Kitabu Cha Biblia Namba 12—2 Wafalme
Mwandikaji: Yeremia
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu na Misri
Uandikaji Ulikamilishwa: 580 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: c. (karibu) 920–580 K.W.K.
1. Ni historia zipi zinazosimuliwa katika kitabu cha Wafalme wa Pili, na zatetea nini?
KITABU cha Wafalme wa Pili chaendelea kueleza mwendo wenye msukosuko wa falme za Israeli na Yuda. Elisha alitwaa joho la Eliya na akabarikiwa na sehemu maradufu za roho ya Eliya, akafanya miujiza 16, ikilinganishwa na 8 ya Eliya. Yeye aliendelea kutoa unabii wa maangamizi kwa Israeli iliyoasi imani, ambako Yehu tu ndiye aliyetoa mmweko wa muda mfupi wa bidii kwa ajili ya Yehova. Wafalme wa Israeli walikwama zaidi na zaidi ndani ya tope la uovu, hadi mwishowe ufalme wa kaskazini ukaanguka mbele ya Ashuru katika 740 K.W.K. Katika ufalme wa kusini wa Yuda, wafalme wachache wenye kutokeza, hasa Yehoshafati, Yehoashi, Hezekia, na Yosia, waliondosha wimbi la uasi-imani kwa muda, lakini Nebukadreza alitekeleza hukumu ya Yehova mwishowe kwa kufanya ukiwa Yerusalemu, hekalu lao, na bara la Yuda katika 607 K.W.K. Kwa njia hiyo unabii mbalimbali wa Yehova ukatimizwa, na neno lake likatetewa!
2. Ni nini kinachoweza kusemwa juu ya uandikaji na kukubaliwa kwa kitabu cha Wafalme wa Pili, na ni kipindi gani kinachohusishwa nacho?
2 Kwa kuwa kitabu cha Wafalme wa Pili kilikuwa hapo awali sehemu ya kunjo lile lile kama kitabu cha Wafalme wa Kwanza, yale ambayo yamekwisha semwa juu ya uandikaji wa Yeremia yanatumika hapa kwa kadiri ile ile, sawa na vithibitisho vya kukubaliwa na uasilia wa kitabu hicho. Kilikamilishwa yapata 580 K.W.K. na chahusisha kipindi cha kuanzia na utawala wa Ahazia wa Israeli katika karibu 920 K.W.K. na kumalizika katika mwaka wa 37 wa kuhamishwa kwa Yehoyakini, 580 K.W.K.—1:1; 25:27.
3. Ni vitu gani vilivyopatikana vya kiakiolojia vyenye kutokeza vinavyounga mkono kitabu cha Wafalme wa Pili?
3 Vitu vilivyopatikana kiakiolojia (kwa kuchimbuliwa) vinavyounga mkono maandishi ya kitabu cha Wafalme wa Pili hutoa ushuhuda zaidi juu ya uhalisi wacho. Kwa kielelezo, kuna lile Jiwe la Moabu lijulikanalo sana, ambalo nakshi yalo yatoa hadithi ya mfalme Mesha Mmoabi kuhusu vita baina ya Moabu na Israeli. (3:4, 5) Pia kuna jiwe jeusi la basalti lenye umbo la yai la Shalmanesa 3 Mwashuri, ambalo sasa ni wonyesho katika Jumba la Ukumbusho la Uingereza, London, ambalo hutaja mfalme Yehu Mwisraeli kwa jina. Kuna nakshi za mfalme Tiglath-pileseri 3 (Pulu) Mwashuri, zinazotaja kwa jina wafalme kadhaa wa Israeli na Yuda, kutia na Menahemu, Ahazi, na Peka.—15:19, 20; 16:5-8.a
4. Ni nini kinachothibitisha kwamba kitabu cha Wafalme wa Pili ni sehemu halisi ya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu?
4 Uthibitisho ulio wazi wa uasilia wa kitabu hicho cha Biblia wapatikana katika kule kusimulia waziwazi kutekelezwa kwa hukumu za Yehova juu ya watu wake mwenyewe. Kwa kuwa kwanza ufalme wa Israeli na kisha ufalme wa Yuda zafanywa ukiwa, nguvu kubwa ya hukumu ya kiunabii ya Yehova katika Kumbukumbu la Torati 28:15–29:28 yakaziwa kwetu. Katika kuangamizwa kwa falme hizo, ‘hasira ya Yehova iliwaka juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki.’ (Kum. 29:27; 2 Fal. 17:18; 25:1, 9-11) Matukio mengine yaliyoandikwa katika kitabu cha Wafalme wa Pili yamefafanuliwa kwingineko katika Maandiko. Kwenye Luka 4:24-27, baada ya Yesu kurejezea Eliya na yule mjane wa Sarepta, ananena juu ya Elisha na Naamani katika kuonyesha ni kwa nini yeye mwenyewe hakukubaliwa kuwa nabii katika eneo la nyumbani kwake. Kwa hiyo, kitabu cha Wafalme wa Kwanza na wa Pili huonwa kuwa sehemu halisi ya Maandiko Matakatifu.
