Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • it uku. 493
  • Malipo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Malipo
  • Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Habari Zinazolingana
  • Wewe Unapookota Vitu Njiani, Unasema “Bahati Yangu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Sheria
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Ufahamu wa Kina wa Maandiko
it uku. 493

MALIPO

Kiasi kinachotolewa au kupokewa ili kulipia huduma, hasara, au jeraha. Kitenzi cha Kiebrania kinachotafsiriwa ‘kulipa’ (sha·lemʹ) kinahusiana na neno sha·lohmʹ, linalomaanisha “amani.” (Kut 21:36; 1Fal 5:12) Kwa hiyo, kitenzi hicho kinahusiana na kurudisha amani kupitia malipo au fidia. Chini ya Sheria ya Musa, malipo yalihitajika ili kulipia majeraha au hasara katika nyanja zote za mahusiano ya kibinadamu. Vilevile, malipo yalitolewa ili kulipia kazi au huduma zilizotolewa. Wafanyakazi wa kukodiwa, iwe ni Waisraeli, au wakaaji wageni, na wengineo, walipaswa kulipwa mishahara yao siku ileile.​—Law 19:13; Kum 24:14, 15.

Kujeruhiwa. Mtu aliyemjeruhi mwenzake kwa kumpiga alipaswa kulipia muda ambao mtu aliyejeruhiwa alipoteza kwa kutofanya kazi, hadi alipopona kabisa.​—Kut 21:18, 19.

Wanaume wawili walipopigana na kumuumiza mwanamke mwenye mimba au kusababisha mtoto (watoto) wake ‘atoke,’ lakini bila kusababisha kifo, mume wa mke huyo alipaswa kulipwa hasara na mtu mwenye hatia. (Ikiwa mume angedai kiwango cha juu kupita kiasi, waamuzi wangeamua malipo yaliyopaswa kutolewa.)​—Kut 21:22.

Ikiwa ng’ombe dume alikuwa na mazoea ya kuwapiga watu pembe na mwenye ng’ombe alikuwa ameonywa mara nyingi kuhusu jambo hilo lakini hakumzuia mnyama huyo, basi, ikiwa ng’ombe huyo angempiga pembe mtumwa na kumuua, bwana wa mtumwa huyo alipaswa kupokea malipo ya shekeli 30 (Dola 66 za Marekani) kutoka kwa mwenye ng’ombe huyo. Kulingana na wasomi Wayahudi, jambo hilo liliwahusu watumwa wa kigeni bali si Waebrania. Ikiwa ng’ombe dume huyo angempiga pembe mtu aliye huru, mwenye ng’ombe huyo alipaswa kuuawa. Hata hivyo, ikiwa waamuzi wangeamua kwamba hali au mambo mengine yangeruhusu kupunguza adhabu hiyo, mtu huyo angelipia fidia. Katika kisa kama hicho, mmiliki wa ng’ombe dume huyo alipaswa kulipa kiasi chochote ambacho waamuzi wangeamua. Isitoshe, mmiliki wa ng’ombe huyo alipata hasara kwa sababu mnyama huyo angeuawa kwa kupigwa mawe. Nyama yake haingeliwa. (Kut 21:28-32) Inaonekana sheria hiyo ilihusu pia wanyama wengine ambao wangesababisha majeraha yanayoweza kusababisha kifo.

Ikiwa mwanamume angelala na bikira, alipaswa kumchukua awe mke wake; hata ikiwa baba angekataa kumkabidhi binti yake kwa mwanamume huyo, alipaswa kumlipa baba yake kiasi kinacholingana na mahari (shekeli 50; Dola 110 za Marekani) kwa ajili ya bikira huyo, kwa sababu thamani yake akiwa bikira sasa imepungua, na hivyo hasara ilipaswa kulipwa.​—Kut 22:16, 17; Kum 22:28, 29.

Uchongezi. Mwanamume aliyetoa madai ya uwongo kwamba mke wake alidanganya kuwa bikira walipooana alipaswa kumlipa baba ya mwanamke huyo malipo mara mbili ya bei ya bikira (shekeli 50 × 2; Dola 220 za Marekani) kwa kuharibu sifa ya bikira Mwisraeli.​—Kum 22:13-19.

Malipo yalipaswa kutolewa pia ikiwa mwanamume angetoa mashtaka ya uwongo kwamba mke wake si mwaminifu. Ikiwa mashtaka hayo yangekuwa ya kweli, viungo vya uzazi vya mwanamke huyo vingedhoofika, na angepoteza uwezo wake wa kuzaa, lakini, ikiwa asingekuwa na hatia, mume wake alipaswa kumpa mimba. Kwa hiyo angebarikiwa kwa kupata mtoto.​—Hes 5:11-15, 22, 28.

Kuiba. Sheria ilikataza kuiba. Ilisema hivi kumhusu mwizi: “Anapaswa kulipa. Ikiwa hana chochote, basi atauzwa ili kulipia vitu alivyoiba. Kama mnyama aliyeibwa anapatikana akiwa hai mikononi mwake, awe ni ng’ombe dume au punda au kondoo, anapaswa kulipa mara mbili.” Hilo lilihusisha pesa au vitu vingine na vilevile wanyama. Ikiwa mwizi angemchinja mnyama aliyeibiwa au kumuuza, basi alipaswa kutoa kiasi kikubwa zaidi cha malipo, yaani, kwa ajili ya ng’ombe dume mmoja angetoa ng’ombe dume watano, na kwa kondoo mmoja angetoa kondoo wanne. (Kut 22:1, 3, 4, 7) Sheria hiyo ingemlinda na kumlipa yule aliyeibiwa na kumfanya mwizi afanye kazi ili kulipia kosa lake, badala ya kufungwa jela na kuiletea jamii gharama za kumtunza, huku mtu aliyeibiwa akiachwa bila malipo.

Majeraha na Uharibifu wa Mali. Mtu aliyemuua mnyama wa mtu mwingine alipaswa kumlipia. (Law 24:18, 21) Ng’ombe dume alipomuua ng’ombe dume mwingine, mnyama aliye hai aliuzwa, na bei ya mnyama huyo aliye hai na ya yule aliyekufa iligawanywa kati ya wamiliki wa wanyama hao. Hata hivyo, ikiwa ng’ombe huyo alijulikana kuwa mkali, mmiliki wake angemlipa yule mmiliki mwingine kwa kumpa ng’ombe dume aliye hai na kumchukua yule aliyekufa, yaani, mwenye thamani ndogo.​—Kut 21:35, 36.

Mazao bora ya shambani au ya shamba la mizabibu yalipaswa kutolewa kama malipo kwa uharibifu uliosababishwa na mnyama aliyeingia katika shamba na kula au kuharibu mimea. Ikiwa mtu angewasha moto ambao ungeenea katika shamba la mtu mwingine na kusababisha uharibifu, mmiliki wa shamba hilo alipaswa kulipwa kikamili. Hukumu kali zaidi ilitolewa kwa mnyama aliyeingia katika shamba kwa sababu ni rahisi kuwadhibiti wanyama kuliko moto, pia kwa sababu mnyama anayelisha alikuwa akifaidika isivyo haki kama mwizi; hivyo, malipo ya juu zaidi yalipaswa kutolewa.​—Kut 22:5, 6.

Dhamana. Ikiwa mtu angeachiwa bidhaa au mizigo ili kuitunza kisha iibiwe, ikiwa mwizi angepatikana kwa kawaida angetoa malipo mara mbili. Pesa na vitu vingine vyenye thamani ambavyo mtu angeachiwa havikupaswa kutunzwa kwa njia ya pekee bali vilipaswa kuwekwa mahali salama. Ikiwa mtu angepewa jukumu la kumtunza mnyama wa mtu mwingine, alipaswa kumtunza kama mnyama wake. Kwa kawaida mtu huyo alilipwa chakula ambacho mnyama huyo angehitaji, na wakati mwingine malipo kwa ajili ya usumbufu wa ziada wa kumtunza mnyama huyo. Ikiwa mnyama huyo angekufa mwenyewe, kushambuliwa na mnyama wa mwituni, au kuibwa na wavamizi, mtu aliyeachiwa mnyama huyo hangekuwa na hatia. Kwa sababu hangeweza kuzuia hasara hiyo. Hilo lingeweza kuwapata pia wanyama wake, lakini ikiwa angeibiwa (na mtu ambaye angeweza kuzuiwa, au kwa sababu ya kutokuwa makini), mtu huyo alikuwa na hatia na alipaswa kulipa.​—Kut 22:7-13; ona Mwa 31:38-42.

Mtu aliyeazima mnyama kutoka kwa mtu mwingine kwa ajili ya matumizi yake alipaswa kutoa malipo kwa madhara yoyote ambayo yangetokea. (Kut 22:14) Ikiwa mmiliki wa mnyama huyo angekuwapo, hakuna malipo ambayo yangetolewa kwa sababu mmiliki wa mnyama huyo angekuwa akiilinda mali yake mwenyewe. Ikiwa kingekuwa kitu cha kukodiwa, mmiliki ndiye angepata hasara kwa sababu inatarajiwa kwamba angekuwa amejumlisha hasara katika bei ya kukodisha.​—Kut 22:15.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki