Sura 10
Safari za Kwenda Yerusalemu
MASIKA yamefika. Na ni wakati wa familia ya Yusufu, pamoja na marafiki na watu wa ukoo, kufunga safari yao ya wakati wa masika ya kila mwaka kwenda Yerusalemu wakasherehekee Sikukuu ya Kupitwa. Wanapoanza safari ya kilometa 100 hivi, kuna ule msisimko wa kawaida. Sasa Yesu ana miaka 12, na atazamia sherehe hiyo akiwa anapendezwa kipekee.
Kwa Yesu na familia yake, Sikukuu ya Kupitwa si jambo la siku moja tu. Wanakaa pia kwa ajili ya ile Sherehe ya Mikate Isiyotiwa Chachu ya siku saba, ambayo waiona kuwa sehemu ya wakati wa Sikukuu ya Kupitwa. Kama tokeo, safari yote hiyo kutoka nyumbani kwao Nazareti, kutia ndani wakati wa kukaa Yerusalemu, huchukua karibu majuma mawili. Lakini mwaka huu, kwa sababu ya jambo linalomhusu Yesu, inachukua muda mrefu zaidi.
Tatizo hilo linajulikana wakati wa safari ya kurudi kutoka Yerusalemu. Yusufu na Mariamu wanadhani kwamba Yesu yumo miongoni mwa kikundi cha watu wa ukoo na marafiki wanaosafiri pamoja nao. Hata hivyo haonekani wanapopumzika usiku huo, nao wanaenda kumtafuta-tafuta kati ya wasafiri wenzao. Yeye haonekani popote. Kwa hiyo Yusufu na Mariamu wasafiri mwendo wote kurudi mpaka Yerusalemu wakamtafute.
Kwa siku nzima wamtafuta wasifanikiwe. Wala siku ya pili hawamwoni. Mwishowe, siku ya tatu, wanaenda hekaluni. Humo kwenye jumba mojapo wanamwona Yesu ameketi katikati ya walimu Wayahudi, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
‘Mtoto, mbona umetufanyia hivi?’ Mariamu auliza. ‘Babako nami tumekuwa na wasiwasi mwingi sana, tukikutafuta kila mahali.’
Yesu anashangaa kusikia kwamba hawakujua mahali pa kumpata. ‘Mbona ikawa lazima mnitafute?’ auliza. ‘Je! hamkujua kwamba inanipasa kuwa humu katika nyumba ya Baba yangu?’
Yesu ashindwa kuelewa ni kwa nini wazazi wake hawangejua hivyo. Halafu, Yesu arudi nyumbani pamoja na wazazi wake na kuendelea kuwatii. Anazidi kufanya maendeleo katika hekima na ukuzi wa kimwili na kupata kibali cha Mungu na cha wanadamu. Ndiyo, tangu utoto wake na kuendelea, Yesu aweka mfano mwema, si katika kutafuta faida za kiroho tu bali pia katika kuheshimu wazazi wake. Luka 2:40-52; 22:7.
▪ Ni safari gani ya wakati wa masika ambayo Yesu hufunga kwa ukawaida pamoja na familia yake, nayo ni ya urefu gani?
▪ Ni jambo gani latukia wakati wa safari wanayofunga wakati Yesu ana umri wa miaka 12?
▪ Ni kielelezo gani Yesu awekea vijana leo?