YALIYOMO KATIKA WAFALME WA PILI
5. Ni karipio na hukumu gani anayopitisha Eliya juu ya Ahazia, na kwa nini?
5 Ahazia, mfalme wa Israeli (1:1-18). Akianguka nyumbani mwake, mwana huyu wa Ahabu augua. Atuma watu kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, akaulizwe kama atapata nafuu. Eliya awakatiza njiani wajumbe hao na kuwarejesha kwa mfalme, akimkaripia kwa kutokuuliza Mungu wa kweli na amwambia kwamba kwa sababu hakugeukia Mungu wa Israeli, atakufa hakika. Mfalme huyo apelekapo mkuu pamoja na wanaume 50 wakamkamate Eliya na kumleta kwa mfalme, Eliya aita moto kutoka mbinguni uwale. Jambo lilo hilo lampata mkuu wa pili pamoja na wanaume wake 50. Mkuu wa tatu na wanaume 50 wapelekwa, na safari hii Eliya aponyoa uhai wao kwa ajili ya ombi la staha la mkuu huyo. Eliya aenda pamoja nao kwa mfalme na kwa mara nyingine atamka hukumu ya kifo juu ya Ahazia. Mfalme afa kama vile alivyosema Eliya. Kisha Yehoramu ndugu ya Ahazia awa mfalme juu ya Israeli, kwa maana Ahazia hana mwana wa kuchukua mahali pake.
6. Ni chini ya hali gani Eliya atengana na Elisha, na yaonyeshwaje upesi kwamba ‘roho ya Eliya’ imekalia Elisha?
6 Elisha awa mwandamizi wa Eliya (2:1-25). Wawadia wakati wa Eliya kuchukuliwa. Elisha aambatana naye kwenye safari yake ya kutoka Gilgali kwenda Betheli, Yeriko, na hatimaye kuvuka Yordani. Eliya atenganisha maji ya Yordani kwa kuyapiga na joho lake rasmi. Wakati aonapo gari-farasi la vita lenye moto na farasi wenye moto wakija kati yake na Eliya na kuona Eliya akipaa katika dhoruba ya upepo, Elisha apokea sehemu maradufu zilizoahidiwa katika roho ya Eliya. Muda si muda aonyesha kwamba ‘roho ya Eliya’ inakaa juu yake. (2:15) Akitwaa joho la Eliya lililoanguka, alitumia kugawanya maji hayo tena. Kisha atibu maji mabaya kule Yeriko. Akiwa safarini kwenda Betheli, wavulana wadogo waanza kumfanyia dhihaka: “Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa!” (2:23) Elisha amwomba Yehova, na madubu-jike wawili wachomoka msituni na kuua 42 kati ya vijana hao waasi.
7. Yehova anaokoa Yehoshafati na Yehoramu kwa sababu ya nini?
7 Yehoramu, mfalme wa Israeli (3:1-27). Mfalme huyu aendelea kufanya yaliyo mabaya machoni pa Yehova, akishikamana na dhambi za Yeroboamu. Mfalme wa Moabu amekuwa akilipa ushuru kwa Israeli lakini sasa aasi, na Yehoramu apata msaada wa Mfalme Yehoshafati wa Yuda na mfalme wa Edomu kuinuka juu ya Moabu. Wakiwa kwenye safari ya kushambulia, majeshi yao yawasili kwenye nchi isiyo na maji na wanusurika (karibu) kufa. Wafalme hao watatu washuka kwa Elisha waulizie Yehova Mungu wake. Kwa sababu ya Yehoshafati mwaminifu, Yehova awaokoa na kuwapa ushindi juu ya Moabu.
8. Ni miujiza gani zaidi anayofanya Elisha?
8 Miujiza zaidi ya Elisha (4:1–8:15). Wenye kumdai wakaribiapo kutwaa wana wake wawili kwenye utumwa, mjane wa mmoja wa wana wa manabii atafuta msaada kwa Elisha. Yeye azidisha kimwujiza ugavi mdogo wa mafuta katika nyumba yake ili aweze kuuza ya kutosha alipe madeni yake. Mwanamke Mshunami ang’amua Elisha kuwa nabii wa Mungu wa kweli, na yeye na mume wake watayarisha chumba kwa ajili ya matumizi yake wakati atakapokuwa Shunemu. Kwa sababu ya fadhili za mwanamke huyo, Yehova ambariki kwa kumpa mwana. Miaka kadhaa baadaye, mtoto huyo augua na kufa. Bila kukawia mwanamke huyo amtafuta Elisha. Aandamana na mwanamke huyo hadi nyumbani mwake, na kwa nguvu za Yehova afufua mtoto huyo. Arejeapo kwa wana wa manabii kule Gilgali, Elisha aondoa kimwujiza ‘mauti sufuriani’ kwa kufanya matango-mwitu yenye sumu yasiwe na madhara. Kisha alisha wanaume mia moja kwa boflo (mikate) 20 za shayiri, na bado kuna ‘masazo.’—4:40, 44.
9. Ni miujiza gani inayofanywa kwa kuhusiana na Naamani, na pia chuma cha shoka?
9 Naamani, mkuu wa jeshi la Shamu, ni mkoma. Kijakazi Mwisraeli amwambia mke wa Naamani kwamba kuna nabii katika Samaria awezaye kumponya. Naamani afunga safari kwenda kwa Elisha, lakini badala ya kumhudumia yeye binafsi, Elisha ampelekea neno tu kwamba aende akaoge mara saba katika Mto Yordani. Naamani afura kwa hasira kwa ajili ya huo ukosefu ulio wazi wa staha. Je! mito ya Dameski si bora zaidi ya maji ya Israeli? Lakini ashurutishwa atii Elisha, naye aponywa. Elisha akataa kukubali zawadi kuwa thawabu, lakini baadaye mtumishi wake Gehazi akimbia kumfuata Naamani na kuuliza apewe zawadi kwa kutumia jina la Elisha. Arejeapo na kujaribu kumdanganya Elisha, Gehazi apigwa kwa ukoma. Bado mwujiza mwingine wafanywa wakati Elisha afanyapo chuma cha shoka kielee (kiinuke juu ya maji).
10. Vikosi hodari zaidi vya Yehova vyaonyeshwaje, na Elisha awarejeshaje Washami?
10 Elisha aonyapo mfalme wa Israeli juu ya njama ya Shamu ya kumwua, mfalme wa Shamu apeleka kikosi cha kijeshi hadi Dothani ili kumkamata Elisha. Kwa kuona mji umezingirwa na majeshi ya Shamu, mtumishi wa Elisha awa na hofu. Elisha amhakikishia: “Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.” Kisha asali kwa Yehova aruhusu mtumishi wake aone kikosi kikubwa kilicho pamoja na Elisha. ‘Na tazama, kile kilima kimejaa farasi na magari ya moto kumzunguka Elisha pande zote.’ (6:16, 17) Washami washambuliapo, nabii huyo asali kwa Yehova tena, na Washami wapigwa kwa upofu wa akili na kuongozwa kwa mfalme wa Israeli. Lakini, badala ya kuuawa, Elisha amwambia mfalme awatayarishie karamu na kuwarejesha nyumbani.
11. Unabii mbalimbali wa Elisha kuhusu Washami na Ben-hadadi watimizwaje?
11 Baadaye, Mfalme Ben-hadadi wa Shamu azingira Samaria, na kuna njaa kubwa. Mfalme wa Israeli alaumu Elisha, lakini nabii atabiri utele wa chakula siku ifuatayo. Usiku, Yehova asababisha Washami wasikie mvumo wa jeshi kubwa, hata wakimbia, wakiachia Waisraeli vyakula vyao vyote. Baada ya muda fulani Ben-hadadi awa mgonjwa. Anaposikia ripoti kwamba Elisha amewasili Dameski, apeleka Hazaeli akaulizie kama atapata nafuu. Jibu la Elisha ladokeza kwamba mfalme huyo atakufa na kwamba Hazaeli atakuwa mfalme mahali pake. Hazaeli ahakikisha hilo kwa yeye mwenyewe kumwua mfalme na kutwaa ufalme.
12. Yehoramu mwana wa Yehoshafati ajithibitisha kuwa mfalme wa aina gani?
12 Yehoramu, mfalme wa Yuda (8:16-29). Wakati ule ule, katika Yuda, Yehoramu, mwana wa Yehoshafati sasa ni mfalme. Hathibitiki kuwa bora kuliko wafalme wa Israeli, akifanya mabaya machoni pa ya Yehova. Mke wake ni Athalia bintiye Ahabu, ambaye ndugu yake, aitwaye pia Yehoramu, atawala katika Israeli. Yehoramu wa Yuda afapo, mwana wake Ahazia awa mfalme katika Yerusalemu.
13. Yehu afuatisha kupakwa kwake mafuta na kampeni gani ya kasi?
13 Yehu, mfalme wa Israeli (9:1–10:36). Elisha apeleka mmoja wa wana wa manabii akapake mafuta Yehu awe mfalme juu ya Israeli na kumpa utume wa kuangamiza nyumba yote ya Ahabu. Yehu hapotezi wakati. Afunga safari kumfuatia Yehoramu, mfalme wa Israeli, ambaye yuko kule Yezreeli akipata nafuu kutokana na majeraha ya pigano. Mlinzi aona umati wenye kuinuka-inuka wa wanaume ukikaribia, na hatimaye aripoti kwa mfalme: “Mwendo huu ni kama mwendo wa Yehu mwana wa Nimshi; maana analiendesha gari kwa kasi.” (9:20) Yehoramu wa Israeli na Ahazia wa Yuda waulizia madhumuni ya Yehu. Yehu ajibu kwa kuuliza: “Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?” (9:22) Yehoramu ageukapo atoroke, Yehu ampiga mshale mmoja katika moyo wake. Mwili wake watupwa ndani ya shamba la Nabothi, kuwa hatua nyingine ya malipo ya damu isiyo na hatia iliyomwagwa na Ahabu. Baadaye Yehu na wanaume wake wafuatia Ahazia, wakimpiga hata afa kule Megido. Wafalme wawili wafa katika kampeni ya kwanza yenye kasi ya Yehu.
