Maisha na Huduma ya Yesu
Safari za Kwenda Yerusalemu
MASIKA yamefika. Na ni wakati kwa jamaa ya Yusufu, pamoja na marafiki na watu wa ukoo, kufunga safari yao ya kila mwaka kwenda Yerusalemu wakasherehekee Sikukuu ya Kupitwa (Pasaka). Wanapoanza safari ya kilomita 105 hivi, kuna ule mteremo wa kawaida. Sasa Yesu ana miaka 12, na anatazamia kwa kupendezwa kwa pekee na mwadhimisho huo.
Kwa Yesu na jamaa yao, Sikukuu ya Kupitwa si shughuli ya siku moja tu. Wanabaki pia kwa ajili ya Mwadhimisho wa Mikate Isiyotiwa Chachu wa siku saba unaofuata, ambao wanauona kuwa sehemu ya majira ya Sikukuu ya Kupitwa. Kwa hiyo safari yote kutoka makao yao Nazareti, kutia kukaa katika Yerusalemu, inachukua majuma mawili hivi. Lakini mwaka huu, kwa sababu ya jambo linalomhusu Yesu, safari hiyo inachukua muda mrefu zaidi.
Tatizo hilo linajulikana wakati wa safari ya kurudi kutoka Yerusalemu. Yusufu na Mariamu wanadhani Yesu yumo miongoni mwa kikundi cha watu wa ukoo au marafiki wanaosafiri pamoja. Hata hivyo haonekani wanapopumzika usiku huo, nao wanaenda kumtafuta-tafuta kati ya wenzi wao wasafiri. Haonekani po pote. Kwa hiyo Yusufu na Mariamu wanarudia njia yote mpaka Yerusalemu wakamtafute.
Kwa siku nzima wanamtafuta wasifanikiwe. Wala siku ya pili hawamwoni. Mwishowe, siku ya tatu, wanaenda hekaluni. Humo kwenye jumba mojapo wanamwona Yesu ameketi katikati ya walimu Wayahudi, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
‘Mtoto, mbona umetufanyia hivi?’ Mariamu anauliza. ‘Babako na mimi tumekuwa na wasiwasi mwingi sana, tukikutafuta kila mahali!’
Yesu anashangaa kwa kuwa hawakujua mahali pa kumpata. ‘Mbona ikawa lazima mnitafute?’ anauliza. ‘Je! hamkujua kwamba napaswa kuwa humu kwenye nyumba ya Baba yangu?’
Yesu anashindwa kuelewa ni kwa nini wazazi wake hawakujua hivyo. Halafu, Yesu anarudi nyumbani pamoja na wazazi wake na kuendelea kuwatii. Anazidi kufanya maendeleo katika hekima na ukuzi wa kimwili na kupata kibali ya Mungu na wanadamu. Ndiyo, tangu utoto wake na kuendelea, Yesu anaweka mfano mwema, si katika kutafuta faida za kiroho tu bali pia katika kuheshimu wazazi wake. Luka 2:40-52; 22:7.
◆ Ni safari gani ya wakati wa masika ambayo kwa kawaida Yesu alifanya na jamaa yao, na safari hiyo ilichukua muda gani?
◆ Kulitokea nini wakati wa safari hiyo Yesu alipokuwa na miaka 12?
◆ Yesu aliwekea vijana leo mfano gani?