Mafunzo Juu ya Maandiko Yenye Pumzi ya Mungu na Habari ya Msingi Yayo
Funzo Namba 5—Maandishi-Awali ya Kiebrania ya Maandiko Matakatifu
Jinsi Maandiko ya Kiebrania, yakiwa sehemu ya Neno la Mungu alilopulizia, yalivyonakiliwa, kuhifadhiwa bila ya maandishi-awali kubadilishwa, na yakapokezwa mpaka siku hii.
1. (a) ‘Maneno ya Yehova’ hutofautianaje na hazina nyingine za wakati uliopita? (b) Ni maswali gani yanayotokea kwa habari ya uhifadhi wa Neno la Mungu?
‘MANENO ya Yehova’ yaliyoandikwa yaweza kufananishwa na maji ya ukweli yaliyokusanywa katika akiba kubwa ya hati zilizopuliziwa na Mungu. Jinsi tunavyoweza kuwa wenye shukrani kwamba katika kipindi chote cha mawasiliano hayo ya kimbingu, Yehova alisababisha “maji” hayo yakusanywe pamoja ili yawe chanzo kisichokauka cha habari yenye kutoa uhai! Hazina nyingine za wakati uliopita, kama vile taji za kifalme, mali za urithi, na makaburi ya ukumbusho ya wanadamu, zimechakaa, zikamonyolewa, au kubomoka kwa kadiri wakati ulivyopita, lakini semi zilizo kama hazina za Mungu wetu zitadumu kwa wakati usiojulikana. (Isa. 40:8) Hata hivyo, maswali hutokea juu ya kama kumekuwako kuchafuliwa kwa maji hayo ya ukweli baada ya kuingizwa kwenye akiba hiyo. Je! yameendelea kuwa yasiyoghoshiwa? Je! yamepokewa kwa uaminifu kutoka maandishi-awali ya lugha za hapo awali, tokeo likiwa kwamba yanayopatikana kwa vikundi vya watu wa kila lugha duniani leo ni ya kutegemeka? Tutaliona kuwa funzo lenye kusisimua kuchunguza sehemu ya akiba hii inayojulikana kama maandishi-awali ya Kiebrania, tukiangalia uangalifu uliofanywa ili kuhifadhi usahihi wayo, pamoja na mipango ya ajabu iliyofanywa ili yapokezwe na kupatikana kwa mataifa yote ya ainabinadamu kupitia chapa na tafsiri mpya.
2. Maandishi yaliyopuliziwa na Mungu yalihifadhiwaje mpaka siku ya Ezra?
2 Zile hati za awali katika lugha za Kiebrania na Kiaramu zilizoandikwa na waandishi wa Mungu wa kibinadamu, kuanzia Musa katika 1513 K.W.K. mpaka muda mfupi baada ya 443 K.W.K. Kwa kadiri inavyojulikana leo, hakuna yoyote ya maandishi hayo ya awali yanayopatikana sasa. Hata hivyo, tangu mwanzo, uangalifu mkubwa ulifanywa katika kuhifadhi maandishi yaliyopuliziwa na Mungu, kutia ndani nakala zilizoamrishwa zayo. Karibu 642 K.W.K., katika wakati wa Mfalme Yosia, “kitabu cha torati” ya Musa, bila shaka kikiwa ile nakala ya awali, kilipatikana kimewekwa akiba katika nyumba ya Yehova. Kufikia wakati huu kilikuwa kimehifadhiwa kwa uaminifu kwa miaka 871. Mwandikaji wa Biblia Yeremia alidhihirisha upendezi mkubwa sana katika ugunduzi huo hata kwamba akafanya maandishi yaliyoandikwa ya hilo kwenye 2 Wafalme 22:8-10, na karibu mwaka 460 K.W.K., Ezra tena alirejezea kisa icho hicho. (2 Nya. 34:14-18) Yeye alipendezwa na mambo hayo, kwa maana “alikuwa mwandishi mwepesi [stadi, NW] katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa BWANA [Yehova, NW], Mungu wa Israeli.” (Ezra 7:6) Bila shaka Ezra angeliweza kupata hati-kunjo nyinginezo za Maandiko ya Kiebrania zilizokuwa zimetayarishwa kufikia wakati wake, yawezekana zikitia ndani zile za awali za baadhi ya maandishi yaliyopuliziwa na Mungu. Hakika, yaonekana Ezra alikuwa mhifadhi wa maandishi ya kimungu katika siku yake.—Neh. 8:1, 2.
KIPINDI CHA UNAKILIJI WA HATI
3. Ni uhitaji gani uliotokea wa nakala za ziada za Maandiko, nao ulitimizwaje?
3 Kuanzia wakati wa Ezra na kuendelea, kulikuwako uhitaji ulioongezeka wa nakala za Maandiko ya Kiebrania. Si Wayahudi wote waliorejea Yerusalemu na Palestina wakati wa kurejeshwa 537 K.W.K. na baada ya hapo. Badala yake, maelfu walibaki Babuloni, na hali wengine walihama kwa ajili ya biashara na sababu nyinginezo, tokeo likawa kwamba walipatikana katika vitovu vikubwa vya kibiashara vilivyo vingi vya ulimwengu wa kale. Wayahudi wengi walihiji (walisafiri) kila mwaka kurudi Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu za hekalu mbalimbali, na huko wangeshiriki katika ibada iliyoongozwa katika Kiebrania cha Biblia. Katika wakati wa Ezra Wayahudi katika mabara mengi ya mbali walitumia mahali mbalimbali pao pa kukusanyikia palipoitwa masinagogi, ambako usomaji na mazungumzo ya Maandiko ya Kiebrania yalifanywa.a Kwa sababu ya mahali mbalimbali palipotawanyika pa ibada, wanakiliji walihitajiwa wazidishe hati zilizoandikwa kwa mkono.
4. (a) Geniza ilikuwa nini, nayo ilitumiwaje? (b) Ni ugunduzi gani wenye thamani uliopatikana katika mojawapo hizo katika karne ya 19?
