Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 130
  • Kwenye Bahari ya Galilaya

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kwenye Bahari ya Galilaya
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Kwenye Bahari ya Galilaya
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Kwenye Ufuo wa Bahari ya Galilaya
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Yesu Awatokea Wavuvi
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Mtume Petro—Kwa Sababu Gani Anapendwa Sana na Wengi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 130

Sura 130

Kwenye Bahari ya Galilaya

SASA mitume warudi Galilaya, kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza wafanye hapo mapema. Lakini hawana uhakika juu ya wanalopaswa kufanya huko. Baada ya muda, Petro amwambia Tomaso, Nathanaeli, Yakobo na ndugu yake Yohana, na mitume wengine wawili hivi: “Naenda kuvua samaki.”

“Sisi nasi tutakwenda nawe,” wale sita wajibu.

Usiku kucha, wanashindwa kunasa chochote. Hata hivyo, mwangaza unapoanza kuingia, Yesu atokea ukingoni mwa bahari, lakini mitume hawatambui kwamba ni Yesu. Yeye apaaza sauti: “Wanangu, mna kitoweo?”

“La,” wapaaza sauti kwake ikipitia juu ya maji.

“Litupeni jarife [wavu, NW] upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata,” yeye asema. Na wanapofanya hivyo, hawawezi kuuvuta wavu wao kwa sababu ya samaki wote wale.

“Ndiye Bwana,” Yohana asema kwa sauti kubwa.

Kwa kusikia hivyo, Petro ajivika vazi lake la juu, kwa kuwa amevua nguo zake, na kujitupa ndani ya bahari. Kisha yeye aogelea meta tisini hivi kwenda ukingoni mwa bahari. Mitume wale wengine wamfuata katika mashua ile ndogo, wakizivuta nyavu zilizojaa samaki.

Wanapofika pwani, pana moto wa makaa, ulio na samaki juu yao, na pana mkate. “Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi,” Yesu asema. Petro apanda chomboni na kuvuta wavu pwani. Lina samaki wakubwa 153!

“Njoni mfungue kinywa,” Yesu awaalika.

Hakuna yeyote wao aliye na ujasiri wa kutosha kumuuliza, “U nani wewe?” kwa sababu wao wote wajua kwamba ni Yesu. Hii ni mara yake ya saba kuwatokea baada ya ufufuo, na mara yake ya tatu kwa mitume wakiwa kikundi. Sasa apakua kiamsha-kinywa, akimpa kila mmoja wao baadhi ya mkate na samaki.

Wanapomaliza kula, Yesu, labda akitazama kuelekea ule mvuo mkubwa wa samaki, amuuliza Petro: “Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?” Bila shaka amaanisha, Je! umefungamana zaidi na shughuli ya uvuvi kuliko kazi ambayo nimekutayarisha ufanye?

“Wajua kuwa nakupenda,” Petro aitikia.

“Lisha wana-kondoo wangu,” Yesu ajibu.

Tena, kwa mara ya pili, auliza hivi: “Simoni wa Yohana, wanipenda?”

“Ndiyo Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda,” Petro ajibu.

“Chunga kondoo zangu,” Yesu aamuru tena.

Halafu, hata mara ya tatu, auliza hivi: “Simoni wa Yohana, wanipenda?”

Kufikia sasa Petro amehuzunika. Huenda akawa anashangaa akitaka kujua kama Yesu aonea shaka uaminifu wake wa ushikamanifu. Ingawaje, Yesu alipokuwa akihukumiwa hivi karibuni kwa ajili ya uhai wake, Petro alikana mara tatu kwamba hamjui Yesu. Kwa hiyo Petro asema hivi: “Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda.”

“Lisha kondoo zangu,” Yesu aamuru kwa mara ya tatu.

Hivyo Yesu atumia Petro kama mfano ili akazie kwa wale wengine kazi ambayo awataka wafanye. Karibuni ataondoka duniani, naye awataka wachukue uongozi katika kuhudumia wale watakaovutwa katika zizi la kondoo la Mungu.

Kama vile Yesu alivyokamatwa na kuuawa kwa sababu alifanya kazi ambayo Mungu alimwagiza afanye, hivyo, sasa afunua kwamba, Petro atapatwa na jambo kama hilo. “Wakati ulipokuwa kijana,” Yesu amwambia, “ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.” Ijapokuwa kifo cha kufia imani kinachomngoja Petro, Yesu amhimiza hivi: “Nifuate [Endelea kunifuata, NW].”

Anapogeuka, Petro amwona Yohana na kuuliza hivi: “Bwana, na huyu je?”

“Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo,” Yesu ajibu, “imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi [endelea kunifuata, NW].” Wanafunzi walio wengi wakaja kuelewa kwamba maneno hayo ya Yesu yalimaanisha kwamba mtume Yohana hangekufa kamwe. Hata hivyo, kama mtume Yohana alivyoeleza baadaye, Yesu hakusema kwamba yeye hangekufa, bali Yesu alisema tu: “Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?”

Yohana alieleza pia baadaye jambo hili la maana sana: “Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.” Yohana 21:1-25; Mathayo 26:32; 28:7, 10.

▪ Ni jambo gani laonyesha kwamba mitume hawana hakika juu ya wanalopaswa kufanya katika Galilaya?

▪ Mitume wamtambuaje Yesu kwenye Bahari ya Galilaya?

▪ Yesu ametokea mara ngapi tangu ufufuo wake?

▪ Yesu akaziaje anayotaka mitume wake wafanye?

▪ Yesu aonyeshaje jinsi Petro atakufa?

▪ Ni maelezo gani ya Yesu juu ya Yohana yaliyoeleweka kimakosa na walio miongoni mwa wanafunzi?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki