Sura 45
Mmoja Asiyeelekea Kuwa Mwanafunzi
NI JAMBO lenye kuogofya kama nini analoona Yesu anapokanyaga pwani! Wanaume wawili wakali isivyo kawaida wanatoka makaburini yaliyo karibu na kukimbia kumwelekea. Wamepagawa na roho waovu. Kwa kuwa inaelekea mmoja ni mjeuri zaidi na ametaabika kwa muda mrefu zaidi chini ya udhibiti wa roho waovu kuliko yule mwingine, anakuwa wa kukaziwa fikira zaidi.
Kwa muda mrefu mwanamume huyo wa kusikitikiwa amekuwa akiishi akiwa uchi huko maziarani. Sikuzote, mchana na usiku, yeye hupaaza sauti na kujikata-kata kwa mawe. Yeye ni mjeuri sana hivi kwamba hapana mtu aliye na ujasiri wa kupitia njia hiyo. Majaribio yamefanywa ya kumfunga, lakini yeye hukata minyororo na kuvunja vyuma na kuviondoa kwenye miguu yake. Hapana mtu aliye na nguvu za kumtiisha.
Mwanamume huyo anapomkaribia Yesu na kuanguka miguuni pake, wale roho waovu wanaomdhibiti wanamfanya apige makele hivi: “Mimi nina nini la kufanya nawe, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Kupita Wote? Mimi nakuapisha kwa Mungu usinitese.”
“Toka kwake mtu huyo, ewe roho usiye safi,” Yesu anaendelea kusema. Lakini ndipo Yesu anauliza: “Jina lako nani?”
“Jina langu ni Lejioni, kwa kuwa tu wengi,” ndilo jibu. Roho waovu wanafurahia sana kuona kuteseka kwa wale wanaoweza kupagaa, kwa wazi wakifurahia kuwavamia wakiwa kundi lenye roho ya woga. Lakini wakikabiliwa na Yesu, wanasihi wasipelekewe katika ile abiso. Tunaona tena kwamba Yesu ana uwezo mkubwa; aliweza kushinda hata roho waovu wakali mno. Hilo pia linafunua kwamba roho waovu wanajua kwamba kutupwa kwao katika abiso pamoja na kule kwa kiongozi wao, Shetani Ibilisi, ndiyo hukumu ya Yehova kwao hatimaye.
Kundi la nguruwe karibu 2,000 linajilisha karibu mlimani. Kwa hiyo wale roho waovu wanasema: “Tupeleke ndani ya nguruwe, tupate kuwaingia.” Kwa wazi roho waovu wanapata namna fulani ya furaha yenye ukatili mwingi isiyo ya kiasili, katika kuingia miili ya viumbe wa kimnofu. Yesu anapowaruhusu kuwaingia nguruwe hao, nguruwe wote 2,000 wanateremka ghafula gengeni na kufa maji katika bahari.
Wakati wale wanaochunga nguruwe hao wanapoona hilo, wanaenda mbio kuripoti habari hizo katika jiji na katika sehemu za mashambani. Kwa hiyo, watu wanakuja kuona ni jambo gani limetukia. Wanapofika, wanamwona yule mwanamume ambaye roho waovu walikuwa wamemtoka. Kumbe, amevaa nguo na ana akili zake timamu, ameketi miguuni pa Yesu!
Mashahidi waliojionea kwa macho yao wenyewe wanasimulia jinsi mwanamume huyo alivyoponywa. Pia wanawaambia watu juu ya kituko cha kufa maji kwa wale nguruwe. Wakati watu hao wanaposikia hilo, wanashikwa na hofu nyingi sana, nao wanamsihi Yesu kwa bidii aondoke eneo lao. Kwa hiyo yeye anakubali na kuingia mashuani. Yule ambaye hapo kwanza alikuwa amepagawa na roho waovu anamwomba Yesu amruhusu aende pamoja naye. Lakini Yesu anamwambia: “Nenda nyumbani kwa watu wa ukoo wako, na kuripoti kwao mambo yote ambayo Yehova amekufanyia na rehema aliyokuonyesha.”
Kwa kawaida Yesu huwaagiza wale anaoponya wasimwambie mtu yeyote, kwa kuwa yeye hataki watu wakate maneno kwa msingi wa ripoti zenye kusisimua. Lakini jambo hili lililo tofauti linafaa kwa sababu mtu huyo ambaye hapo kwanza alipagawa na roho waovu atakuwa akitoa ushahidi kwa watu ambao labada sasa Yesu hatakuwa na fursa ya kuwafikia. Zaidi ya hilo, kuwapo kwa mwanamume huyo kutaandaa ushahidi juu ya uwezo wa Yesu wa kufanya mema, na kupinga ripoti yoyote isiyopendeza ambayo huenda ikaenezwa juu ya hasara ya wale nguruwe.
Kupatana na maagizo ya Yesu, mtu huyo ambaye hapo kwanza alipagawa na roho waovu anaenda zake. Anaanza kutangaza kotekote katika Dekapoli mambo yote aliyomfanyia Yesu nao watu wanastaajabu sana. Mathayo 8:28-34; Marko 5:1-20; Luka 8:26-39; Ufunuo 20:1-3, NW.
▪ Kwa nini huenda, fikira zaidi zinakazwiwa mtu mmoja mwenye kupagawa na roho waovu hali walikuwapo wawili?
▪ Ni nini linaloonyesha kwamba roho waovu wanajua juu ya kutupwa ndani ya abiso katika wakati ujao?
▪ Kwa wazi, kwa nini roho waovu wanapenda kuwapagaa binadamu na wanyama?
▪ Kwa nini Yesu anafanya tofauti na mtu huyo ambaye hapo kwanza alikuwa amepagawa na roho waovu, akimwagiza aende na kuwasimulia wengine yale ambayo Yeye alimfanyia?