4 Masinagogi hayo kwa kawaida yalikuwa na chumba cha kuwekea akiba kilichojulikana kuwa geniza. Baada ya wakati, Wayahudi walitia ndani ya geniza hati zilizotupwa ambazo zilikuwa zimeraruka au kuchakazwa na umri, na mahali pazo kuweka mpya kwa matumizi ya sinagogi wakati huo. Pindi kwa pindi, vitu vilivyokuwamo ndani ya geniza vingezikwa kirasmi katika ardhi, ili maandishi-awali hayo—yenye jina takatifu la Yehova—yasinajisiwe. Kwa karne nyingi, kwa njia hiyo maelfu ya hati za kale za Biblia ya Kiebrania zilitokomea zisitumiwe. Hata hivyo, geniza yenye vitu vingi ya sinagogi katika Cairo ya Kale haikufanywa hivyo, yawezekana kwa sababu ilikuwa imezungushwa kuta na kusahauliwa mpaka katikati ya karne ya 19. Katika 1890, wakati sinagogi hilo lilipotengenezwa kulikoharibika, vilivyokuwamo ndani ya geniza vilichunguzwa tena na hazina zayo ama ziliuzwa au kutolewa kuwa upaji hatua kwa hatua. Kutokana na chanzo hicho, hati zilizokaribia kuwa kamili na maelfu ya vipande (vingine vinavyosemwa kuwa za karne vya sita W.K.) zimefika kwenye Maktaba ya Chuo Kikuu cha Cambridge na maktaba nyinginezo za Ulaya na Amerika.
5. (a) Ni hati zipi za Kiebrania za kale ambazo sasa zimepangwa katika orodha, nazo zina umri gani? (b) Uchunguzi wazo wafunua nini?
5 Leo, katika maktaba mbalimbali za ulimwengu, hati zipatazo 6,000 za Maandiko ya Kiebrania yote au visehemu zimehesabiwa na kupangwa katika orodha. Mpaka hivi karibuni hakukuwako hati kama hizo (isipokuwa vipande vichache) za umri mkubwa zaidi ya karne ya 10 W.K. Kisha, katika 1947, katika eneo la Bahari ya Chumvi, kuligunduliwa hati-kunjo ya kitabu cha Isaya, na katika miaka iliyofuata hati-kunjo za ziada zenye thamani kubwa za Maandiko ya Kiebrania zilikuja kupatikana wakati mapango katika eneo la Bahari ya Chumvi yalitoa hazina kubwa za hati zilizokuwa zimefichwa kwa miaka karibu 1,900. Wataalamu sasa wamezipa tarehe baadhi yazo kuwa zilinakiliwa katika karne chache za mwisho za K.W.K. Uchunguzi wa ulinganishaji wa hati zipatazo 6,000 za Maandiko ya Kiebrania hutoa msingi thabiti wa kuthibitisha maandishi-awali ya Kiebrania na hufunua uaminifu katika upokezi wa maandishi-awali hayo.
LUGHA YA KIEBRANIA
6. (a) Historia ya kale ya lugha ya Kiebrania ilikuwa nini? (b) Ni kwa nini Musa alistahili kuandika Mwanzo?
6 Ile ambayo wanadamu leo huiita lugha ya Kiebrania, katika namna yayo ya awali, ilikuwa lugha ambayo Adamu alinena katika bustani ya Edeni. Kwa sababu hiyo yaweza kurejezewa kuwa lugha ya mwanadamu. Ndiyo lugha iliyonenwa katika siku ya Nuhu, ingawa ikiwa na msamiati uliokuwa ukikua. Kwa kupanuka zaidi bado, ilikuwa ndiyo lugha ya msingi iliyookoka wakati Yehova alipovuruga uneni wa ainabinadamu kwenye Mnara wa Babeli. (Mwa. 11:1, 7-9) Kiebrania ni sehemu ya kikundi cha lugha za mataifa yaliyotokana na Shemu, kikiwa ndicho kichwa cha familia hiyo. Yaonekana kinahusiana na lugha ya Kanaani katika wakati wa Abrahamu, na kutokana na tawi lao la Kiebrania, Wakanaani walifanyiza lahaja mbalimbali. Kwenye Isaya 19:18 hurejezewa kuwa “lugha ya Kanaani.” Katika wakati wake Musa alikuwa msomi, aliyekuwa amefunzwa si hekima ya Wamisri pekee bali pia lugha ya Kiebrania cha babu zake. Kwa sababu hiyo angeweza kusoma hati za kale ambazo angeweza kupata, nazo zaweza kuwa ziliweka msingi wa baadhi ya habari aliyoandika katika kile kinachojulikana sasa kuwa kitabu cha Biblia cha Mwanzo.
7. (a) Ni ukuzi gani wa baadaye wa Kiebrania uliotukia? (b) Kiebrania cha Kibiblia kilitumika kama nini?
7 Baadaye, katika siku za wafalme Wayahudi, Kiebrania kilikuja kujulikana kuwa “lugha ya Kiyahudi.” (2 Fal. 18:26, 28) Katika wakati wa Yesu, Wayahudi walinena umbo la Kiebrania kilicho kipya zaidi au kilichopanuliwa, nacho baadaye kikaja bado kuwa Kiebrania cha kirabi. Hata hivyo, yapasa kuangaliwa kwamba katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, lugha hiyo ingali yarejezewa kuwa lugha ya “Kiebrania,” wala si Kiaramu. (Yn. 5:2; 19:13, 17; Mdo. 22:2; Ufu. 9:11) Tangu nyakati za kale zaidi, Kiebrania cha Kibiblia kilikuwa ndiyo lugha yenye kuunganisha ya uwasiliano, iliyoeleweka na walio wengi wa mashahidi wa Yehova wa kabla ya Ukristo na pia na mashahidi Wakristo wa karne ya kwanza.
