Sura 47
Machozi Yakabadilika Kuwa Pindi Yenye Furaha Kubwa
YAIRO anapomwona yule mwanamke mwenye mtiririko wa damu amepona, uhakika wake katika nguvu za kimuujiza za Yesu bila shaka unaongezeka. Mapema siku hiyo, Yesu alikuwa ameulizwa na Yairo aje na kumsaidia binti yake mpendwa mwenye umri wa miaka 12, aliyekuwa analala akikaribia kufa. Lakini sasa, jambo ambalo Yairo anahofia zaidi ya yote latukia. Wakati Yesu angali ananena na yule mwanamke, wanaume fulani kutoka katika nyumba yake wanawasili na kumwambia Yairo hivi polepole: “Binti yako amekwisha kufa! Mbona umsumbue Mwalimu tena?”
Lo! habari hizo ni zenye kukumba kama nini! Ebu fikiria tu: Mwanamume huyu, anayeheshimiwa sana katika mtaa huo, sasa anakuwa hoi kabisa anapopata kujua juu ya kifo cha binti yake. Hata hivyo, Yesu anapata kuyasikia mazungumzo hayo. Hivyo, akimgeukia Yairo, anasema hivi kwa kumtia moyo: “Usiwe na woga, tumia imani tu.”
Yesu anaandamana na mtu huyo mwenye huzuni kurudi nyumbani kwake. Wanapowasili, wanapata makelele ya watu wakilia na kuomboleza. Umati umekusanyika, nao wanajipiga-piga kwa huzuni. Yesu anapoingia ndani, anauliza: “Kwa nini nyinyi mnasababisha mvurugo wenye makelele na kutoa machozi? Huyo mtoto mchanga hajafa, bali analala.”
Kusikia hivyo, watu wale wanaanza kumcheka Yesu kwa dharau kwa sababu wao wanajua kwamba msichana huyo amekufa kweli kweli. Hata hivyo, Yesu anasema kwamba analala tu. Kwa kutumia nguvu alizopewa na Mungu, yeye ataonyesha kwamba watu wanaweza kurudishwa kutoka kwenye kifo kwa urahisi kama vile wanavyoweza kuamshwa kutoka katika usingizi mzito.
Yesu sasa anaagiza watu wote watolewe nje isipokuwa Petro, Yakobo, Yohana, na mama na baba ya yule msichana aliyekufa. Ndipo anapowachukua hao watano pamoja naye kwenye mahali ambapo msichana huyo mchanga analala. Akimshika mkono, Yesu anasema: “Talʹi·tha cuʹmi,” ambayo, yakitafsiriwa, humaanisha: “Msichana, Mimi nakuambia, Amka!” Na mara hiyo msichana yule anaamka na kuanza kutembea! Kuona hivyo wazazi wake karibu warukwe akili kwa kuhisi furaha kubwa.
Baada ya kuagiza kwamba mtoto huyo apewe chakula, Yesu anaamuru Yairo na mkewe wasimwambie yeyote jambo ambalo limetukia. Lakini ijapokuwa jambo ambalo Yesu amesema, habari zalo zinaenea katika jimbo lote. Huu ndio ufufuo wa pili anaofanya Yesu. Mathayo 9:18-26; Marko 5:35-43; Luka 8:41-56, NW.
▪ Yairo anapokea habari gani, naye Yesu anamtiaje moyo?
▪ Hali inakuwaje wanapowasili nyumbani mwa Yairo?
▪ Kwa nini Yesu anasema kwamba mtoto ambaye amekufa amelala tu?
▪ Ni nani hao watu watano walio pamoja na Yesu ambao wanaona ushahidi wa ufufuo huo?