14. Unabii wa Eliya kuhusu Yezebeli watimizwaje?
14 Sasa ni zamu ya Yezebeli! Yehu aendapo kwa ushindi kuingia Yezreeli, Yezebeli atokea dirishani mwake akiwa amejirembesha kabisa. Yehu havutiwi. “Mtupeni chini!” apaaza sauti kwa baadhi ya watumishi. Huyo-o, avurumishwa chini, damu yake ikitapakaa kwenye ukuta na kwenye farasi wanaomkanyagia chini. Waendapo kumzika, wakuta fuvu lake la kichwa, nyayo zake, na viganja vya mikono yake peke yake. Huo ni utimizo wa unabii wa Eliya, ‘mbwa wamemla, naye amekuwa mavi juu ya uso wa kiwanja cha Yezreeli.’—2 Fal. 9:33, 36, 37; 1 Fal. 21:23.
15. Ni mapambano gani ya aina tofauti ambayo Yehu akabili njiani kwenda Samaria?
15 Kisha, Yehu aagiza wana 70 wa Ahabu wauawe, na kupanga vichwa vyao penye lango la Yezreeli. Vibaraka wote wa Ahabu katika Yezreeli wapigwa dharuba. Sasa, ni kusonga mbele hadi mji mkuu wa Israeli, Samaria! Njiani akutana na ndugu 42 wa Ahazia, wanaosafiri kwenda Yezreeli, bila kujua yanayotukia. Watwaliwa na kuuawa. Lakini sasa kuna kabiliano la aina tofauti. Yehonadabu mwana wa Rekabu aja kulaki Yehu. Katika kujibu swali la Yehu, “Je! moyo wako umenyoka, kama moyo wangu ulivyo pamoja na moyo wako?” Yehonadabu ajibu, “Ndio.” Kisha Yehu aandamana naye katika kigari-farasi chake cha vita akajionee ‘wivu wake kwa Yehova.’—2 Fal. 10:15, 16.
16. Kitendo cha Yehu juu ya nyumba ya Ahabu na juu ya Baali ni kamili jinsi gani?
16 Awasilipo Samaria, Yehu aangamiza kila kitu kilichosalia cha Ahabu, kulingana na neno la Yehova kwa Eliya. (1 Fal. 21:21, 22) Hata hivyo, vipi juu ya dini yenye kuchukiza sana ya Baali? Yehu ajulisha rasmi hivi, “Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.” (2 Fal. 10:18) Aitapo waabudu wote hao wa roho waovu kwenye nyumba ya Baali, aamuru wavae mavazi yao ya kitambulisho na ahakikisha hakuna mwabudu yeyote wa Yehova miongoni mwao. Kisha apeleka wanaume wake ndani wawapige dharuba, wasiache mmoja atoroke. Nyumba ya Baali yabomolewa, na mahali hapo pageuzwa kuwa misalani (vyoo), inayoendelea kuwapo hadi siku ya Yeremia. “Ndivyo Yehu alivyomharibu Baali katika Israeli.”—10:28.
17. Yehu ashindwa kufanya nini, na ni jinsi gani Yehova aanza kuleta adhabu juu ya Israeli?
17 Hata hivyo, hata Yehu mwenye bidii ashindwa. Katika nini? Kwa kuwa aendelea kufuata ndama za dhahabu ambazo Yeroboamu alisimamisha katika Betheli na Dani. Yeye “hakuangalia, aende katika sheria ya BWANA [Yehova, NW], Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote.” (10:31) Lakini kwa sababu ya tendo lake juu ya nyumba ya Ahabu, Yehova aahidi kwamba wazao wake watatawala juu ya Israeli hadi kizazi cha nne. Katika siku zake, Yehova aanza kukata kisehemu cha mashariki cha ufalme, akimleta Hazaeli wa Shamu kupigana na Israeli. Baada ya kutawala miaka 28, Yehu afa na mwandamizi wake ni mwana wake, Yehoahazi.
18. Ni kwa njia gani njama ya Athalia katika Yuda yazuiwa, na ni nini kinachopasa kuangaliwa juu ya utawala wa Yoashi?
18 Yoashi, mfalme wa Yuda (11:1–12:21). Mama malkia, Athalia, ni binti ya Yezebeli katika mnofu na katika roho. Asikiapo juu ya kifo cha mwana wake Ahazia, aagiza familia yote ya kifalme iangamizwe naye anyakua kiti cha enzi. Mwana mdogo wa Ahazia peke yake, Yoashi ndiye anaponyoka kifo afichwapo. Katika mwaka wa saba wa utawala wa Athalia, Yehoyada kuhani apaka mafuta Yoashi na aagiza Athalia auawe. Yehoyada aelekeza watu katika ibada ya Yehova, aagiza mfalme kijana katika wajibu wake mbalimbali mbele za Mungu, naye apanga nyumba ya Yehova itengenezwe kulikoharibika. Kwa kutoa zawadi, Yoashi ageuza shambulio la Hazaeli mfalme wa Shamu. Baada ya kutawala kwa miaka 40 katika Yerusalemu, Yoashi auawa na watumishi wake, na Amazia mwana wake aanza kutawala mahali pake.
