Sura 51
Uuaji Kimakusudi Wakati wa Karamu ya Siku ya Kuzaliwa
BAADA ya kuwapa mitume wake maagizo, Yesu anawatuma kwenye eneo wakiwa wawili wawili. Labda Petro na Andrea ambao ni ndugu wanaenda pamoja, kama wanavyofanya Yakobo na Yohana, Filipo na Bartholomayo, Tomaso na Mathayo, Yakobo na Thadayo, na Simoni na Yuda Iskariote. Jozi hizi sita za waevanjeli zatangaza habari njema za Ufalme wa Mungu na kufanya maponyo ya kimuujiza kokote waendako.
Wakati ule ule, Yohana Mbatizaji angali gerezani. Amekuwa humo yapata miaka miwili sasa. Huenda ukakumbuka kwamba Yohana alikuwa ametangaza peupe kwamba ilikuwa kosa kwa Herode Antipa kumtwaa Herodia, mke wa Filipo ndugu yake, awe wake mwenyewe. Kwa kuwa Herode Antipa alidai kwamba alifuata Sheria ya Musa, kwa kufaa Yohana alikuwa amefunua muungano huu wa uzinzi. Kwa hiyo Herode akaagiza Yohana atupwe gerezani, labda kwa kuhimizwa na Herodia.
Herode Antipa anatambua kwamba Yohana ni mwanamume mwadilifu na hata anamsikiliza kwa furaha. Kwa hiyo, anashindwa asijue jambo la kumfanyia. Kwa upande mwingine, Herodia, anamchukia Yohana naye anaendelea kutafuta njia ya kufanya auawe. Mwishowe, fursa ambayo amekuwa akingojea inafika.
Muda mfupi kabla ya Sikukuu ya Kupitwa ya 32 W.K., Herode apanga mwadhimisho mkubwa wa siku ya kuzaliwa kwake. Maofisa wa Herode wote wenye vyeo vya juu na maofisa wa jeshi wamekusanyika kwenye karamu, pamoja na raia mashuhuri wa Galilaya. Jioni hiyo inapoendelea, Salome, yule binti kijana wa Herodia aliyemzaa na Filipo aliyekuwa hapo kwanza mume wake, anapelekwa akawachezee wageni dansi. Wanaume watazamaji wanashangazwa na uchezaji-dansi wake.
Herode anapendezwa sana na Salome. “Niombe chochote kile unataka, nami nitakupa hicho,” atangaza. Yeye hata anaapa: “Chochote kile uniombacho, mimi nitakupa hicho, kufikia nusu ya ufalme wangu.”
Kabla ya kujibu, Salome atoka nje akatafute shauri kwa mama yake. “Inanipasa kuomba nini?” anauliza.
Hatimaye ile fursa inapatikana! “Kichwa cha Yohana mbatizaji,” ajibu Herodia bila kusita.
Upesi Salome anarudi kwa Herode na kufanya ombi hili: “Mimi nataka unipe mara hii kichwa cha Yohana Mbatizaji kikiwa juu ya kombe.”
Herode anahuzunika sana. Hata hivyo kwa kuwa wageni wake wamesikia kiapo chake, anafadhaika asipokitimiza, hata ingawa inamaanisha kumuua mwanamume asiye na hatia. Mara muuaji atumwa gerezani akiwa na maagizo ya mfalme yenye kuogofya. Baada ya muda mfupi anarudi akiwa na kichwa cha Yohana katika kombe, naye ampa mamaye. Wanafunzi wa Yohana wanaposikia jambo ambalo limetukia, wanaenda na kuuchukua mwili wake na kuuzika, kisha wanaripoti jambo hilo kwa Yesu.
Baadaye, Herode anaposikia kwamba Yesu anaponya watu na kufukuza roho waovu, yeye anaogopa, akihofu kwamba Yesu ni Yohana ambaye amefufuliwa kutoka kwa wafu. Baadaye, anatamani sana kumwona Yesu, si ili asikie mahubiri yake, bali ahakikishe kama hofu zake zina msingi mzuri au la. Mathayo 10:1-5; 11:1; 14:1-12; Marko 6:14-29; Luka 9:7-9, NW.
▪ Kwa nini Yohana yumo gerezani, na kwa nini Herode hataki kumuua?
▪ Mwishowe Herodia amewezaje kufanya Yohana auawe?
▪ Baada ya kifo cha Yohana, kwa nini Herode anataka kumwona Yesu?