Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • lfb somo la 40 uku. 98-uku. 99 fu. 2
  • Daudi na Goliathi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Daudi na Goliathi
  • Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Habari Zinazolingana
  • “Vita Ni vya Yehova”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2016
  • Daudi na Goliathi
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Daudi hakuogopa
    Wafundishe Watoto Wako
  • Daudi—Kwa Nini Hakuogopa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
lfb somo la 40 uku. 98-uku. 99 fu. 2
Daudi akimrushia Goliathi jiwe kwa kombeo

SOMO LA 40

Daudi na Goliathi

Yehova alimwambia Samweli hivi: ‘Nenda kwenye nyumba ya Yese. Mmoja kati ya wanawe atakuwa mfalme wa Israeli anayefuata.’ Kwa hiyo, Samweli akaenda kwenye nyumba ya Yese. Alipomwona mwana mkubwa wa Yese, akawaza hivi: ‘Kijana huyu ndiye anayepaswa kuwa mfalme.’ Lakini Yehova akamwambia Samweli hakuwa amemchagua kijana huyo. Yehova akasema: ‘Mimi ninaona kilicho moyoni mwa mtu, si jinsi alivyo kwa nje tu.’

Samweli akimtia Daudi mafuta

Yese akawaleta watoto wake wengine sita mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema: ‘Yehova hajamchagua yeyote kati yao. Je, una wana wengine?’ Yese akasema: ‘Nina mwana mwingine mmoja, yule wa mwisho, Daudi. Yuko nje anachunga kondoo zangu.’ Daudi alipoingia, Yehova akamwambia Samweli: ‘Huyu ndiye!’ Samweli akamimina mafuta juu ya kichwa cha Daudi na kumtia mafuta kuonyesha kwamba atakuwa mfalme wa Israeli wakati ujao.

Goliathi

Muda fulani baada ya hapo, Waisraeli wakaenda kupigana na Wafilisti. Walikuwa na jitu shujaa lililowapigania lililoitwa Goliathi. Siku baada ya siku, Goliathi aliwadhihaki Waisraeli. Alisema hivi kwa sauti kubwa: ‘Leteni mwanamume apigane nami. Akishinda, sisi tutakuwa watumwa wenu. Lakini mimi nikishinda, ninyi mtakuwa watumwa wetu.’

Daudi akaja kwenye kambi ya jeshi la Waisraeli kuwaletea ndugu zake chakula. Ndugu zake walikuwa askari-jeshi. Aliposikia maneno ya Goliathi, Daudi akasema: ‘Mimi nitapigana naye!’ Mfalme Sauli akamwambia hivi: ‘Wewe ni mvulana tu.’ Daudi akamjibu: ‘Yehova atanisaidia.’

Sauli akajaribu kumvisha mavazi yake ya vita, lakini Daudi akasema: ‘Siwezi kupigana nikiwa nimevaa mavazi haya ya vita.’ Daudi akachukua kombeo lake na kwenda mtoni. Akachagua mawe matano laini na kuyatia ndani ya mfuko. Kisha Daudi akakimbia kumwelekea Goliathi. Jitu hilo likasema hivi kwa sauti: ‘Njoo hapa wewe mvulana. Nitawapa nyama yako ndege wa mbinguni na wanyama wa mwituni.’ Daudi hakuogopa. Akajibu kwa sauti: ‘Unakuja ukiwa na upanga na mkuki, lakini mimi ninakuja kwa jina la Yehova. Wewe hupigani nasi; unapigana na Mungu. Kila mtu hapa ataona kwamba Yehova ni mwenye nguvu kuliko upanga au mkuki. Yeye atawatia ninyi nyote mkononi mwetu.’

Daudi akatia jiwe katika kombeo lake na kulitupa kwa nguvu zake zote. Kwa msaada wa Yehova, jiwe likampiga Goliathi kwenye paji la uso wake na kupenya ndani. Jitu hilo likaanguka chini kwa kishindo likiwa limekufa. Kisha Wafilisti wakakimbia ili wasiuawe. Je, wewe unamtegemea Yehova, kama Daudi alivyofanya?

“Kwa wanadamu haiwezekani, lakini sivyo ilivyo kwa Mungu, kwa maana mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”—Marko 10:27

Maswali: Yehova alimchagua nani awe mfalme wa Israeli aliyefuata? Daudi alimshindaje Goliathi?

1 Samweli 16:1-13; 17:1-54

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki