Sura Ya Tano
Uumbaji—Ulitoka Wapi?
KAMA ilivyotajwa katika sura zilizotangulia, ugunduzi wa kisasa wa mambo ya sayansi unatoa uthibitisho mwingi kwamba ulimwengu na uhai duniani ulikuwa na mwanzo fulani. Ni nini kilichouanzisha?
Baada ya kuchunguza uthibitisho unaopatikana, wengi wamekata kauli ya kwamba kulikuwa na Chanzo fulani cha uumbaji. Hata hivyo, huenda wao wakasita kutaja kwamba Chanzo hicho ni mtu fulani. Hali hiyo ya kusita kutaja Muumba yaonyesha mtazamo wa wanasayansi fulani.
Kwa mfano, Albert Einstein alisadiki kwamba ulimwengu ulikuwa na mwanzo, naye alitamani “kujua jinsi Mungu alivyoumba ulimwengu.” Lakini Einstein hakusema kwamba anaitikadi Mungu aliye mtu halisi; yeye alisema juu ya “hisia ya kidini iliyo katika [ulimwengu wote], ambayo haina fundisho lolote wala haitambui Mungu aliye kama wanadamu.” Vivyo hivyo, mshindi wa tuzo la Nobeli aliye pia mtaalamu wa kemia Kenichi Fukui alitaja kwamba aliitikadi kuwa kuna mpango mkuu katika ulimwengu. Alisema kwamba “mipango hii ambayo imeingiliana vizuri sana yaweza kufafanuliwa na maneno kama vile ‘Mwongozo wa Mtu’ au ‘Mungu.’” Lakini akaiita ile miunganisho “tabia ya maumbile.”
Je, wajua kwamba kuitikadi kisababishi kisicho na utu ni kama tu kufuata mafundisho ya kidini ya Mashariki? Watu wengi wa Mashariki huamini kwamba maumbile yalitokea yenyewe tu. Wazo hilo hata linaonyeshwa na herufi za Kichina zinazomaanisha maumbile, ambazo kihalisi zinamaanisha “-enye kutokea -enyewe” au “-enye kuwako bila kuumbwa.” Einstein aliamini kwamba nadharia yake ya hisia ya kidini ya ulimwengu wote iliungwa mkono na Ubudha. Buddha aliamini kwamba si jambo muhimu kama Muumba alishiriki kuumba ulimwengu na binadamu. Vivyo hivyo, dini ya Shinto haiandai ufafanuzi wowote wa jinsi maumbile yalivyotokea, na wafuasi wa dini ya Shinto waamini kwamba miungu ni roho za wafu ambazo huchangamana na maumbile.
Ajabu ni kwamba mawazo kama hayo yanafanana na maoni yaliyopendwa na wengi katika Ugiriki ya kale. Inasemekana kwamba mwanafalsafa Epikurasi (341-270 K.W.K.) aliamini kwamba ‘miungu wako mbali sana hivi kwamba hawawezi kuathiri wanadamu.’ Yeye aliamini kwamba mwanadamu ametokana na kani za asili, labda akitokana na kitu kisicho hai na vilevile kupitia kusalimika kwa viumbe bora. Unaweza kuona kutokana na mambo haya kwamba kumbe mawazo ya leo si mapya.
Mbali na Waepikurea, kulikuwa na Wastoiki Wagiriki, ambao waliona kani za asili kuwa Mungu. Wao walidhani ya kwamba wanadamu wanapokufa, nishati isiyo na utu kutoka kwa wafu hao huingia katika nishati kubwa inayofanyiza Mungu. Wao walihisi kwamba kushirikiana na sheria za asili ndiko jambo bora zaidi. Je, umesikia maoni kama hayo katika siku zetu?
