Sura 34
Kuchagua Mitume Wake
MWAKA na nusu umepita tangu Yohana Mbatizaji alipojulisha kwamba Yesu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu na Yesu akaanza huduma yake ya peupe. Wakati huo Andrea, Simoni Petro, Yohana na labda Yakobo (Ndugu yake Yohana), pia Filipo na Nathanaeli (aitwaye pia Bartholomayo), walikuwa wamekuwa wafuasi wake wa kwanza. Baada ya muda, wengine wengi walijiunga nao kumfuata Kristo.
Sasa Yesu yuko tayari kuchagua mitume wake. Hao watakuwa ndio washirika wenye uhusiano wa kindani pamoja naye watakaopewa mazoezi ya pekee. Lakini kabla ya kuwachagua, Yesu anaenda mlimani na kukaa huko usiku kucha akisali, inaelekea kuwa anaomba hekima na baraka ya Mungu. Kunapokucha, awaita wafuasi wake na kati yao achagua 12. Lakini, kwa kuwa Yesu aendelea kuwafunza, bado wanaitwa wanafunzi pia.
Sita kati ya wale anaowachagua Yesu, watajwao juu, ndio wale ambao walipata kuwa wanafunzi wake wa kwanza. Mathayo, ambaye Yesu alimwita kutoka ofisi yake ya kutozea kodi, pia achaguliwa. Wale wengine watano wachaguliwao ni Yuda (aitwaye Thadayo), Yuda Iskariote, Simoni yule Mkananayo, Tomaso, na Yakobo mwana wa Alfayo. Yakobo huyo aitwa pia Yakobo yule Mdogo, labda ni kwa sababu ama alikuwa mdogo kidogo kwa kimo au mchanga zaidi kidogo kwa umri kuliko yule mtume mwingine Yakobo.
Kufikia sasa hawa 12 wamekuwa pamoja na Yesu kwa muda fulani, naye awajua vizuri. Kwa kweli, hesabu fulani kati yao ni watu wa ukoo wake mwenyewe. Inaonekana kwamba Yakobo na ndugu yake Yohana ni binamu za kwanza za Yesu. Na inawezekana kwamba Alfayo alikuwa ndugu yake Yusufu, baba mlezi wa Yesu Kristo. Kwa hiyo mtume Yakobo aliye mwana wa Alfayo, angekuwa pia ni binamu ya Yesu.
Bila shaka, Yesu hakuwa na tatizo la kukumbuka majina ya mitume wake. Lakini je! wewe waweza kuwakumbuka? Basi, kumbuka tu kwamba kuna wawili waitwao Simoni, wawili waitwao Yakobo, na wawili waitwao Yuda, na kwamba Simoni ana ndugu aitwaye Andrea, na kwamba Yakobo ana ndugu aitwaye Yohana. Huo ndio ufunguo wa kukumbuka mitume wanane. Wale wengine wanne ni kutia na mkusanya kodi (Mathayo), mmoja aliyetia shaka baadaye (Tomaso), mmoja aliyeitwa akiwa chini ya mti (Nathanaeli), na Filipo rafiki yake.
Kumi na mmoja kati ya mitume watoka Galilaya, eneo la nyumbani kwake Yesu. Nathanaeli ni wa kutoka Kana. Filipo, Petro, na Andrea hapo kwanza walitoka Bethsaida, Petro na Andrea wahamia Kapernaumu baadaye, ambako inaonekana Mathayo aliishi. Yakobo na Yohana walikuwa katika biashara ya uvuvi na inaelekea wao pia waliishi katika au karibu na Kapernaumu. Inaelekea kuwa Yuda Iskariote, aliyemsaliti Yesu baadaye, ndiye mtume pekee aliyetoka Yudea. Marko 3:13-19; Luka 6:12-16.
▪ Ni mitume gani huenda wakawa walikuwa watu wa ukoo wa Yesu?
▪ Mitume wa Yesu ni nani, nawe unaweza kukumbukaje majina yao?
▪ Mitume walitoka maeneo yapi?