19. (a) Ni ibada gani bandia inayoendelea wakati wa tawala za Yehoahazi na Yoashi katika Israeli? (b) Elisha amalizaje mwendo wake akiwa nabii wa Yehova?
19 Yehoahazi na Yoashi, wafalme wa Israeli (13:1-25) Yehoahazi mwana wa Yehu aendelea katika ibada ya sanamu, na Israeli waja chini ya mamlaka ya Shamu, ijapokuwa Yehoahazi hapinduliwi. Kwa wakati wake Yehova aweka huru Waisraeli, lakini waendelea katika ibada ya ndama ya Yeroboamu. Yehoahazi afapo, mwana wake Yoashi atwaa mahali pake kuwa mfalme katika Israeli, huku Yoashi yule mwingine akitawala katika Yuda. Yoashi wa Israeli aendelea katika ibada ya sanamu ya baba yake. Afapo mwana wake Yeroboamu awa mfalme. Ni wakati wa utawala wa Yoashi kwamba Elisha augua na kufa, baada ya kutoa unabii wake wa mwisho kwamba Yoashi atapiga Shamu mara tatu, nao watimizwa kabisa. Mwujiza wa mwisho anaohesabiwa Elisha watukia baada ya kifo chake, wakati mwanamume mfu atupwapo katika mahali papo hapo pa kuzikia, asimama akiwa hai mara tu agusapo mifupa ya Elisha.
20. Simulia utawala wa Amazia katika Yuda.
20 Amazia, mfalme wa Yuda (14:1-22). Amazia afanya yaliyonyooka machoni pa Yehova, lakini ashindwa kuangamiza sehemu za juu zinazotumiwa kwa ajili ya ibada. Ashindwa katika vita na Yoashi wa Israeli. Baada ya utawala wa miaka 29, auawa katika njama. Azaria mwana wake afanywa kuwa mfalme mahali pake.
21. Ni nini kinachotokea wakati wa utawala wa Yeroboamu 2 katika Israeli?
21 Yeroboamu 2, mfalme wa Israeli (14:23-29). Yeroboamu wa pili kuwa mfalme katika Israeli aendelea katika ibada bandia ya babu yake. Atawala katika Samaria kwa miaka 41 na afaulu kushinda maeneo ya Israeli yaliyokuwa yamepotezwa. Zekaria mwana wake awa mwandamizi wake kwenye kiti cha enzi.
22. Ni nini yanayosimuliwa kuhusu utawala wa Azaria katika Yuda?
22 Azaria (Uzia), mfalme wa Yuda (15:1-7). Azaria atawala kwa miaka 52. Yeye ni mnyofu mbele za Yehova lakini ashindwa kuangamiza zile sehemu za juu. Baadaye, Yehova ampiga kwa ukoma, na mwana wake Yothamu ashughulikia wajibu mbalimbali wa kifalme, na kuwa mfalme Azaria afapo.
23. Israeli wanapatwa na maovu gani wakati tisho la Kiashuri litokeapo?
23 Zekaria, Shalumu, Menahemu, Pekahia, na Peka, wafalme wa Israeli (15:8-31). Kulingana na ahadi ya Yehova, kiti cha enzi cha Israeli chabaki katika nyumba ya Yehu hadi Zekaria wa kizazi cha nne. (10:30) Basi, awa mfalme katika Samaria, na miezi sita baadaye apigwa dharuba na mwuaji. Shalumu, mnyakuaji, aendelea kwa mwezi mmoja tu. Ibada bandia, mauaji, na njama vyaendelea kupiga Israeli wakati wafalme Menahemu, Pekahia, na Peka wapita kwa kufuatana. Wakati wa utawala wa Peka Ashuru yazingira ishambulie. Hoshea amwua Peka, na kuwa mfalme wa mwisho wa Israeli.
24. Baada ya Yothamu, Ahazi wa Yuda atendaje dhambi kuhusiana na ibada?
24 Yothamu na Ahazi, wafalme wa Yuda (15:32–16:20). Yothamu azoea ibada safi lakini aruhusu sehemu za juu kuendelea. Ahazi mwana wake aiga wafalme wa Israeli jirani kwa kuzoea yaliyo mabaya machoni pa Yehova. Ashambuliwapo na wafalme wa Israeli na Shamu, aomba mfalme wa Ashuru msaada. Waashuri waja kumsaidia, na kuteka Dameski, na Ahazi aenda huko alaki mfalme wa Ashuru. Aonapo madhabahu ya ibada huko, Ahazi ajenga moja katika Yerusalemu ya kiolezo icho hicho, naye aanza kutoa dhabihu juu yayo badala ya kwenye madhabahu ya shaba katika hekalu la Yehova. Mwana wake Hezekia awa mfalme wa Yuda akiwa mwandamizi wake.