8. Tukiwa tunafikiria kusudi la Maandiko, twaweza kuwa wenye shukrani kikweli kwa ajili ya nini?
8 Maandiko ya Kiebrania yalitumika kuwa akiba ya maji maangavu yenye kutakata ya ukweli, yakawasilishwa na kukusanywa chini ya upulizio wa kimungu. Hata hivyo, wale peke yao walioweza kusoma Kiebrania ndio wangeweza kujifaidi moja kwa moja na maji hayo yaliyotolewa kimungu. Wanadamu wa mataifa yenye kuzungumza ndimi nyingi wangewezaje pia kupata njia ya kunywa maji hayo ya ukweli, hivyo wapate uongozi wa kimungu na burudisho kwa ajili ya nafsi zao? (Ufu. 22:17) Njia pekee ilikuwa ni kwa kutafsiri Kiebrania mpaka kwenye lugha nyingine, kwa njia hiyo kupanua mtiririko wa kijito cha ukweli wa kimungu kwa umati wote wa ainabinadamu. Twaweza kuwa wenye shukrani kweli kweli kwa Yehova Mungu kwamba tangu karibu karne ya nne au ya tatu K.W.K. mpaka wakati wa kisasa, visehemu vya Biblia vimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 1,900. Kimekuwa kichocheo kama nini kwa watu wote wenye mwelekeo wa uadilifu, ambao kweli kweli wamewezeshwa kupata ‘upendezi’ katika maji hayo yenye thamani!—Zab. 1:2; 37:3, 4.
9. (a) Biblia yenyewe yatoa mamlaka gani ya tafsiri? (b) Ni kusudi gani la ziada zuri ambalo tafsiri za Biblia za kale zimetimiza?
9 Je! Biblia yenyewe hutoa mamlaka au haki ya kutafsiri maandiko yayo mpaka lugha nyingine? Hakika ndivyo! Neno la Mungu kwa Israeli, “Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake,” na amri ya kiunabii ya Yesu kwa Wakristo, “Habari njema hizi za ufalme zitahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ushahidi kwa mataifa yote,” lazima itimizwe. Ili hilo litukie, tafsiri ya Maandiko ni jambo la lazima. Kwa kuangalia nyuma karne zaidi ya 24 zilizopita za kutafsiri Biblia, ni wazi kwamba baraka ya Yehova imeambatana na kazi hiyo. Zaidi ya hayo, tafsiri za kale za Biblia ambazo zimeokoka zikiwa hati zimetumika pia kuthibitisha uaminifu wa kiwango cha juu wa maandishi-awali ya akiba ya kweli ya Kiebrania.—Kum. 32:43; Mt. 24:14, NW.
CHAPA ZA MAPEMA ZAIDI ZILIZOTAFSIRIWA
10. (a) Pentateuki ya Kisamaria ni nini, na kwa nini ni yenye mafaa kwetu leo? (b) Toa kielelezo cha matumizi ya Pentateuki ya Kisamaria katika New World Translation.
10 Pentateuki ya Kisamaria. Ya tarehe ya nyakati za mapema, ni tafsiri inayojulikana kuwa Pentateuki ya Kisamaria, ambayo, kama jina linavyoonyesha, ina vitabu vitano vya kwanza peke yake vya Maandiko ya Kiebrania. Kwa halisi hiyo ni utohoaji wa maandishi-awali ya Kiebrania kuwa maandishi ya Kisamaria, yaliyositawishwa kutokana na maandishi ya Kiebrania ya kale. Hiyo hutoa kionyeshi chenye msaada kwa maandishi-awali ya Kiebrania ya wakati huo. Kutohoa huko kulifanywa na Wasamaria—wazao wa wale walioachwa katika Samaria baada ya kushindwa kwa ufalme wa Israeli wa makabila kumi katika 740 K.W.K. na wale walioletwa na Waashuri wakati huo. Wasamaria walichanganya ibada ya Israeli na ile ya miungu yao wenyewe ya kipagani, nao walikubali Pentateuki. Hudhaniwa kwamba walijifanyia nakala yayo karibu na karne ya nne K.W.K., ingawa baadhi ya wasomi hudokeza kwamba yaweza kuwa ilikuwa baadaye sana katika karne ya pili K.W.K. Walipokuwa wakisoma maandishi-awali yayo, kwa kweli, wao wangekuwa wakitamka Kiebrania. Ijapokuwa maandishi-awali hayo yana tofauti zipatazo 6,000 kutoka kwa maandishi-awali ya Kiebrania, nyingi zazo ni vijambo vidogo. Nakala za hati chache zilizopo ni za kale zaidi ya karne ya 13 W.K. Marejezo fulani hufanywa kwa Pentateuki ya Kisamaria katika vielezi-chini vya New World Translation.b
11. Targum ni nini, nazo ni zenye mafaa gani kuhusiana na maandishi-awali ya Maandiko ya Kiebrania?
11 Targum za Kiaramu. Neno la Kiaramu kwa “fasiri” au “fanya muhtasari” ni targum. Tangu wakati wa Nehemia na kuendelea, Kiaramu kilikuja kutumiwa kama lugha ya kawaida ya wengi wa Wayahudi walioishi katika eneo la Uajemi, na kwa hiyo ikawa lazima kufuatisha maandishi ya Maandiko ya Kiebrania na tafsiri katika lugha hiyo. Yaelekea yalichukua namna yayo ya kisasa si mapema kupita karne ya tano hivi W.K. Ingawa hayo ni mihtasari isiyo kamili kabisa ya maandishi-awali ya Kiebrania, na wala si tafsiri sahihi, yanatokeza habari ya msingi yenye mambo mengi ya maandishi-awali hayo na hutoa msaada katika kuamua vifungu fulani vigumu-vigumu. Marejezo mengi-mengi hufanywa kwa Targum katika vielezi-chini vya New World Translation.c
12. Septuagint ni nini, na kwa nini ni yenye maana sana?
12 Septuagint ya Kigiriki. Tafsiri yenye maana zaidi kati ya zile za mapema za Maandiko ya Kiebrania, na tafsiri ya kwanza iliyoandikwa kihalisi kutoka Kiebrania, ni Septuagint ya Kigiriki (maana yake, “Sabini”). Tafsiri yayo ilianza karibu 280 K.W.K., kulingana na mapokeo, ikifanywa na wasomi 72 wa Kiyahudi wa Aleksandria, Misri. Baadaye, kwa njia fulani hesabu 70 ikaja kutumiwa, na kwa hiyo chapa hiyo ikaitwa Septuagint. Kwa wazi ilikamilishwa wakati fulani katika karne ya pili K.W.K. Ilitumika kuwa Andiko kwa ajili ya Wayahudi wenye kunena Kigiriki na ilitumiwa sana mpaka wakati wa Yesu na mitume wake. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, manukuu ya moja kwa moja yaliyo mengi kati ya yale 320 na jumla iliyounganishwa ya labda manukuu na marejezo 890 ya Maandiko ya Kiebrania hutegemea Septuagint.
