndivyo, ni wazo lenye kutokeza kwamba kule kuwapo kwetu kwenyewe tukiwa watu wenye fahamu ni tokeo lisilokanushika la kusababu kuzuri.”—Italiki ni zetu.

17. (a) Ubuni na kusudi katika ulimwengu wote mzima vyaonyesha nini waziwazi? (b) Hilo lathibitishwaje katika Biblia?

17 Twaweza kukata kauli gani kutokana na yote hayo? Kwanza kabisa, ikiwa ulimwengu wote mzima unaongozwa na sheria, basi lazima pawe mfanya sheria mwenye akili ambaye alifanyiza au kusimamisha sheria hizo. Zaidi ya hayo, kwa kuwa sheria zinazoongoza utendaji wa ulimwengu wote mzima zaonekana zilifanywa kukiwa na taraja la uhai na hali zinazofaa kuuendeleza, kusudi lahusika kwa wazi. Ubuni na kusudi—hizo si sifa za nasibu isiyo na lengo; hizo hasa ndizo Muumba mwenye akili angedhihirisha. Na hilo ndilo Biblia hasa yajulisha rasmi hivi: “Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake.”—Warumi 1:19, 20; Isaya 45:18; Yeremia 10:12.

Uthibitisho Tele Kutuzunguka Sisi

18. (a) Ubuni na kusudi vyaweza kuonekana katika nini kingine? (b) Unaweza kutoa vielelezo gani vingine vyenye kujulikana sana vya ubuni wenye akili? (b) Twaweza kujifunza nini kwa kuchunguza ulimwengu unaotuzunguka?

18 Bila shaka, ubuni na kusudi vyaonekana si katika utendaji tu wa utaratibu wa ulimwengu wote mzima bali pia katika njia ambayo viumbe vilivyo hai, sahili na vilivyotatanika, huendeleza utendaji wavyo wa kila siku, na pia katika njia ambayo vinatenda kwa uhusiano wa vyenyewe kwa vyenyewe na pamoja na mazingira. Kwa kielelezo, karibu kila sehemu ya mwili wetu wa kibinadamu—ubongo, jicho, sikio, mkono—huonyesha ubuni uliotatanika sana hivi kwamba sayansi ya kisasa haiwezi kuufafanua kikamili. Kisha kuna malimwengu ya wanyama na ya mimea. Mhamo wa kila mwaka wa ndege fulani kwa maelfu ya kilometa za bara na bahari, utaratibu wa usanisi (photosynthesis) katika mimea, ukuzi wa yai lililorutubishwa kuwa kiumbe kilichotatanika chenye mamilioni ya chembe-chembe zilizotofautishwa zenye kazi maalumu—tukitoa vielelezo vichache tu—yote hayo ni uthibitisho wenye kutokeza wa ubuni wa kiakili.a

19. (a) Je! ufafanuzi wa kisayansi wa jinsi vitu fulani hufanya kazi wathibitisha kwamba hakuna ubuni au mbuni mwenye akili?

19 Hata hivyo, wengine hubisha kwamba maarifa yaliyoongezeka ya sayansi yametoa mafafanuzi kuhusu mengi ya maajabu hayo. Ni kweli sayansi imefafanua, kwa kadiri fulani, vitu vingi ambavyo wakati mmoja vilikuwa fumbo. Lakini uvumbuzi wa mtoto jinsi saa inavyofanya kazi hauthibitishi kwamba saa hiyo haikubuniwa na kutengenezwa na mtu fulani. Vivyo hivyo, kuelewa kwetu njia za ajabu ambazo katika hizo vingi vya vitu katika ulimwengu halisi vyafanya kazi hakuthibitishi kwamba hakuna mbuni mwenye akili aliyevifanyiza. Kinyume cha hilo, kadiri tunavyojua mengi zaidi juu ya ulimwengu unaotuzunguka sisi, ndivyo tulivyo na uthibitisho zaidi wa kuwapo kwa Muumba mwenye akili, Mungu. Kwa hiyo, tukiwa na akili iliyo tayari kujifunza, twaweza kukubaliana na mtunga zaburi alipokiri: “Ee BWANA [Yehova, NW], jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.”—Zaburi 104:24.

Biblia—Je! Waweza Kuiamini?

20. Ni nini kinachoonyesha kwamba kuamini tu Mungu hakutoshi kusukuma mtu amtafute?

20 Hata hivyo, kuamini tu juu ya kuwapo kwa Mungu hakutoshi ili kusukuma watu wamtafute. Leo kuna mamilioni ya watu ambao hawajakataa kwa ujumla imani katika Mungu, lakini hilo halijawasukuma wamtafute Mungu. Mtafuta kura ya maoni ya watu Mwamerika George Gallup, Mdogo, aonelea kwamba “kwa kweli huoni tofauti kubwa kati ya watu wa kanisa na wasio wa kanisa kwa habari ya kudanganya, kuepa kodi, na wizi mdogo mdogo, hasa kwa sababu kuna dini nyingi za kijamii.” Yeye aongeza kwamba “wengi wanafanyiza tu dini ambayo ni ya starehe kwao na yenye kuwasisimua na kwa lazima isiyo na matakwa. Mtu fulani aliita dini kuwa yenye kuruhusu chochote. Huo ndio udhaifu mkuu wa Ukristo katika nchi hii [U.S.A.] leo: Hakuna uthabiti wa imani.”

