Kondoo Wanaitikia Sauti ya Mchungaji
◇ Katika mmojawapo wa mifano yake, Yesu Kristo alionyesha kwamba kondoo wanajifunza kutambua sauti ya mchungaji na kuitikia sauti yake yeye peke yake: “Kondoo humsikia sauti yake; . . . wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.” (Yohana 10:3, 4) Msafiri aliyetembelea Nchi Takatifu majuzi aliona ukweli wa maneno hayo. Anasema hivi: “Tulitaka kupiga picha ya sinema ya kondoo fulani tukajaribu kuwafanya wakaribie. Lakini hawakutufuata kwa sababu hawakujua sauti zetu. Kisha mvulana mdogo mchungaji akaja; hata hakuwa amemaliza kuwaita nao wakamfuata. Tukatia sauti ya mchungaji huyo katika utepe na baadaye tukaifungulia tuisikie. Salaala! sasa kondoo wakatufuata na sisi pia!”