13. Ni vipande vipi vyenye thamani vya Septuagint vilivyookoka mpaka siku hii, navyo ni vyenye thamani gani?
13 Kungali kwapatikana kwa ajili ya funzo leo hesabu kubwa ya vipande vya Septuagint vilivyoandikwa kwenye mafunjo. Ni vyenye thamani kwa sababu ni vya nyakati za mapema za Ukristo, na ingawa mara nyingi hivyo ni mistari au sura chache, husaidia katika kukadiria maandishi-awali ya Septuagint. Mkusanyo wa Mafunjo ya Fouad (Inventory No. 266) uligunduliwa katika Misri katika 1939 na umeoonekana kuwa ni wa karne ya kwanza K.W.K. Una visehemu vya vitabu vya Mwanzo na Kumbukumbu la Torati. Katika vipande vya Mwanzo, jina la kimungu halionekani kwa sababu ya uhifadhi usio kamili. Hata hivyo, katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, huonekana katika mahali mbalimbali, likiwa limeandikwa katika herufi za Kiebrania za mraba ndani ya maandishi-awali ya Kigiriki.d Mafunjo mengine ni ya tarehe ya baadaye ya karibu karne ya nne W.K., wakati ambapo mchapo wenye kudumu zaidi, namna nzuri ya ngozi ambayo kwa ujumla ilitengenezwa kwa ngozi ya ndama, mwana-kondoo, au mbuzi, ilianza kutumiwa kwa kuandikia hati.
14. (a) Origen ashuhudia nini kuhusu Septuagint? (b) Septuagint ilikorofishwa wakati gani na jinsi gani? (c) Ni lazima Wakristo wa mapema wawe walitoa ushahidi gani katika kutumia Septuagint?
14 Yapendeza kwamba jina la kimungu, katika namna ya Tetragrammatoni, laonekana pia katika Septuagint ya Hexapla ya Origen yenye safu sita, iliyokamilishwa karibu 245 W.K. Akieleza juu ya Zaburi 2:2, Origen aliandika hivi juu ya Septuagint: “Katika hati zilizo sahihi zaidi LILE JINA hutokea katika herufi za Kiebrania, lakini si katika [herufi] za leo za Kiebrania, bali katika zile za kale zaidi.”e Uthibitisho waonekana ni wenye kukata maneno kwamba Septuagint ilikorofishwa (ilichafuliwa) katika tarehe ya mapema, Kyʹri·os (Bwana) na The·osʹ (Mungu) yakawekwa badala ya Tetragrammatoni. Kwa kuwa Wakristo wa mapema walitumia hati zenye jina la kimungu, haiwezi kuwaziwa kwamba walifuata mapokeo ya Kiyahudi ya kushindwa kutamka “LILE JINA” wakati wa huduma yao. Lazima wawe waliweza kutoa ushahidi kwa jina la Yehova moja kwa moja kutoka Septuagint ya Kigiriki.
15. (a) Ukitumia chati kwenye ukurasa 314, eleza juu ya hati za mchapo na za ngozi za Septuagint. (b) New World Translation yafanya marejezo gani kwazo?
15 Kungali mamia ya hati za mchapo na ngozi za Septuagint ya Kigiriki. Hesabu kadhaa yazo, zilizofanyizwa kati ya karne ya nne W.K. na karne ya tisa W.K., ni za maana kwa sababu ya visehemu vikubwa vya Maandiko ya Kiebrania vinayohusishwa. Zajulikana kuwa uncial kwa sababu zimeandikwa kwa ujumla katika herufi kubwa sana, zilizoachana. Zinazosalia huitwa minuschule kwa sababu zimeandikwa katika mwandiko mdogo zaidi, wa namna ya mviringo. Hati za minuschule, au mwandiko wa mviringo, zilibaki kwa mtindo huo tangu karne ya tisa mpaka kuanzishwa kwa uchapaji. Hati zenye kutokeza za uncial za karne ya nne na ya tano, yaani, Vatican No. 1209, Sinaitic, na Alexandrine, zote zina Septuagint ya Kigiriki kukiwako tofauti ndogo-ndogo. Marejezo mengi-mengi hufanywa kwa Septuagint katika vielezi-chini na maelezo katika New World Translation.f
16. (a) Vulgate ya Kilatini ni nini, na kwa nini ni yenye thamani sana? (b) Toa kielelezo cha mrejezo wa New World Translation kwayo.
16 Vulgate ya Kilatini. Tafsiri hii imekuwa ndiyo maandishi-awali makuu yanayotumiwa na umati wa watafsiri Wakatoliki katika kutokeza chapa nyingine katika lugha zilizo nyingi za Jumuiya ya Wakristo ya Magharibi. Chanzo cha Vulgate kilikuwa nini? Neno la Kilatini vulgatus humaanisha “kawaida, kinachopendwa na wengi.” Wakati Vulgate ilipotokezwa hapo kwanza, ilikuwa katika Kilatini, kilichokuwa kinatumiwa na wengi, cha kawaida cha siku hiyo hivi kwamba ingeweza kueleweka rahisi na makabwela wa Milki ya Magharibi ya Kirumi. Msomi Jerome, aliyefanyiza tafsiri hiyo, hapo awali alikuwa amefanya masahihisho mawili ya Zaburi za Kale za Kilatini, kwa kulinganisha na Septuagint ya Kigiriki. Hata hivyo, tafsiri yake ya Biblia ya Vulgate ilifanywa moja kwa moja kutoka lugha za awali za Kiebrania na Kigiriki na kwa hiyo haikuwa tafsiri iliyotolewa kwa tafsiri nyingine. Jerome alifanyia kazi tafsiri yake ya Kilatini kutoka Kiebrania kuanzia karibu 390 W.K. mpaka 405 W.K. Ingawa kazi iliyokamilishwa ilitia ndani vitabu vya Apocrypha (visivyokubalika), ambavyo kufikia wakati huo vilikuwamo ndani ya nakala za Septuagint, Jerome alionyesha waziwazi vitabu vilivyokubalika na ambavyo havikukubalika. New World Translation hurejezea mara nyingi katika Vulgate ya Jerome katika vielezi-chini vyayo.g
MAANDISHI-AWALI YA LUGHA YA KIEBRANIA
17. Waandishi, au Wasoferi walikuwa nani, naye Yesu aliwalaani vikali kwa ajili ya nini?
17 Wasoferi. Wanaume walionakili Maandiko ya Kiebrania kuanzia siku za Ezra na kuendelea mpaka wakati wa Yesu waliitwa waandishi, au Wasoferi. Baada ya wakati, walianza kujichukulia daraka la kubadili maandishi-awali. Kwa kweli, Yesu mwenyewe aliwalaani vikali hao waliopaswa kuwa wahifadhi wa Sheria kwa kujichukulia mamlaka isiyokuwa yao.—Mt. 23:2, 13.
18. (a) Wamasora walikuwa nani, na wametoa maelezo gani yenye thamani kwenye maandishi-awali ya Kiebrania? (b) Ni vipi baadhi ya vielelezo vya masahihisho yao, kama inavyoonyeshwa katika New World Translation?
18 Masora Yafunua Mabadilisho. Waandamizi wa waandishi Wasoferi katika karne zilizofuata Kristo walikuja kujulikana kuwa Wamasora. Wao waliona mabadilisho yaliyofanywa na Wasoferi wa mapema, wakayaandika katika pambizo au kwenye mwisho wa maandishi-awali ya Kiebrania. Maandishi hayo ya pambizoni yakaja kujulikana kuwa Masora. Masora yaliorodhesha mambo 15 yasiyo ya kawaida ya Wasoferi, yaani, maneno au semi 15 katika maandishi-awali ya Kiebrania yaliyokuwa yametiwa alama ya nukta au vistari. Baadhi ya mambo hayo yasiyo ya kawaida hayabadili tafsiri wala fasiri ya Kiingereza, lakini mengine hubadili na ni yenye umaana.h Wasoferi waliruhusu hofu yao ya ushirikina ya kutotamka jina la Yehova iwatege wakalibadili lisomeke ʼAdho·naiʹ (Bwana) katika sehemu 134 na kusomeka ʼElo·himʹ (Mungu) katika visa fulani. Masora huorodhesha mabadilisho hayo.i Wasoferi au waandishi wa mapema hushtakiwa pia kufanya masahihisho 18, kulingana na maandishi fulani katika Masora, ingawa kwa wazi kulikuwako hata mengi zaidi.j Masahihisho hayo yaelekea sana yalifanywa kwa nia nzuri kwa sababu kifungu cha awali kilionekana ama kikionyesha ukosefu wa kumcha Mungu au kukosa heshima kwa wawakilishi wake wa kidunia.
19. Maandishi-awali ya Kikonsonanti ya Kiebrania ni nini, nayo yalithibitishwa lini yakawa katika umbo lililoandikwa?
19 Maandishi-awali ya Kikonsonanti. Alfabeti ya Kiebrania hufanyizwa na konsonanti 22, bila ya irabu (vokali). Hapo awali, msomaji alipaswa kutia sauti za irabu kutokana na maarifa yake ya lugha hiyo. Uandishi wa Kiebrania ulikuwa kama hati iliyofupizwa. Hata katika Kiswahili cha ki-siku-hizi kuna vifupizo vingi vinavyokubalika kila mahali na kutumiwa na watu vikionyesha konsonanti pekee. Kwa kielelezo n.k. kuwa kifupi cha na kadhalika. Vivyo hivyo, lugha ya Kiebrania ilitia ndani mfululizo wa maneno yaliyofanyizwa kwa konsonanti pekee. Kwa hiyo, kwa “maandishi-awali ya kikonsonanti” humaanishwa maandishi-awali ya Kiebrania bila ya alama zozote za irabu. Maandishi-awali ya kikonsonanti ya hati za Kiebrania yaliimarishwa umbo layo kati ya karne ya kwanza na ya pili W.K., ijapokuwa hati zenye maandishi-awali yenye kutofautiana ziliendelea kutawanywa kwa wakati fulani. Mabadilisho hayakufanywa tena, tofauti na kipindi cha hapo awali cha Wasoferi.
20. Wamasora walifanya nini kuhusu maandishi-awali ya Kiebrania?
20 Maandishi-awali ya Kimasora. Katika nusu ya pili ya mileani ya kwanza W.K., Wamasora (Kiebrania, ba·ʽalehʹ ham·ma·soh·rahʹ, maana yake “Wataalamu wa Mapokeo”) walianzisha mfumo wa nukta za irabu na alama za lafudhi. Hizo zilitumika kuwa msaada ulioandikwa katika kusoma na kutamka sauti za irabu, ambapo hapo awali matamshi yalikuwa yakipokezwa kwa mapokeo simulizi. Wamasora hawakufanya mabadilisho yoyote katika maandishi-awali waliyopokeza bali waliandika maandishi ya pambizoni katika Masora kwa kadiri walivyoona yafaa. Walitumia uangalifu mkubwa wa kutojichukulia daraka lolote la kubadilisha maandishi-awali. Kuongezea hayo, katika Masora yao, walivuta fikira kwenye mitofautiano ya maandishi-awali na kuonyesha maneno sahihi waliyofikiria kuwa ya lazima.
21. Maandishi-awali ya Kimasora ni nini?
21 Shule tatu za Wamasora zilishiriki katika ukuzi wa kutia alama za irabu na lafudhi kwa maandishi-awali ya kikonsonanti, yaani, ya Kibabuloni, ya Kipalestina, na ya Tiberia. Sasa maandishi-awali ya Kiebrania yaliyo katika chapa zilizochapwa za Biblia ya Kiebrania hujulikana kuwa maandishi-awali ya Kimasora na hutumia mfumo uliobuniwa na shule ya Tiberia. Mfumo huo ulisitawishwa na Wamasora wa Tiberia, jiji moja katika pwani ya magharibi ya Bahari ya Galilaya. Vielezi-chini katika New World Translation hurejezea mara nyingi kwenye maandishi-awali ya Kimasora (chini ya mfano M) na kwenye maandishi yayo ya pambizoni, Masora (chini ya mfano Mmargin).k
22. Ni hati gani ya maandishi-awali ya Kibabuloni inatumika, nayo yalinganaje na maandishi-awali ya Tiberia?
22 Shule ya Palestina iliweka ishara za irabu juu ya konsonanti. Ni hesabu ndogo ya hati hizo iliyotufikia sisi, kuonyesha kwamba mfumo huo wa lafudhi ulikuwa usiokamilika. Mfumo wa Kibabuloni wa kuonyesha irabu pia ulikuwa juu ya mistari. Hati moja yenye kutoa kizibiti cha uonyeshaji huo wa Kibabuloni ni Petersburg Codex of the Prophets, ya 916 W.K., iliyohifadhiwa katika Leningrad Public Library, U.S.S.R. Kodeksi hiyo ina Isaya, Yeremia, Ezekieli, na manabii “wenye umaana mdogo,” ikiwa na maandishi ya pambizoni (Masora). Wasomi wameichunguza kwa shauku hati hiyo na kuilinganisha na maandishi-awali ya Tiberia. Ingawa hutumia mfumo wa lafudhi juu ya mistari, hiyo kwa kweli hufuata maandishi-awali ya Tiberia kuhusiana na maandishi-awali ya kikonsonanti na irabu na Masora zayo. Jumba la Ukumbusho la Uingereza lina nakala ya maandishi-awali ya Kibabuloni ya Pentateuki, ambayo imeonekana inakubaliana sana na maandishi-awali ya Tiberia.
23. Ni mfululizo gani wa ugunduzi wa hati za Kiebrania umefanywa karibu na Bahari ya Chumvi?
23 Hati-Kunjo za Bahari ya Chumvi. Katika 1947 sura mpya yenye kusisimua katika historia ya hati za Kiebrania ilianza. Katika pango kule Wadi Qumran (Nahal Qumeran), katika eneo la Bahari ya Chumvi, hati-kunjo ya kwanza ya Isaya, pamoja na hati-kunjo nyingine za Kibiblia na zisizo za Kibiblia, ziligunduliwa. Muda mfupi baada ya hapo, nakala kamili yenye kufanana kabisa na hati-kunjo hiyo ya Isaya iliyohifadhiwa vizuri (1QIsa) ilitangazwa kwa wasomi ili wajifunze. Huaminiwa ni ya tarehe ya kuelekea mwisho wa karne ya pili K.W.K. Hakika, huo ulikuwa ugunduzi mkubwa ajabu—hati ya Kiebrania yenye umri zaidi wa karibu miaka elfu moja kuliko hati ya kale zaidi iliyokuwapo ya maandishi-awali ya Kimasora ya Isaya yenye kutambulika!l Mapango mengine katika Qumran yalitokeza vipande vya hati-kunjo zaidi ya 170 zenye kuwakilisha vitabu vyote vya Maandiko ya Kiebrania isipokuwa Esta. Uchunguzi wa hati-kunjo hizo ungali unaendelea.
24. Hati hizo zalinganaje na maandishi-awali ya Kimasora, na New World Translation huzitumiaje?
24 Msomi mmoja huripoti kwamba uchunguzi wake wa Zaburi 119 iliyo ndefu katika mojawapo Hati-Kunjo ya Bahari ya Chumvi ya Zaburi (11QPsa) huonyesha kuwa karibu yapatana kabisa katika maneno na maandishi-awali ya Kimasora ya Zaburi 119. Kuhusu Hati-Kunjo za Zaburi, Profesa J. A. Sanders aliandika hivi: “[Tofauti] zilizo nyingi ni za maendelezo sahihi ya maneno na ni zenye umaana tu kwa wasomi wale wanaopendezwa na vidokezi vya matamshi ya Kiebrania cha kale, na mambo kama hayo.”a Vielelezo vingine vya hati hizi za kale vyenye kutokeza havionyeshi tofauti kubwa katika visa vilivyo vingi. Hati-kunjo ya Isaya yenyewe, ijapoonyesha tofauti fulani-fulani katika kuendeleza maneno na katika utunzi wa kisarufi, haitofautiani kwa mambo ya kimafundisho. Hati-kunjo ya Isaya iliyotangazwa ilichunguzwa kuhusu tofauti zayo katika kutayarisha New World Translation, na marejezo yamefanywa kwayo.b
25. Ni maandishi-awali gani ya Kiebrania ambayo sasa yamekwisha zungumzwa, na uchunguzi wayo watuhakikishia nini?
25 Njia kuu za upokezaji wa Maandiko ya Kiebrania sasa zimekwisha zungumzwa. Hasa, hizo ni Pentateuki ya Kisamaria, Targum za Kiaramu, Septuagint ya Kigiriki, maandishi-awali ya Kiebrania ya Tiberia, maandishi-awali ya Kiebrania ya Kipalestina, maandishi-awali ya Kiebrania ya Kibabuloni, na maandishi-awali ya Kiebrania ya Hati-Kunjo za Bahari ya Chumvi. Likiwa tokeo la uchunguzi na ulinganishi wa maandishi-awali hayo, sisi tumehakikishiwa kwamba kwa ujumla Maandiko ya Kiebrania yametufikia sisi leo yakiwa katika umbo ambalo watumishi waliopuliziwa wa Mungu waliyaandika hapo kwanza.
MAANDISHI-AWALI YA KIEBRANIA YALIYOCHUJWA
26. (a) Uchunguzi wenye uchambuzi wa maandishi-awali ya Kiebrania uliendelezwa wakati gani, na ni ipi baadhi ya maandishi-awali yaliyosahihishwa yaliyokwisha chapishwa? (b) Maandishi-awali ya Ginsburg yametumiwaje?
