Sura 126
“Hakika Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”
YESU hajawa juu ya ule mti kwa muda mrefu wakati ambapo, katika mchana kakati, giza la kifumbo, lenye urefu wa saa tatu latukia. Halisababishwi na kupatwa kwa jua, kwa kuwa kupatwa kwa jua hutukia tu wakati wa mwezi mpya na mwezi ni mpevu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa. Zaidi ya hilo, kupatwa kwa jua huwa kwa dakika chache tu. Hivyo basi giza hili lina chanzo cha kimungu! Labda lawaachisha kidogo wale wanaomdhihaki Yesu, hata kusababisha dhihaka zao kali zikome.
Ikiwa ajabu hii yenye kutia woga yatukia kabla ya yule mtenda maovu mmoja kumtia adabu mwandamani wake na kumwomba Yesu amkumbuke, huenda hilo likawa ni jambo moja linaloleta toba yake. Labda ni wakati wa giza hilo kwamba wanawake wanne, yaani, mama ya Yesu na Salome dada yake, Mariamu Magdalene, na Mariamu mama ya mtume Yakobo Mdogo, wasogelea kuja karibu na mti wa mateso. Yohana, mtume mpendwa wa Yesu, yupo hapo pamoja nao.
Lo, jinsi moyo wa mama ya Yesu ‘wachomwa’ atazamapo mwana aliyemlea na kumtunza kwa mapenzi akining’inia hapo kwa maumivu makali! Lakini Yesu afikiria, si maumivu yake mwenyewe, bali hali njema ya mama yake. Kwa jitihada kubwa, amtolea Yohana ishara kwa kichwa chake na kusema hivi kwa mama yake: “Mama [mwanamke, NW], tazama, mwanao”! Halafu, akitoa ishara iyo hiyo kuelekea Mariamu, asema hivi kwa Yohana: “Tazama, mama yako”!
Kwa njia hiyo Yesu akabidhi utunzaji wa mama yake, ambaye ushuhuda waonyesha kwamba sasa yeye ni mjane, mikononi mwa mtume wake aliyependwa kipekee. Afanya hivyo kwa sababu wana wengine wa Mariamu hawajadhihirisha bado imani katika yeye. Hivyo yeye aweka mfano mzuri wa kutoa riziki si kwa mahitaji ya kimwili tu ya mama yake bali pia kwa mahitaji yake ya kiroho.
Karibu saa tisa mchana, Yesu asema hivi: “Naona kiu.” Yesu ajisikia ni kama kwamba Baba yake ameondoa ulinzi kutoka kwake ili ukamilifu wake ujaribiwe kabisa. Hivyo apaaza sauti hivi: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Wasikiapo hayo, watu fulani waliosimama karibu washangaa na kusema kwa sauti kubwa: “Tazama, anamwita Eliya.” Mara hiyo mmoja wao akimbia na, akitia sifongo iliyofyonza divai chungu kwenye ncha ya kishina cha hisopo, ampa kinywaji. Lakini wengine wasema hivi: “Acheni; na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha.”
Yesu apokeapo ile divai chungu, alia kwa sauti kubwa: “Imekwisha.” Ndiyo, amemaliza kila jambo ambalo Baba yake amemtuma duniani afanye. Mwisho, asema hivi: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Kwa njia hiyo Yesu amkabidhi Mungu nguvu ya uhai wake akiwa na hakika kwamba Mungu atamrudishia huo. Halafu ainamisha kichwa chake na kufa.
Yesu avutapo pumzi yake ya mwisho, tetemeko kali la dunia latukia, likipasua wazi miamba. Tetemeko hilo lina nguvu sana hivi kwamba maziara ya ukumbusho nje ya Yerusalemu yaachwa wazi na maiti zatupwa nje yayo. Wapita-njia, ambao waona miili mifu ambayo imefichuliwa wazi, waingia katika jiji na kuripoti jambo hilo.
Zaidi ya hilo, Yesu afapo, lile pazia kubwa sana ligawanyalo Patakatifu na Patakatifu Zaidi katika hekalu la Mungu lapasuliwa mara mbili, kutoka juu hadi chini. Kwa wazi pazia hilo lililopambwa vizuri lina urefu wa kwenda juu wa meta 18 na ni zito sana! Muujiza huo wa kushangaza sana si kwamba wadhihirisha tu hasira kali ya Mungu juu ya walioua Mwana Wake bali pia wamaanisha kwamba njia ya kuingia Patakatifu Zaidi, mbinguni penyewe, sasa imewezeshwa na kifo cha Yesu.
Basi, watu hao waonapo tetemeko hilo la dunia na kuona mambo yanayotendeka, waogopa sana. Ofisa wa jeshi mwenye kusimamia mambo kwenye mahali hapo pa mauaji hayo ampa Mungu utukufu. “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu,” atangaza. Yaelekea alikuwapo wakati dai la uana wa kimungu lilipozungumzwa kwenye jaribu la Yesu mbele ya Pilato. Na sasa yeye asadiki kwamba Yesu ndiye Mwana wa Mungu, ndiyo, kwamba kweli yeye ndiye binadamu mkubwa zaidi aliyepata kuishi.
Wengine pia washangazwa mno na matukio hayo ya kimuujiza, nao waanza kurudi nyumbani wakijipiga-piga vifua vyao kama ishara ya huzuni kuu na aibu yao nyingi sana. Wanafunzi wengi wa Yesu wa kike ambao waguswa moyo sana na matukio hayo ya maana sana wanatazama tamasha hii kwa mbali. Mtume Yohana yupo pia. Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; 2:34, 35; Yohana 19:25-30.
▪ Kwa nini kupatwa kwa jua hakuwezi kuwa ndiko kumesababisha zile saa tatu za giza?
▪ Muda mfupi kabla ya kifo chake, Yesu aweka mfano gani mzuri kwa ajili ya wale walio na wazazi wazee?
▪ Yesu asema maneno gani ya mwisho kabla ya kufa?
▪ Tetemeko la dunia latimiza nini, na ni nini maana ya kupasuliwa kwa pazia la hekalu vipande viwili?
▪ Miujiza hiyo yawa na matokeo gani juu ya ofisa wa jeshi mwenye kusimamia mambo kwenye mahali hapo pa mauaji?