21, 22. (a) Ni nini kinachofanya Biblia kuwa kitabu chenye kutokeza? (b) Ni nini ulio uthibitisho wa msingi wa uasilia wa Biblia? Fafanua.

21 “Udhaifu mkuu” huo hasa ni tokeo la ukosefu wa maarifa na imani katika Biblia. Lakini kuna msingi gani wa kuamini Biblia? Kwanza, yapasa kuangaliwa kwamba katika enzi zote, labda hakuna kitabu kinginecho chote ambacho kimehakikiwa isivyo haki, kikatendwa vibaya, kuchukiwa, na kushambuliwa zaidi ya Biblia. Hata hivyo, kimepona yote hayo kikaonekana kuwa kitabu kilichotafsiriwa na kuenezwa kwa wingi zaidi kilichoko kwenye kumbukumbu zilizotunzwa. Hilo peke yalo lafanya Biblia kuwa kitabu chenye kutokeza. Lakini kuna ushuhuda tele, uthibitisho wa kusadikisha, kwamba Biblia ni kitabu kilichopuliziwa na Mungu na kinachostahili imani yetu.—Ona kisanduku, kurasa 340-1.

22 Hata ingawa watu wengi wamedhania kwamba Biblia si ya kisayansi, yajipinga, na ni ya kikale, mambo ya hakika yaonyesha vingine. Utungaji wayo wa pekee, usahihi wayo wa kihistoria na kisayansi, na unabii wayo mwingi usiokosea, yote hayo yaelekeza kwenye mkataa mmoja usioepukika: Biblia ndilo Neno la Mungu alilopulizia. Ni kama alivyosema Paulo: “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa.”—2 Timotheo 3:16.

Kukabili Tatizo la Kutokuamini

23. Twaweza kufikia mkataa gani kuhusu Biblia tunapotazama mambo ya hakika?

23 Baada ya kuchunguza uthibitisho wa kitabu cha uumbaji na Biblia, twaweza kufikia mkataa gani? Kwa usahili, ni kwamba vitabu hivi vyafaa leo kama ambavyo sikuzote vimefaa. Tunapokuwa na nia ya kuliangalia jambo hilo kama lilivyo badala ya kupeperushwa na mawazo yaliyokwisha kuwazwa, twapata kwamba vipingamizi vyovyote vyaweza kushindwa kwa njia inayofaa. Majibu yapo, ikiwa tuna nia tu ya kuyatafuta. Yesu alisema, “Endeleeni kutafuta, na nyinyi mtapata.”—Mathayo 7:7, NW; Matendo 17:11.

24. (a) Ni kwa nini wengi wameacha jitihada yao ya kutafuta Mungu? (b) Twaweza kupata faraja katika nini? (c) Ni nini kitakachofikiriwa katika sura zinazosalia za kitabu hiki?

24 Kwa kumalizia, watu walio wengi ambao wameacha kutafuta Mungu hawakufanya hivyo kwa sababu wamejichunguzia kwa uangalifu uthibitisho na kukuta kwamba Biblia si ya kweli. Badala yake, wengi wao wamekata tamaa kwa sababu ya kushindwa kwa Jumuiya ya Wakristo kumtokeza Mungu wa kweli wa Biblia. Ni kama mwandikaji Mfaransa P. Valadier alivyotoa taarifa hii: “Pokeo la Kikristo lililotokeza matunda ya uatheisti; liliongoza kwenye kuua Mungu katika dhamiri za watu kwa sababu liliwatokezea Mungu asiyeweza kuaminika.” Hata iwe hivyo, sisi twaweza kufarijiwa na maneno haya ya mtume Paulo: “Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo.” (Warumi 3:3, 4) Ndiyo, kuna kila sababu ya kuendelea kutafuta Mungu wa kweli. Katika sura zinazosalia za kitabu hiki, tutaona jinsi jitihada hiyo ya kutafuta imefikia ukamilisho uliofanikiwa na mambo ambayo wakati ujao umewekea ainabinadamu.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa maelezo zaidi juu ya uthibitisho huo wa kuwapo kwa Mungu, ona kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1985, kurasa 142-78.