26 Chapa ya kawaida iliyochapishwa ya Biblia ya Kiebrania mpaka kuingia karne ya 19 ilikuwa ni Biblia ya Pili ya Kirabi ya Jacob ben Chayyim iliyotangazwa katika 1524-25. Haikuwa mpaka karne ya 18 kwamba wasomi wakaanza kusogeza mbele uchunguzi wa kuchambua wa maandishi-awali ya Kiebrania. Katika 1776-80, kule Oxford, Benjamin Kennicott alitangaza usomaji mbalimbali wenye kutofautiana kutokana na hati za Kiebrania zaidi ya 600. Kisha, katika 1784-98, kule Parma, msomi Mwitalia J. B. de Rossi alitangaza usomaji mbalimbali wenye kutofautiana wa hati nyingine zaidi ya 800. Msomi wa Kiebrania S. Baer, wa Ujerumani, pia alitokeza maandishi-awali yaliyosahihishwa. Katika nyakati za kisasa zaidi, C. D. Ginsburg alitumia miaka mingi kutokeza maandishi-awali yenye kuchambua yaliyosahihishwa ya Biblia ya Kiebrania. Hiyo ilitokea kwanza katika 1894, kukiwa na chapa mpya yenye masahihisho ya mwisho katika 1926.c Joseph Rotherham alitumia chapa ya 1894 ya maandishi-awali hayo katika kutokeza tafsiri yake ya Kiingereza, The Emphasised Bible, katika 1902, na Profesa Max L. Margolis na wafanya kazi wenzake walitumia maandishi-awali ya Ginsburg na ya Baer katika kutokeza tafsiri yao ya Maandiko ya Kiebrania katika 1917.
27, 28. (a) Biblia Hebraica ni nini, nayo imesitawishwaje? (b) New World Translation imetumiaje maandishi-awali hayo?
27 Katika 1906 msomi Mwebrania Rudolf Kittel alitokeza katika Ujerumani chapa yake ya kwanza (na baadaye, chapa ya pili) ya maandishi-awali ya Kiebrania yaliyochujwa yenye kichwa Biblia Hebraica, au “Biblia ya Kiebrania.” Katika kitabu hicho Kittel alitokeza mfumo wa maandishi-awali kupitia vielezi-chini vyenye kutia mengi, ambavyo vilikusanya au kulinganisha zile hati nyingi za maandishi-awali ya Kiebrania ya Kimasora yaliyopatikana wakati huo. Yeye alitumia maandishi-awali yaliyokubaliwa kwa ujumla ya Jacob ben Chayyim kuwa msingi wa maandishi-awali hayo. Maandishi-awali ya Kimasora ya Ben Asher ya kale zaidi na bora zaidi, yaliyokuwa yamekuwa ndiyo kiwango yapata karne ya 10 W.K., yalipoweza kupatikana, Kittel alianza kutokeza chapa ya tatu iliyo tofauti kabisa ya Biblia Hebraica. Kazi hiyo ilikamilishwa na washiriki wake baada ya kifo chake.
28 Biblia Hebraica ya Kittel, chapa ya 7, ya 8, na ya 9 (1951-55), ilifanyiza maandishi-awali ya msingi yaliyotumiwa kwa sehemu ya Kiebrania ya New World Translation katika Kiingereza. Chapa mpya ya maandishi-awali ya Kiebrania, yaani Biblia Hebraica Stuttgartensia, yenye tarehe ya 1977, yalitumiwa kufanya iwe ya kisasa habari iliyotolewa katika vielezi-chini vya New World Translation iliyotangazwa katika 1984.
29. Ni sehemu gani ya Biblia Hebraica iliyokuwa yenye thamani maalumu katika kurudisha jina la kimungu?
29 Utumizi wa Kittel wa Masora za pambizoni, ambao huonyesha mabadilisho mengi ya maandishi-awali ya waandishi wa kabla ya Ukristo, umetokeza tafsiri sahihi katika New World Translation, ukitia ndani kurudishwa kwa jina la kimungu, Yehova. Utaalamu wenye kuongezeka daima wa usomi wa Kibiblia huendelea kutokezwa kupitia New World Translation.
30. (a) Ukitumia chati katika ukurasa 308 inayoonyesha vyanzo vya sehemu ya Andiko la Kiebrania ya New World Translation, fuatisha historia ya maandishi-awali ya Kiebrania mpaka kwenye Biblia Hebraica ikiwa chanzo kikuu cha New World Translation. (b) Ni vipi baadhi ya vyanzo vingine ambavyo Halmashauri ya Tafsiri ya Biblia ya New World imerejezea?
30 Yenye kufuatana na funzo hili ni chati inayotokeza vyanzo vya maandishi-awali ya Maandiko ya Kiebrania katika New World Translation. Chati hii yaonyesha kifupi ule ukuzi wa maandishi-awali ya Kiebrania yenye kuongoza kwenye Biblia Hebraica ya Kittel, ambayo ndiyo iliyokuwa chanzo kikuu kilichotumiwa. Vyanzo vya pili vilivyoshauriwa vimeonyeshwa kwa vistari vyenye mapengo meupe. Hilo halikusudiwi kuonyesha kwamba katika kisa cha tafsiri kama vile Vulgate ya Kilatini na Septuagint ya Kigiriki, kazi zile za awali zilishauriwa. Kama ilivyo kwa maandishi yaliyopuliziwa na Mungu ya Kiebrania yenyewe, nakala za awali za chapa hizo hazipo sasa. Vyanzo hivyo vilishauriwa kupitia chapa zenye kutegemeka za maandishi-awali au kutokana na tafsiri zenye kutegemeka za kale na maelezo ya uchambuzi. Kwa kushauri vyanzo hivyo mbalimbali, Halmashauri ya Tafsiri ya Biblia ya New World iliweza kutokeza tafsiri yenye amri na yenye kutegemeka ya Maandiko ya Kiebrania yaliyopuliziwa na Mungu ya awali. Vyanzo hivyo vyote vimeonyeshwa katika vielezi-chini vya New World Translation.
