Sura 121
Mbele ya Sanhedrini, Kisha kwa Pilato
USIKU unakaribia mwisho. Petro amekana Yesu kwa mara ya tatu, na washiriki wa Sanhedrini wamemaliza kesi yao ya bandia na wametawanyika. Hata hivyo, wanakutana tena asubuhi ya Ijumaa mara tu kunapopambazuka, wakati huu wakiwa kwenye jumba la Sanhedrini yao. Inaelekea kusudi lao ni kufanya ionekane eti kesi yao ya usiku ilifuata uhalali wa sheria. Yesu anapoletwa mbele yao, wanasema hivi, kama vile walivyofanya usiku: “Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie.”
“Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa,” Yesu anajibu. “Tena, nikiwauliza, hamtajibu.” Hata hivyo, kwa moyo mkuu Yesu anaelekeza kwenye utambulishi wake, akisema: “Tangu sasa Mwana wa Adamu [Mwana wa binadamu, NW] atakuwa ameketi [akiketi, NW] upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi.”
“Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu?” wote wataka kujua.
“Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye,” Yesu ajibu.
Kwa wanaume hawa ambao wameazimia kuua, jibu hili linatosha. Wanaliona kuwa kufuru. “Tuna haja gani tena ya ushuhuda?” wanauliza. “Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake.” Hivyo basi wanamfunga Yesu, wanamwongoza kutoka hapo, na kumpa kwa gavana Mroma Pontio Pilato.
Yudasi, msaliti wa Yesu, amekuwa akitazama hatua za mambo hayo. Anapoona kwamba Yesu amelaaniwa vikali, ahisi majuto. Hivyo yeye aendea makuhani wakuu na wanaume wazee kurudisha vile vipande 30 vya fedha, akieleza hivi: “Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.”
“Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe”! wajibu bila moyo wa huruma. Hivyo basi Yuda atupa vile vipande vya fedha hekaluni na kwenda zake na kujaribu kujinyonga. Hata hivyo, inaonekana kwamba tawi ambalo Yuda afungilia kamba linakatika, na mwili wake waporomoka kwenye miamba iliyoko chini, ambako wapasuka-pasuka.
Makuhani wakuu hawana hakika wafanye nini na vile vipande vya fedha. “Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka,” wakata shauri, “kwa kuwa ni kima cha damu.” Hivyo basi, baada ya kushauriana, kwa pesa hizo wanunua shamba la mfinyanzi ili kuzika wageni. Hivyo shamba hilo laja kuitwa “konde la damu.”
Bado ni mapema asubuhi wakati Yesu anapopelekwa kwenye jumba la gavana. Lakini Wayahudi ambao wameandamana naye wakataa kuingia kwa sababu wanaamini kwamba huo uhusiano wa kindani pamoja na Wasio Wayahudi utawatia unajisi. Hivyo basi ili ajipatanishe na maoni yao, Pilato aja nje. “Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?” auliza.
“Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako,” wajibu.
Akitaka kuepuka kuhusika, Pilato ajibu hivi: “Haya! mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!”
Wakifunua azimio lao la uuaji, Wayahudi wadai hivi: “Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.” Kwa kweli, kama wangeua Yesu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa, inaelekea ingeleta msukosuko wa watu wote, kwa kuwa wengi wamheshimu Yesu sana. Lakini wakiweza kufanya Waroma wamuue kwa shtaka la kisiasa, hiyo itaelekea kuwaondolea daraka mbele ya watu.
Hivyo basi viongozi wa kidini, bila kutaja kesi yao ya mapema ambamo walilaani Yesu vikali juu ya kukufuru, sasa watunga mashtaka tofauti. Wafanyiza lile shtaka lenye sehemu tatu: “Tumemwona huyu [1] akipotosha taifa letu, na [2] kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, [3] akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.”
Lile shtaka la kwamba Yesu adai kuwa mfalme ndilo lahangaisha Pilato. Kwa hiyo, yeye aingia tena katika jumba, aita Yesu aende alipo, na kuuliza: “Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Ndiyo kusema, je! umevunja sheria kwa kujijulisha wazi kuwa mfalme kwa kupinga Kaisari?
Yesu ataka kujua ni mengi kadiri gani ambayo tayari Pilato amesikia juu yake, hivyo basi auliza hivi: “Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?”
Pilato adai hana maarifa yoyote juu yake na ana tamaa ya kujua mambo hakika. “Ama! Ni Myahudi mimi!” ajibu. “Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?”
Yesu hajaribu kwa njia yoyote kuepa suala hilo, ambalo ni la kuwa na ufalme. Jibu ambalo Yesu anatoa sasa bila shaka lashangaza Pilato. Luka 22:66–23:3; Mathayo 27:1-11; Marko 15:1; Yohana 18:28-35; Matendo 1:16-20.
▪ Sanhedrini yakutana tena asubuhi kwa kusudi gani?
▪ Yuda afaje, na ni jambo gani lafanywa na vile vipande 30 vya fedha?
▪ Badala ya Wayahudi wamuue Yesu wao wenyewe, kwa nini wataka Waroma wamuue Yesu?
▪ Ni mashtaka gani ambayo Wayahudi wafanyia Yesu?