Bishano Juu ya Mungu Mwenye Utu
Hata hivyo, hatupaswi kupuuza habari zote kutoka Ugiriki ya kale kuwa historia tu yenye kupendeza. Akiongea juu ya zile itikadi ambazo zimetajwa, mwalimu mmoja mashuhuri katika karne ya kwanza alitoa mojawapo ya hotuba zenye maana zaidi katika historia. Luka, tabibu aliye pia mwanahistoria, alirekodi hotuba hiyo, nasi twaipata katika sura ya 17 ya kitabu cha Matendo ya Mitume. Inaweza kutusaidia kuwa na maoni thabiti juu ya Chanzo cha uumbaji na kuona mahali petu kwa kuhusiana na kile Chanzo. Lakini, hotuba iliyotolewa miaka 1,900 iliyopita inaweza kuhusianaje na maisha zetu leo tukiwa watu wenye mioyo myeupe ambao wanatafuta maana ya maisha?
Mwalimu mashuhuri, Paulo, alialikwa kwenye mahakama kuu katika Athene. Huko aliwakabili Waepikurea na Wastoiki, ambao hawakuamini kuwako kwa Mungu mwenye utu. Katika utangulizi wake, Paulo alitaja kwamba aliona katika jiji lao madhabahu iliyoandikwa “Kwa Mungu Asiyejulikana” (kwa Kigiriki, A·gnoʹstoi The·oiʹ). Na wengine hufikiri kwamba mtaalamu wa biolojia Thomas H. Huxley (1825-1895) alirejezea jambo hili alipounda neno la Kiingereza “agnostic.” Huxley alitumia neno hilo kwa wale ambao wanaamini kwamba “kisababishi kikuu (Mungu) na asili ya mambo hazijulikani au haziwezi kujulikana.” Lakini, je, kweli Muumba ‘hawezi kujulikana’ kama ambavyo wengi wameamini?
Kwa wazi, hiyo ni kutumia vibaya maneno ya Paulo; ni kukosa kuelewa jambo alilomaanisha Paulo. Badala ya kusema kwamba Muumba hawezi kujulikana, Paulo alikuwa akisema tu kwamba Waathene hao hawakumjua Yeye. Paulo hakuwa na uthibitisho mwingi wa kisayansi wa kuwako kwa Muumba kama tulivyo nao leo. Lakini Paulo hakuwa na shaka kwamba kuna Mbuni mwenye akili na mwenye utu ambaye alikuwa na sifa zenye kutuvutia kwake. Ona yale ambayo Paulo aliongezea kusema:
“Kile mnachokipa ujitoaji-kimungu bila kujua, hicho ninawatangazia nyinyi. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyo katika huo, akiwa, kama Huyu alivyo, Bwana wa mbingu na dunia, hakai katika mahekalu yaliyofanywa kwa mikono, wala yeye hahudumiwi kwa mikono ya kibinadamu kama kwamba yeye ahitaji kitu chochote, kwa sababu yeye mwenyewe huwapa watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso mzima wa dunia.” (Matendo 17:23-26) Njia nzuri sana ya kutoa sababu, sivyo?
Ndiyo, badala ya kudokeza kwamba Mungu alikuwa hawezi kujulikana, Paulo alikuwa akikazia kwamba wale waliotengeneza madhabahu ya Athene, na vilevile wengi waliokuwa wakimsikiliza, bado hawakumjua Yeye. Kisha Paulo akawahimiza—na wale ambao wamepata kusoma hotuba hiyo—watafute kumjua Muumba, kwa kuwa “hayuko mbali sana na kila mmoja wetu.” (Matendo 17:27) Unaweza kuona kwamba Paulo alitokeza kwa busara jambo la kwamba twaweza kuona uthibitisho wa kuwapo kwa Muumba wa vitu vyote kwa kutazama uumbaji wake. Kwa kufanya hivyo, twaweza pia kutambua baadhi ya sifa zake.
Tumechunguza uthibitisho kadhaa unaothibitisha kwamba kuna Muumba. Mmoja ni ulimwengu mkubwa sana ambao umepangwa vizuri kwa kutumia akili, na ambao kwa wazi ulikuwa na mwanzo fulani. Mwingine ni uhai duniani, kutia ndani ubuni unaoonekana katika chembe za mwili wetu. Na wa tatu ni ubongo wetu, ambao unahusiana na hali ya kuweza kujitambua na upendezi wetu katika wakati ujao. Lakini ebu tutazame mifano mingine ya uumbaji wa Muumba ambayo hutuhusu kila siku. Tunapofanya hivyo, jiulize, ‘Kitu hiki chanifundisha nini kuhusu utu wa Yule aliyekibuni na kukiandaa?’
Kujifunza Kutokana na Uumbaji Wake
Kutazama tu uumbaji wake kwatuambia mambo mengi kuhusu Muumba. Pindi moja, Paulo alitaja mfano mmoja wa jambo hili alipoambia umati uliokuwa katika Asia Ndogo: “Katika vizazi vilivyopita [Muumba] aliruhusu mataifa yote yaendelee katika njia zayo, ijapokuwa, kwa kweli, hakujiacha mwenyewe bila ushahidi kwa kuwa alitenda mema, akiwapa nyinyi mvua kutoka mbinguni na majira yenye kuzaa matunda, akijaza mioyo yenu kikamili kwa chakula na uchangamfu.” (Matendo 14:16, 17) Ona mfano ambao Paulo alitoa juu ya jinsi ambavyo Muumba, kwa kuandaa chakula kwa wanadamu, amefunua utu Wake.
Katika nchi fulani leo, watu waweza kuchukua kivivi hivi kupatikana kwa chakula. Katika sehemu nyinginezo, wengi hujitahidi sana ndipo tu wapate chakula cha kutosha. Katika hali hizo zote, hata uwezekano wa kuwa na chakula cha kutuendeleza kwategemea hekima na wema wa Muumba wetu.
Chakula cha wanadamu na wanyama hutokana na mizunguko yenye kutia ndani mambo mengi—kutia ndani mzunguko wa maji, mzunguko wa kaboni, mzunguko wa fosforasi, na mzunguko wa nitrojeni. Inajulikana wazi kwamba katika utaratibu muhimu unaoitwa usanidimwanga wa mimea kujifanyizia chakula chake, mimea hutumia kaboni dioksidi na maji ili kutokeza sukari, huku ikitumia jua likiwa chanzo cha nishati. Inatukia kwamba wakati inapofanyiza chakula, mimea hutoa nje oksijeni. Je, oksijeni hiyo yaweza kuitwa “takataka”? Kwetu, hiyo si takataka kamwe. Ni muhimu sana kwamba tupumue oksijeni na kuitumia kuvunja-vunja kemikali mwilini. Twatoa kaboni dioksidi, ambayo mimea hutumia tena na kutoa nje oksijeni inapotengeneza chakula chake. Huenda tulijifunza utaratibu huu katika somo la sayansi ya msingi, lakini ni muhimu sana na ni wa ajabu sana. Na huo ni mwanzo tu.
Katika chembe za mwili wetu na wa wanyama, fosforasi ni muhimu katika kusafirisha nishati. Tunapata fosforasi wapi? Tena, kutoka kwa mimea. Mimea hufyonza fosfati za madini kutoka kwenye udongo na kuzigeuza kuwa zenye kaboni. Sisi hula mimea yenye fosforasi za kaboni na kuitumia kwa utendaji muhimu. Baadaye, fosforasi hurudi udongoni ikiwa “takataka” ambazo zinaweza tena kufyonzwa na mimea.