31. (a) Kwa hiyo, sehemu hii ya Andiko la Kiebrania ya New World Translation ni tokeo la nini? (b) Kwa hiyo twaweza kuonyesha shukrani na tumaini gani?
31 Kwa hiyo sehemu ya Andiko la Kiebrania ya New World Translation ni tokeo la usomi na utafiti wa Kibiblia wa kipindi kirefu. Msingi wayo ni maandishi-awali ya uaminifu mkubwa, tokeo lililokirimiwa sana la upokezaji mwaminifu wa maandishi-awali. Kwa mtiririko na mtindo wenye kuvutia, yatolea funzo la Biblia lenye uzito tafsiri ambayo mara moja ni yenye kufuatia haki na sahihi. Shukrani zimwendee Yehova, Mungu mwenye kuwasiliana, kwamba Neno lake liko hai na lina tokeo lenye nguvu leo! (Ebr. 4:12) Watu wenye mioyo ya kufuata haki na waendelee kujenga imani kupitia funzo la Neno la Mungu lenye thamani na kuamshwa wafanye mapenzi ya Yehova wakati wa hizi siku zenye matukio makubwa-makubwa.—2 Pet. 1:12, 13.
[Maelezo ya Chini]
a Ona “Sam” katika vielezi-chini, kwenye Mwanzo 4:8; Kutoka 6:2; 7:9; 8:15; na 12:40. Uandishi huo wa mwisho hutusaidia kuelewa Wagalatia 3:17.
b Haijulikani ni wakati gani matumizi ya masinagogi yalianzishwa. Huenda ikawa ilikuwa wakati wa uhamisho wa miaka 70 wa Kibabuloni wakati ambapo hakukuwapo hekalu lolote, au huenda ikawa ilikuwa muda mfupi baada ya kurejea kutoka uhamisho, katika siku ya Ezra.
c Ona “T” katika vielezi-chini kwenye Hesabu 24:17; Kumbukumbu la Torati 33:13; na Zaburi 100:3.
d Reference Bible, Appendix 1C, “Jina la Kimungu Katika Tafsiri za Kale za Kigiriki.”
e Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 9.
f New World Translation huonyesha tofauti hizo kwa mfano LXXא kwa Sinaitic, LXXA kwa Alexandrine, na LXXB kwa Vatican. Ona vielezi-chini kwenye 1 Wafalme 14:2 na 1 Nyakati 7:34; 12:19.
g Ona “Vg” katika kielezi-chini kwenye Kutoka 37:6, NW.
h Reference Bible, appendix 2A, “Mambo Yasiyo ya Kawaida.”
i Reference Bible, appendix 1B, “Mabadilisho ya Waandishi Yanayohusu Jina la Kimungu.”
j Reference Bible, appendix 2B, “Masahihisho ya Wasoferi.”
k Ona vielezi-chini kwenye Zaburi 60:5; 71:20; 100:3; na 119:79, NW.
l Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 322.
a The Dead Sea Psalms Scroll, 1967, J. A. Sanders, ukurasa 15.
b Ona “1QIsa” katika vielezi-chini kwenye Isaya 7:1; 14:4.
c Ona “Gins.” katika kielezi-chini kwenye Walawi 11:42, NW.
[Mchoro katika ukurasa wa 308]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Vyanzo vya Maandishi-awali ya New World Translation—Maandiko ya Kiebrania
Maandishi ya Awali ya Kiebrania na Nakala za Mapema
Targum za Kiaramu
Hati-Kunjo za Bahari ya Chumvi
Pentateuki ya Kisamaria
Septuagint ya Kigiriki
Kilatini cha Kale
ya Coptic, ya Kiethiopia, ya Kiarmenia
Maandishi-awali ya Kikonsonati ya Kiebrania
Vulgate ya Kilatini
Tafsiri za Kigiriki—Akila, Theodotion, Symmachus
Peshitta ya Siria
Maandishi-awali ya ya Kimasora
Cairo Codex
Aleppo Codex
Maandishi-awali ya Kiebrania ya Ginsburg
Codex Leningrad B 19A
Biblia Hebraica (BHK), Biblia Hebraica
Stuttgartensia (BHS)
New World Translation
Maandiko ya Kiebrania—Kiingereza; Kutoka Kiingereza Mpaka Lugha Nyingine Nyingi za Ki-siku-hizi
[Mchoro katika ukurasa wa 309]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Vyanzo vya Maandishi-awali ya New World Translation—Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo
Maandiko ya Kigiriki ya Awali na Nakala za Mapema
Tafsiri ya Kiarmenia
Tafsiri za Coptic
Tafsiri za Syria—Curetonian, Philoxenian, Harclean,
Palestinian, Sinaitic, Peshitta
Kilatini cha Kale
Vulgate ya Kilatini
Maandishi-awali ya Kilatini Yaliyoandikwa Upya ya Sixtus na Clement
Hati ya Mwandiko-Mviringo
Maandishi-awali ya Erasmo
Maandishi-awali ya Stefano
Textus Receptus
Maandishi-awali ya Kigiriki ya Griesbach
Emphatic Diaglott
Mafunjo—(e.g., Chester Beatty P45, P46, P47; Bodmer P66, P74, P75)
Hati ya Maandishi-Mviringo ya Kigiriki ya Mapema—Vatican 1209 (B),
Sinaitic (א), Alexandrine (A), Ephraemi Syri rescriptus (C), Bezae (D)
Maandishi-awali ya Kigiriki ya Westcott na Hort
Maandishi-awali ya Kigiriki ya Bove
Maandishi-awali ya Kigiriki ya Merk
Maandishi-awali ya Kigiriki ya Nestle-Aland
Maandishi-awali ya Kigiriki ya United Bible Societies
Tafsiri 23 za Kiebrania (Karne ya 14-ya 20), zilizotafsiriwa
ama kutoka Vulgate ya Kigiriki au kutoka ya Kilatini,
Tetragrammatoni ikitumiwa kwa jina la kimungu
New World Translation
Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo—Kiingereza; Kutoka Kiingereza Mpaka Lugha Nyingine Nyingi za Ki-siku-hizi