Sura 20
Muujiza wa Pili Anapokuwa Kana
YESU anaporudi eneo la nyumbani kwao baada ya shughuli ndefu ya kuhubiri katika Yudea, hafanyi hivyo ili apumzike. Bali, aanza huduma kubwa zaidi katika Galilaya, nchi aliyokulia. Lakini wanafunzi wake, badala ya kukaa pamoja naye, warudi nyumbani kwenye jamaa zao na shughuli zao za zamani.
Yesu aanza kuhubiri ujumbe gani? Huu: “Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.” Nalo itikio lawa nini? Wagalilaya wampokea Yesu. Yeye aheshimiwa na wote. Lakini, haiwi hivyo hasa kwa sababu ya ujumbe wake, bali, ni kwa sababu wengi wao walikuwa kwenye Sikukuu ya Kupitwa katika Yerusalemu miezi kadhaa kabla ya hapo wakaona ishara za kustaajabisha alizozifanya.
Inaonekana kwamba Yesu aanza huduma yake kuu ya Galilaya akiwa Kana. Huenda ukakumbuka kwamba, mapema kidogo, aligeuza maji yakawa divai kwenye karamu ya arusi iliyofanywa huko, akiisha kurudi kutoka Yudea. Pindi hii ya pili, mtoto wa ofisa wa kiserikali wa Mfalme Herode Antipa ni mgonjwa sana. Anaposikia kwamba Yesu ametoka Yudea akaja Kana, ofisa huyo asafiri mwendo wote huo kutoka nyumbani kwake Kapernaumu akatafute Yesu. Kwa kujawa na kihoro, mtu huyo asihi hivi: ‘Tafadhali uje bila kukawia, kabla mtoto wangu hajafa.’
Yesu naye aitikia hivi: ‘Rudi nyumbani. Mwana wako ameponywa!’ Ofisa wa Herode aamini na kuanza ile safari ndefu ya kurudi nyumbani. Anapofika njiani watumishi wake wanamlaki, nao wafanya haraka kumwambia kwamba mambo ni mazuri—mwanae amepona! ‘Alipata nafuu wakati gani?’ auliza.
‘Jana saa 7:00 alasiri,’ wajibu.
Ofisa huyo atambua kwamba saa hiyo hiyo ndipo Yesu aliposema, ‘Mwana wako ameponywa!’ Baada ya hapo, mwanamume huyo na nyumba yake yote wawa wanafunzi wa Kristo.
Hivyo Kana pakawa mahali palipopata upendeleo wa kufanyiwa miujiza miwili na Yesu kama ishara ya kwamba amerudi kutoka Yudea. Bila shaka, hiyo siyo tu miujiza aliyofanya kufikia wakati huo, lakini ina maana kubwa kwa sababu ilikuwa alama ya kuonyesha amerudi Galilaya.
Sasa Yesu aelekea nyumbani Nazareti. Anangojewa na mambo gani huko? Yohana 4:43-54; Marko 1:14, 15; Luka 4:14, 15.
▪ Yesu anaporudi Galilaya, inakuwaje kwa wanafunzi wake, na watu wanampokeaje?
▪ Yesu afanya muujiza gani, nao unakuwa na matokeo gani juu ya wenye kuhusika?
▪ Hivyo Kana pakawa ni mahali panapopendelewa na Yesu kwa njia gani?