Sura 15
Muujiza Wa Kwanza wa Yesu
IMEKUWA tu siku moja au mbili hivi tangu Andrea, Petro, Yohana, Filipo, Nathanaeli, na labda Yakobo wawe wanafunzi wa kwanza wa Yesu. Sasa hao wako njiani kwenda nyumbani katika wilaya ya Galilaya, ambako wote walitoka. Waenda Kana, mji wa nyumbani kwake Nathanaeli, ambao uko vilimani na si mbali na Nazareti, ambako Yesu mwenyewe alikulia. Wamealikwa kwenye karamu ya arusi katika Kana.
Mama ya Yesu pia amekuja arusini. Akiwa ni rafiki ya familia ya wenye kuoana, Mariamu aonekana ni kama amekuwa akihudumia mahitaji ya wale wageni wengi. Kwa hiyo yeye aona kwa haraka kwamba kuna upungufu wa kitu fulani, naye aripoti kwa Yesu jambo hilo: “Hawana divai.”
Mariamu adokezapo kwa njia hiyo kwamba Yesu afanye jambo fulani amalize ukosefu wa divai, Yesu awa hapo kwanza hana nia ya kuchukua hatua. “Tuna nini mimi nawe?” auliza. Akiwa ni Mfalme-Mchaguliwa wa Mungu, yeye hapaswi kuelekezwa na familia au marafiki wake katika utendaji wake. Kwa hiyo Mariamu atumia hekima kuliacha jambo hilo mikononi mwa mwanaye, akiwaambia tu wale wenye kuhudumu: “Lo lote atakalowaambia, fanyeni.”
Basi, kuna mitungi ya mawe mikubwa sita, na kila mmoja waweza kuchukua zaidi ya galani kumi. Yesu awaagiza hivi wale wahudumiao: “Jalizeni [mitungi] maji.” Kisha watumishi waijaliza pomoni. Halafu Yesu asema: “Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza [mwelekezi wa karamu, NW].”
Mwelekezi huyo ashangazwa na uzuri wa divai, asijue imetokezwa kimuujiza. Akiita bwana-arusi, asema: “Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.”
Huo ndio muujiza wa kwanza wa Yesu, nao kwa kuuona, imani ya wanafunzi wake wapya yatiwa nguvu. Baadaye, pamoja na mamaye na nduguze wenye mzazi mmoja naye, wasafiri kwenda jiji la Kapernaumu karibu na Bahari ya Galilaya. Yohana 2:1-12.
▪ Ni wakati gani katika huduma ya Yesu kwawa na ile arusi katika Kana?
▪ Ni kwa nini Yesu akataa dokezo la mamaye?
▪ Yesu afanya muujiza gani, na matokeo yawa nini juu ya wengine?