[Sanduku katika ukurasa wa 340, 341]]

Uthibitisho wa Uasilia wa Biblia

Utungaji wa Pekee: Tangu kitabu chayo cha kwanza, Mwanzo, mpaka kile chayo cha mwisho, Ufunuo, Biblia ina vitabu 66 vilivyoandikwa na waandikaji wapatao 40 wa malezi ya kijamii, kielimu, na kikazi, yenye utofautiano mkubwa sana. Uandikaji ulifanywa kwa kipindi cha karne zaidi ya 16, tangu 1513 K.W.K. mpaka 98 W.K. Hata hivyo, tokeo la mwisho ni kitabu chenye upatano na ushikamano, kikionyesha ukuzi ufaao wa kichwa kikuu maarufu—kutetewa kwa Mungu na kusudi lake kupitia Ufalme wa Kimesiya.—Ona kisanduku, ukurasa 241.

Usahihi wa Kihistoria: Matukio yaliyoandikwa katika Biblia yapatana kabisa na mambo ya hakika ya kihistoria yaliyothibitishwa. Kitabu A Lawyer Examines the Bible chatamka hivi: “Ingawa masimulizi ya kimahaba, kihekaya na ushuhuda bandia huepuka kutaja tarehe na mahali pa matukio yanayosimuliwa mahali pa mbali na wakati fulani usio dhahiri, . . . masimulizi ya Biblia hutupa sisi tarehe na mahali pa mambo yanayosimuliwa kwa usahihi kamili.” (Ezekieli 1:1-3) Na The New Bible Dictionary chatoa taarifa hii: “[Mwandikaji wa Matendo] atia usimulizi wake kwa kuambatana na historia ya wakati huo; kurasa zake zimejaa marejezo ya mahakimu wa majiji, maliwali wa mikoa, wafalme vibaraka, na kadhalika, na marejezo hayo pindi baada ya pindi huthibitika kuwa sahihi kabisa kwa habari ya mahali na wakati unaohusika.”—Matendo 4:5, 6; 18:12; 23:26.

Usahihi wa Kisayansi: Sheria za karantini (kutengwa kwa wagonjwa) na afya zilipewa kwa Waisraeli katika kitabu cha Mambo ya Walawi wakati ambao mataifa yaliyozunguka hayakujua chochote juu ya mazoea hayo. Majira ya mvua na mvukizo kutoka bahari, mambo ambayo hayakujulikana nyakati za kale, yasimuliwa kwenye Mhubiri 1:7. Kwamba dunia ni duara na imening’inizwa angani, jambo ambalo halikuthibitishwa na sayansi mpaka karne ya 16, limeelezwa katika Isaya 40:22 na Ayubu 26:7. Miaka zaidi ya 2,200 kabla ya William Harvey kutangaza utafiti wake juu ya mzunguko wa damu, Mithali 4:23 ilitaja fungu linalotimizwa na moyo wa binadamu. Kwa hiyo, ingawa Biblia si kitabu cha kufundisha sayansi, inapogusia mambo yanayohusiana na sayansi, huonyesha kina cha kuelewa kunakozidi sana maarifa ya wakati wayo.

Unabii Mbalimbali Usiokosea: Uharibifu wa Tiro, anguko la Babuloni, kujengwa upya kwa Yerusalemu, na kuinuka na kuanguka kwa wafalme wa Umedi-Uajemi na Ugiriki kulitabiriwa kwa kirefu sana hata wahakiki wakashtaki, wasifaulu, kwamba hayo yaliandikwa baada ya kutukia. (Isaya 13:17-19; 44:27–45:1; Ezekieli 26:3-7; Danieli 8:1-7, 20-22) Unabii mbalimbali juu ya Yesu uliotolewa karne nyingi kabla ya kuzaliwa kwake ulitimizwa kabisa. (Ona kisanduku, ukurasa 245.) Unabii mbalimbali wa Yesu mwenyewe juu ya kuharibiwa kwa Yerusalemu ulitimizwa kwa usahihi. (Luka 19:41-44; 21:20, 21) Unabii mbalimbali juu ya siku za mwisho uliotolewa na Yesu na mtume Paulo unatimizwa katika wakati wetu. (Mathayo 24; Marko 13; Luka 21; 2 Timotheo 3:1-5) Hata hivyo, Biblia yampa Yehova Mungu sifa ya kuwa ndiye Chanzo kimoja cha unabii wote.—2 Petro 1:20, 21.

[Picha katika ukurasa wa 333]

Darwin, Marx, Freud, Nietzsche, na wengine walipendekeza nadharia zilizobomoa imani katika Mungu

[Picha katika ukurasa wa 335]

“Kitabu” cha uumbaji na Biblia vyatoa msingi wa imani katika Mungu

[Picha katika ukurasa wa 338]

Kadiri tunavyojua zaidi juu ya ulimwengu unaotuzunguka, ndivyo tunavyokuwa na uthibitisho zaidi wa Muumba mwenye akiliy

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 337]

Uhai na ulimwengu wote mzima vingekuwa haviwezekani kama mambo fulani ya ubuni yangetofautiana kwa kisehemu kidogo sana tu

[Mchoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

VIFANYIZA ATOMI YA HAIDROJENI

Gamba la Elektroni

Protoni + Kiini (Nucleus)

ELEKTRONI

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki