SOMO LA 42
Yonathani Alikuwa Hodari na Mshikamanifu
Yonathani, mwana wa kwanza wa mfalme Sauli, alikuwa shujaa hodari wa vita. Daudi alisema kwamba Yonathani alikuwa na mbio kuliko tai na alikuwa na nguvu kuliko simba. Siku moja, Yonathani aliona wanajeshi Wafilisti 20 wakiwa juu ya mlima. Alimwambia hivi mtumishi aliyembebea silaha: ‘Tutawashambulia ikiwa tu Yehova atatupa ishara. Wafilisti wakituambia twende mahali walipo, hiyo itakuwa ishara kwamba tunapaswa kuwashambulia.’ Wafilisti wakapaaza sauti: ‘Njooni tupigane!’ Kwa hiyo, wanaume hao wawili wakapanda mlima huo na kuwashinda askari-jeshi hao.
Kwa kuwa Yonathani alikuwa mtoto wa kwanza wa Sauli, yeye ndiye aliyepaswa kuwa mfalme baada ya baba yake. Lakini Yonathani alijua kwamba Yehova alikuwa amemchagua Daudi kuwa mfalme wa Israeli anayefuata. Yonathani hakumwonea Daudi wivu. Yonathani na Daudi wakawa marafiki wa karibu. Waliahidi kulindana na kuteteana. Yonathani akampa Daudi koti, upanga, upinde, na mshipi wake kama ishara ya urafiki wao.
Daudi alipokuwa akimkimbia Sauli, Yonathani alimwendea na kumwambia hivi: ‘Usiogope, uwe jasiri. Yehova amekuchagua kuwa mfalme. Hata baba yangu anajua jambo hilo.’ Je, ungependa kuwa na rafiki mzuri kama Yonathani?
Zaidi ya mara moja, Yonathani alihatarisha maisha yake ili kumsaidia rafiki yake. Alijua kwamba Mfalme Sauli alitaka kumuua Daudi, kwa hiyo akamwambia baba yake hivi: ‘Ukimuua Daudi utakuwa ukifanya dhambi; hajafanya kosa lolote.’ Sauli alimkasirikia Yonathani. Miaka michache baadaye, Sauli na Yonathani wakafa vitani.
Baada ya Yonathani kufa, Daudi alimtafuta Mefiboshethi, mwana wa Yonathani. Daudi alipompata Mefiboshethi, alimwambia hivi: ‘Kwa sababu baba yako alikuwa rafiki yangu wa karibu, nitakutunza maisha yako yote. Utaishi katika nyumba yangu ya kifalme na utakula mezani pangu.’ Daudi hakumsahau kamwe rafiki yake Yonathani.
“Mpendane kama vile nilivyowapenda. Hakuna mtu aliye na upendo mkuu kuliko huu, kwamba mtu atoe uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”—Yohana 15:12, 13