Sura 1
Jumbe Kutoka Mbinguni
BIBLIA yote ni kama ujumbe kutoka mbinguni, uliotolewa na Baba yetu wa kimbingu ili kutufundisha. Lakini, jumbe mbili za pekee zilizotolewa karibu miaka 2,000 iliyopita na malaika mmoja ‘asimamaye mbele za Mungu.’ Jina lake ni Gabrieli. Na tuchunguze hali za ziara hizo mbili za duniani zenye maana.
Ni mwaka wa 3 K.W.K. Katika vilima vya Yudea, yaelekea si mbali sana na Yerusalemu, kuhani wa Yehova jina lake Zakaria aishi huko. Amezeeka, na mkeye Elisabeti amezeeka pia. Nao hawana watoto. Ni zamu ya Zakaria kutoa utumishi wa kikuhani katika hekalu la Mungu katika Yerusalemu. Ghafla Gabrieli amtokea upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia uvumba.
Zakaria aogopa sana. Lakini Gabrieli atuliza woga wake, na kusema: “Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.” Gabrieli aendelea kutangaza kwamba Yohana ‘atakuwa mkuu mbele za Yehova’ na kwamba ‘atamwekea Yehova tayari watu waliotengenezwa.’
Hata hivyo, Zakaria ashindwa kuamini. Laonekana kuwa jambo lisilowezekana hata kidogo kwamba yeye na Elisabeti wangeweza kupata mtoto katika umri wao. Kwa hiyo Gabrieli amwambia: “Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu.”
Basi, wakati uo huo, watu walio nje wanashangaa wakitaka kujua kwa nini Zakaria anachukua muda mrefu hivyo hekaluni. Atokapo nje mwishowe, yeye hawezi kusema ila aweza tu kufanya ishara kwa mikono yake, nao watambua kwamba ameona kitu fulani kipitacho nguvu za kibinadamu.
Baada ya Zakaria kumaliza kipindi chake cha kutumikia hekaluni, arudi nyumbani. Na baada ya muda mfupi yanatimia kweli—Elisabeti awa na mimba! Anapongojea mtoto wake azaliwe, Elisabeti akaa nyumbani mbali na watu kwa miezi mitano.
Baadaye Gabrieli atokea tena. Naye asema na nani? Asema na mwanamke kijana asiyeolewa aitwaye jina lake Mariamu kutoka mji wa Nazareti. Wakati huu apeleka ujumbe gani? Sikiliza! “Umepata neema kwa Mungu,” Gabrieli amwambia Mariamu. “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.” Gabrieli aongeza: “Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu, . . . [naye] ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”
Tunaweza kuwa na hakika kwamba Gabrieli ajiona kuwa amependelewa sana kupeleka jumbe hizi. Na tusomapo mengi zaidi juu ya Yohana na Yesu, tutaona kwa wazi zaidi kwa nini hasa jumbe hizi kutoka mbinguni ni za maana sana. 2 Timotheo 3:16; Luka 1:5-33.
▪ Ni jumbe gani mbili maana zilizotolewa kutoka mbinguni?
▪ Ni nani ambaye apeleka jumbe hizo, na awapelekea nani?
▪ Kwa nini ni vigumu kuamini jumbe hizo?