Maisha na Huduma ya Yesu
Kuchagua Mitume Wake
MWAKA na nusu umepita tangu Yohana Mbatizaji alipojulisha kwamba Yesu ndiye “Mwana-kondoo wa Mungu” na Yesu akaanza huduma yake ya waziwazi. Wakati huo Andrea, Simoni, Petro, Yohana na labda Yakobo (ndugu yake Yohana), pia Filipo na Nathanaeli (aliyeitwa pia Bartholomayo), walikuwa wamekuwa wafuasi wake wa kwanza. Baada ya muda, wengine wengi walijiunga nao kumfuata Kristo.
Sasa Yesu yuko tayari kuchagua mitume wake. Hao watakuwa ndio washirika wenye uhusiano wa kindani pamoja naye watakaopewa mazoezi ya pekee. Lakini kabla ya kuwachagua, Yesu anaenda mlimani na kukaa kule usiku kucha akisali, inaelekea kuwa anaomba hekima na baraka ya Mungu, iwe juu ya kila mmoja wao. Kunapokucha, anaita wafuasi wake na kati yao anachagua 12. Lakini, kwa kuwa wanaendelea kuwa wafunzwa wa Yesu, bado wanaitwa wafuasi.
Sita kati ya wale anaowachagua Yesu, waliotajwa juu, ni wale ambayo wakawa wafuasi wake wa kwanza. Mathayo, ambaye Yesu alimwita kutoka afisi yake kutozea kodi, anachaguliwa pia. Wale wengine watano wanaochaguliwa ni Yuda (aliyeitwa pia Tadayo), Yuda Iskariote, Simoni yule Mkananayo, Tomaso, na Yakobo mwana wa Alfayo. Yakobo huyo anaitwa pia Yakobo yule Mdogo, labda sababu ikiwa ni kumtofautisha na mtume yule mwingine Yakobo.
Kufikia sasa hawa 12 wamekuwa pamoja na Yesu kwa muda fulani, naye anawajua vizuri. Kwa kweli, hesabu fulani kati yao ni watu wa ukoo wake mwenyewe. Inaonekana kwamba Yakobo na ndugu yake Yohana ni binamu za kwanza za Yesu. Na inawezekana kwamba Alfayo alikuwa ndugu yake Yusufu, baba mlezi wa Yesu Kristo. Kwa hiyo mtume Yakobo aliye mwana wa Alfayo, angekuwa pia ni binamu ya Yesu.
Bila shaka, Yesu hakuwa na tatizo la kukumbuka majina ya mitume wake. Lakini je! wewe unaweza kuwakumbuka? Basi, kumbuka tu kwamba kuna wawili wanaoitwa Simoni, wawili wanaoitwa Yakobo, na wawili wanaoitwa Yuda, na kwamba Simoni ana ndugu anayeitwa Andrea, na kwamba Yakobo ana ndugu anayeitwa Yohana. Huo ndio ufunguo wa kukumbuka mitume wanane. Wale wengine wanne ni kutia na mkusanya-kodi (Mathayo), mmoja aliyetia shaka baadaye (Tomaso), mmoja aliyeitwa akiwa chini ya mti (Nathanaeli), na Filipo rafiki yake.
Kumi na mmoja kati ya mitume ni watu wa kutoka Galilaya, eneo la nyumbani kwao Yesu. Nathanaeli ni wa kutoka Kana. Filipo, Petro, na Andrea asili yao ni Bethsaida. Lakini, Petro na Andrea wanahamia Kapernaumu baadaye, ambako inaonekana Mathayo alikuwa ameishi. Yakobo na Yohana walikuwa katika biashara ya samaki na inaelekea wao pia waliishi katika au karibu na Kapernaumu. Inaelekea kuwa Yuda Iskariote, aliyemshaliti Yesu baadaye, ndiye mtume mmoja tu aliyetoka Yudea. Marko 3:13-19, Luka 6:12-16.
◆ Ni mitume gani huenda wakawa walikuwa watu wa ukoo wa Yesu?
◆ Mitume wa Yesu ni nani, nawe unaweza kukumbukaje majina yao?
◆ Wengine wa mitume walikuwa watu wa kutoka wapi?
[Picha katika ukurasa wa 9]
Kuanzia juu katikati na kuzunguka kuelekea upande wa kuume mitume wameonyeshwa katika utaratibu ulioorodheshwa kwenye Luka 6:12-16