Maisha na Huduma ya Yesu
Uuaji Wakati wa Karamu Moja ya Siku ya Kuzaliwa
BAADA ya kuwapa mitume wake maagizo, Yesu anawatuma kwenye eneo wakiwa wawili wawili. Labda Petro na Andrea ambao ni ndugu walienda pamoja, kama walivyofanya Yakobo na Yohana, Filipo na Bartholomayo, Tomaso na Mathayo, Yakobo na Thadayo, na Simoni na Yuda Iskariote. Vikundi hivi sita vya waeneza-evanjeli wakiwa wawili wawili vinatangaza habari njema za Ufalme na kuponya kwa miujiza ko kote viendako.
Wakati uu huu, Yohana Mbatizaji angali gerezani. Amekuwa humo yapata miaka miwili sasa. Huenda ukakumbuka kwamba Yohana alikuwa ametangaza peupe kwamba ni kosa kwa Herode Antipa kumchukua Herodia, mke wa Filipo ndugu yake, awe mke wake. Kwa kuwa Herode Antipa alidai kwamba alifuata sheria ya Musa, kwa kufaa Yohana alikuwa amefunua muungano huu wa uzinzi. Hii ndiyo sababu Yohana alitupwa gerezani, labda kwa kusihi kwa Herodia.
Herode Antipa anatambua kwamba Yohana ni mwanamume mwadilifu na hata anamsikiliza kwa furaha. Kwa hiyo anashindwa asijue jambo la kumfanyia. Kwa upande ule mwingine, Herodia, anamchukia Yohana naye anaendelea kutafuta njia ya kufanya auawe. Mwishowe, nafasi ambayo amekuwa akingojea inafika.
Muda mfupi kabla ya sikukuu ya Kupitwa, katika 32 W.K., Herode apanga mwadhimisho mkubwa wa siku ya kuzaliwa kwake. Maafisa wa Herode wote wenye vyeo vya juu na maafisa wa jeshi wamekusanyika kwenye karamu, pamoja na raia mashuhuri wa Galilaya. Jioni hiyo inapoendelea, Salome, yule binti kijana wa Herodia aliyemzaa na mume wake wa kwanza Filipo, anapelekwa akawachezea wageni dansi. Wanaume wasikilizaji wanashangazwa na jinsi alivyocheza, kucheza ambako bila shaka kulikuwa kwenye kuvutia sana.
Herode apendezwa sana na Salome. “Niombe lo lote utakalo, nitakupa,” anatangaza. Hata anaapa: “Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.”
Kabla ya kujibu, Salome aenda kutafuta shauri kutoka kwa mamaye. “Niombe nini?” auliza.
Hatimaye nafasi inapatikana! “Kichwa cha Yohana Mbatizaji,” ajibu Herodia bila kusita-sita.
Mara moja Salome amrudia Herode na kuomba: “Unipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
Herode anahuzunika sana. Hata hivyo kwa kuwa wageni wake wamesikia kiapo chake, anafadhaika asipokitimiza, hata ingawa inamaanisha kumuua mwanamume asiye na hatia. Mara muuaji atumwa gerezani akiwa na maagizo ya mfalme yenye kuogofya. Baada ya muda mfupi anarudi akiwa na kichwa cha Yohana katika kombe, naye ampa Salome. Yeye naye, ampelekea mamaye. Wanafunzi wa Yohana wanaposikia jambo ambalo limetukia, wanakwenda na kuuchukua mwili wake na kuuzika, kisha wanampasha Yesu habari kuhusu jambo hilo.
Baadaye, Herode anaposikia juu ya kuponya watu kwa Yesu na kuondoa mashetani, yeye anaogopa, akihofu kwamba Yesu ni Yohana ambaye amefufuliwa kutoka kwa wafu. Baadaye, anatamani sana kumwona Yesu, si kusikia mahubiri yake, bali ahakikishe kama hofu zake zina msingi mzuri au la. Mathayo 10:1-5; 11:1; 14:1-12; Marko 6:14-29; Luka 9:7-9.
◆ Kwa nini Yohana yuko gerezani, na kwa sababu gani Herode hataki kumuua?
◆ Mwishowe Herodia amewezaje kufanya Yohana auawe?
◆ Baada ya kifo cha Yohana, kwa nini Herode anataka kumwona Yesu?
[Picha ya Ukurasa nzima katika ukurasa wa 9]