Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • jy sura 19 uku. 48-uku. 51 fu. 4
  • Amfundisha Mwanamke Msamaria

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Amfundisha Mwanamke Msamaria
  • Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • WASAMARIA WENGI WAAMINI
  • Kufundisha Mwanamke Msamaria
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Kufundisha Mwanamke Msamaria
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Wasamaria Wengi Wanaamini
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Mwanamke Kisimani
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
Pata Habari Zaidi
Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
jy sura 19 uku. 48-uku. 51 fu. 4
Yesu anazungumza na mwanamke Msamaria kwenye kisima

SURA YA 19

Amfundisha Mwanamke Msamaria

YOHANA 4:3-43

  • YESU AMFUNDISHA MWANAMKE MSAMARIA NA WATU WENGINE

  • IBADA INAYOKUBALIKA KWA MUNGU

Wakiwa njiani kutoka Yudea kwenda Galilaya, Yesu na wanafunzi wake wanasafiri kuelekea kaskazini kupitia wilaya ya Samaria. Wamechoka kwa sababu ya safari hiyo. Karibu saa sita mchana wanasimama karibu na jiji la Sikari ili kupumzika kando ya kisima ambacho huenda Yakobo alikichimba au aliwalipa watu wakichimbe karne nyingi mapema. Mpaka leo, kisima kama hicho kinapatikana katika jiji la kisasa la Nablus.

Yesu akiwa anapumzika karibu na kisima hicho, wanafunzi wake wanaenda katika jiji lililo karibu ili kununua chakula. Wakiwa wameondoka, mwanamke Msamaria anakuja kuteka maji. Yesu anamwambia: “Naomba maji ninywe.”—Yohana 4:7.

Yesu anapumzika kwenye kisima, wanafunzi wake wanaondoka, kisha mwanamke Msamaria anakuja kuteka maji

Kwa kawaida Wasamaria na Wayahudi hawashirikiani kwa sababu ya ubaguzi mwingi kati yao. Kwa hiyo yule mwanamke anashangaa na kuuliza: “Wewe ni Myahudi, nami ni mwanamke Msamaria, unawezaje kuniomba maji ya kunywa?” Yesu anajibu: “Kama ungejua zawadi ya bure inayotoka kwa Mungu na ni nani ambaye anakuambia, ‘Naomba maji ninywe,’ ungemwomba, naye angekupa maji yaliyo hai.” Yule mwanamke anasema: “Bwana, huna hata ndoo ya kutekea maji, na kisima ni kirefu. Basi, umeyatoa wapi hayo maji yaliyo hai? Je, wewe ni mkuu kuliko babu yetu Yakobo, aliyetupatia kisima hiki ambacho yeye pamoja na wanawe na mifugo yake walikunywa maji yake?”—Yohana 4:9-12.

Yesu anasema: “Kila mtu anayekunywa maji haya atakuwa na kiu tena. Yeyote atakayekunywa maji nitakayompa hatakuwa na kiu kamwe, kwa sababu maji ambayo nitampa yatakuwa kama chemchemi ya maji ndani yake, inayobubujika ili kumpa uzima wa milele.” (Yohana 4:13, 14) Naam, ingawa amechoka, Yesu yuko tayari kumwambia yule mwanamke Msamaria maneno yanayoongoza kwenye uzima.

Kisha yule mwanamke anasema: “Bwana, nipe maji hayo ili nisiwe na kiu tena wala nisiendelee kuja hapa kuteka maji.” Sasa Yesu anabadili mazungumzo na kumwambia: “Nenda ukamwite mume wako uje naye hapa.” Mwanamke huyo anajibu: “Sina mume.” Lakini anashtuka sana kusikia mambo ambayo Yesu anajua anapomwambia: “Umesema kweli kwamba huna mume. Kwa maana umekuwa na waume watano, na mwanamume uliye naye sasa si mume wako.”—Yohana 4:15-18.

Anatambua maana ya maneno hayo, naye anasema kwa mshangao: “Bwana, ninaona kwamba wewe ni nabii.” Kisha anaonyesha kwamba anapendezwa na mambo ya kiroho. Jinsi gani? Anaendelea kusema: “Mababu zetu [Wasamaria] waliabudu katika mlima huu [Mlima Gerizimu, ulio hapo karibu], lakini ninyi [Wayahudi] mnasema tunapaswa kumwabudu Mungu huko Yerusalemu.”—Yohana 4:19, 20.

Hata hivyo, Yesu anaeleza kwamba mahali pa kuabudu si muhimu. Anasema: “Saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalemu.” Kisha anamwambia: “Saa inakuja, nayo ipo sasa, ambayo waabudu wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli, kwa maana kwa kweli, Baba anawatafuta watu wa namna hiyo wamwabudu.”—Yohana 4:21, 23, 24.

Anachotafuta Baba katika waabudu wa kweli si mahali wanapoabudu bali jinsi wanavyoabudu. Mwanamke huyo anapendezwa na jambo hilo. Anasema: “Ninajua kwamba Masihi anakuja, anayeitwa Kristo. Atakapokuja, atatutangazia mambo yote waziwazi.”—Yohana 4:25.

Kisha Yesu anafunua ukweli muhimu: “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.” (Yohana 4:26) Fikiria jambo hilo! Mwanamke huyu amekuja kuteka maji saa sita mchana. Lakini Yesu anamwonyesha kibali kwa njia ya kustaajabisha. Anamwambia moja kwa moja jambo ambalo inaonekana bado hajawaambia watu wengine waziwazi—kwamba yeye ndiye Masihi.

WASAMARIA WENGI WAAMINI

Wanafunzi wa Yesu wanarudi kutoka Sikari wakiwa na chakula. Wanampata kando ya kisima cha Yakobo ambapo walimwacha, lakini sasa anazungumza na mwanamke Msamaria. Wanafunzi wanapofika, yule mwanamke anaacha mtungi wake wa maji na kuelekea jijini.

Wanafunzi wa Yesu wanarudi kwenye kisima kisha mwanamke Msamaria anaondoka

Anapofika Sikari, yule mwanamke anawasimulia watu mambo ambayo Yesu alimwambia. Kwa usadikisho, anawaambia: “Twendeni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichofanya.” Kisha, labda ili kuwafanya wawe na hamu ya kujua mengi, anawauliza: “Je, inawezekana kwamba yeye ndiye Kristo?” (Yohana 4:29) Swali hilo linahusu jambo muhimu—jambo ambalo limezungumziwa tangu siku za Musa. (Kumbukumbu la Torati 18:18) Linawachochea watu wa jiji hilo waende kujionea Yesu kwa macho yao wenyewe.

Huko Sikari, mwanamke Msamaria anawaambia watu wa jiji hilo mambo ambayo Yesu alimwambia

Wakati huohuo, wanafunzi wanamhimiza Yesu ale chakula ambacho wameleta. Lakini anajibu: “Nina chakula ambacho hamkijui.” Wanafunzi wanashangazwa na maneno hayo, kisha wanaambiana: “Hakuna mtu aliyemletea chakula, sivyo?” Kwa fadhili, Yesu anafafanua kwa maneno ambayo ni muhimu kwa wafuasi wake wote: “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya yule aliyenituma na kuimaliza kazi yake.”—Yohana 4:32-34.

Kazi ambayo Yesu anazungumzia si kazi ya kuvuna nafaka, ambayo itaanza baada ya miezi minne. Badala yake, Yesu anamaanisha mavuno ya kiroho, kama anavyoendelea kusema: “Inueni macho yenu mtazame mashamba, kwamba ni meupe kwa ajili ya kuvunwa. Tayari mvunaji anapokea mshahara na anakusanya matunda kwa ajili ya uzima wa milele, ili mpandaji na mvunaji washangilie pamoja.”—Yohana 4:35, 36.

Huenda tayari Yesu anatambua matokeo ya kukutana na yule mwanamke Msamaria. Wengi kutoka Sikari wanamwamini Yesu kwa sababu ya ushahidi wa mwanamke huyo, kwa maana anawaambia watu hivi: “Aliniambia mambo yote niliyofanya.” (Yohana 4:39) Kwa hiyo, wanapotoka Sikari na kuja kwenye kisima, wanamwomba Yesu akae pamoja nao ili awaambie habari zaidi. Yesu anakubali mwaliko wao naye anakaa Samaria kwa siku mbili.

Wasamaria wanapomsikiliza Yesu, wengi zaidi wanamwamini. Wanamwambia yule mwanamke: “Hatuamini kwa sababu tu ya maneno yako; kwa maana sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba kwa hakika mtu huyu ndiye mwokozi wa ulimwengu.” (Yohana 4:42) Kwa kweli, mwanamke Msamaria anaweka mfano mzuri wa jinsi tunavyoweza kutoa ushahidi kumhusu Kristo, kwa kuwachochea wasikilizaji wetu wawe na hamu ya kujua mengi ili wakubali habari zaidi.

Kumbuka kwamba ni miezi minne kabla ya mavuno—inaonekana ni mavuno ya shayiri, ambayo katika eneo hili hufanywa katika majira ya kuchipua. Kwa hiyo, inawezekana kwamba sasa ni Novemba au Desemba. Hilo linamaanisha kwamba baada ya Pasaka ya 30 W.K., Yesu na wanafunzi wake wamekaa miezi minane hivi huko Yudea, wakifundisha na kubatiza. Sasa wanaelekea kaskazini katika eneo lao la nyumbani huko Galilaya. Ni nini kinachowasubiri huko?

WASAMARIA WALIKUWA NANI?

Eneo linaloitwa Samaria lilipakana na Yudea upande wa kusini na Galilaya upande wa kaskazini. Baada ya kifo cha Mfalme Sulemani, makabila kumi ya kaskazini ya Israeli yalijitenga na makabila ya Yuda na Benjamini.

Watu wa makabila hayo kumi walianza kuabudu ndama. Kwa hiyo, mwaka wa 740 K.W.K., Yehova aliruhusu Waashuru washambulie Samaria. Wavamizi hao waliwachukua mateka watu wengi, kisha wakawaleta huko watu kutoka maeneo mengine ya Milki ya Ashuru. Watu hao walioabudu miungu ya kigeni walifunga ndoa na Waisraeli waliobaki katika nchi hiyo. Baada ya muda, watu wa eneo hilo walianzisha ibada iliyohusisha baadhi ya itikadi na desturi zilizo katika Sheria ya Mungu, kama vile kutahiriwa. Lakini bado mazoea yao ya kidini hayangeweza kuitwa ibada ya kweli.—2 Wafalme 17:9-33; Isaya 9:9.

Katika siku za Yesu, Wasamaria walivikubali vitabu vya Musa lakini hawakuabudu katika hekalu lililokuwa Yerusalemu. Kwa miaka mingi walitumia hekalu lililojengwa kwenye Mlima Gerizimu, uliokuwa karibu na Sikari, na waliendelea kuabudu kwenye mlima huo hata baada ya hekalu hilo kuharibiwa. Uadui kati ya Wasamaria na Wayahudi ulikuwa wazi wakati wa huduma ya Yesu.—Yohana 8:48.

  • Kwa nini mwanamke Msamaria anashangaa Yesu anapozungumza naye?

  • Yesu anamfundisha nini mwanamke huyo kuhusu maji yaliyo hai na mahali pa kumwabudu Mungu?

  • Yesu anajifunua kwa mwanamke Msamaria kwamba yeye ni nani, na anaunga mkono ibada ya aina gani?

  • Mwanamke Msamaria anafikia mkataa gani kumhusu Yesu, naye anafanya nini?

  • Yesu na wanafunzi wake wamekuwa wakifanya nini baada ya Pasaka ya mwaka wa 30 W.K.?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki