Sura 19
Kufundisha Mwanamke Msamaria
WAKIWA njiani kutoka Yudea kwenda Galilaya, Yesu na wanafunzi wake wasafiri kupitia wilaya ya Samaria. Wakiwa wamechoshwa na safari, wakati kama adhuhuri hivi watua kidogo wapumzike kwenye kisima karibu na jiji la Sikari. Kisima hicho kilichimbwa na Yakobo karne nyingi zilizopita, na mpaka leo hii kingali kipo, karibu na jiji la kisasa la Nablus.
Yesu apumzikapo hapo, wanafunzi wake waingia jijini wanunue chakula. Mwanamke Msamaria ajapo kuteka maji, Yesu aomba hivi: “Nipe maji ninywe.”
Kwa kawaida Wayahudi na Wasamaria hawashughulikiani kwa sababu ya ubaguzi ulioimarika sana. Hivyo, kwa kushangaa sana, mwanamke huyo auliza: “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria?”
‘Kama ungalijua,’ akajibu Yesu, “ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.”
“Bwana,” akajibu mwanamke yule, “huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?”
“Kila anywaye maji haya ataona kiu tena,” akaonelea Yesu. “Atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele, bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.”
“Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka,” akajibu mwanamke huyo.
Yesu sasa akamwambia: “Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.”
“Sina mume,” akajibu mwanamke huyo.
Yesu akahakiki taarifa yake. “Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako.”
“Bwana, naona ya kuwa u nabii,” mwanamke huyo asema kwa kustaajabu. Akionyesha wazi mapendezi yake ya kiroho, mwanamke asema kwamba Wasamaria “waliabudu katika mlima huu [Gerazimu, usimamao karibu], nanyi [Wayahudi] husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.”
Hata hivyo, mahali pa ibada silo jambo la maana, Yesu ataja hivyo. “Saa inakuja,” akasema, “ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
Mwanamke huyo avutwa sana. “Najua ya kuwa yuaja Masihi, aitwaye Kristo,” asema mwanamke. “Naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.”
“Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yesu ajulisha wazi. Ebu fikiria hilo! Mwanamke huyo ajaye wakati wa adhuhuri kuteka maji, labda ili aepuke kuonana na wanawake wengine wa mji huo wanaomdharau kwa sababu ya njia yake ya maisha, apendelewa na Yesu kwa njia ya ajabu. Yesu amtobolea wazi kabisa jambo ambalo hajakiri waziwazi kwa mtu mwingine yeyote. Matokeo yawa nini?
Wasamaria Wengi Waamini
Warudipo kutoka Sikari wakiwa na chakula, wanafunzi wamkuta Yesu kisimani cha Yakobo walipomwacha, na ambapo sasa anasema na mwanamke Msamaria. Mwanamke huyo aondoka wakati wanafunzi wafikapo, aacha mtungi wake, na kuelekea jijini.
Kwa kupendezwa sana na mambo ambayo Yesu amemwambia, mwanamke huyo awaambia watu jijini hivi: “Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda.” Halafu, kwa kutumia njia ya kuamsha hamu yao ya kutaka kupashwa habari, auliza: “Je! haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Swali hilo latimiza kusudi lalo—watu hao waenda wakajionee wenyewe.
Wakati uo huo, wanafunzi wamhimiza Yesu ale chakula ambacho wamenunua jijini. Lakini yeye ajibu: “Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.”
“Je! mtu amemletea chakula?” wanafunzi waulizana. Yesu aeleza: “Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno?” Hata hivyo, akielekeza kwenye mavuno ya kiroho, Yesu asema: “Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja.”
Labda Yesu tayari aweza kuona matokeo makubwa ambayo yangetokana na kukutana na mwanamke huyo Msamaria—ya kwamba wengi wamwamini kwa sababu ya ushahidi wake. Mwanamke huyo awatolea watu wa jiji ushahidi akisema: ‘Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.’ Basi, wakati watu wa Sikari wanapomjia pale kisimani, wamwomba akae aendelee kusema nao zaidi. Yesu akubali mwaliko na kukaa siku mbili.
Wasamaria wamsikilizapo Yesu, wengine wengi wamwamini. Ndipo wamwambia mwanamke yule: “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.” Kwa hakika mwanamke huyo Msamaria ni kielelezo kizuri sana cha jinsi sisi tunavyoweza kutoa ushahidi juu ya Kristo kwa kuamsha hamu ili wasikilizaji watake kuchunguza habari zaidi!
Kumbuka kwamba sasa imebaki miezi minne kabla ya mavuno—kwa wazi mavuno ya shayiri, ambayo katika Palestina yatukia katika majira ya masika. Kwa hiyo labda sasa ni Novemba au Desemba. Hiyo maana yake ni kwamba baada ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 30 W.K., Yesu na wanafunzi wake walikaa miezi minane hivi katika Yudea wakifundisha na kubatiza. Sasa waondoka kwenda kwenye eneo la nyumbani kwao la Galilaya. Ni mambo gani yanayowangojea huko? Yohana 4:3-43.
▪ Kwa nini yule mwanamke Msamaria ashangaa kwamba Yesu alinena naye?
▪ Yesu amfundisha nini juu ya maji yaliyo hai na mahali pa kuabudia?
▪ Yesu amfunuliaje kuwa yeye ni nani, na kwa nini ufunuo huo washangaza sana?
▪ Mwanamke huyo Msamaria atoa ushahidi gani na matokeo yawa nini?
▪ Chakula cha Yesu chahusianaje na mavuno?
▪ Twaweza kuamuaje urefu wa huduma ya Yesu katika Yudea kufuata Sikukuu ya Kupitwa ya 30 W.K.?