25. Israeli waendaje kwenye utumwa, na kwa nini?
25 Hoshea, mfalme wa mwisho wa Israeli (17:1-41). Sasa Israeli waja chini ya mamlaka ya Ashuru. Hoshea aasi na kutafuta msaada kutoka Misri, lakini katika mwaka wa tisa wa utawala wake, Israeli yashindwa na Ashuru na kupelekwa utumwani. Ndivyo unavyokoma ufalme wa Israeli wa makabila kumi. Kwa nini? “Kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA [Yehova, NW], Mungu wao . . . Wakatumikia sanamu, ambazo BWANA [Yehova, NW] aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili. Kwa hiyo BWANA [Yehova, NW] akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake.” (17:7, 12, 18) Waashuri waleta watu kutoka mashariki wakalie bara hilo, nao wawa ‘wacha Yehova,’ ingawa waendelea kuabudu miungu yao wenyewe.—17:33.
26, 27. (a) Hezekia wa Yuda afanyaje yaliyo haki machoni pa Yehova? (b) Yehova ajibuje sala ya Hezekia kwa kuwafukuza Waashuri? (c) Unabii wa Isaya wapata utimizo gani zaidi?
26 Hezekia, mfalme wa Yuda (18:1–20:21). Hezekia afanya yaliyo haki machoni pa Yehova, kwa kulingana na yote ambayo Daudi babu yake alikuwa amefanya. Ang’oa ibada bandia na kubomoa zile sehemu za juu, na kwa sababu sasa watu waiabudu, aiharibu pia nyoka ya shaba iliyofanyizwa na Musa. Senakeribu, mfalme wa Ashuru, sasa azingira Yuda na kuteka majiji mengi yenye ngome. Hezekia ajaribu kumhonga na ushuru mkubwa, lakini Senakeribu apeleka mjumbe wake Rabshake, anayekaribia kuta za Yerusalemu na kudai wasalimu amri na adhihaki Yehova masikioni mwa watu wote. Nabii Isaya amhakikishia Hezekia mwaminifu kwa ujumbe wa maangamizi juu ya Senakeribu. ‘Yehova asema hivi, Usiogope.’ (19:6) Senakeribu anapoendelea kutisha, Hezekia asihi Yehova: “Basi sasa, Ee BWANA [Yehova, NW], Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA [Yehova, NW] Mungu, wewe peke yako.”—19:19.
27 Je! Yehova anajibu sala hii isiyo ya ubinafsi? Kwanza, kupitia Isaya, apeleka ujumbe kwamba “wivu wa BWANA [Yehova]” wa majeshi utafukuza adui. (19:31) Kisha, usiku uo huo, apeleka malaika wake apige dharuba 185,000 katika kambi ya Waashuri. Asubuhi ‘wote ni maiti.’ (19:35) Senakeribu arudi akiwa ameshindwa na kufanya makao katika Ninawi. Huko mungu wake Nisroki ashindwa kumtetea tena, kwa maana ni wakati amemsujudia katika ibada kwamba wana wake mwenyewe wamwua, kwa utimizo wa unabii wa Isaya.—19:7, 37.
28. Hezekia ni maarufu katika nini, lakini atenda dhambi katika jambo gani?
28 Hezekia augua mahututi, lakini Yehova kwa mara nyingine asikiliza sala yake na kurefusha maisha yake kwa miaka 15 zaidi. Mfalme wa Babuloni apeleka wajumbe wakiwa na zawadi, na Hezekia ajitanguliza awaonyeshe nyumba yake yote ya hazina. Ndipo Isaya anapotabiri kwamba kila kitu katika nyumba yake siku moja kitapelekwa Babuloni. Kisha Hezekia afa, akiwa maarufu kwa uhodari wake na kwa mtaro wa chini ya ardhi aliojenga ili kuingiza ugavi wa maji ya Yerusalemu ndani ya jiji hilo.
29. Manase aanzisha ibada gani ya sanamu, Yehova atabiri msiba gani, na ni dhambi gani zaidi anayofanya Manase?
29 Manase, Amoni, na Yosia, wafalme wa Yuda (21:1–23:30). Manase awa mwandamizi wa baba yake, Hezekia, na atawala miaka 55, akifanya mabaya machoni pa Yehova kwa kadiri kubwa. Yeye arejesha sehemu za juu za ibada bandia, asimamisha madhabahu ya Baali, afanyiza nguzo takatifu kama alivyofanya Ahabu, na afanya nyumba ya Yehova kuwa mahali pa ibada ya sanamu. Yehova atabiri kwamba ataleta msiba juu ya Yerusalemu kama ambavyo amefanya juu ya Samaria, “kuifuta na kuifudukiza.” Manase pia amwaga damu “nyingi sana” zisizo na hatia. (21:13, 16) Mwandamizi wake ni mwana wake Amoni, anayeendelea kufanya mabaya kwa miaka miwili, hadi apigwapo dharuba na wauaji wawili.
