Maisha na Huduma ya Yesu
Kufundisha Mwanamke Msamaria
WANAPOKUWA wakitoka Yudea kwenda Galilaya, Yesu na wanafunzi wake wanasafiri kupitia wilaya ya Samaria. Kwa kuwa wamechoka kwa sababu ya kusafiri, wakati kama adhuhuri hivi wanangoja kidogo wapumzike kwenye kisima karibu na mji wa Sikari. Kisima hicho kilichimbwa na Yakobo karne nyingi zilizopita, na mpaka leo hii kingali kipo, karibu na mji wa kisasa wa Nablus.
Yesu anapopumzika hapo, wanafunzi wake wanaingia mjini wanunue chakula. Mwanamke Msamaria anapokuja kuteka maji, Yesu anaomba hivi: “Nipe maji ninywe.”
Kwa kawaida Wayahudi na Wasamaria hawashughulikiani kwa sababu ya ubaguzi wa kindani. Kwa hiyo, mwanamke anashangaa sana na kuuliza: “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria?”
Yesu anajibu kwamba kama mwanamke huyo angejua yeye ni nani, angemwomba “maji yaliyo hai.” Anasema kwamba maji hayo yatakuwa “chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.”
“Bwana, unipe maji hayo,” mwanamke huyo anajibu.
Sasa Yesu anasema: “Nenda kamwite mumeo.”
“Sina mume,” mwanamke anajibu.
Yesu anamwambia amesema kweli. “Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako.”
“Bwana, naona ya kuwa u nabii,” mwanamke huyo anasema kwa kustaajabu. Kwa kuonyesha wazi ana mapendezi ya kiroho, mwanamke anasema kwamba Wasamaria waliabudu kwenye Mlima Gerizimu, lakini Wayahudi katika Yerusalemu.
Hata hivyo mahali pa ibada silo jambo la maana, Yesu anaonyesha. “Mungu ni Roho,” anaeleza, “nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
Mwanamke anavutwa sana. “Najua ya kuwa yuaja Masihi, aitwaye Kristo,” mwanamke anasema. “Naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.”
“Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yesu anatamka. Ebu fikiria hilo! Mwanamke huyo anayekuja wakati wa adhuhuri kuteka maji, labda ili aepuke kuonana na wanawake wengine wa mji huo wanaomdharau kwa sababu ya njia yake ya maisha, anapendelewa na Yesu kwa njia ya ajabu. Yesu anamtobolea wazi kabisa jambo ambalo hajaeleza wazi mtu mwingine ye yote. Matokeo yanakuwa nini? Makala katika toleo letu linalokuja itaeleza. Yohana 4:3-26.
◆ Kwa sababu gani mwanamke yule Msamaria alishangaa kuona Yesu akisema naye?
◆ Yesu anamfundisha nini juu ya maji yaliyo hai na mahali pa kuabudia?
◆ Yesu anamfunuliaje yeye ni nani, na kwa sababu gani ufunuzi huo ni wa kustaajabisha sana?
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 9]