Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w78 4/1 kur. 3-4
  • Wewe Unapookota Vitu Njiani, Unasema “Bahati Yangu”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wewe Unapookota Vitu Njiani, Unasema “Bahati Yangu”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ANGALIA USISHAWISHIKE
  • JITAHIDI KUMTAFUTA MWENYEWE
  • Malipo
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Je, Unapaswa Kuwa Mnyoofu Nyakati Zote?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • ‘Wao Huzingatia Mazoezi Yao ya Kidini’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Maana Yake Nini Kuwa Mfuataji Haki?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
w78 4/1 kur. 3-4

Wewe Unapookota Vitu Njiani, Unasema “Bahati Yangu”

WEWE unaonaje unapopata kitu chenye thamani ambacho kimepotezwa na mtu mwingine?

Je! unajisikia kwamba sasa umepata mali, usitake kumrudishia aliyeipoteza kwa sababu hiyo ni ‘bahati yako’?

Labda wewe husemi hiyo sasa ni mali yako. Lakini, je! unaanza kusitasita kurudisha kitu hicho, ukiwaza hivi: ‘Mtu huyo asingalipaswa kuwa mzembe sana hata akipoteze,’ au ‘Mimi simjui mwenyewe. Si shauri langu kumjua​—⁠ingawaje, ni kazi nyingi mno kumtafuta’?

Ni vyepesi sana mtu kuwa na mawazo hayo. Lakini Mungu ana maoni gani juu ya kurudishia watu vitu walivyopoteza?

Tunaweza kujua maoni yake kwa kuichunguza sheria aliyoitoa kupitia kwa Musa kuhusu hali hiyo. Inasema: “Umwonapo ng’ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea, usijifiche kama usiyemwona; sharti utamrudisha kwa nduguyo. Na kwamba yule nduguyo hayupo karibu nawe, au ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie. Tena fanya vivyo kwa punda wake; tena fanya vivyo kwa mavazi yake; tena fanya vivyo kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo, kilichompotea ukakiona wewe; usijifiche kama usiyekiona.”​—⁠Kum. 22:1-3.

Ikiwa mtu alikuta wanyama waliopotea, angalilazimika kutumia pesa zake mwenyewe kuwalisha mpaka mwenyewe aonekanapo, lakini jambo hilo halikumpa mtu huyo kisababu cha kujiwekea wanyama hao wawe wake wala kuwaachilia wapotee, labda waibwe au washambuliwe na mbwa au wanyama-mwitu.

Kwa upande mwingine, ingekuwaje kama mtu mwenye kukipata kilichopotea angekichanganya pamoja na mali zake mwenyewe, asikirudishe? Akipatikana na kuonekana na hatia, angehesabiwa kuwa mwivi. Sheria ilisema hivi: “Kila jambo la kukosana, kama ni la ng’ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu cho chote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili.”​—⁠Kut. 22:9; linganisha Kutoka 22:1, 4.

Kisa cha namna hiyo kingeletwa mbele ya wazee wa mji huo, waliokuwa mawakili wa Mungu katika kuamua mambo hayo. Kwa kufanya uchunguzi wangejua mambo yalivyo, halafu wafikilize sheria. Kwa kawaida, vitu vinavyopotea na kupatikana vikiwa na mtu mwingine vinaweza kujulikana kwa sababu ya alama fulani za pekee, na vilevile vinaweza kutambuliwa na mashahidi wanaovijua. Ingalikuwa vyepesi kuvitambua hasa katika mitaa midogo zaidi ya Israeli.

Kama mtu angekutwa akiwa na kitu fulani alichookota, kungekuwa na haki gani ya kumshtaki kuwa mwivi? Waamuzi wangejuaje kama alikuwa amekiweka kwa muda tu mpaka mwenyewe apatikane? Wangejua alikuwa mwivi kwa sababu hakukitangaza wala hakujitahidi vya kutosha kumtafuta mwenyewe. Mtu mnyofu angaliwaeleza wazee na watu wengine wa mji huo kwamba aliokota kitu fulani na kukiweka akimtafuta mwenyewe. Hapo asingeweza kushtakiwa.

