Sura 97
Wafanya Kazi Katika Shamba la Mizabibu
WENGI walio wa kwanza,” ndipo tu Yesu alikuwa amesema, “watakuwa wa mwisho.” Sasa yeye anatolea jambo hili kielezi kwa kusimulia hadithi. “Ufalme wa mbinguni” anaanza, “umefanana na mtu mwenye nyumba, aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.”
Yesu aendelea hivi: “Naye [mwenye nyumba] alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.”
Mwenye nyumba, au mwenye shamba la mizabibu, ni Yehova Mungu, nalo shamba la mizabibu ni taifa la Israeli. Wafanya kazi katika shamba la mizabibu ni watu walioingizwa katika agano la Sheria; wao hasa ni wale Wayahudi wenye kuishi siku za mitume. Patano la mshahara limefanywa na wale tu wafanya kazi wa mchana mzima. Mshahara ni dinari moja kwa kazi ya siku. Kwa kuwa “saa tatu” ni saa 3:00 asubuhi, hao walioitwa mnamo saa 3, saa 6, saa 9, na saa 11 wanafanya kazi, kama inavyofuatana, kwa muda wa saa 9, 6, 3, na 1 tu.
Wafanya kazi wa muda wa saa 12, au mchana mzima, wawakilisha viongozi Wayahudi ambao wamekuwa wakiendelea kujishughulisha sana katika utumishi wa kidini. Wao si kama wanafunzi wa Yesu, ambao kwa sehemu kubwa ya maisha zao wamekuwa wameajiriwa kuvua samaki au katika shughuli nyinginezo za kimwili. Ilipofika vuli ya 29 W.K., ndipo “mwenye nyumba” alipomtuma Yesu Kristo akawakusanye hawa kuwa wanafunzi wake. Hivyo wakawa “wa mwisho,” au wafanya kazi wa saa 11 katika shamba la mizabibu.
Mwishowe, siku ya kazi ya ufananisho yafikia mwisho kwa kifo cha Yesu, na wakati waja wa kuwalipa wafanya kazi. Kanuni isiyo ya kawaida ya kuwalipa kwanza walio wa mwisho yafuatwa, kama ielezwavyo: “Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung’unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?” Kwa kumalizia, Yesu alirudia jambo lililotajwa mapema akisema hivi: “Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Kupokea dinari zile kwatukia si wakati wa kifo cha Yesu, bali kwenye Pentekoste 33 W.K., wakati ambapo Kristo yule “msimamizi,” alipomimina roho takatifu juu ya wanafunzi wake. Wanafunzi hawa wa Yesu ni kama watu wale “wa mwisho,” au wafanya kazi wa saa 11. Dinari ile haiwakilishi zawadi ya roho takatifu yenyewe. Dinari ni kitu cha kutumiwa na wanafunzi hao hapa duniani. Ni kitu kinachomaanisha riziki yao, uhai wao wa milele. Ni lile pendeleo la kuwa Mwisraeli wa kiroho, aliyepakwa mafuta kuhubiri juu ya Ufalme wa Mungu.
Muda si muda wale walioajiriwa kwanza wanaona kwamba wanafunzi wa Yesu wamelipwa, nao wawaona wakiitumia dinari ya ufananisho. Lakini wao wanataka mengi zaidi ya roho takatifu na mapendeleo ya Ufalme yaliyoshirikishwa nayo. Kunung’unika kwao na vitendo vyao vya kukinza vinakuwa vya namna ya kunyanyasa wanafunzi wa Kristo, walio wafanya kazi “wa mwisho” katika shamba la mizabibu.
Je! utimizo huo wa karne ya kwanza ndio utimizo wa pekee wa kielezi cha Yesu? Hapana, kwa sababu ya vyeo na madaraka yao, makasisi wa Jumuiya ya Wakristo katika karne ya 20 wamekuwa “wa kwanza” kuajiriwa kazi katika shamba la mizabibu la Mungu lililo la ufananisho. Wao waliwaona wahubiri waliojiweka wakfu wenye kushirikiana na Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi Biblia na Trakti kuwa “wa mwisho” kupata mgawo wowote halali katika utumishi wa Mungu. Lakini, kwa uhakika, watu hawa hawa, ambao makasisi waliwadharau, ndio waliopokea dinari—ile heshima ya kutumikia wakiwa mabalozi wapakwa-mafuta wa Ufalme wa kimbingu wa Mungu. Mathayo 19:30–20:16.
▪ Ni nini kinachowakilishwa na shamba la mizabibu? Ni nani wanaowakilishwa na mwenye shamba la mizabibu na wale wafanya kazi wa saa 12 na wa saa 1?
▪ Siku ya kazi iliyo ya ufananisho ilikwisha lini, na malipo yalifanywa lini?
▪ Ni nini kinachowakilishwa na malipo ya ile dinari?