Maisha na Huduma ya Yesu
Muujiza wa Kwanza wa Yesu
YESU na wanafunzi wake aliojipatia karibuni wameondoka sasa hivi kwenye Bonde la Yordani. Ni siku moja au mbili tu zilizopita tangu Andrea, Petro, Yohana na labda Yakobo, Filipo na Nathanaeli wawe wanafunzi wa kwanza wa Yesu.
Sasa wako njiani kurudi makwao kwenye wilaya ya Galilaya, ambako wote walitoka. Mahali wanakoenda ni Kana, mji wa nyumbani kwa Nathanaeli, ulio katika vilima ambavyo haviko mbali na Nazareti ambako Yesu mwenyewe alikulia. Wamealikwa kwenye karamu ya arusi katika Kana.
Mama ya Yesu, pia, amekuja arusini. Akiwa ni rafiki wa jamaa ya wenye kuoana, Mariamu anaonekana ni kama amekuwa akihudumia mahitaji ya wageni wengi. Kwa hiyo anaona haraka kwamba kuna upungufu wa kitu fulani, naye anamweleza Yesu jambo hilo: “Hawana divai.”
Mariamu anapodokeza kwa njia hiyo kwamba Yesu amalize kwa njia fulani ukosefu wa divai, Yesu hapo kwanza anakuwa hana nia ya kuchukua hatua. “Tuna nini mimi nawe?” anauliza. Akiwa ni Mfalme-mwekwa wa Mungu, yeye hapaswi kuelekezwa na jamaa au rafiki zake katika utendaji wake. Kwa hiyo Mariamu anatumia hekima kuliacha jambo hilo mikononi mwa mwanaye, kisha anawaambia wenye kuhudumu maneno haya machache tu: “Lo lote atakalowaambia, fanyeni.”
Basi, kuna mitungi sita ya maji iliyotengenezwa kwa mawe, na kila mmoja unaweza kuchukua zaidi ya galani kumi. Yesu anawaagiza hivi wale wanaohudumu: “Jalizeni [mitungi] maji.” Kisha watumishi wanaijaza pomoni. Halafu Yesu anasema: “Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza.”
Mkurugenzi huyo anashangazwa na uzuri wa divai, asijue imetokezwa kimuujiza. Akiita bwana-arusi, anasema: “Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.”
Huo ndio muujiza wa kwanza wa Yesu, nao wanafunzi wake wapya wanatiwa imani nguvu wanapouona. Baadaye wao, pamoja na mamaye na nduguze, wanasafiri kwenda mji wa Kapernaumu karibu na Bahari ya Galilaya. Yohana 2:1-12.
◆ Arusi katika Kana inatukia wakati gani?
◆ Ni kwa sababu gani Yesu anakataa dokezo la mamaye?
◆ Ni muujiza gani anaoufanya Yesu, na matokeo yanakuwa nini juu ya wengine?