30. Ni kwa nini na ni jinsi gani Yosia arudia Yehova kwa moyo wake wote?
30 Sasa watu wafanya Yosia mwana wake Amoni kuwa mfalme. Wakati wa utawala wake wa miaka 31, ageuza kifupi mzamo wa Yuda kuelekea uharibifu ‘kwa kwenda katika njia yote ya Daudi baba yake.’ (22:2) Aanza kutengeneza nyumba ya Yehova ilikoharibika, na humo kuhani mkuu apata kitabu cha Sheria. Hicho chathibitisha kwamba uharibifu utakuja juu ya taifa kwa ajili ya ukosefu walo wa utii kwa Yehova, lakini Yosia ahakikishiwa kwamba kwa sababu ya uaminifu wake, hautakuja katika siku yake. Aondoa ibada ya kishetani katika nyumba ya Yehova na katika bara lote na apanua utendaji wake wa kuponda-ponda sanamu hadi Betheli, ambako aharibu madhabahu ya Yeroboamu kwa utimizo wa unabii kwenye 1 Wafalme 13:1, 2. Aanzisha tena sherehe ya Kupitwa kwa ajili ya Yehova. “Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea BWANA [Yehova, NW] kwa moyo wake wote, na kwa roho [nafsi, NW] yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa.” (23:25) Hata hivyo, bado kasirani ya Yehova inawaka kwa sababu ya makosa ya Manase. Yosia afa katika pambano pamoja na mfalme wa Misri kule Megido.
31. Ni matatizo gani yanayopata Yuda kufuatia kifo cha Yosia?
31 Yehoahazi, Yehoyakimu, na Yehoyakini, wafalme wa Yuda (23:31–24:17). Baada ya utawala wa miezi mitatu, Yehoahazi mwana wa Yosia atwaliwa mateka na mfalme wa Misri, na ndugu yake Eliakimu, ambaye jina lake labadilishwa kuwa Yehoyakimu, awekwa juu ya kiti cha enzi. Afuata mwendo wenye kosa wa mababu wake na atiishwa kwa Nebukadreza, mfalme wa Babuloni, lakini amwasi baada ya miaka mitatu. Yehoyakimu afapo mwana wake Yehoyakini aanza kutawala. Nebukadreza azingira Yerusalemu, auteka, na kutwaa hazina za nyumba ya Yehova hadi Babuloni, “kama BWANA [Yehova, NW] alivyosema” kupitia Isaya. (24:13; 20:17) Yehoyakini na maelfu ya raia zake wapelekwa uhamishoni katika Babuloni.
32. Ni matukio gani makubwa yanayoongoza kwenye kufanywa ukiwa kwa Yerusalemu na bara hilo?
32 Sedekia, mfalme wa mwisho wa Yuda (24:18–25:30). Nebukadreza afanya Matania, mjomba wake Yehoyakini kuwa mfalme na kubadili jina lake kuwa Sedekia. Atawala miaka 11 katika Yerusalemu na aendelea kufanya mabaya machoni pa Yehova. Aiasi Babuloni, kwa hiyo katika mwaka wa tisa wa Sedekia, Nebukadreza na jeshi lake lote waja na kujenga ukuta wa mazingiwa kulizunguka Yerusalemu lote. Baada ya miezi 18 jiji hilo laharibiwa na njaa kali. Kisha kuta zavunjwa, na Sedekia atekwa akijaribu kutoroka. Wana wake wachinjwa mbele yake, naye apofushwa. Katika mwezi ufuatao, nyumba zote za wakuu wa jiji, kutia na nyumba ya Yehova na nyumba ya mfalme, zateketezwa na kuta za mji kubomolewa. Waokokaji walio wengi wapelekwa utumwani Babuloni. Gedalia awekwa kuwa liwali juu ya watu wachache wa cheo cha chini wanaobaki katika sehemu ya mashambani ya Yuda. Hata hivyo, auwawa, na watu watorokea Misri. Hivyo, kuanzia mwezi wa saba wa 607 K.W.K., bara labaki ukiwa kabisa. Maneno ya mwisho ya kitabu cha Wafalme wa Pili yaeleza juu ya hisani ambayo mfalme wa Babuloni aonyesha Yehoyakini katika mwaka wa 37 wa utekwa wake.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
33. Ni vielelezo gani vizuri vinavyotolewa katika kitabu cha Wafalme wa Pili kwa ajili yetu tufuate?
33 Ingawa kinahusisha uzorotaji wenye kuleta madhara wa falme za Israeli na Yuda, kitabu cha Wafalme wa Pili chameremeta kwa vielelezo vingi vya baraka ya Yehova juu ya watu mmoja mmoja walioonyesha upendo kwake na kwa kanuni zake za haki. Kama yule mjane wa Sarepta aliyemtangulia, yule mwanamke Mshunami alipokea baraka tele kwa ukaribishaji-wageni wake alioonyesha kwa nabii wa Mungu. (4:8-17, 32-37) Sikuzote uwezo wa Yehova wa kutoa riziki ulionyeshwa wakati Elisha alipolisha wanaume mia moja kwa boflo (mikate) 20, kama vile Yesu angekuja kufanya miujiza kama hiyo baadaye. (2 Fal. 4:42-44; Mt. 14:16-21; Mk. 8:1-9) Angalia jinsi Yehonadabu alivyopokea baraka kwa kualikwa aandamane katika gari-farasi la vita la Yehu akaone uharibifu wa waabudu wa Baali. Na kwa nini? Kwa sababu alichukua tendo linalofaa kwa kuja kusalimu Yehu mwenye bidii. (2 Fal. 10:15, 16) Hatimaye, kuna vielelezo vizuri sana vya Hezekia na Yosia, katika unyenyekevu wao na heshima inayofaa kwa ajili ya jina na Sheria ya Yehova. (19:14-19; 22:11-13) Hivyo ni vielelezo vizuri sana kwetu sisi kufuata.
34. Kitabu cha Wafalme wa Pili chatufunza nini kuhusu heshima kwa ajili ya watumishi rasmi na kuhusu hatia ya damu?
34 Yehova havumilii utovu wowote wa heshima kuelekea watumishi wake rasmi. Wakati wale wavunja sheria walipomdhihaki Elisha akiwa nabii wa Yehova, Yeye alilipiza kisasi kwa upesi. (2:23, 24) Zaidi ya hayo, Yehova huheshimu damu ya wasio na hatia. Hukumu yake ilikalia sana nyumba ya Ahabu si kwa sababu tu ya ibada ya Baali bali pia kwa sababu ya umwagaji wa damu ulioambatana nayo. Kwa hiyo, Yehu alipakwa mafuta alipize kisasi “damu ya watumishi wote wa BWANA [Yehova, NW], mkononi mwa Yezebeli.” Wakati hukumu ilipotekelezwa juu ya Yehoramu, Yehu alikumbuka tamko la Yehova kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya “damu ya Nabothi, na damu ya wanawe.” (9:7, 26) Vivyo hivyo, hatia ya damu ya Manase ndiyo iliyotia muhuri ya mwisho ya maangamizi ya Yuda. Kuongezea dhambi yake ya ibada bandia, Manase ‘alijaza Yerusalemu kwa damu tangu upande huu hata upande huu.’ Hata ingawa Manase alitubu baadaye juu ya mwendo wake mbaya, hatia ya damu ilibaki. (2 Nya. 33:12, 13) Hata utawala mwema wa Yosia, na kuondosha kwake ibada yote ya sanamu, haungeweza kufutilia mbali hatia ya damu ya jumuiya iliyosalia kutoka kwa utawala wa Manase. Miaka mingi baadaye, wakati Yehova alipoanza kuleta wafishaji wake juu ya Yerusalemu, yeye alijulisha rasmi kwamba ilikuwa ni kwa sababu Manase alikuwa ‘amejaza Yerusalemu damu zisizo na hatia, wala Yehova hakukubali kusamehe.’ (2 Fal. 21:16; 24:4) Vivyo hivyo, Yesu alijulisha rasmi kwamba Yerusalemu la karne ya kwanza W.K. lilipasa kuangamizwa kwa sababu makuhani walo walikuwa wana wa wale waliomwaga damu ya manabii, ili ‘ije juu yao damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi.’ (Mt. 23:29-36) Mungu aonya ulimwengu kwamba atalipiza kisasi damu isiyo na hatia ambayo imemwagwa, hasa damu ya wale “waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu.”—Ufu. 6:9, 10.
35. (a) Eliya, Elisha, na Isaya wathibitishwaje kuwa manabii wa kweli? (b) Kuhusiana na Eliya, Petro asema nini juu ya unabii?
35 Uhakika usiokosea ambao kwao Yehova hutimiza hukumu zake za kiunabii waonyeshwa katika kitabu cha Wafalme wa Pili. Manabii watatu maarufu waelekezewa uangalifu wetu, Eliya, Elisha, na Isaya. Unabii mbalimbali wa kila mmoja waonyeshwa kuwa na utimizo wenye kutokeza. (2 Fal. 9:36, 37; 10:10, 17; 3:14, 18, 24; 13:18, 19, 25; 19:20, 32-36; 20:16, 17; 24:13) Pia Eliya athibitishwa kuwa nabii wa kweli katika kuonekana kwake pamoja na nabii Musa na Nabii Mkuu, Yesu Kristo, katika ule mbadiliko wa sura juu ya mlima. (Mt. 17:1-5) Akirejeza kwenye fahari ya pindi hiyo, Petro alisema: “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.”—2 Pet. 1:19.
36. Ni kwa nini Yehova alionyesha watu wake rehema, na matumaini yetu katika Ufalme wa Mbegu hiyo yameongezeka jinsi gani?
36 Matukio yaliyoandikwa katika kitabu cha Wafalme wa Pili yafunua kwamba hukumu ya Yehova juu ya wazoeaji wa dini bandia na wote wanaomwaga kimakusudi damu isiyo na hatia ni kuangamizwa. Hata hivyo, Yehova alionyesha watu wake kibali na rehema “kwa ajili ya agano lake na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.” (2 Fal. 13:23) Aliwahifadhi “kwa ajili ya Daudi mtumishi wake.” (8:19) Ataonyesha rehema hiyo kwa wale wanaomgeukia katika siku hii. Tupitiapo maandishi na ahadi za Biblia, jinsi tunavyotazamia kwa uhakika wenye kuongezeka Ufalme wa “mwana wa Daudi,” Yesu Kristo Mbegu aliyeahidiwa, ambao katika huo umwagaji wa damu na uovu havitakuwapo tena!—Mt. 1:1; Isa. 2:4; Zab. 145:20.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 152, 325; Buku 2, kurasa 908, 1101.