Bila shaka, ikiwa mtu alijitahidi sana kumtafuta mwenyewe muda wa kutosha, angeruhusiwa kukiuza kitu hicho au kukiondoa mikononi mwake kwa njia nyingine.

ANGALIA USISHAWISHIKE

Mtu ambaye kwa kawaida hawezi kuiba anaweza kushawishwa na kitu alichookota. Anaweza kupatwa na tamaa nyingi na kuwa sawa na mwivi. Mungu anamwona mtu wa namna hiyo kama anamtendea Yeye dhambi pamoja na mwenye kitu kile kilichopotea. Dhamiri ya mtu huyo ikimjulisha kwamba amefanya jambo baya, inampasa afanye haraka alinyoshe jambo hilo pamoja na mtu aliyemkosea na kumwomba Mungu msamaha,-​—⁠Mt. 5:23, 24.

Ni tabia gani inayofanya mtu anayeokota kitu, au anayedai apewe zawadi kwa sababu ya kukiokota, asijitahidi sana kumtafuta mwenyewe kwa uangalifu ili amrudishie? Tabia inayomwongoza ni PUPA. Nao wenye pupa (tamaa) hawatapewa na Mungu uzima wa milele.​—⁠1 Kor. 6:10.

JITAHIDI KUMTAFUTA MWENYEWE

Huenda mtu akauliza, ‘Nijitahidi kadiri gani kutafuta mwenye kitu kilichopotea?’ Angalia jambo lifuatalo lililoonwa kuhusu mfano mwema uliowekwa na mmoja wa Mashahidi wa Yehova:

Mwanamume mmoja wa San Francisco alipoteza kifuko chenye dola 395 (Zaire 343 au shilingi kama 3,160) alipokuwa akitoka katika gari dogo la kusafirishia watu mjini New York. Mmoja wa Mashahidi wa Yehova alikiokota kifuko hicho. Kwa kuwa maandishi yaliyokuwa katika kifuko hicho yalionyesha kwamba mwenye kukipoteza alikuwa akikaa katika hoteli fulani ya New York, Shahidi huyo alipigia hoteli hiyo simu. Lakini, mtu huyo alikuwa amekwisha ondoka kwenda London. Kwa kuangalia karatasi zilizokuwa zimeandikwa wakati wa kumpa mtu huyo mahali pa kukaa hotelini, Shahidi aliweza kumpigia simu ya mbali, mtu huyo akiwa London. Mtu huyo alipiga asante, nacho kifuko chake kikasafirishwa mahali anakofanya kazi katika San Francisco kikiwa na pesa zote isipokuwa zile zilizotumiwa kukisafirisha.

Ni vigumu kuokota vitu vyenye thamani nyingi hivyo. Hata hivyo, kanuni aliyoitaja Yesu inahusika: “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.”​—⁠Luka 16:10-13.

Ingawa kwa ujumla kurudisha kitu kilichopotea ni jambo dogo, kunahusu maulizo haya, Mimi nataka kutumikia nani au nini kama Mungu wangu? Je! nawatendea wengine kama ninavyotaka wanitendee?​—⁠Mt. 7:12.

Mtu mnyofu hadai apewe zawadi kwa sababu ya kuokota kitu, maana kufanya hivyo ni kutaka kitu cha mwenzake. Zawadi kubwa zaidi inapatikana kwa kuwa na dhamiri njema, pamoja na furaha. “Heri washikao hukumu, na kutenda haki sikuzote.” (Zab. 106:3) Zaidi ya hilo, tukiwa na unyofu bila kutaka kujionyesha kuwa wenye haki, unyofu wetu unaweza kumfanya mwenzetu atake kuijua kweli ya Neno la Mungu, pamoja na kanuni zake njema. Hiyo ni mojawapo njia tunazoweza kutumia ‘tuidhihirishe kweli,’ kisha tuwe “tukijipendekeza wenyewe kwa kila dhamiri ya kibinadamu machoni pa Mungu,”‏ tukiwa wahudumu wake,​—⁠2 Kor. 4:2, NW.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki