Sura 33
Kutimiza Unabii wa Isaya
BAADA ya Yesu kupata habari kwamba Mafarisayo na wafuasi wa chama cha Herode wanapanga kumwua, yeye na wanafunzi wake waondoka kwenda kwenye Bahari ya Galilaya. Huko umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Palestina, na hata kutoka nje ya mipaka yake, wammiminikia. Yeye aponya wengi na matokeo ni kwamba wote wenye magonjwa ya kuhuzunisha sana wasogelea wamguse.
Kwa sababu umati wa watu ni mkubwa sana, Yesu awaambia wanafunzi wake wamwekee mashua pale aendelea kuitumia. Kwa kuiendesha atoke ufuoni, anaweza kuuzuia umati wa watu hao wasimsonge. Anaweza kuwafundisha akiwa mashuani au kusafiri kwenye eneo jingine kandokando ya ufuo wa bahari ili kuwasaidia watu kule.
Mwanafunzi Mathayo aandika kwamba utendaji wa Yesu unatimiza “neno lililonenwa na nabii Isaya.” Halafu Mathayo anukuu maneno ya unabii ambao Yesu anatimiza:
“Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.”
Bila shaka, Yesu ndiye mtumishi mpendwa ambaye Mungu anakubali. Na Yesu anafahamisha wazi ni nini haki ya kweli, ambayo mapokeo ya dini bandia yanaifunika isionekane. Mafarisayo hawataki hata kwenda kusaidia mgonjwa siku ya Sabato kwa sababu wanatumia sheria ya Mungu kwa njia isiyo haki! Kwa kufahamisha wazi haki ya Mungu ni nini, Yesu anawaondolea watu mzigo wa mapokeo yasiyo ya haki, na kwa sababu hiyo, viongozi wa kidini wanajaribu kumwua.
Inamaanisha nini kwamba ‘hatateta, wala hatapaaza sauti yake ili asikiwe katika njia pana’? Wakati anapoponya watu, Yesu ‘awakataza sana wasimdhihirishe.’ Yeye hataki kujitangaza kwa makelele mengi katika barabara wala hataki habari zilizopotoshwa zipitishwe kwa msisimuko kutoka kinywa kimoja mpaka kinywa kingine.
Pia, Yesu awapelekea ujumbe wenye faraja wale ambao kwa njia ya mfano ni kama mwanzi uliopondwa, walioinama na kugongwa katika sehemu ya chini ya nyayo. Wao ni kama utambi utokao moshi, ambao mwali wao wa mwisho u karibu kuzimika. Yesu hauvunji mwanzi uliopondeka wala hauzimi utambi utokao moshi. Bali kwa wororo na upendo, awainua wapole kwa ustadi. Kwa kweli, Yesu ndiye ambaye mataifa waweza kutumainia! Mathayo 12:15-21; Marko 3:7-12; Isaya 42:1-4.
▪ Yesu anafahamishaje wazi maana ya haki, bila kuteta wala kupaaza sauti katika njia pana?
▪ Ni nani walio kama mwanzi uliopondeka na utambi, na Yesu anawatendeaje?