Somo la 10
Mazoea Ambayo Mungu Huchukia
Wapaswa uhisije kuhusu mambo ambayo Mungu husema ni mabaya? (1)
Ni aina zipi za mwenendo wa kingono zilizo mbaya? (2)
Mkristo apaswa aoneje kusema uwongo? (3) kucheza kamari? (3) kuiba? (3) ujeuri? (4) uwasiliani-roho? (5) ulevi? (6)
Mtu aweza kuachaje mazoea mabaya? (7)
1. Watumishi wa Mungu hupenda yaliyo mema. Lakini ni lazima pia wajifunze kuchukia yaliyo mabaya. (Zaburi 97:10) Hilo lamaanisha kuepuka mazoea fulani ambayo Mungu huchukia. Ni nini baadhi ya mazoea hayo?
2. Uasherati: Ngono kabla ya ndoa, uzinzi, ngono na mnyama, kufanya ngono na mtu wa ukoo, na ugoni-jinsia-moja hayo yote ni dhambi nzito dhidi ya Mungu. (Mambo ya Walawi 18:6; Warumi 1:26, 27; 1 Wakorintho 6:9, 10) Ikiwa mwanamume na mwanamke hawajaoana lakini wanaishi pamoja, wanapaswa watengane ama sivyo waoane kihalali.—Waebrania 13:4.
3. Kusema Uwongo, Kucheza Kamari, Kuiba: Yehova Mungu hawezi kusema uwongo. (Tito 1:2) Watu wanaotaka kibali chake ni lazima waepuke kusema uwongo. (Mithali 6:16-19; Wakolosai 3:9, 10) Kila namna ya kucheza kamari ina pupa. Kwa hiyo Wakristo hawashiriki katika aina yoyote ile ya kucheza kamari, kama vile bahati-nasibu, mashindano ya farasi, na kucheza karata. (Waefeso 5:3-5) Na Wakristo hawaibi. Hawanunui mali iliyoibwa wakijua hivyo wala hawachukui vitu bila ruhusa.—Kutoka 20:15; Waefeso 4:28.
4. Hasira za Ghafula, Ujeuri: Hasira isiyodhibitiwa yaweza kuongoza kwenye vitendo vya ujeuri. (Mwanzo 4:5-8) Mtu mjeuri hawezi kuwa rafiki ya Mungu. (Zaburi 11:5; Mithali 22:24, 25) Ni jambo baya kulipiza kisasi au kurudisha ovu kwa mambo mabaya ambayo wengine huenda wakatufanyia.—Mithali 24:29; Warumi 12:17-21.
5. Ulogi wa Kimizungu na Uwasiliani-Roho: Watu wengine huomba kwa bidii msaada wa nguvu za roho ili kujaribu kuponya magonjwa. Wengine huloga maadui wao ili kuwafanya wawe wagonjwa au hata kuwaua. Nguvu inayounga mkono mazoea hayo yote ni Shetani. Kwa hiyo ni lazima Wakristo wasishiriki katika yoyote ya hayo. (Kumbukumbu la Torati 18:9-13) Kuendelea kuwa karibu sana na Yehova ndio ulinzi ulio bora zaidi dhidi ya ulogi ambao huenda wengine wakaelekeza kwetu.—Mithali 18:10.
6. Ulevi: Kunywa divai kidogo, pombe, au kinywaji kingine cha alkoholi si kubaya. (Zaburi 104:15; 1 Timotheo 5:23) Lakini kunywa kupita kiasi na ulevi ni kubaya machoni pa Mungu. (1 Wakorintho 5:11-13; 1 Timotheo 3:8) Kunywa kileo kingi sana kwaweza kuharibu afya yako na kuivuruga familia yako. Kwaweza pia kukufanya ushindwe kwa urahisi na vishawishi vinginevyo.—Mithali 23:20, 21, 29-35.
7. Watu ambao huzoea mambo ambayo Mungu husema ni mabaya “hawataurithi ufalme wa Mungu.” (Wagalatia 5:19-21) Ikiwa wampenda Mungu kwelikweli na wataka kumpendeza, wewe waweza kuyaacha mazoea hayo. (1 Yohana 5:3) Jifunze kuchukia yale ambayo Mungu husema ni mabaya. (Warumi 12:9) Shirikiana na watu walio na tabia za kimungu. (Mithali 13:20) Washiriki Wakristo walio wakomavu waweza kuthibitika kuwa chanzo cha msaada. (Yakobo 5:14) Zaidi ya yote, tegemea msaada wa Mungu kupitia sala.—Wafilipi 4:6, 7, 13.
[Picha katika ukurasa wa 20, 21]
Mungu huchukia ulevi, kuiba, kucheza kamari, na vitendo vya ujeuri