SOMO LA 29
Ubora wa Sauti
KWA KAWAIDA watu hawavutiwi tu na mambo yanayosemwa, bali wanavutiwa pia na jinsi yanavyosemwa. Ikiwa mtu anayezungumza nawe ana sauti nzuri, changamfu, ya kirafiki, na yenye fadhili, utafurahia kumsikiliza kuliko kama ana sauti kali isiyo ya kirafiki, sivyo?
Kukuza sifa hizo nzuri hakutegemei tu kuboresha sauti. Kunaweza kuhusu utu wa mtu pia. Mtu anapoendelea kujifunza kweli ya Biblia na kuifuata, kwa wazi njia yake ya kuzungumza inabadilika. Sauti yake huonyesha sifa kama vile upendo, shangwe, na fadhili. (Gal. 5:22, 23) Anapojali wengine sana, sauti yake inaonyesha. Anapokuwa mwenye shukrani badala ya kulalamika daima, maneno anayosema na sauti yake inaonyesha hivyo. (Wim. 3:39-42; 1 Tim. 1:12; Yuda 16) Hata kama huelewi lugha fulani, ni rahisi kujua ikiwa mtu anazungumza kwa njia ya ufidhuli, hana uvumilivu, anachambua, ni mkali, na pia ni rahisi kujua kama mwingine anazungumza kwa unyenyekevu, subira, fadhili, na upendo.
Nyakati nyingine sauti isiyofaa inaweza kusababishwa na kasoro fulani ambayo mtu amezaliwa nayo au ugonjwa uliodhuru zoloto. Huenda kasoro hizo zisiweze kurekebishwa katika mfumo huu wa mambo. Lakini, unaweza kuboresha sauti yako ukijifunza kutumia vizuri viungo vya usemi.
Kwanza, tufahamu kwamba sauti za watu hutofautiana. Kwa hiyo, usijaribu kuiga sauti ya mtu mwingine. Badala yake, boresha sauti yako mwenyewe pamoja na hali zake. Unawezaje kufaulu? Kuna mambo mawili makuu.
Pumua Vizuri. Ili sauti yako iwe nzuri, unahitaji hewa ya kutosha na unahitaji kupumua vizuri. Bila kufanya hivyo, sauti yako inaweza kuwa dhaifu mno na unaweza kukata-kata maneno katika hotuba yako.
Sehemu kubwa za mapafu haziko juu kifuani; sehemu hizo huonekana kubwa kwa sababu tu ya mifupa ya mabega. Lakini, sehemu za mapafu zilizo pana zaidi ziko chini, juu tu ya kiwambo. Kiwambo kinashikana na mbavu za chini na kinatenganisha kifua na tumbo.
Ukivuta pumzi na kujaza tu sehemu za juu za mapafu, utakosa pumzi haraka. Sauti yako itakosa nguvu na utachoka haraka. Ili uvute pumzi vizuri, unahitaji kuketi au kusimama vizuri na kurejesha mabega nyuma. Jaribu sana usipanue sehemu ya juu pekee ya kifua unapovuta pumzi. Kwanza vuta pumzi kabisa. Sehemu za chini za mapafu zikijaa hewa, mbavu zako za chini zitapanuka. Kwa wakati huohuo, kiwambo kitasonga chini, kikisukuma chini kwa utaratibu sehemu za tumbo hivi kwamba utasikia mkazo kwenye mshipi wako au kwenye vazi katika eneo la tumbo. Lakini mapafu hayako kwenye eneo la tumbo; yamefunikwa na mbavu. Unaweza kuthibitisha jambo hilo kwa kuweka mkono mmoja kila upande wa mbavu za chini. Kisha vuta pumzi kabisa. Kama unavuta pumzi vizuri, utaona kwamba huingizi hewa tumboni na kuinua mabega. La, badala yake, utasikia mbavu zikisonga juu kidogo na kupanuka.
Kisha, jaribu kushusha pumzi. Usishushe pumzi kwa ghafula. Ishushe polepole. Usijaribu kuzuia pumzi kwa kukaza koo kwa sababu sauti itajikaza au itakuwa nyembamba sana. Mkazo wa misuli ya tumbo na mkazo wa misuli iliyo kati ya mbavu huondosha pumzi, lakini kiwambo hudhibiti mwendo wa pumzi hiyo.
Msemaji anaweza kudhibiti jinsi anavyopumua kwa kujizoeza kama vile tu mwanariadha anavyofanya mazoezi ya mbio. Simama vizuri kama umerejesha nyuma mabega, vuta pumzi kabisa ili sehemu za chini za mapafu zijae hewa, kisha shusha pumzi polepole na kwa utaratibu ukihesabu kwa kadiri uwezavyo kabla ya kuvuta tena pumzi. Kisha jizoeze kusoma kwa sauti ukipumua kwa njia hiyo.
Tuliza Mkazo wa Misuli. Jambo jingine muhimu linalotokeza sauti nzuri ni utulivu! Unaweza kuboresha sana sauti yako ukijifunza kutulia unapozungumza. Ni lazima akili na mwili zitulie, kwa kuwa mkazo wa akili husababisha mkazo wa misuli.
Ondoa mkazo wa akili kwa kuwa na maoni mazuri juu ya watu unaozungumza nao. Ikiwa unakutana nao katika huduma ya shambani, kumbuka kwamba hata kama umejifunza Biblia kwa miezi michache tu, unajua mambo mazuri sana kuhusu kusudi la Yehova ambayo unaweza kuwaeleza. Na unawatembelea kwa sababu wanahitaji msaada, iwe wanatambua jambo hilo au la. Na kama unatoa hotuba katika Jumba la Ufalme, wengi wa wasikilizaji ni watu wa Yehova. Wao ni rafiki zako na wanataka ufaulu. Hakuna wasemaji wengine duniani ambao huhutubia wasikilizaji wenye urafiki na wenye upendo kama sisi.
Ifikirie misuli ya koo na kujaribu kuituliza. Kumbuka kwamba nyuzi zako za sauti hutikisika zinapopitisha hewa. Sauti hubadilika misuli hiyo ikikazika au ikitulia kama tu vile uzi wa gitaa hubadili sauti ukikazwa au ukilegezwa. Sauti hurudi chini nyuzi za sauti zinapotulia. Kutuliza misuli ya koo pia hufanya mianzi ya pua ibaki wazi, na hiyo huboresha sauti.
Tuliza mwili wako mzima—magoti, mikono, mabega, na shingo. Ukifanya hivyo, utaweza kuvumisha sauti vizuri ili isikike wazi. Sauti huvumishwa wakati mwili wote unapohusika kuitokeza, lakini mkazo huizuia. Sauti hutokezwa kwenye zoloto nayo huvumishwa katika mianzi ya pua, kwenye mifupa ya kifua, meno, na kaakaa ya mdomo na mianya iliyo katika mifupa ya pua. Sehemu hizo zote zinaweza kuchangia ubora wa sauti. Ukiweka kitu kwenye kibao cha gitaa cha kupaazia sauti, sauti itafifia; ni lazima kibao hicho kisiwe na kitu ili kitikisike na kutoa sauti vizuri. Ndivyo ilivyo pia na mifupa ya mwili wetu ambayo imeshikiliwa na misuli. Uvumishaji mzuri wa sauti unakuwezesha kuwa na ubadilifu wa sauti na kuweza kuonyesha hisia mbalimbali unapozungumza. Pia utaweza kuhutubia watu wengi zaidi bila kukaza sauti.