Twahitaji nitrojeni pia, ambayo ni sehemu ya kila protini na molekuli za DNA katika mwili wetu. Tunapataje elementi hii ambayo ni muhimu sana kwa uhai? Ingawa asilimia 78 ya hewa inayotuzunguka ni nitrojeni, wala mimea wala wanyama hawawezi kuifyonza moja kwa moja. Kwa hiyo, nitrojeni iliyo katika hewa ni lazima igeuzwe kabla ya kuweza kutumiwa na mimea na baadaye kutumiwa na wanadamu na wanyama. Nitrojeni hiyo hugeuzwaje? Katika njia nyingi. Njia moja ni kupitia radi.a Nitrojeni hugeuzwa pia na bakteria ambazo hupatikana katika mizizi ya mimea ya mkunde, kama vile mbaazi, maharagwe, na alfalfa. Bakteria hizo hugeuza nitrojeni ipatikanayo hewani iwe kwa namna ambayo mimea inaweza kutumia. Kwa njia hiyo, unapokula mboga za kijani-kibichi, unapata nitrojeni, ambayo mwili wako unahitaji ili kutokeza protini. Kwa kushangaza, kuna aina za mkunde katika misitu ya mvua ya kitropiki, jangwa, na hata zile sehemu za baridi kali. Na eneo likichomeka, jamii ya mkunde huwa ya kwanza kumea.
Hiyo ni mizunguko ya ajabu kama nini! Kila mmoja wa mizunguko hiyo hutumia vizuri takataka kutoka kwa mizunguko mingine. Nishati inayohitajiwa hutokana hasa na jua nayo ni safi, inategemeka, na ni ya daima. Jinsi hilo linavyotofautiana na jitihada za wanadamu za kutengeneza upya vitu vilivyotumiwa tayari! Hata vitu vilivyofanyizwa na wanadamu ambavyo husemwa eti havidhuru mazingira huenda visichangie usafi wa dunia kwa sababu ya mifumo tata ya utengenezaji-upya wa wanadamu. Kwa habari hii, U.S.News & World Report lilisema kwamba vitu vinapasa kutengenezwa kwa njia ya kwamba visehemu vyake vinaweza kutengenezwa upya kwa urahisi. Je, hilo si jambo tunaloona katika mizunguko hiyo ya asili? Basi, jambo hilo lafunua nini kuhusu hekima ya Muumba na uwezo wake wa kuona mbali?
Asiyependelea na Mwenye Haki
Ili tuone zaidi baadhi ya sifa za Muumba, ebu tufikirie mfumo mwingine mmoja tu—mfumo wa kinga katika mwili wetu. Huo pia wahusisha bakteria.
“Ingawa upendezi wa mwanadamu katika bakteria mara nyingi hukazia madhara yake,” chasema kitabu The New Encyclopædia Britannica, “bakteria nyingi hazidhuru wanadamu, na nyingi hata ni zenye manufaa.” Kwa kweli hizo ni muhimu sana. Bakteria hutimiza fungu muhimu katika mzunguko wa nitrojeni kama ilivyotajwa, na vilevile katika mizunguko inayohusu kaboni dioksidi na elementi nyinginezo. Na twahitaji pia bakteria katika matumbo yetu. Tuna aina 400 za bakteria katika utumbo mpana pekee, nazo husaidia kuyeyusha vitamini K na kuondoa takataka. Na manufaa nyingine zaidi kwetu ni kwamba bakteria husaidia ng’ombe kugeuza nyasi kuwa maziwa. Bakteria nyinginezo ni muhimu katika kuchacha kwa vitu—katika kutengeneza jibini, mtindi, siki, na vyakula vyenye kuchacha. Lakini namna gani bakteria zikienda mahali ambapo hazitakikani mwilini mwetu?
Basi, chembe nyeupe za damu zipatazo trilioni mbili zilizo katika mwili wetu hupigana na bakteria ambayo huenda ikatudhuru. Daniel E. Koshland, Jr., ambaye ni mhariri wa gazeti la Science, aeleza: “Mfumo wa kinga umefanyizwa ili utambue vitu vya kigeni vyenye kushambulia. Ili mfumo wa kinga ufanye hivyo, huo hutokeza molekuli za kinga za aina 100,000,000,000 tofauti-tofauti ili vitu hivyo vyenye kushambulia hata viwe na umbo jipi vitambuliwe na kuondoshwa na molekuli.”
Aina moja ya chembe ambayo mwili wetu hutumia kupigana na vitu hivyo vyenye kushambulia ni macrophage; jina lake lamaanisha “mlaji mkubwa,” ambalo linafaa kwa sababu hiyo chembe hunyafua vitu visivyojulikana vilivyo katika damu. Kwa mfano, baada ya kukila kirusi chenye kushambulia, mlaji mkubwa hukivunja vipande vidogo-vidogo. Kisha mlaji mkubwa huonyesha protini kutoka kwenye hicho kirusi. Protini hiyo iliyotiwa alama hutumikia kuwa onyo kwa mfumo wetu wa kinga, ikitahadharisha kwamba kuna vitu visivyojulikana katika mwili. Ikiwa chembe nyingine iliyo katika mfumo wa kinga, ile iitwayo chembe-T, inatambua protini hiyo ya kirusi, inawasiliana kikemikali na yule mlaji mkubwa. Kemikali hizo zenyewe ni protini zisizo za kawaida ambazo zina kazi nyingi sana tofauti-tofauti, zikidhibiti na kuimarisha mfumo wa kinga wa mwili wakati wa shambulio. Utaratibu huo hutokeza vita kali dhidi ya aina fulani ya kirusi. Kwa hiyo, mara nyingi sisi hushinda maambukizo.
Kwa hakika, mambo mengi zaidi huhusika, lakini hata ufafanuzi huu mfupi wafunua jinsi mfumo wetu wa kinga ulivyo na mambo mengi. Tulipataje mfumo wenye mambo mengi kama huu? Tuliupata bure, bila kujali hali ya kifedha ya familia yetu au hali yetu ya kijamii. Linganisha jambo hilo na hali mbaya ya tiba inayowapata watu wengi. “Kwa maoni ya WHO [Shirika la Afya Ulimwenguni], hali inayozidi kuongezeka ya watu wengi kukosa tiba ni hatari sana, kwa kuwa walio maskini hawatibiwi,” akaandika mkurugenzi wa WHO, Dakt. Hiroshi Nakajima. Unaweza kuelewa ni kwa nini mwanamke mmoja aliye mkazi wa mtaa wa mabanda kule São Paulo alisema: “Kwetu, afya nzuri ni kama kitu chenye kutangazwa katika maduka ya anasa. Twaweza kukiona, lakini hatuwezi kukipata.” Mamilioni ya watu duniani pote wana maoni kama hayo.
Ukosefu wa haki kama huo ulimsukuma Albert Schweitzer aende Afrika ili awatibu maskini, na jitihada zake zilimfanya ashinde tuzo la Nobeli. Ni sifa zipi unazohusisha na wanaume na wanawake ambao wamefanya mema kama hayo? Labda unatambua kwamba wanapenda wanadamu na wanafuatia haki, wakiamini kwamba watu walio katika nchi zinazoendelea pia wana haki ya kutunzwa kiafya. Basi, vipi Mwandaliaji wa mfumo wa kinga ulio mzuri ajabu ambao tumepewa bila kujali hali ya kifedha ya familia yetu na hali yetu ya kijamii? Je, hilo halionyeshi hata zaidi upendo, kutobagua, na haki ya Muumba?
Kupata Kumjua Muumba
Hiyo mifumo iliyotajwa ni mifano michache tu ya msingi ya uumbaji wa Muumba, lakini je, haionyeshi kwamba yeye ni mtu halisi mwenye akili ambaye sifa zake hutufanya tuvutiwe naye? Kuna mifano mingine mingi ambayo inaweza kufikiriwa. Hata hivyo, labda tumeona katika maisha yetu ya kila siku kwamba kutazama tu kazi za mtu huenda kusitoshe kumjua vizuri. Hata inawezekana kumwelewa vibaya kama hatungalimjua vizuri! Na ikiwa mtu huyo amesemwa vibaya, je, halingekuwa jambo zuri kukutana naye na kusikia maoni yake? Tunaweza kuongea naye ili kujua jinsi anavyotenda katika hali tofauti-tofauti na sifa anazoonyesha.
Bila shaka, hatuwezi kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Muumba wa ulimwengu mwenye nguvu. Lakini, amefunua mengi kujihusu akiwa mtu halisi katika kitabu ambacho kinapatikana, kwa sehemu au chote, katika zaidi ya lugha 2,000, kutia ndani lugha yako. Kitabu hicho—Biblia—chakualika umjue na kusitawisha uhusiano na Muumba: “Mkaribieni Mungu,” chasema, “naye atawakaribia.” Pia chaonyesha jinsi inavyowezekana kuwa rafiki yake. (Yakobo 2:23; 4:8) Je, ungependa kufanya hivyo?
Basi, twakualika ufikirie masimulizi ya kweli na yenye kuvutia ya Muumba juu ya utendaji wake wa uumbaji.
[Maelezo ya Chini]
a Radi hugeuza nitrojeni fulani ziwe kwa namna ambayo inaweza kufyonzwa, ambayo nayo hunyesha na mvua. Mimea hutumia hiyo ikiwa mbolea inayoandaliwa na asili. Baada ya wanyama na wanadamu kula mimea na kutumia hiyo nitrojeni, hiyo hurudia udongo ikiwa misombo ya amonia na hatimaye nyingi hugeuzwa na kuwa nitrojeni tena.
[Sanduku katika ukurasa wa 79]
Uamuzi Wenye Kupatana na Akili
Wanasayansi wengi wanakubali kwamba ulimwengu ulikuwa na mwanzo. Wengi wanakubali pia kwamba kabla ya mwanzo huo, ni lazima kitu fulani halisi kilikuwako. Wanasayansi wengine husema juu ya nishati iliyokuwako nyakati zote. Wengine husema kulikuwa na mvurugo kabla ya uhai kuwako. Hata maneno yapi yatumiwe, wengi hudhani kwamba kulikuwako kitu—kitu kisicho na chanzo—kilichokuwa kimekuwako tangu milele.
Basi suala ni kama twadhani ni kitu cha milele au mtu fulani wa milele aliyeanzisha uhai. Baada ya kufikiria kile ambacho sayansi imejifunza kuhusu chanzo na asili ya ulimwengu na uhai uliopo, kwa maoni yako ni lipi kati ya mambo hayo lionekanalo kuwa lenye kupatana na akili?
[Sanduku katika ukurasa wa 80]
“Kila mojawapo ya elementi zilizo muhimu kwa uhai—kaboni, nitrojeni, sulfuri—hubadilishwa na bakteria kutoka kwenye hali ya madini na gesi hadi kuwa namna iwezayo kutumiwa na mimea na wanyama.”—The New Encyclopædia Britannica.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 78]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Umeamuaje?
Ulimwengu Wetu
↓ ↓
Haukuwa Ulikuwa
na Mwanzo na Mwanzo
↓ ↓
Haukutokezwa Ulitokezwa
↓ ↓
Na KITU Na MTU
cha Milele wa Milele
[Picha katika ukurasa wa 75]
Watu wengi wa Mashariki huamini kwamba maumbile yalitokea yenyewe tu
[Picha katika ukurasa wa 76]
Paulo alitoa hotuba yenye kuchochea kufikiri kuhusu Mungu aliposimama kwenye kilima hiki, Akropolisi ikionekana nyuma
[Picha katika ukurasa wa 83]
Mungu alimpa kila mmoja wetu mfumo wa kinga unaoshinda kitu chochote ambacho tiba ya kisasa yaweza kuandaa